Tuesday, September 22, 2009

Tanzania Yangu.. Yenye vyombo vingi vya habari visivyo na habari zaidi ya taarifa

Ni kweli kuwa na mimi nilikuwa mmoja wao. Najua nitarejea habarini kwani nilikuwa na bado nawapenda na ndio sababu nasema

Tanzania ni moja kati ya nchi zinazosemekana kuwa na vyombo vingi vya habari hasa katika ukanda wetu. Lakini hivyo vyombo vyetu vya habari vinakera na kuchosha kwani asilimia kubwa wanaripoti na wachache saaana huchambua. Ni kama vile vyombo vya habari nchini mwetu (zaidi Redio na Televisheni) havina kazi zaidi ya kukusanya taarifa mbalimbali na kuziwakilisha bila kuzichambua. Yaonesha kinachojaliwa zaidi ni uhakiki wa chanzo kilichosema habari hiyo na si uhakiki wa kile kilichosemwa. Yaani ukiskiliza Taarifa za Habari na hata vipindi kama Matukio, Majira na vingine, kinachofanyika ni ripoti ya nani kasema nini, ili kitendeke lini, lakini si kuangalia uhakiki wa takwimu za kilichosemwa, si uhakiki wa undani wa tatizo linalozungumziwa na si uhakiki wa uwezekano wa kupata suluhisho ama mafanikio kupitia kile kilichosemwa.
Tanzania tuna wataalamu wengi ambao tungeweza kuwahusisha. Tuna wachambuzi wa elimu mbalimbali ambao wangeweza kuweka mgongano wa mawazo (debate) endelevu katika hoja na taarifa zinazotolewa viongozi mbalimbali lakini wengi hawawatumii. Kuna wanasiasa wa pande mbalimbali ambao wangeweza kuchangia kiuendelevu katika kuzichambua hoja na masuluhisho mbalimbali zitolewazo na viongozi mbalimbali katika serikali na pengine kuangalia uwiano wa manufaa kati ya kisemwacho na serikali na kiwazwacho na wananchi. Labda UKWELI, lakini UHAKIKA???? ............Yaani TRUTH lakini sio FACT
Cha kusikitisha zaidi ni hata Redio inayomilikiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) inaendesha vipindi vilivyojaa kauli kama "akiongea na TBC", "kwa mujibu wa ....", "katika taarifa iliyotolewa na ..." ama "akizungumza na waandishi wa habari" ilhali wanajua kuwa wao (TBC) ndio chombo cha wananchi (kama kweli wananchi ndio wenye serikali) na wanastahili kuwaelimisha na kuwapa wananchi HABARI ZILIZO SAHIHI, ZA KWELI, ZILIZO NA UKINZANI SAHIHI KWA KUANGALIA PANDE ZOTE NA KUZICHAMBUA KWA KUSHIRIKIANA NA WATAALAMU. Kama unataka kupata sehemu ya hizo "habari nyepesi nyepesi" zilizostahili kuchimbwa zaidi lakini hazijafanyiwa hivyo, sikiliza mifano iliyopo kwa kuBOFYA HAPA katika vipindi vyao vya HARAKATI na MCHANA HUU.
TBC wana uwezo na inastahili kuwakusanya watu walio na uwezo wa kuchambua hotuba mbalimbali (kama wahadhiri wa masuala ya Uchumi, Siasa, Siasa za kimataifa, wataalamu wa kilimo, wataalamu wa biashara na wengine) na kisha kuzipitia kwa umakini hotuba na taarifa kila zitolewapo. Ndivyo wafanyavyo wahabarishaji makini niwaonao katika ulimwengu wa sasa na ni kwa hakika TBC wangefungua njia hiyo, basi hata redio na Televisheni nyingine zingefanya hivyo.
Ninafurahi kila nipatapo nafasi ya kuangalia Jenerali on Monday kwani anaonesha ufahamu wa hali ya juu katika kuhoji na kuchambua mambo mbalimbali na hasa linapokuja suala la siasa na siasa za kimataifa. Ni kwa kuwa ana ufahamu na ana upeo na pia anaalika wageni walio na uwezo wa kuelewesha mengi. Nakumbuka nilivyokuwa napenda kipindi cha "THE HEAT" cha Redio One kilipokuwa chini ya Dj JD na Sos B ambapo walihoji na kuuzungumzia muziki kwa undani kwa kuwa wote walikuwa kwenye tasnia hiyo na wanaijua vilivyo.
Waandishi (ama niseme wakusanya taarifa) wanang'ang'ania Idara ya Habari Melezo, kwenye ofisi za viongozi, kwenye "taarifa kwa vyombo vya habari" na viwanjani na pengine wanaripoti kile ambacho takribani watu wote wamekisikia ama kukiona (kama matukio ya michezo na sherehe zitangazwazo moja kwa moja) na hata hawatumii wataalamu kama makocha ama wakufunzi ama maafisa wa jeshi wastaafu ama wataalamu wa masuala ya ujasusi ama wanasheria kufafanua kinachoendelea michezoni, ama katika maonesho ya kielimu / kiteknolojia, ama kwenye maonesho ya kijeshi ama kwenye kesi na matokeo yake wananchi wanshindwa kuelewa kinachoendelea. Ndio maana kwenye kesi kama ya kina Zombe, wananchi wanaendelea kuamini kuwa wameachiwa kwa sababu ya kufahamika ama rushwa ama vyopvyote na kushindwa kutambua ukweli wa namna ambavyo MAHAKAMA IMESHINDWA KUTHIBITISHIWA MAKOSA YA WATUHUMIWA.
Na ndio maana ni rahisi kuwa na "connection" unapomsikiliza Soggy Doggy akiendesha Uhuru Flava kwani anafanya apendacho na alicho na historia na ujuzi nacho kuliko kumsikiliza naniii anayefanya kile waitacho "hard news"
Lakini hii yaonekana kuwa kawaida kwenye vyombo vya habari. Hata walio na dhamana ya kuendeleza na ambao wanajua kila kitu kuhusu utaratibu huu na ambao wameufanya na kuufuata wakati fulani wa maisha yao ya kazi wanashindwa kuuhimiza ilhali tunajua ni muhimu kwa jamii.
Lakini hii ndio TANZANIA YANGU...ILIYO NA VYOMBO VINGI VYA HABARI VISIVYO NA HABARI ZAIDI YA TAARIFA
Mungu Ibariki Tanzania
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

