![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgmKQuuJ_oDk-FkFtqlLyWzQud7uXiVZtGYP9Q-vBlv_yNyhRzgW8Bp_QYHqbpAYv1-tllMT5K1qfajQG52mNd3gzs2eSe8AuSoytH7j7dM7Kp4ndHGuVI4A6UKGoyR9U9e3poOLU8tVB8/s400/Bob-Marley-1-.jpg)
Waweza kuwa na tafsiri yako ya Bob Marley na pengine hata hadhi utakayompa kulingana na mtazamo wako kwake, lakini ushahidi wa kazi yake waonesha kuwa alikuwa zaidi ya mwanafalsafa, zaidi ya mtabiri, zaidi ya muona mbali na aliyeona njia sahihi za kuikwamua dunia miongo kadhaa iliyopita, aliyehimiza kuhusu KUJITAMBUA kama njia ya kutuweka huru na pia alikuwa askari wa jeshi la amani aliyetumia kazi yake yake ya muziki kama silaha halisi.
Aliimba wimbo aliouita Real Situation uliohusu wanyang'anyi wa mali za watu wanaoamini kuwa "the total destruction is the only solution" na tunaona yatokeayo ulimwenguni sasa. Katika wimbo huo huo alisema "Give them an inch, they take a yard; Give them a yard, they take a mile" akiwaeleza wale ambao wakipata kisa cha kuingia nchini mwako hawatoki na kila siku watakuwa na sababu ya kuendelea kuwepo kuinyonya nchi. Ndio tuonayo leo.
Lakini pamoja na mengi aliyoonya, Bob aliliasa bara la Afrika na wana wa Afrika kuungana kama njia pekee ya kuweza kusonga mbele. Japo wapo waliopinga alilosema (kwa kuhukumu muonekano wake), alilosema lilifanyiwa kazi (kinadharia) takribani miaka 21 baada ya kifo chake. Waligundua ukweli wa alilosema na kujitahidi kujipachika uasili wa wazo japo yajulikana alisema nani, kwanini na ili kiwe nini.
Bob aliweka bayana katika wimbo wake wa AFRICA UNITE kuwa kuna umuhimu na ulazima wa kuungana kikweli kwani twahitaji ku"Unite for the benefit of your children, Unite for it’s later than you think". Kibaya ni kuwa WATAWALA wetu wajiitao viongozi na ambao wana upeo mdogo zaidi ya Bob hawasikilizi usia wa kutupeleka tutakako.Wanacheza POLI=TRIX
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjt8BMFrGuELJZ1aqlZ1V9GzyLQB0S4TnNwrNRcvEHjiW0w7OmcWJ2Ije5fAT57dnVJ6isPwmokVq6hh4KEZ_ZypZtcTgrfz8O42Mw4_J24_x9qENFLOwytIr48qL1cgskj_LEWz1LPmttf/s400/18_smiling.jpg)
Lakini Bob hakuwazungumzia wanasiasa pekee. Alisisitiza pia namna ya kujikwamua kutoka katika lindi la matatizo ambalo wanyonge wamekuwa wakiwekwa. Katika wimbo wake wa Redemption Song, Marley amewaasa wananchi na wanyonge kujua kuwa hatma ya maisha yao imo miongoni mwao kwa kuwakumbusha kuwa hakuna mwingine zaidi ya sisi wenyewe. Anasema "Emancipate yourself from mental slavery, none but ourselves can free our minds...". Na hili ndilo tatizo kwa wananchi wengi nchini mwetu ambapo tunalalamika kuhusu MAENDELEO japo HATUSHIRIKI kuyaleta (iwe kwa kuweka viongozi sahihi ama kuchagua wale walio tayari kutushirikisha kuyatafuta) Tunataka yule anayesema ATALETA MAENDELEO japo hakuna ukweli wa maendeleo halisi bila ushiriki wa wananchi husika.
Kwa wale waliokata tamaa na kufungwa na msongo wa maisha kutokana na kuwaza wasiyo na suluhisho nayo, Bob Marley anasemawakumbusha kuwa "Life is one big road with lots of signs. So when you riding through the ruts, don't complicate your mind. Flee from hate, mischief and jealousy. Don't bury your thoughts; put your vision to reality. Wake Up and Live!"
Leo ambayo ni kumbukumbu ya kufariki kwake miaka 31 iliyopita, tunaendelea kukumbuka aliyoimba Bob Marley kwa kuwa yalihusu maisha halisi. Yaligusa uhitaji halisi wa wanajamii na bado yanagusa. Ni hili lililomfanya aamini kuwa muziki wake hautakufa kwani unaeleza ukweli. Alinukuliwa akisema "My music will go on forever. Maybe it's a fool say that, but when me know facts me can say facts. My music will go on forever."
ONE LOVE TO YOU ALL AND LET US (PEOPLE) GET READY
No comments:
Post a Comment