Monday, April 19, 2010

Tunawapenda, Hatuwathamini.....Kwa kuwa hatuwajui

Agosti 8 2009 niliweka bandiko lenye kichwa cha habari Ni lini tutawaenzi WATU hawa? (jikumbushe hapa) na nilichohimiza ni kuwepo kwa namna ya kurejea kumbukumbu za WATU MUHIMU WALIOLITUMIKIA TAIFA KWA UFANISI NA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU ZAIDI KULIFIKISHA TAIFA HAPA LILIPO.
Lakini ni nani wa kufanya haya? Iwapo hata serikali yenye ina ikulu isiyo na tovuti iliyo hai?
Matokeo yake ni kuwa watu hawa muhimu wanakuja kukumbushwa kwetu na watu binafsi.
Mfano mzuuri saana ni Monsignor Fabby ambaye kupitia wavuti ya Dada Subi ameweka kumbukumbu nzuuri sana (kulingana na uwezo wake) ambayo kwa hakika imerejesha nyuma akili yangu na hisia juu ya kazi njema iliyokuwa ikifanywa na watu hawa.
Lakini ni wapi ambapo tunaweza kupata habari kama hizi? Mtandao wa TBC ambapo ndipo wahusika wa kwenye post hii hapa chini walifanya kazi hauna historia yao? Leo hii ukurasa wa TBC International ambao umekuwa "updated" March 03,2010 unasema "It is proposed that the official launch of TBC International to be January 1 2009." Soma mwenyewe mstari wa mwisho HAPA (kama bado wako hewani maana wana kwikwi)

Anyway, wacha nikurejeshee alichokumbusha Ndg Mnsignor nilillipata HAPA kwa Da Subi. Nimeongeza taswira

Wahenga walisema ya kale ni dhahabu, leo naomba niwakumbushe baadhi ya watangazaji wetu mahiri waliokuwa wakilitumikia taifa katika kutupasha habari, kutuelimisha, na kutuburudisha. Ni kumbukumbu ya muda mrefu kidogo hivi nitakapowasahau wengine tafadhali karibuni sana tukumbushane ili tuwakumbuke na kuwaenzi hawa wanahabari wetu mahiri katika eneo la utangazaji miaka hiyo.

Mzee David Wakati enzi zake. Picha:Ukurasa wa historia wa BBC Swahili
Alikuwepo David Wakati (Mkurugenzi) – pamoja na vipindi vingine alikuwa maarufu zaidi kwenye kipindi cha Nipe habari. Kisha kuna Ahmed Kipozi -Taarifa ya habari na External Service, Khalid Ponera – Maarufu kwenye Zilipendwa Jumapili asubuhi subuhi kwenye na robo mara baada ya taarifa ya habari na matangazo ya vifo, Nassoro Nsekeli akitangaza majira asubuhi saa kumi na mbili na nusu na saa tatu usiku. Hapo kwa mwanafunzi majira ikikukuta bado upo nyumbani unajua umeshachelewa shule siku hiyo jiandae kwa bakora. Mhe: Sarah Dumba ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya. Picha: Mwananchi
Pia kulikuwa na Sarah Dumba (Mkuu wa Wilaya) – maarufu kwenye taarifa ya habari, Salim Seif Nkamba mwenyewe akijiita SS Mkamba maarufu kwa taarifa ya habari pia, Salim Mbonde akitangaza mpira huyu tulikuwa tunaamini eti alikuwa mnazi wa Simba, Ahmed Jongo (Mungu Amrehemu) – tuliamini alikuwa mnazi wa Yanga kwelikweli tukawa tunawekeana utani eti Jongo kasema Simba bila sisi mbili halafu Hassan Mkumba akipiga matangazo ya vifo baada tu ya taarifa ya habari.
Waliong'ara RTD Mhe Betty Mkwasa, Sango Kipozi na Ahmed Kipozi siku ya uzinduzi wa TBC. Picha Habari na Matukio Blog
Walikuwepo pia Chalz Hilary mwenyewe akiwa hataki aitwe Charless huyu ndo pro mwenyewe wa mpira kabla ya kuhamia Radio One na kujichukulia umaarufu mpaka kufikia kuitwa mzee wa Macharanga, Julius Nyaisanga- Brazamen wa RTD miaka hiyo. Akitangaza Club Raha Leo Show utamsikia mimi ni mtangazaji wako wa kawaida uncle J Nyaisanga ukipenda ni super tall...adios Sayonara (sasa hii sayonara nikawa siielewi nikawa nasema adios ‘seremala’), Siwatu Luwanda –alikuwa maarufu kwenye mama na mwana Jumamosi saa tisa na dk 2 na marudio Ijumaa jioni na mahiri kwenye taarifa ya habari. Ilikuwa ni mwiko kwa mtoto kukosa hiki kipindi. Halafu akawepo Bibi Debora Mwenda - mtaalamu mwenyewe wa mama na mwana enzi za ua jekundu, binti chura, Salama Mfamao akituletea taarifa ya habari na mchana mwema, Christina Chokunogela wakiichangamsha RTD enzi hizo maarufu kwenye ombi lako eti muombaji wimbo anasema tafadhali mtangazaji usiniweke kapuni, naomba nipigie wimbo wa Solemba....maana kila nikiusikia wimbo huu hata kama nilikuwa nakula huacha kula mpaka wimbo uishe ah...

