Showing posts with label Zilipendwa. Show all posts
Showing posts with label Zilipendwa. Show all posts

Sunday, November 13, 2011

Za Kale vs Maisha ya sasa....BINADAMU HAWANA WEMA


Kama kuna kiumbe hatari duniani, basi ni kiumbe ambacho chaweza kuwa bora zaidi. Nacho ni BINADAMU. Ubaya na ubaya wa binadamu ni kutokana na uwezo wao wa kuonesha na kuvuta hisia na imani ya watu ambao si lazima awe ana nia aoneshayo usoni mwake mbele yao. Martin Luther aliwahi kusema kuwa binadamu anaweza kufanya ukatili ambao haudhaniki na hautendeki na kiumbe kingine chochote ulimwenguni. Anaweza kutenda kila awezacho kukuonesha anakuali ilihali anafanya juhudi mchana na usiku kukuondoa katika unyoofu wa maisha yako ikiwa ni pamoja na kukukatisha uhai wako. Sikilia kisa kiimbwacho naye Hassan Rehani Bitchuka akiwa na wana OSS katika wimbo huu Binadamu Hawana Wema



** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Sunday, September 18, 2011

Za Kale vs Maisha ya Sasa...NAJIBU TELEGRAM

Maisha yetu yanabadilika jinsi tukuavyo na tuishivyo. Yanabadilika na kubadilisha mfumo mzima wa maisha ambao unabadilisha fikra zetu kila uchao. Tulishapa kuongelea namna ambavyo DUNIA IMANI IMEKWISHA hapa, na sote tunatambua kuwa kuisha kwa imani ndiko kunakotulazimisha kuishi kwa msaada wa "fulani" ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa. Tunahitaji jicho la ziada ama kuhitaji shuhuda kwa karibu kila kitu tufanyacho. Kusaini chochote, kununua chochote na hata kusuluhisha kitu tunahitaji kuwa na shuhuda kwa kuwa imani si kama zamani na mfumo mzima wa maisha umeondoa kujiamini ama kuaminiana ndani mwetu. Ukweli ni kwamba imani kwa sasa ni tofauti na zamani.
Zamani migongano ya kifamilia ilikuwa ya kifamilia na ilisuluhishwa na wanafamilia zaidi. Heshima baina ya wanafamilia ilionekana kuwa kubwa kuliko sasa, na hata masuluhisho miongoni mwa wanafamilia nayo ilikuwa ya ndani. Sasa hivi mambo yamebadilika na sina hakika kama ni maendeleo ama la, lakini bado naamini MAMBO YA NDANI YANASTAHILI KUBAKI NDANI (japo yategemea ndani kukoje).
Ndoa zilikuwa zikisemekana kujadiliwa na kutatuliwa ndani ya nyumba / familia tofauti na sasa ambapo yaonekana "pesa" na mawakili wamechukua nafasi kubwa ya UAMINIFU WETU. Lakini tunaendelea kukumbushana kuwa japo twaishi tuishivyo, zipo zama ambazo maisha yalikuwa na MIPAKA. Na ndio maana leo tumeamua kujiburudisha, kujielimisha na kujikomboa kwa kibao hiki.
Leo katika kipengele hiki tunao DDC Mlimani Park wana Sikinde Ngoma ya Ukae ambao chini yake Cosmas Thobias Chidumule wanaeleza walivyosuluhisha "mgogoro" uliopo kati ya kaka ya Chudumule na Mke wa Kakaye huyo.Burudika ukijifunza.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, June 20, 2011

Za Kale vs Maisha ya Sasa.....SOLEMBA

Katika albamu yake ya mwaka 2005, mkongwe Burning Spear aliimba kuhusu Mapenzi katika wimbo wake FIX ME ambapo baadhi ya mashairi yanasomeka kuwa
"Love can make so Happy,
Love can make you so sad,
love can make you so lonely,
Love can make you accomplish,
Love can make you go places,
Love can make you so strong,
Love can make you your future,
love can make you REMEMBER THE GOOD TIMES AND BAD TIMES, ....."
Spear aliimba mengi katika ukweli wa maisha ya mahusiano miaka ya sasa, lakini pia yalikuwa hivyo tangua zamani na bila shaka yataendelea kuwa hivyo.
Mapenzi ni kitu kizuri saana kama kilivyo kibaya. Namaanisha uwezo wa uzuri wake ni sawa na uwezo wa ubaya wake iwapo yatakwenda visivyo ama kinyume na matarajio.
Katika kujikumbusha muziki wa kale, leo tunao wana Msondo Ngoma enzi hizo wakijulikana kama Juwata Jazz Band wakiwa naye marehemu Nico Zengekala ambao wanakuja na kibao chao SOLEMBA. Kisa mwanana juu ya binti aliyeamua kutotekeleza ahadi yake kwa mtindo / style ya kukomoa ambapo mwimbaji anasema alipomuuliza Solemba aliambiwa kuwa anajipendekeza kwake na yeye hampendi. Kama kuna kitu nilitamani, basi ni kusikia upande wa hadithi hii ukisimuliwa na Solemba mwenyewe kujua kama alichoimba Zengekala ndio hadithi kamili ama la. Labda itatokea, lakini kwa leo burudika na sehemu hii ya kisa SOLEMBA kama kisimuliwavyo naye Nico Zengekala

