Nakumbuka mwaka 2000 nilikuwa nikihudhuria mazoezi ya mgongo pale Muhimbili baada ya ajali ya Dec 1999. Siku moja niliamini kuwa katika maumivu makali saana. Na nilikuwa nikisubiri zamu yangu kwenda kuonwa na Daktari (pale taasisi ya mifupa) kabla ya kurejea mazoezini na nikiwa nimekaa nikaona wenzangu wakiongea na nilidhani hawakuwa katika maumivu kama niliyokuwa nayo. Nilihisi kuwa mwenye maumivu kuliko wote. Baada ya dk kama 30 kupita, ikaongezeka sauti ya kaka mwingine aliyekuwa akiongea kwenye simu kwa sauti ambayo haikuonesha kuwa anaumia. Mawazoni mwangu nikawaza tena kuwa "hawajui niko katika maumivu kiasi gani". Niliponyanyua uso, nikamuona kaka aliyesimama pembeni yangu ambaye alionekana kuharibiwa vibaya mguu wake ajalini. Nilishangaa kuwa ndiye aliyekuwa akiongea vile. Nilijihisi kupona na nilimpisha akae mahali nilipokuwa nimekaa. NIKAJIFUNZA.
Katika maisha ya kila mmoja kuna maanguko meeengi ambayo yanapotokea huwa tunajiona kama ndio tumefika mwisho wa maisha. Tunafikiria "kwanini" na pengine kuwaza kama "kuna anayepitia haya?" Hatujui kuwa wapo walio katika mataabiko zaidi ya tuliyopo.
Jana usiku nilienda kumtembelea mtoto mchanga wa rafiki yangu ambaye anaumwa saana. Na nikiwa katika hospitali hiyo ya watoto niliona watoto weeengi walio katika hali za kuendeshewa maisha yao kwa mashine. Nikasikitika. Nina mpenzi makubwa saana na watoto kwa hiyo hali hiyo ilichukua sehemu kubwa ya furaha ya asili ndani mwangu. Nilijiuliza maswali mengi saaana kuhusu hali ile na kunifanya kurejesha taswira za maisha yangu tangu pale nilipoweza kukumbuka. Kisha nikarejea katika ukweli kuwa na mimi nilikuwa mtoto kama wao na niliweza kuvuka umri walionao. Niliona nyuso za wazazi wakiwa na matumaini ilhali wana uoga mwingi na ilinifanya kumuomba Mungu juu ya watoto hao. Niliporejea nyumbani ilinichukua muda kurejea katika hali ya kawaida. Na bado naendelea kuwaza na kujiuliza kama NILISTAHILI KUWA NAKATA TAMAA NIPATAPO MAKWAZO / MAJARIBU? Najiuliza kama TUNA HAJA YA KUONA KAMA MUNGU HAYUKO UPANDE WETU KWA KUWA HATUNA UHAKIKA WA KUWA NA AKIBA YA KUTOSHA MPAKA WAKATI WA MALIPO YAJAYO, AMA KWA KUWA TUNAHISI TUTASHINDWA MTIHANI DARASANI AMA KWA KUWA HATUWEZI KUNUNUA TUNACHOPENDA KUWA NACHO AMA KWA KUWA TUMEPOTEZA KAZI.
Nikiwaangalia watoto wale, nilihisi kama wangepewa uchaguzi wa kuendelea kuwa pale walipo, ama wakue na wakutane na yale yatukatishayo tamaa, sina shaka wangekubali kukua na kupambana na tupambanayo sasa.
Nimezidi kugundua na kujifunza kuwa kila kitokeacho kina sababu na naamini Mungu ana kila sababu ya kutuweka mahala fulani, wakati fulani, tukutane na fulani na tujifunze kitu fulani. Safari yangu ya jana imenifungua macho ya ki-Imani na kunifanya kuuangalia uhai wangu kwa "vipindi" vifupifupi ambavyo nimejaribu kufikiri mengi niliyoepushwa katika vipindi hivyo. Maradhi na mapungufu ya kabla na baada ya kuzaliwa, ajali na hatari mbalimbali na nimeona kuwa wengi wetu (nikiwemo) tunaishi kama vile kila siku ILIAHIDIWA KWETU. Si kweli
Ni kwa kutojua namna tulindwavyo ama namna namna tulivyoepushwa ma vyanzo vingi vya kifo, tunashindwa kumshukuru Mungu kwa uwepo wetu licha ya yale tupambanayo nayo.
Tunastahili kumshukuru Mungu kwa maisha yetu, kisha kumuomba aendelee kutuonesha yaliyo mapenzi yake.
Hivi niandikavyo nakaribia kuelekea hospitali kuona hatua za mwisho za madaktari kuokoa maisha ya binti wa rafiki yangu huyo (hajatimiza hata mwezi mmoja) kabla hawajazima mashine zimsaidiazo kuishi sasa ambazo zimepangwa kuanza kuzimwa takriban masaa mawili kamili yajayo.
KATIKA KILA GUMU TUPITIALO, TUSHUKURU MUNGU NA TUSIKATE TAMAA KABLA HATUJAONA YOTE KWANI KUNA WEEENGI WANAOTAMANI KAMA WANGEKUWA TULIPO SISI PAMOJA NA MATATIZO YETU. Hawawezi na pengine hawatafika tulipo kwani hawana muda wa kuishi.
JUMAPILI NJEMA
hakuna jmabo baya maishani, ila kuna matukio tu. na kila litusibulo, basi kuna sababu na mojawapo ikiwa ni kujifunza. kwa hiyo kupokea kila jambo lijavyo na kushukuru, ndio furaha kwani hata bible inawaasa kushukuru kwa kila jambo
ReplyDeleteNi kweli binadamu hatutosheki. Na kweli kila kitu tufanyacho ni muhimu kumshukuru mungu. Kwani ni kweli wengi huwa wanafikiri wao wana shida zaidi wakati kuna mwingine ana zaidi yako. Kwani kuna watu wana hali ngumu zaidi.
ReplyDelete