Halafu alikuwepo Chisunga Steven mzee wa kanda ya Ziwa Magharibi alikuwa mtaalamu wa Ugua pole na akituripotia habari za RTC Kigoma kuzigagadua Simba au Yanga, Pale Arusha alikuwepo Batty Kombwa - Mzee wa Arusha huyu yeye alikuwa mtaalamu wa Wakati wa Kazi ile mida ya asubuhi mchana kabla ya saa sita. Inapofika kwenye wataalamu wa kutangaza mpira, Dominic Chilambo (Mungu amrehemu)- ndiyo alikuwa kipenzi changu. Huyu Mzee wa TP Lindanda wana Kawekamo alikuwa ananikosha sana utamsikia Marsha kwakeee Massatu, anampelekea Kitwana Seleman kwake Mao Mkamy Ball Dancer kwake Beya Simba anarudisha pembeni kuleee kwake Edward Hizza ...enzi hizo Pamba inakanyaga acha tu. Alijua sana kuipamba Pamba na alikuwa na mapenzi ya kweli kwa hiyo timu. Baadaye akaja Bujaga Izengo wa Kadago alikuwa na sauti fulani hivi mtaalamu wa Taarifa ya habari, Edda Sanga (Mkuu wa wilaya sasa) - Mama na Mwana alikuwa na sauti ya upole hivi ya kimama hasa wakati mwingine akitangaza External Service. Aloycea Maneno- akitangaza kwa umahiri kabisa Ombi lako, Mama na Mwana, na CheiChei Shangazi...

Wengine ambao siwezi kuwasahau ni Barnabas Mluge (jamaa alikuwa mnazi wa CDA huyu acha tu enzi hizo zikitamba pamoja na Kurugenzi na Waziri Mkuu - Ukimsikia ameanza watoto wa Nyumbani CDA ya Dodoma hapo basi mjue Simba au Yanga mshalala hapo. Walikuwepo pia Omar Jongo (mpira), Mohamed Amani (Mohamed Dahman), Idrissa Sadallah - kanda ya nyanda za juu kusini akiifagilia Tukuyu Stars huyu, Abisay Steven wa Kanda ya Ziwa Nyasa yeye na Majimaji humtoi huyu. Hapo akiwapamba akina Celestine Sikinde Mbunga, Octavian Mrope, Dadi Athuman, Samli Ayoub ‘beki mstaarabu’...acha tu, Peter Makorongo na sauti yake nzito hivi akiwa Arusha kule kabla hajaamishiwa Mtwara, Angalieni Mpendu maarufu sana kwenye hisia na muziki kipindi kilichojichotea washabiki wengi kwa ule umahiri wake wa kupangilia stori na muziki, Titus Phillipo, Nazir Mayoka, Abdul Ngalawa (taarifa ya habari na mazungumzo baada ya habari yamewajia kutoka redio Tanzania DSM….halafu anaanza stori fulani mwisho unapewa ujumbe wa siasa ni kilimo, ujamaa na kujitegemea, mtu ni afya, na vitu kama hivyo), Juma Ngondae, Mohamed Kissengo, Malima Ndelema, Abdala Mlawa alikuwa mtaalamu mwingine huyu wa ombi lako, Hendrick Michael Libuda mtaalamu wa Mkoa kwa Mkoa, Mikidadi Mahmoud maarufu sana kwenye kutangaza mpira, Rosemary Mkangala (External Service na taarifa ya habari), na Abdallah Majura kabla hajahamia Radio One na kisha BBC. Halafu kule Zanzibar alikuwepo Yusuph Omar Chunda, zaidi namkumbuka kwenye kipindi cha michezo mida ile ya saa mbili kasorobo hivi nyakati hizo Small Simba na KMKM zikitamba kwelikweli kabla ya kuja Miembeni na Malindi.

