Monday, August 30, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....MWISHO WA MWEZI


Na hizi ndizo tarehe.Tarehe za UNDUGU KUKUA.
Tarehe za wengine kuzikimbia nyumba zao (halisi).
Tarehe za wengine kuvalisha na kupendezesha vimada.
Tarehe za vimada na familia zao kula Chips Kuku ilhali mke wa ndoa ala na watoto wala Ugali kwa ndimu
Tarehe za kinamama wauza "pampula" (pombe za kienyeji) kuona ongezeko la mapato.
Tarehe za watu kuchelewa kurejea nyumbani.
Tarehe za nyimbo kuongezeka nyakati za usiku toka kwa walevi wanaotoka vilabuni.
Tarehe za vipigo kuongezeka ndani ya nyumba (kwa kuwa tu fulani kaulizwa amechelewa wapi).
Tarehe za wezi kujiajiri zaidi (kwani wanajua mifuko imetuna).
Tarehe za wengine kuhatarisha maisha ya wengine.
Hivi nimesema kuhusu tarehe za wengi kuambukizwa maradhi (kwa kuwa tu wamelewa na kila aliye mbele yao ni mrembo hata kama kaathirika). Ndio zileee siku ambazo Prof Jay alisema ni "mwendo wa viti virefu jirani na nyama choma na toto mbili tatu ..........hii watu wa pombe wanasema ni kupoteza mawazo ingawa mara nyingi hutokea wakati unazo"
Ni mwisho wa mwezi. Wenye mambo na vijambo. Ambao kila ufikapo basi wengi twajua iwavyo. Hapa watu wanapata "moja baridi moja moto" kisha lugha inabadilika kama alivyoimba Hayati Hemedi Maneti kuwa "Mwisho wa mwezi hata lugha hubadilika. Habari gani hugeuka kuwa HOW ARE YOU? Hakuna tabu hugeuka kuwa NO SWEAT. Samahani wanasema SORRY".
Ni "mishemishe" kila mahala, kila mtu ni "busy" kwa kwenda mbele na kwa hakika muda unaohitaji umakini kwani watu wanakuwa wanaendeshwa na pesa kuliko akili zao binafsi. Hapa UTU ndipo unapopitia "mlango wa nyuma" na wauza vitu wanabambikiza tuu. Alijiimbia Hayati Eddie Sheggy kuwa "Mwisho wa mwezi ukifika aaeee ukifika eee, abiria chunga mzigo maaama, Mwananyamala, Posta eee, Manzese, Kariakoo, Tandika, Shule ya Uhuru kaka eeee OGOPA KANYABOYA.".MWISHO WA MWEZI una mambo mengi na kama unashani yalianza sasa hivi, sikiliza Vijana Jazz Band (enzi za kina Hayati Hemedi Maneti na Eddie Sheggy) wanavyokukumbusha tangu enzi hizo jinsi mwisho wa mwezi ulivyokuwa.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia siku za Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

1 comment:

emu-three said...

Yah, za kale zahabu, za kale hazikinahishi. Na zakale zitakunaya hata kama mwisho wa mwezi utatoka kapa kwa kukopa sana, lakini ukiusikia wimbo wa kale unajifannya upo `kipindi kile' ambacho senti tano uliweza kununua maandani matano....!