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, March 7, 2011

Za kale vs Maisha ya Sasa.....MASAFA MAREFU

TABORA
NAMANGA
BUKOBA
Naamini sote tunaweza kuangalia picha zetu za namna ambavyo tulikuwa tukisafiri miaka kumi na tano ama iliyopita na namna ambavyo maisha ya safari wakati ule yalivyokuwa na kutofautisha na sasa. tofauti ni kubwa.
Binafs wacha nizungumzie safari nefu ambazo nilikuwa nikisafiri. Safari nilizo na uzoefu nazo na ninazozikumbuka vema na ambazo nikilinganisha na sasa naona mabadiliko. Nakumbuka safari ya Dar-Mwanza kwa terni ilivyokuwa na namna ambavyo ilikuwa ikiandaliwa, amaa kweli. na kufika Mwanza ni kuingia kwenye meli kisha mpaka Bukoba (ambako ndiko asili yetu). Kwa siku hizo kadhaa mnazokuwa safarini, hakukuwa na mawasiliano ya karibu. Kumbuka ni kabla ya kuenea kwa simu za viganjani na sasa simu za kisasa mabazo zinaweza kukufanya uwe na mtu aliye mbali kama vile mko "beneti".
Nyakati za zamani kidogoilikuwa ni jambo la kawaida kwa mtu kusafiri kwa mwezi mzima na kwa muda wote huo anakuwa hana mawasiliano na familia yake ama na watu aliowaacha nyuma. ilikuwa kawaida na watu hawakuona kama ni mapungufu. WALIYAKUBALI MAZINGIRA.
Leo hii ni jambo la kawaida kwa mtu kujua fulani yuko wapi kwa wakati gani. Kuona hata maendeleo na mabadiliko ya safari kwa njia ya picha na video. MAISHA YA SASA YANAZIDI KUTUTENGA KWA KUTUWEKA KARIBU, na ni wakati ambao pengine ukaribu tunaopewa ama kujengewa na ndio unaosababisha umbali wa hisia na uhalisia wa maisha.
Tumeweka imani katika VIFAA na kusababisha kuamini matumizi yake kuliko nia na dhamira zetu
NIREJEE KATIKA MUZIKI...
Leo tunao wana Tancut Almasi Orchestra na kibao hiki cha MASAFA MAREFU ambacho kinazungumzia hali halisi ya zama hizo.

Nilipomaliza kutayarisha post hii nimekutana na video hii ya THE KILIMANJARO BAND almaaruf kama WANA NJENJE walipoimba wimbo huu jukwaani. ITAZAME

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, February 21, 2011

Namba moja na Mbili zangu...Si "REMIX"

Ndioooo...Enzi zetu za UZEE WA UJANA....Yaani ni "Enzi zijazo". Upo hapo????
Sina hakika kama ni sahihi kwa wimbo unaorudiwa "UPYA"na msanii kuitwa REMIX, lakini ninafurahi kuona baadhi ya wasanii wana uwezo wa kutunga huku wakiona mbali kwa kuweka MUENDELEZO wa nyimbo zao.
Ni jumatatu, ambapo mara nyingi huwa tunapata nyimbo za kale kuhusiana na maisha ya sasa. Lakini kwa siku ya leo, naomba nikushirikishe nyimbo kadhaa (ambazo zaweza kutokuwa za kale sana) lakini zenye muendelezo mwema wa "hadithi" inayoimbwa.
Na hizi si nyimbo pekee zenye muendelezo, lakini ndizo nilizoona vema kushiriki nanyi.
Tunanze na Vijana Jazz Band.
Katika wimbo wao PENZI HALIGAWANYIKI (sehemu ya kwanza) wanazungumzia RUHUSA aliyopata Mume kuoa mke wa pili, lakini anaonekana kuvunja ahadi hiyo na kuhamishia penzi lote kwa mke wa pili. SIKILIZA

Katika sehemu ya pili, wanaimba juu ya muonekano mpya alionao mke aliyeachwa kiasi cha kutamaniwa na mume wa zamani.
SIKILIZA

Kisha tuhamie kwa ROGATI HEGGA almaarufu kama KATAPILA

katika wimbo FADHILA KWA WAZAZI aliimba sehemu ya kwanza akizungumzia NIA YA KUWALEA WAZAZI.
MSIKILIZE

Lakini kwa bahati mbaya, wazazi hao wakafariki kabla hajatimiza nia hiyo. MSIKILIZE

Na mwisho tumsikilize MUUMINI MWINJUMA
ambaye akiwa na African Revolution na Double M Sound alitoa wimbo wa Mgumba sehemu ya kwanza na ya pili.
Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhusu kukosa mwana kwa mwanamama huyu, MSIKILIZE