Halafu kuna Michael Katembo huyu jamaa vipindi vyake alikuwa anavipamba mpaka utapenda kusikiliza tumbuizo asilia na mkoa kwa mkoa. Pale Mbeya baadaye akaenda Nswiiiiiima Ernest maarufu sana kwenye Majira na kuripoti matukio, halafu kanda ya ziwa alikuwepo Nathan Rwehabura. Siwezi kumsahau Jacob Tesha mwenye sauti nene yenye mkwaruzo hivi maarufu sana kwenye taarifa ya habari na External Service. Akisoma habari utapenda maana anasoma kwa utulivu na umahiri mkubwa. Lakini mwisho wa yote alikuwepo Ben Kiko, mzee mwenye mbwembwe na madoido ambaye kila ukisikia sauti yake ni lazima uvutike kumsikiliza. Waliokuwepo wakati wa vita ya Kagera wanasimulia jinsi walivyokuwa hawakosi kuketi pembeni ya redio zao kumsikiliza huyu bwana mkubwa akiwapa simulizi ya jinsi wazee wetu wa JWTZ walivyokuwa wakimvurumusha Amin.

Ama kwa hakika ya kale ni dhahabu na haina budi kutunzwa hata kwa kukumbukwa na kuenziwa tu. Asanteni sana watangazaji wetu, Taifa daima litawakumbuka.

Monsignor

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

7 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka Mubelwa umeifanya Jumatatu yangu kuanza kwa tabasamu la bashasha kwa kumbukumbu hii ya watangazaji ambao nilivutiwa nao sana. Nikiwa mdogo, wakati huo nyumbani hakuna televisheni, nilipenda sana kusikiliza RTD. Nilivutiwa sana na watangazaji wale waliokuwa mahiri kweli kweli.

Ahsante sana.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

tatizo ama changamoto ni kuwa hatuna mifumo makini ya kumbukumbu kabisa.

Hii kumbukumbu imenifurahisha kwa kweli.

Thanks weye na Da Subi

Subi Nukta said...

Asante Mzee kwa kuboresha posti kwa kuiongezea picha. Napotoa shukrani kwa niaba ya Fabby (yupo huko Uchina walikozuia google na blogger basi inanipasa ku-copy na ku-paste kumfahamisha yanayoenziwa maandiko yake, basi yeye anaishia tu kutoa shukrani kedekede kwa wote).
Hayo uliyozungumzia wewe na Chacha na wengine kuhusu kumbukumbu, mi nasikia hata kizunguzungu kujaribu kuongelea tena. Watu gani kila siku lazima kusukumana katika suala la kumbukumbu? utadhani siye wakimbizi katika nchi yetu ya kuzaliwa! kha!

Anonymous said...

Umenifurahisha sana na kumbukumbu hii. Umenikumbusha mbali sana hasa kipindi cha majira kikikukuta nyumbani unajua umechelewa shule yaani nimecheka kama vile tulikuwa pamoja. Umemsahanu Idi Rashid Mchatta, Stephen Lyimo na Karim Besta hawa wote sasa ni marehemu lakini walikuwa na sauti zao za kipekee. Lyimo alikuwa maarufu katika kipindi cha salam, akisoma kadi utapenda

Anonymous said...

Labda niweke sawa tu Ahmed Jongo bado yu hai, Jongo aliyetangulia mbele za haki ni Omar. Naomba urekebishe hilo.

Mzee wa Changamoto said...

Hello Anon.
Asante kwa mnarekebisho ndugu yangu. Kama nilivyosema, hii post niliichukua KAMA ILIVYO kwenye ukurasa niliounukuu na iliandikwa na Ndugu niliyemnukuu.
Naenda kufuatilia hili na kisha nitarekebisha accordingly.
ASANTE SANA

Fadhy Mtanga said...

Daaaah! Umerudisha nyuma kumbukumbu za kukuwa kwangu. Ahsante sana mkuu.