Monday, September 28, 2009

Naitamani zamani


Labda ni akili zangu, lakini naona uwiano kati ya mazuri na mabaya ya kile kiitwacho maendeleo unaonekana kunufaisha zaidi upande wa mabaya.
Lakini "MAENDELEO" ya sasa ni yale ambay watawala wetu WANAKARIRISHWA na wenye nguvu wao. Yaani nchi fulani ndio zaitafsiria Tanzania nini cha kuita maendeleo hata kama ni kwa manufaa ya nchi hiyo / hizo kuinyonya Tanzania yangu. NDIO USASA huu wa kuchaguliwa nani awe rafiki, nani wa kutuletea Demokrasia na nani aangalie kama tumefanya uchaguzi wetu kwa huru na haki na pia kutueleza kama rais wetu ni mwanademokrasia na kama anatufaa ata kama hawajawahi kufika kwetu. Duhhhh!!!!!!!!!!!!
Haya ni baadhi ya mambo yanayonifanya niuchukie U-SASA na ndio maana naitamani zamani.

NAITAMANI ZAMANI ambayo sio tu maisha yalikuwa na unafuu, lakini ambayo tulijawa IMANI baina yetu, UTU, MSHIKAMANO na hata UPENDO.
NAITAMANI ZAMANI ambayo sherehe kama Idd na Krismas zilimaanisha uchaji wa kiroho zaidi na kukua kwa mauzo ya bidhaa ziendanazo na masuala ya kidini na sio kama ilivyo sasa ambapo sikukuu hizi ni "fashion-show" na ongezeko la mauzo ni kwenye nyama choma, chips, kondom na oda za vyumba kwenye guest houses.
NAITAMANI ZAMANI ambayo familia zilijaliana na si kubaguana na kuchujana kama ilivyo sasa kwa vigezo kama kipato na muonekano wa wanafamilia.
NAITAMANI ZAMANI ambayo Baba yangu alienda kusomea ualimu kwa kuwa alikuwa na wito na sio sasa ambako wengi wanapelekwa kusomea ualimu kwa kuwa hawakufaulu vema. Zamani ambayo Mama yangu alienda kwenye uuguzi kwa kuwa ana wito na si kwa kuwa alitegemea kupata pesa nyingi ama kwa kuwa hakufanya vema shuleni. (Thanx to them. They're my Forever Heroes)
NAITAMANI ZAMANI ambayo TENDO LA NDOA lilikuwa na maana sawa na jina lake na si sasa ambako linatumika "KULAZIMISHA UHALALI WA NDOA" na kuonesha urijali na utendaji kazi wa "wapendanao" kama sio kuonesha "ustahimilizu" wa mikikimikiki baina ya wajinga katika jamii.
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijisitiri sehemu za siri tu na hilo halikuwa tatizo walipoangaliana na hawakubakana na hakuna aliyetumia hicho kama kisingizio cha kuhalalisha tabia zao za UZINZI na UASHERATI tunayosikia watu wanasema kuwa inatokana na mavazi ya kinadada.
NAITAMANI ZAMANI ambayo teknolojia ilikuwa yenye nia ya kuboresha maisha na sio sasa ambayo yazidi kuwekeza katika saratani (cancer) zijazo. Kila kitu ni mionzi na kila muonzi una athari na tunasema "tunaendelea"
ZAMANI ambayo hatukuwa na njia nyingi za kurahisisha utendaji kazi na kutembeleana lakini tulipata muda mwingi wa kuonana na kujuliana hali na sio sasa ambako kila mtu yuko "busy".
NAITAMANI ZAMANI ambayo hatukuwa na madaktari wengi kulingana na idadi ya watu na hata madawa hayakuwa utitiri kama sasa lakini ulimwengu ulikuwa na afya njema kuliko ilivyo sasa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na silaha za kutulinda na hatari na si sasa ambako silaha ni matoleo ya kila mwaka kama magari na hazileti usalama zaidi ya ongezeko la hofu.
ZAMANI ambayo tulikuwa wazi "kudumisha fikra za Mwenyekiti" na sio sasa mabko mwenyekiti na watawala wenzake wanadumisha fikra zao kwa mgongo wetu.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na "wataalamu" wachache waliojitahidi kila kukicha kujenga kilicho bora kwa nchi yetu na si sasa ambako utaalamu unaweza kupimwa kwa kuangalia ni kiasi gani umeweza kujinufaisha ndani ya muda mfupi uliokuwa kazini z9hasa serikalini). Yaani kuwa na wataalamu wengi ni kuongeza matatizo mengi
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijitahidi kuongeza maisha katika miaka tuishiyo na si sasa ambako tunahangaika kila kukicha kuongeza miaka katika maisha mafupi tuishiyo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tuliona SIASA isiyo VISA NA MIKASA na ulafi, wizi, uchoyo na ujinga wa kunyonyana uliopo sasa.
ZAMANI ambayo tulikuwa na warembo halisi weeengi japo hatukuwa na mashindano utitiri ya urembo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo ukikutana na binti mrembo ungesema umekutana na mtu na sio sasa kukutana na plastiki zilizobandikwa nyusoni mwa watu kwa gharama za juu kuwafanya wawe wanavyodhani wanaweza kuwa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na vyakula vichache vyenye uchunguzi mdogo wa kujua nini kilichomo ndani mwake lakini tukawa na lishe bora na si sasa ambapo tuna vyakula vingi vyenye maelezo mengi na afya ni mbovu kuliko maelezo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijua kuwa kuna maendeleo yetu na "wao" wana maendeleo yao na sio sasa ambako kila chao ni chema na ni maendeleo na kilicho chetu ni cha kupuuzwa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo kama ungepata ajali ungesafishwa kidonda na msamaria na si sasa ambako watakimbilia kusafisha mifuko na pochi.