Na sehemu ya pili ilikuwa ni matokeo ya "nani alikuwa mgumba kati ya mume na mke"
MSIKILIZE

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, December 13, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....KIFO

Wachambuzi Kaka Kaluse na Kaka Kamala wamezungumzia saana kuhusu Kifo. Wamezungumzia kuhusu majina na matukio na hata hisia zake na pia namna tunavyotakiwa kukichukulia. Mada zao juu ya hili hazikuwa rahisi kuzikubali hasa kama hukubaliani ama kuamini katika "maisha baada ya maisha". Lakini hapa sijiulizi juu ya tafsiri wala namna kijavyo, bali najiuliza kuwa endapo tungekuwa tunajua siku ya kufa kwetu, tungekuwa watu wa namna gani? Tungekuwa wema tukiamini kuwa tunamalizia siku zetu kwa wema zaidi? Tungekuwa wakatili hasa tukijua kuwa hakuna jema tunaloweza kufanya likatusaidia kuishi kuiona kesho? Tungekuwa na maandalizi mema kwa vizazi vijavyo kwa kupanga maandalizi ya kifo, msiba na gharama zote ama ingekuwaje?
Sijawahi kupata jibu la swali hili ambalo kwa namna moja ama nyingine mwimbaji Remmy Mtoro Ongala aliuliza alipokuwa "akikihoji" kifo kuhusu uwepo, uhalali na hata matendo yake kwa wanadamu. Ukimsikiliza kwa makini utasikia maandalizi anayosema anataka kuyafanya kuepusha matatizo yanayojitokeza kwa waroho wa mali za wafiwa akisema "sitakulaumu maana nitakuwa nimeacha msimamo nyuma yangu."
Swali ni kuwa tungekuwa binadamu wa namna gani leo, kama tungekuwa tukijua kuwa kifo chetu ni kesho?

Habari zilinizonifikia sasa hivi ni kuwa Dr Remmy amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Kuna mengi ya kukumbuka kuhusu Dr Remmy, lakini kubwa ni uwezi wake wa kutunga nyimbo zilizogusa maisha halisi ya mTanzania MHITAJI mpaka kufikia hatua ya kuitwa SAUTI YA WANYONGE.
Ulale mahala panapostahili Dr Remmy
** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, December 6, 2010

Za Kale vs Maisha ya sasa.......MASUDI

Kwa wazazi wengi, hatua za mwisho kabla ya kumuona ama kumpokea mwana wao anapozaliwa ni kumfikiria na pengine "kupiga picha" ya nini ama vipi mwana wao atakuwa pale atakapokua mkubwa.
Ni hizi hisia ambazo wazazi wengi (haijalishi wana asili ama wanaishi wapi) huwa wanafikia na wengine KUMUOMBEA MWANA WAO na kuweka MATUMAINI kuwa na mtoto mwema.
Si kila mzazi huiona "ndoto" hiyo ikitimia na kwa masikitiko wazazi wengi huona ulimwengu kama umewageuka na kujiona kama wana mikosi.
Haya ni mambo yaliyoanza zamaaani na yaliimbwa na wasanii miaka mingi iliyopita.
Jumatatu ya leo nakuacha na kisa hiki kilichosimuliwa naye Marijani Rajabu katika maisha halisi ya wana-wapotevu katika kibao hiki MASUDI.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

Sunday, November 21, 2010

Za Kale vs Maisha ya sasa....LAU NAFASI

Jinsi miaka inavyozidi kusonga ndivyo mabadiliko katika ubora wa muziki yanavyozidi kuwepo. Kwa nchini kwetu ni kugugumizi kuzungumzia muziki kwa ujumla kama una maendeleo ama kuna maendeleo katika muziki japo wenyewe umegota.
Miongo kadhaa iliyopita Tanzania ilikuwa ikiheshimika sana katika sanaa ya muziki na wasanii wengi wakubwa Afrika waliutambua muziki wetu. Hii ilifanya kuwe na utata kiasi juu ya nani alikuwa anaiga muziki wa nani hasa katika mapigo.
Lakini leo hii tunaambiwa kuwa muziki Tanzania umekuwa. Tunaoneshwa studio utitiri na vyombo vya kisasa, lakini wasanii wachache kuliko waimbaji ambao hawawezi kufululiza masaa mawili ya tamasha kabla sauti hazijawatoka. Sijui tunaendelea kimuziki ama muziki unaendelea kivyetu?
Basi leo tuwasikilize wana Kilwa Jazz. Moja kati ya bendi zilizofanya vema saana. Mtandao shirika wa BONGO CELEBRITY katika bandiko hili la wimbo wa ROSE WAUA, umeeleza historia fupi ya bendi hii nami nainukuu. Ilisema bendi ya Kilwa Jazz ilianzishwa "tarehe 15 Julai mwaka 1953 na kundi la wanamuziki waliokuwa wanatokea Kilwa na waliojimega kutoka Tanganyika Jazz Band.Hao waliongozwa na Ahmed Kipande na kaka yake Hassan Kipande (walihamia jijini Dar-es-salaam wakitokea Kilwa katika miaka ya 1940s,Hassani alitangulia mjini). Huyu Ahmed nasikia alijifunza mwenyewe kupiga Saxaphone. Aliinunua moja kuukuu kutoka kwa mlami mmoja aliyekuwa anafanya kazi Barclays Bank,akajifunza mwenyewe.Dah! Baadaye yeye na kaka yake wakajiunga na Tanganyika Jazz Band iliyokuwa na makao yake makuu pale New Street(siku hizi Lumumba Street).Kaka yake,Hassan,alikuwa anapiga gitaa.Hao walibakia na Kilwa Jazz mpaka ilipovunjika mwaka 1967.