6 comments:

  1. Tatizo 'wenyewe' hawasomi blog hizi. Wanasoma tovuti za BBC, CNN, Sky News na kadhalika.
    Natamani wangesoma na blog, wana mengi ya kujifunza.

    ReplyDelete
  2. Kweli Mungu ibaribi Tanzania. Tatizo hili ni tatizo kubwa sana kwani hata hizo televisheni kuna wengine wanasikia tu jina mpaka hizo redio. Na kuna sehemu nyingine hata kupata gazeti kazi kweli. Sasa watajuaje yanayotekea Ulimwenguni.

    Nakubaliana na mtani Fadhy kuwa ingekuwa elimu kubwa sana kama wote wangekuwa wanasoma hizi blog wangekuwa wanajifunza mengi sana. Nakumbuka Kissima alitoa hili wazo pia kuwa tufanya juhudi watu wote wasome hizi blog kwani ni mengi ya kujifunza. Nasema tena MUNGU IBARIKI TANZANIA PIA WATU WAKE.

    ReplyDelete
  3. watanzania tunapenda saana mambo ya kihisia kama fulani ampiga fulani. hbr muhimu hazijulikani. kwa mfano, ni watanzania wachache sana wanaojua habari za global warming. babari kama za barafu ya k'njaro au maji victoria kuisha nk hazijulikani.. tupo kisiasa na kushabikia umbea zaidi. hata nchi haijulikani. vyombo vya habari haviandiki juu ya utalii, hali ya hewkilimo nk.

    makala zangu katika majarida mengi zinagonga mwamba. hazijulikani na wanataka zile za kisiasa zaidi. nilifurahi jana kupigiwa simmu na mmiliki mmoja wa gazeti fulanianataka liwe la kiutambi zaidi. ni hatua muhimu.

    ReplyDelete
  4. Posti hii ni elimu kuuuubwa kwa wananchi wanaoletewa habari pamoja na vituo vya utangazaji na utoaji habari kwa ujumla.
    Kweli wananchi tumekuwa tunaridhika na chanzo cha habari kuliko ukweli wa habari husika baada ya uchambuzi yakinifu.
    Yasikitisha sana kwani kuna vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi wayajuayo wenyewe wanadiriki hata kutoa habari za upotoshaji na kwa bahati mbaya wanatokea wananchi na kushabikia upotoshaji huo.Posti hii ni darasa tosha kabisa kwa wananchi na vyombo vya habari.


    Kama alivyosema dada Yasinta, juhudi za pekee kabisa hazina budi kufanywa ili angalao asilimia kubwa ya watanzania waweze kupata yale yaandikwayo bloguni.Sote kwa pamoja tuendelee kulitafakari hili ili tujue ni kwa namna gani litawezekana.

    Kuna watu wenye access na internet lakini tatizo ni kwamba hawafahamu kama kuna blogs na ni yapi yanaendelea ktk blogs.Binafsi naona hata kutoa matangazo tu kuhusu blogs itasaidia sana.

    ReplyDelete
  5. Mzee umefunika kabisa. Ndio ukweli wa mambo huo

    ReplyDelete
  6. kweli kabisa sasa nimekupata..safari bado tunayo..

    tutafika tu

    ReplyDelete