Yaani naitamani zamani japo najua kuwa zamani hiyo mimi na wewe tusingeweza kuwasiliana tuwasilianavyo sasa, japo tungeweza kusakana na kuongea haya badala ya kupitishiana hapa changamotoni.
Naitamani zamani jamaniiiiiiiiiiiiiiiiiii!!!!!!!!!!!!!!!!!!
Salamu zenu toka hapa "Shamba"
Tuonane Next Ijayo

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**
NAWATAKIA SIKU NJEMA

7 comments:

  1. je unaitamani zamani ambayo blog hazikuwepo?

    Acha tamaa ndg yangu kwani ni chanzo cha matatizo

    ReplyDelete
  2. Duh!! Kamala. KARIBU, NGEGERAGE. Si unajua ninapoandika naendelea kujiuliza maswali mengi kuhakikisha naeleweka??? Mwishoni kabisa nikajiuliza "hivi Kamala anaweza akaulizaje?" Jibu likawa atauliza "unaitamani zamani ambayo hakukuwa na blog? Ungeandikaje haya?" Na ndio maana nikajibu kwenye aya ya mwisho (kujikinga na "kombora" lako") nikisema
    "Yaani naitamani zamani japo najua kuwa zamani hiyo mimi na wewe tusingeweza kuwasiliana tuwasilianavyo sasa, japo tungeweza kusakana na kuongea haya badala ya kupitishiana hapa changamotoni."
    Kumbe zamani watu hawakuwa na cellphones lakini habari zilisambaa kijijini kwa haraka na kwa ujalifu kuliko sasa. Kwa hiyo hata haya yaonekanayo sasa si kitu kama nitaweka uwiano wake na hali ya zamani.
    Si unaona sasa hivi unaaga asubuhi kwenye blog kuwa unaenda Bukoba, na usiku unatujulisha kuwa umefika. Sio siku kadhaa tena. Lakini unadhani hiyo (ya kutumia siku moja Dar mpaka Bk) imekuja na mangapi maovu katikati yake??
    Asante kwa CHANGAMOTO na kwa kuendelea kuwepo changamotoni.

    ReplyDelete
  3. Nakubaliana nawe "naitamani zamani" pia maana zamani ilikwa safi sana hata kama zamani nilikuwa mdogo lakini yale nikumbukayo nayatamani. Hasa la kujuana hali kutembeleana siku hizi hii misimu tuu hata barua siku hizi hazipostiwi tena .

    ReplyDelete
  4. Natamni zamani kwa vili nilikuwa mdogo na sikuhitaji kufanya kazi:-)

    ReplyDelete
  5. kijana wa C/moto. mimi naitamani sasa! siitamani zamani wala kesho kwa sababu sasa ndio pekee niliyonayo na niwezayo kulinga nayo. kuishi zamani ni majuto na kesho ni hofu

    ReplyDelete
  6. zamani hiyo ipi...ya kwangu labda ndio utoto...ila haya yote uliyoyaelezea (you should be proud of me that I read every single line loool!!!) they sound interesting kwa sababu sidhani kama wakati wangu mambo meeengi hayo yalikuwepo...labda yalikuwepo ila siyakumbuki...nice one tho

    ReplyDelete
  7. nautamani mustakabali ambao kamala luta atakuwa ni mbunge machachari bungeni,mubelwa anakuwa mmiliki mkubwa wa vyombo vya habari nchini, nautamani mustakabali ambao Dada subi anamiliki pharmacy kubwa tano tanzania.Nautamani mustakabali ambao tutakuwa na maprofesa wengi wanaoblog zaid ya MBELE na NZUZULIMA nautamani mustakabali ambapo dada yasinta Ngonyani atakuwa waziri wa jinsia na utamaduni, nautamani mustakabali, nautamani kweli kweli.

    ReplyDelete