Ingawa mwanzoni Kilwa Jazz ilianzishwa na watu waliokuwa na asili ya Kilwa na marafiki zao zaidi,baadaye wanamuziki kutoka pande mbalimbali walijiunga na Kilwa Jazz.Kufikia mwaka 1966 ilikuwa na wanamuziki takribani 26(15 wa bendi “A” na 11 Bendi “B”) na wanachama zaidi ya 50 wakiwemo baadhi ya viongozi enzi hizo.Usishangae,enzi hizo bendi zilikuwa na wanachama. Katikati ya miaka ya 60s Kilwa walihamia katika jengo lililokuwa linaitwa Madobi pale Kariakoo kuelekea Jangwani. Wakati huo bendi kubwa zilikuwa Western Jazz Band,Dar-es-salaam Jazz Band na wenyewe Kilwa Jazz Band."

Tukumbuke kilio cha Wana Kilwa Jazz waliokuwa wakiumia rohoni kwa kuhitaji nafasi ya kusema na fulani kidogo.
Burudika na elimika kwa kibao hiki
Lau Nafasi

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, October 25, 2010

Za Kale vs Maisha ya sasa.....MESENJA

Miaka inakwenda na siku mifumo ya maisha inabadilika. Japo si yote ibadilikayo na hata ile ibadilikayo haimaanishi kuwa lazima itabadilika kuelekea kwenye uzuri, lakini kuna mengi ya kukumbuka uangaliapo mfumo wa maisha miongo miwili tu iliyopita.
Enzi za ofisi kufungwa saa sita mchana, enzi za kuwa na msaidizi wa kuunganisha shughuli za kiofisi kama kufuata barua, enzi za kuamini kuwa kuna mwandiko wa kiume na wa kike na mengine mengi ambayo ukiyasikia sasa hayaonekani kuwa na nafasi katika jamii yetu.
Lakini kuna ambalo halijabadilika. Tatizo la baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali kuendekeza mahusiano nje ya ndoa. Na sasa teknolojia ya simu za mkononi na barua pepe vinawawezesha kuendeleza uhuni huo kwa uraisi zaidi. Hii si bahati aliyokuwa nayo Bosi aliyeimbwa na wana Magnet-Tingisha (Bima Lee Orchestra) katika kisa hiki cha Mesenja.
Sikiliza kisa hiki ambacho bado kinaendelea kuitesa jamii yetu kwa baadhi ya "mabosi" wakware kuendeleza uhuni kwa nafasi zao za kiofisi. Pengine kwa wasanii wa sasa waangalie uwezo mkubwa waliouonesha Bima Lee kwa kutumia mapigo yaliyofaa katika kuongea, kuimba na hata kujibizana.
Kazi nzuri sana isiyochuja

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

Monday, September 27, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa........FUNDISHO

Baadhi ya wasanii wa Tancut Almas. Picha toka Michuzi Blog
Kuna wakati ambao unasikia wimbo na unakuwa ukijieleza wenyewe. Wakati ambao wimbo unaweza kuhusisha maisha ya nyakati ukiimbwa na sasa. Na hilo ndilo tulilonalo leo.
Jumatatu hii tunao wanaKinyekinye kisonzo, tisa kumi mangala. Wana Tancut Almas na ni katika wimbo FUNDISHO. Yanayoimbwa humu ni mafunzo tosha kwa maisha yetu.
Burudika


** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

Monday, September 6, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....YALIYOPITA SI NDWELE

Mara ya kwanza kabisa kusikia habari za wimbo huu, ilikuwa ni kutoka kwa aliyekuwa Mwl Mkuu wa Shule ya Mazoezi Kigurunyembe Mwl Mihambo ambaye alikuja kuongea nasi wanafunzi tulipokuwa "mstarini".
Alitueleza faida za kusamehe na kisha akasema kuna urahisi wa kusamehe lakini si rahisi kusahau na ugumu wa kusahau ndio ambao husababisha ama kuleta akili na fikra za kulipiza kisasi. Kisha akauliza kama tumeshasikia wimbo mpya unaosema nimekusamehe lakini sitakusahau. Ndipo nilipopata HAMU ya kuusikia.
Na nilipousikia, sikuwahi kupoteza "pendo" na wimbo huu. Ndipo nilipounganisha sauti ya Eddie Sheggy na nyimbo zake za awali, gitaa la Hamza Kalala na kazi za awali (hao ndio nilibahatika kuwatambua kwa wakati huo) na kisha nikawa mpenzi mkubwa wa Washirika Tanzania Stars.
Lakini kuna UJUMBE wake kuwa japo hatuwezi sahau, haimaanishi kuwa tusisamehe. Nakumbuka post ya karibuni ya Kaka Matondo kuhusu Madaktari waliogombana ilhali mama mjamzito anasubiri upasuaji wao (iko hapa) na matokeo yake bandiko linasema "kutokana na kuchelewa kufanyiwa operesheni hiyo, mfuko wa uzazi wa mwanamke yule ilibidi uondolewe kabisa. Isitoshe mtoto alipata matatizo ya moyo na kuna uwezekano huenda amepata madhara ya kudumu ya ubongo kutokana na ukosefu wa hewa ya Oksijeni."
Ni nini unaloweza kufanya kwa watu waliokusababishia haya? Ni adhabu gani waweza kuwapa kutosheleza yaliyokukuta?
HAKUNA
Utakalopambana nalo ni juhudi za kuwasamehe ilhali unajua kuwa HUTASAHAU. Tunaishi na mambo kama haya kila siku na kwa namna na viwango tofauti. Iwe ni kwa watu wa nje ama wale "wandani" wetu. Na si mapya kwani yalionwa zamani.
Jikumbushe wimbo huu ulioteka mioyo ya wengi kutoka kwao Washirika Tanzania Stars Band wakisema YALIYOPITA SI NDWELE

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

Monday, August 30, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....MWISHO WA MWEZI


Na hizi ndizo tarehe.Tarehe za UNDUGU KUKUA.
Tarehe za wengine kuzikimbia nyumba zao (halisi).
Tarehe za wengine kuvalisha na kupendezesha vimada.
Tarehe za vimada na familia zao kula Chips Kuku ilhali mke wa ndoa ala na watoto wala Ugali kwa ndimu
Tarehe za kinamama wauza "pampula" (pombe za kienyeji) kuona ongezeko la mapato.
Tarehe za watu kuchelewa kurejea nyumbani.
Tarehe za nyimbo kuongezeka nyakati za usiku toka kwa walevi wanaotoka vilabuni.
Tarehe za vipigo kuongezeka ndani ya nyumba (kwa kuwa tu fulani kaulizwa amechelewa wapi).
Tarehe za wezi kujiajiri zaidi (kwani wanajua mifuko imetuna).
Tarehe za wengine kuhatarisha maisha ya wengine.
Hivi nimesema kuhusu tarehe za wengi kuambukizwa maradhi (kwa kuwa tu wamelewa na kila aliye mbele yao ni mrembo hata kama kaathirika). Ndio zileee siku ambazo Prof Jay alisema ni "mwendo wa viti virefu jirani na nyama choma na toto mbili tatu ..........hii watu wa pombe wanasema ni kupoteza mawazo ingawa mara nyingi hutokea wakati unazo"
Ni mwisho wa mwezi. Wenye mambo na vijambo. Ambao kila ufikapo basi wengi twajua iwavyo. Hapa watu wanapata "moja baridi moja moto" kisha lugha inabadilika kama alivyoimba Hayati Hemedi Maneti kuwa "Mwisho wa mwezi hata lugha hubadilika. Habari gani hugeuka kuwa HOW ARE YOU? Hakuna tabu hugeuka kuwa NO SWEAT. Samahani wanasema SORRY".
Ni "mishemishe" kila mahala, kila mtu ni "busy" kwa kwenda mbele na kwa hakika muda unaohitaji umakini kwani watu wanakuwa wanaendeshwa na pesa kuliko akili zao binafsi. Hapa UTU ndipo unapopitia "mlango wa nyuma" na wauza vitu wanabambikiza tuu. Alijiimbia Hayati Eddie Sheggy kuwa "Mwisho wa mwezi ukifika aaeee ukifika eee, abiria chunga mzigo maaama, Mwananyamala, Posta eee, Manzese, Kariakoo, Tandika, Shule ya Uhuru kaka eeee OGOPA KANYABOYA.".MWISHO WA MWEZI una mambo mengi na kama unashani yalianza sasa hivi, sikiliza Vijana Jazz Band (enzi za kina Hayati Hemedi Maneti na Eddie Sheggy) wanavyokukumbusha tangu enzi hizo jinsi mwisho wa mwezi ulivyokuwa.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

Monday, August 23, 2010

Za Kale vs Maisha ya sasa MASAFA MAREFU

Kwa mujibu wa Uncle Kitime, Tancut Almasi Orchestra, hapa wakiwa Jamhuri Stadium Dodoma. Toka kushoto.. Ray Mlangwa, Bakari Buhero, Hashim Kasanga, Mohamed Shaweji, John Kitime, Kalala Mbwebwe, Kawelee mutimwana,Abdul Mngatwa, Kibambe Ramadhan, Zacharia daniel, Akuliake 'King Maluu' Salehe. Bahati mbaya Ray, Hashim, Kalala, Zacharia wameshatangulia mbele ya haki. Kuna utata kuhusu alipo Mohamed Shaweji.
Ni Jumatatu nyingine njema. Baada ya pilika za mwisho wa wiki, tunaianza wiki mpya ya kazi. Wengi wetu tumelazimishwa na maisha kusafiri toka mahala pamoja kwenda pengine. Na katika safari hizo, si nyakati zote tumeweza kusafiri na wale tuwapendao. Na wakati mwingine tunasafiri kwa muda mrefu na umbali mrefu.
Labda sasa hivi mambo ya mawasiliano si tatizo hasa kwa kuwa hii "teknolojia" inatuweka karibu. Twaongea na kuonaa kwenye mitandao ya kisasa na hili latufanya tuwe karibu ingali tuko mbali.
Lakini bado nawaza MAAGANO waliyokuwa wakiyafanya WAPENDANO pale wanapojua kuwa hawataonana kwa muda mrefu ujao. Nawaza na kufananisha na waaganavyo wanajeshi waendao vitani ambao wanakuwa na nafasi chache ya kuwasiliana kama tufanyavyo wengi tuishio URAIANI.
Nawaza ilivyokuwa na ilivyo kwa wale waaganao pale waendapo MASAFA MAREFU.
Sikiliza kibao hiki chao wana Tancut Almasi Orchestra walipoimba kibao hiki MASAFA MAREFU. Nilibahatika kumuomba UNCLE JOHN KITIME, mwamuziki mkongwe amilikiye Blogu ya WANAMUZIKI TANZANIA! na ambaye ameshiriki katika utunzi na nyimbo nyiingi ukiwemo huu na nilipomuomba maelezo ya wimbo huu, alinieleza kwa ufupi kuwa "Nyimbo hii ilirekodiwa katika awamu ya pili ya Tancut, Naiita awamu ya pili kwa kuwa Kawele alikuwa kishajiunga japo hakupiga chochota katika kazi hii. Ulitungwa na Kasaloo Kyanga akishirikiana na pacha wake Kyanga onga japo naona walikubaliana kuwa Kasaloo ndo mtunzi. Solo, Shaban Wanted, Rythm John Kitime, Second solo Ikunji Ramadhani, Bass Amani Ngenzi,Keyboards Abdul Salvador,Trumpets Ray Mlangwa na Buhero Bakari, Saxophone,Mafumu Bilali, na Abdul Mngatwa, Drums Kejeli Mfaume, waimbaji Kasaloo Kyanga, Kyanga Songa, Hashim Kasanga, Mohamed Shaweji. Kazi hii ilirekodiwa RTD."
ASANTE UNCLE KITIME KWA UELIMISHAJI WAKO USIOKOMA.
Sikiliza, burudika na elimika kwa kibao hiki, MASAFA MAREFU

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, July 19, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa...TOP QUEEN

Ukianza kutafuta SIFA mbalimbali ambazo anaweza kuwa nazo mtu udhaniaye ndiye chaguo lako, unaweza kushangazwa na kile utakachogundua.
Lakini kawaida ya wengi huwa twasubiri mtu mwingine atuambie sifa ya yule tunayempenda. Ina maana hatuzioni na hata tukiambiwa hatuonekani kuzithamini. Na ndio maana hata mwenye mke ama mwenye mwenye busara na upendo wa dhati (hasa kwa mazingira ya nyumbani) anaweza kuamka na kuondoka na kurejea na kuelekea kulala bila hata kumwambia ama kudhihirisha BARAKA aliyonayo kuwa na mume ama mke mwenye busara na upendo.
Kama walivyoimba Vijana Jazz kwenye wimbo wao, wamesema "hapa ulimwenguni kila binadamu Mungu kamuumba kwa sifa zake". Na huu ndio ukweli wa mambo. Lakini pia kulingana na maisha yetu, na pengine mahitaji ya nyoyo zetu, tunajikuta tuna mahitaji tofauti. Na ni kwa wale wajao na suluhisho la mahitaji yetu wanaokuwa na nafasi ya kipekee kwetu. Vijana Jazz kwenye wimbo Top Queen wamemueleza Regina (ambaye ndiye aliyeimbwa kama Top Queen) kuwa uzuri wake "..tabia njema na busara zake......zimefanya wazazi waheshimu maamuzi yake".
Na hili la kuwa na maamuzi ya busara linazidi kujidhihirisha pale ambapo aliamua kuwaweka kando wale waliokuja na magari ya fahari, pesa nyingi, waliokuja na nguo za kuazima na wenye kujionesha na kuishia kuolewa na MFUGA BATA ambaye hali yake kimaisha (naamini kulingana na wale waliomtangulia "kurusha karata" imetajwa kama HOHEHAHE.
Yes!!! Ni mimi na TOP QUEEN wangu.
Na hawa wenye fikra na mitazamo hii myema wako wengi ulimwengu wa sasa. Well!!! Nami ni mmoja wa walionufaika na TOP QUEEN wangu. Busara nyingi zilizotajwa kuwemo ama kuwa nazo Top Queen aliyeimbwa na Vijana Jazz amekuwa nazo. Na hii ndiyo sababu inayonifanya niamini NYIMBO HIZI ZIKINGALI NA MAANA MPAKA LEO.
Sikiliza wimbo huu Top Queen toka kwao Vijana Jazz Band uburudike na kuelimika.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, July 5, 2010

Old School Tanzania.......Mwanzo mzuri kuenzi sanaa na wasanii wetu

Kikosi kamili cha Old Skul Tanzania
Februari 18 niliandika kuwa NATAMANI KUONA (bofya hapa kuirejea) na kama naweza kunukuu sehemu kubwa ya toleo hilo niliposema "Nikiwa mpenzi mkubwa wa muziki wa kiTanzania, NATAMANI KUONA kitu ambacho kitakuwa kikitoa mjumuisho wa muziki huo na KUENZI KAZI NA WASANII wa muziki wa Dansi nchini.
Natamani kuona SIKU YA DANSI NCHINI ambayo bendi zitajumuika kuimba nyimbo za wasanii mbalimbali waliochangia kwa kiasi kikuuubwa kuufanya muziki wa Tanzania kuheshimika. Waliotumika kuelimisha, kuburudisha na pia kukamilisha harakati mbalimbali katika jamii.
Natamani kuona tamasha litakalowaenzi nyota wengi wanaoendelea kutuelimisha kwa miaka nenda rudi na pia waliotangulia mbele ya haki...."

Na leo ikiwa ni Jumatatu ya mwisho kabla ya Jula 7, napenda kujumuika na wanaChangamoto wote kuwapongeza wanamuziki wote waliofanikisha kwa namna yoyote uwepo wa onesho hili kubwa la muziki wa dansi liwakutanishalo wasanii wengi wakongwe waliojiita Old School Tanzania mablao lategemewa kufanyika ukumbi wa Karimjee.
Japi sitaweza kuhudhuria, bado nashukuru kuwa KILE AMBACHO NILIKIONA KAMA TAMAA NA AMBACHO NDUGU ZANGU WATOA MAONI WALINIFARIJI KUWA NAWEZA KUONA KIKITOKEA, leo kinamaliziwa.
Shukrani saana kwa washiriki woote waliofanikisha hili na siku ya leo ya Jumatatu ambayo mara nyingi huwa twaweka miziki ya kale, tunajiunga na wapenda burudani woote kupongeza juhudi hizi.
Kwanza pata ufafanuzi wake Waziri Ally kuhusu Old Skul Tanzania.

Na kisha kutazama na kusikiliza mazoezi ya kundi hili hapa chini

PICHA NA VIDEO KWA HISANI YA Michuzi Blog
** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

Monday, May 31, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa......USIA KWA WATOTO & TUPATUPA

Baadhi ya wasanii wa Juwata Jazz Band. Watatu waliosimama toka kushoto (kwao) ni Joseph Maina, Tx Moshi William na Athuman Momba ambao wote sasa ni marehemu. Lakini ujumbe wao utadumu milele
Sina hakina ni wangapi walibahatika kupata nafasi ya kuusiwa na wazazi wao kuhusu mabadiliko ya maisha kulingana na nyakati mbili (ujana wa wazazi na wetu sisi). Ni ukweli kuwa kuna mabadiliko meengi ya kimaisha kuanzia thamani ya pesa mpaka, matumizi yake, umuhimu wa kuweka akiba na mengine mengi.
Pengine huwa tunausiwa lakini si kwa kuongea kama BABA/ MAMA NA MWANA, bali mara nyingi ni wakati wa kugombezwa na kufokewa.
Lakini pia si wengi ambao katika hali ya kirafiki wanaweza kueleza matatizo wanayopitia kwa kuwa walishindwa kuwa na umiliki mzuri wa pesa zao. Ni CHANGAMOTO YETU sote kuweka malengo mema na kuelekeza mabadiliko ya maisha kwa wale watutegemeao.
Leo hii tunao JUWATA JAZZ BAND (ambao sasa wanafahamika kama Msondo Ngoma Music Band) ambao wanakuja na nyimbo zao mbili kuhusu umuhimu wa kupanga vema matumizi. Wa kwanza ni Usia kwa watoto na wa pili ni Tupatupa ambao ni juu ya kijana anayejutia matumizi yake mabaya ya pesa.
Katika USIA KWA WATOTO, twasikia nafasi ya BABA anayewakusanya watoto na kuwaeleza maisha yalivyokuwa huko alikotoka na kuwafananishia na namna yalivyo hivi sasa. Si jambo lionekanalo kufanyika zaidi kwa jamii yetu hivi sasa, lakini ni lazima VIJANA watambue maisha yalivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ili kuweza kutambua fika kama wanaendelea kwa kuwa na mambo mapya ama wanaendeleza yale yaliyowahi tokea.
Lakini pia katika TUPATUPA tunamsikia kijana ambaye maisha yalimnyookea na sasa yamemgeuka na anatumia nafasi hiyo kutoa USHUHUDA wa namna ambavyo maisha yanaweza kubadilika na kukufanya uwe na maisha ambayo hukuwahi kuyawaza ulipokuwa na pesa.
ANAISHI KUWAONYA WALIMWENGU KUWA "mkifuata anasa mtapoea kaka mimi"
Sikiliza, burudika na jifunze.

Kisha TUPATUPA

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Monday, May 3, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa.......SOPHIA

Moja ya "jumuiko" la bendi ya Marquis (sina hakika ni wangapi walioshiriki katika muziki huu) lakini kwa mujibu wa Blogu ya WANAMUZIKI TANZANIA, "mwenye nyeusi tupu akiwa na gitaa ni Dekula Kahanga Vumbi, wa pili toka kushoto na suruali nyeusi ni Issa Nundu" Picha@ Wanamuziki Tanzania Blog
Ni wiki iliyopita niliposhiriki mjadala kuhusu KUONGEZEKA KWA TALAKA NCHINI KENYA NA KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (dodosa hapa) na katika mjadala huo kuna mengi yalijadiliwa. Na licha ya kuonekana kuwepo kwa sababu nyingi, kilichokuja kuonekana kuwa sababu ya tatizo hilo ni MFUMO MZIMA WA MALEZI.
Na tatizo la talaka kwa nchi zetu za Afrika lazidi kuongezeka kila uchao kwa kuwa wale wanaooa na kuolewa hivi sasa, ni wale ambao HAWAKUANDALIWA kutafuta watu walio makini na sahihi katika mahusiano na pia hawapati msaada wa kukabiliana na misukosuko ya kimahusiano.
Tatizo kuu tulilonalo kwenye suala zima la ndoa ni
1: Hatuelimishw kuhusu changamoto za ndoa, ama
2: Tunaelimishwa kidooogo sana kuhusu changamoto za ndoa, ama / au
3: Tunaelimishwa visivyo kuhusu suala zima la ndoa
Lakini kuna wale wanaopata mafunzo ya ndoa, ila kama nilivyosema, mafunzo haya (ambayo siku hizi ni kwa kina mama zaidi) mara nyingi hutolewa na watu ambao wameachika. Jaribu kufikiri mafunzo kuhusu ndoa toka kwa mtu ambaye ndoa imemshinda.
Lakini hivi sivyo ilivyokuwa miongo kadhaa iliyopita. Licha ya ile tabia ya wazazi kuwachagulia watoto wao mwanamke ama mwanaume wa kuoana naye (tabia ambayo sijawahi kuiunga mkono), lakini pia wazazi walikuwa wakiwafunza watoto ama kuwaasa wale wakaribiao kuingia maisha ya kinyumba kuhusu dunia na suala zima la ndoa. Na hili lilikuwa msaada kwa ndoa nyingi kwani kukumbana na magumu hakukumfanya mhusika kujiona aliye ama mkosi ama mwenye matatizo kuliko wengine.
Na kama tujuavyo, kilichotokea kwenye JAMII zetu, kilielezwa ama kuoneshwa ama kutunziwa kumbukumbu na wanamuziki wetu. Hakukuwa na tofauti katika hili la USIA WA NDOA NA MAISHA KWA UJUMLA.
Sikia wasanii katika wimbo ufuatao wakiasa kuwa hata ukiwa na cheo YAKUPASA KUHESHIMU maoni ya wazazi wako kwani kwa kuwabishia kuna uwezekano wa mambo kutokukuendea vema. Na hapa simaanishi LAANA, bali kwa kuwa wazazi wanaokupenda watakueleza kila wajualo kuhusu maisha, na kwa wewe kutotenga muda wa kuwasikiliza, kuna uwezekano wa kukosa yale ambayo unaweza kuyaepuka kutokana na makosa ama ujasiri wao.
Ni katika kuoanisha nyimbo hizi na maisha haya ya sasa na hasa suala hili la Maisha, Ndoa na Talaka, tunakutana na Marquiz du Zaire wana Zembwela katika wimbo SOPHIA. Kwa mujibu wa Uncle Dekula "Vumbi" Kahanga (msome hapa) (niliyemuomba orodha ya walioshiriki katika wimbo huu) "wimbo wa Sophia ulitungwa na Nguza Viking na yeye ndiye alipiga Gitaa la Solo,waimbaji walikua,Kasaloo Kyanga,Mutombo Audax,trombone ilipulizwa na Berry Kankonde,tarumbeta zilipulizwa na Kaumba na Bizos,Sax ni King Maluu"
Burudika ukielimika.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA