Showing posts with label Chemsha Bongo. Show all posts
Showing posts with label Chemsha Bongo. Show all posts

Sunday, November 10, 2013

UBUNIFU WA VIPINDI radioni.

Kwa hapa Marekani, napenda kusikiliza kituo hiki cha Radio ya kiJamii ama National Public Radio (NPR) ambayo vipindi vyake ni elimishi sana.
NPR hawajihusishi na masuala ya BURUDANI bali ni vipindi vya habari na makala.
Lakini...
NDANI YA MAKALA HIZO HUWA WANA VIPENGELE VYA KUBURUDISHA NA VILIVYOANDALIWA VEMA SANA
Kimoja wapo ni hiki cha CHEMSHA BONGO ambacho husikika kwenye kipindi cha WEEKEND EDITION SUNDAY
Sikiliza cha wiki hii. Fikiria UBUNIFU WA MTAALAMU HUYU WA CHEMSHA BONGO Will Shortz 
 Lakini pia fikiria UELIMISHAJI ULIOMO KATIKA HILI

Monday, December 26, 2011

CHEMSHA AKILI......!

Nguo inauzwa sh. 10,000 we huna pesa, ukaamua kukopa kwa dada yako sh.5000 na kwa kaka sh.5000 ukapata sh.10,000. Uloenda kununua hiyo nguo ukaomba upunguziwe ukauziwa kwa 9700/= ukarudishiwa sh.300. Ukaamua kupunguza deni ukatoa sh.100 kwa kaka na sh.100 kwa dada. Ukabakiwa na sh.100. Hivyo ikawa una deni kwa kaka sh.4900 na dada sh.4900. Ukijumlisha ya kaka 4900 na dada 4900 unapata 9800 ukiongeza na ile sh.100 uliyobaki nayo inakuwa 9900. Je? sh.100 imekwenda wapi?

Nova Kambota
www.novakambota.com

Wednesday, May 18, 2011

Chemsha bongo...Mjini ni wapi?

Juzi kwenye ukurasa wa Facebook wa mdogo wangu nilikutana na maelezo yasemayo "While individuals embrace each other in rural, they stay apart in Urban."
Kisha nikawaza kuwa MJINI NI WAPI? Nikaweka majibu kuwa "Hivi Mjini ni wapi? Nikiwa Nyakibale niliona Omuluhamila kama mjini. Kufika pale nikaona Kaagya kama mjini, Na Kaagya wanaona Kashozi kama mjini na wa Kashozi wanaona Bukoba Mjini ndio kumekucha. Aliye Bikoba mjini anaamini Mwanza ndio kwen...yewe (tena anywhere in Mwanza) na aliye Mwanza anaamini Arusha ama Dar ama etc ndio haswaaaaa. Aliye Dar Kibondemaji anaamini Kariako ndio mjini na wa Kariakoo anaangalia Masaki. Wa Masaki anatazama Nairobi na nje ya nchi hata Marekani na hata hapa Marekani kuna aliye DC ama Los Angeles na bado anautafuta mji. KWANI MJINI NI WAPI? Labda hata ndani a nyumba yenu kuna mjini ambapo ni Master bedroom na aliye humo naye anaamini choo cha humo ndimo mjini mwake. KWA MAANA NYINGINE, LABDA MJI NA KIJIJI NI FIKRA TU. Kwa kuwa anayekula raha sana duniani na kuamini ana kila kitu, anaambiw na kuwa KUNA MBINGUNI KULIKO NA MANONO KULIKO ANAYOPATA. Labda huko ndio MJINI. Lakini tukifia huko hatutaambiwa kuna "mji mwingine?" NAWAZA KWA SAUTI TUUUUUUU..."
Na bado nawaza..........MJINI NI WAPI?

Saturday, April 23, 2011

Labda UTUPU kwetu watokana na U-TUPU wa fikra zetu.

Ni majuzi tu wakati napitia kibaraza cha Mzee wa Duh!!! Simon Kitururu nikakutana na "topiki" kwamba "....May be hakuna mtu Open Mided aisee (irejee hapa)" nami nikawaza kwanini awaze hayo? Kisha nikawaza labda kila anayeweza kujua kuwa kuna uwezekano wa kuwepo na kutokuwepo OPEN MINDS, huyo atakuwa na OPEN MIND japo anaweza kuitumia kuwaza kwamba HAKUNA ALIYE OPEN MINDED.Hiyo ikawa CHANGAMOTO kuwaza upya juu ya kile kilichopo nyuma ya pazia kwa mtu awazapo.
Ni kweli kwamba kuna kitu kibaya na kizuri ama ni mtazamo wa mtu juu ya ubaya na uzuri huo? Nimewaza jinsi watu walivyomuamini Mch ambaye alikuwa mlawiti wakati huo akiwa mtendaji wa hayo mabaya, halafu wakaja kumtenga baada ya kuwa ametubu na kuacha tabia hiyo.
Kwani hapa mtu huyu anatengwa kwa yale atendayo, ama yale yajulikanayo juu ya matendo yake? LABDA wasingejua wangeendelea kumuona kama MTAKATIFU, na sasa wamejua, na yeye kaumbuka na katubu na AMEKUWA MPYA tena, wao ndio wanamtenga.TUACHANE NAYE..............
Ukiitazama hii picha hapa chini unaona nini? Kwani ingekuwa ndani ya uwezo wako ungenunua? Na pengine unadhani ni USANII AMBAO UNGEWEZA KUU-SUPPORT?
Ukimaliza kujibu, angalia "making" yake HAPA iliyochukua masaa 24. Na baada ya kuona uhalisia wa kilichomo, unasemaje?
Kwani kuna kilichobadilika? Ahaaaaa...Yawezekana. na kama ndivyo, ni kwa kuwa fikra zako zimewekwa wazi, zimefunuliwa, zimeanuliwa, ZIMEWEKWA TUPU. Na kwa uTUPU huo umeweza kuona ambacho hukuona na sasa umekuwa na mawazo mengine.
Labda ni kweli kwamba UTUPU MAWAZONI KWETU UNATOKANA NA U-TUPU WA FIKRA ZETU.
Nawaza kwa sauti tuuu!!!!!

Saturday, March 5, 2011

Weka maelezo yako.....

Maelezo ya Kaka Francis Godwin wa blogu ya MATUKIO DAIMA (mwenye hakimiliki ya picha hii) yanaeleza HAPA kuwa "Wazee wa wilaya ya Ludewa wakiwa katika maombi ya kumwombea mbunge wao na kuombea chakula kilichoandaliwa na mbunge huyo baada ya kumalizika kwa kikao cha kupokea mawazo ya wananchi juu ya vipaumbele vya jimbo hilo bungeni"
AMA KWELI PICHA MOJA YAELEZA MENGI. Kwa mimi ambaye ndio kwaanza nimemaliza darasa la Photography Appreciation, naona mengi "ya kuvutia"

Wewe waona nini na waonaje?

Wednesday, February 23, 2011

Kizazi...Nini kipimo chake? Wakati, Mazingira ama Nyenzo?

Photo Credits: Jack Graham Blog
Labda wapo wanaoshangaa kuwa mtu na mzazi wake wanahesabika kuwa watu wa vizazi tofauti licha ya kwamba wote wako hai.
Wengine wanakubali kuwa wao na wazazi na wazazi wa wazazi wao ni vizazi tofauti licha ya kwamba wote wako hai.
Lakini wapo ambao pengine bila kufikiria wanaamini kuwa kila UZAO ni KIZAZI.
Na pia wapo ambao wanaamini kuwa yachukua miaka mingi kutoweka kwa kizazi kimoja kwenda kingine.
Kwani kila siku si tunasikia muziki huu wa "bongo flava" ukiitwa muziki wa kizazi kipya? Hata kama anayeuimba amevutiwa na muziki miaka michache iliyopita baada ya kumsikiliza "mkongwe" ambaye (kwa tafsiri "yao") si mtu wa kizazi chao?
Hujasikia wasanii wakirudia nyimbo za miaka kadhaa iliyopita na kusema wamezirudia katika MUZIKI WA KIZAZI kipya katika harakati za kutenga kizazi cha "remix" na MUZIKI HALISI?
ACHANA NA HAYA....
Juzi tukiwa shuleni katika kujadili KIJANA NA TEKNOLOJIA, binti mmoja akasimama na kuchangia akisema "maisha yangu yote sasa ni elektroniki. Ndio kalenda, kumbukumbu, miadi, barua, simu, sauti nk. Vyote nafanya kwenye simu yangu ya Iphone." Hapo mie nikawa natikisa kichwa kukubaliana naye. Kisha akasema KWA KIZAZI CHA SASA HUWEZI KUISHI BILA NYENZO KAMA IPHONE.
Hapoooooooooooooooo sasa....Sikusubiri "kunyoosha mkono"
Nikamuuliza kuwa anaamini kuwa kila pembe na mtu / kijana wa rika yake anaijua Iphone achilia mbali simu hata ya kukoroga?
Nikamuuliza anaposema KIZAZI CHA SASA anamaanisha katika nyumba, kijiji, mkoa ama jimbo analoishi ama anamaanisha ULIMWENGU MZIMA?Ni kweli kuwa binti huyu wa miaka 18 wa hapa Maryland yupo kwenye kizazi tofauti na binti ya jirani yetu mwenye miaka 18 pale Bushasha? Kama wana umri sawa, si wako kizazi kimoja? Lakini kama hawatumii nyenzo moja kutokana na mazingira, ina maana mazingira ni kigezo? Na je, ni kweli kuwa "Uncle" nanilii anayetumia kompyuta saana pale Bongo atakuwa katika kizazi sawa na haka kabinti ka hapa kwa kuwa nyenzo zainawaweka kwenye "usawa" wa matumizi?
Ndipo nilipopata wazo la kuja kuuliza hapa kwamba KIZAZI....KIPIMO CHAKE NI NINI? NI WAKATI, MAZINGIRA, AMA NYENZO?Labda nikuonyeshe tu kuwa.....................Hawa hapa chini
Photo Credits: Broadcasting Corporation of China
Ni wanafunzi wa elimu ya awali kama ilivyo kwa hawa hapa chini.
JE!! Japo wanaweza kuwa na umri unaolingana ama kukaribiana, unaamini wako katika KIZAZI KIMOJA?Kwani kizazi ni nini?
Innocent Galinoma aliuliza "what is life? Is life a gift, or a test, or a punishment for my people?"
MSIKILIZE

JUST THINKING OUT LOUD.

Tuesday, February 8, 2011

Familia huishia wapi?


Tumezaliwa watano. Nina dada wakubwa waili na Kaka wadogo wawili. Yamaanisha ni mimi niliye kati. Na sina shaka kuwa wengi tutakubali kuwa hii ni familia. Na kama ambavyo nilishasema, nafurahia saana uhusiano tulio nao baina yetu. Lakini pia kuna Baba na Mama. Nao naamini tutawahesabu kama familia. Nao kila mmoja ana ndugu zake waliozaliwa pamoja. Hao kwao ni familia. Ni kwa mamtiki hiyo nahisi kuwa nao ni familia yetu maana ni familia ya sehemu ya familia yetu. Sasa mjomba na Shangazi wote si wana familia katika miji yao? Na hao ni familia za wazazi wetu na sisi na wazazi ni familia. Ina maana nisiwaite familia?
Najiuliza kama sisi sote si familia kwa mwendo huu na kama sivyo, basi basi naendelea kujiuliza kuwa hivi familia huishia wapi? Ama niseme mtu ni ndugu yako mpaka uzazi upi?

Wednesday, January 26, 2011

Kipi chazeeka kwanza? Miili ama akili?

Nikiwa kazini na "rafiki" yangu (ambaye ana umri mkubwa), tulikuwa tukiongelea jinsi watu wanavyoukimbia muonekano wa umri wao. Na yeye alionekana kutetea hilo na kusema kuwa awali alikuwa akionekana ana mvi nyingi kichwani na alijihisi MZEE. Lakini baadae akapata dawa ya kubadili rangi ya nywele zake na hilo likamrejesha katika "ujana" aliokuwa akiutaka. Na baada ya kuonekana kuwa kijana zaidi, akaanza kujihisi kuwa na hata nguvu na uwezo wa kufanya mazoezi. Sasa hivi anakimbia dk 30 za mapumziko ya mchana kazini na amebadili mfumo wake wa chakula, amebadili mfumo wa maisha na kwa hakika sasa anaishi "maisha ya afya" zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hakuna anayebisha kuwa KUJIONA KIJANA kumemsaidia kubadili mfumo mzima wa maisha. Lakini kwangu maswali yakabaki kuwa
1: alizeeka mwili ama akili?
2: Ni kweli kuwa kabla hajajiona kuwa kijana zaidi mwili wake usingeweza kutenda mazoezi afanyayo sasa?
3: Na je! kama angekuwa amezeeka mwili, angeweza kutenda atendayo hata kama angekuwa anapenda kufanya hayo?
Ninawaona wengi ambao kwa kujiona "wamezeeka" hawajiendelezi na shule, hawawekezi maishani na hata hawafanyi mengi mema ambayo yangewasaidia miaka michache ijayo. Wanaokimbia vivuli vyao kwa kujifanyia upasuaji kutafuta muonekano wa ujana, kutumia makemikali "kijijananisha" na hata kuvaa ki-ujanaujana wakiamini hilo litawapa HISIA nzuri za namna walivyo. Pengine inawasaidia kwani wapo ambao wakishakuwa katika "ujana" wautakao huanza kutenda yale ambayo ni ya manufaa kwa maisha yao na zaidi kwa wale wategemezi wao lakini ambayo wangekuwa wamefanya ama walistahili kuyafanya kabla "hawajajibadilisha."
Hivi sasa Baba huyu anaendelea na mazoezi na imekuwa kama desturi. Anaonekana mjana kuliko alivyokuwa takriban mwaka na robo uliopita. Na ndipo ninapoendelea kuwa na kuwaza kuwa alizeeka akili ama mwili? Na kama ni akili, mwili wazeeka vipi? Kama ni mwili, kwanini aonekane kijana sasa kuliko nilipoandika mara ya kwanza?
Haya na mengine mengi hunifanya nijiulize tena na tena.
KIPI CHAZEEKA KWANZA? MIILI AMA AKILI?

KUMBUSHO: Haya ni marejeo ya August 11, 2009. Ni kwa kuwa swali likingaliapo.

Friday, January 14, 2011

Tafakari ya leo

Labda UNYOOFU si suluhisho la kutufikisha kila tunakotaka kwenda, japo twatumia unyoofu kama kielelezo cha kuelekea mafanikioni.Labda waTanzania tu-wanyoofu saana ilhali Tanzania yetu imeshapinda. Ndio maana ni kama twaendesha ki-ajali ajali
Labda Rais Kikwete yu-mnyoofu ilhali serikali na Tanzania yake imepinda. Ina maana hatatufikisha
Labda twajitahidi kuwaza ki-nyoofu ilhali suluhisho la mawazo hayo tayari limepinda. Ndio maana matokeo ni kutofika tutakako
LABDA HATUWAZI KULINGANA NA MAZINGIRA NA LABDA ILI TUSONGE MBELE, TWAHITAJI DEREVA ANAYEONA BARABARA IMEPINDA NAYE AKAPINDA KULINGANA NA BARABARA HIYO ILI TUFIKE TUENDAPO.

NAWAZA KWA SAUTI TU

Thursday, September 30, 2010

Majina haya ya wa-Haya....na haya majina kwa wa-Haya

Ni zaidi ya majina haya na wa-Haya
Nyumba ya asili ya waHaya
Photo credit: Zenjidar.co.uk
Sina hakika kama naweza kukueleza kwa ufasaha kwanini tuna majina. Lakini bado nayaona kama kiunganishi cha sisi tuliokuwa, sisi tuliopo na sisi tujao. Novemba 24, 2008 niliuliza Ni kweli majina yetu huathiri mustakabali wa maisha yetu? (bofya hapa ) na bado naendelea kuliwaza hilo. Lakini pia najua kuwa baadhi ya majina yetu huathiriwa ama kutokana na baadhi ya matukio ama kuonesha ama kutabiri kitu kutuhusu.
Nawajua ndugu zangu ambao majina yao huendana na msimu waliozaliwa. Wapo ambao majina hutokana na kitu ama tukio kubwa la siku waliyozaliwa (mfano rafiki yangu Sisiemu ambaye alizaliwa siku ya kuanzishwa kwa chama cha Mapinduzi ama VALENTINE aliyezaliwa Februari 14).
Nimepata kujiuliza haya baada ya kumaliza kuandika kazi ya shule ambayo ni RIPOTI ya habari, na aliyetakiwa kuisoma akaniomba kuandika "Ban-dee-oh" kumuwezesha kusoma. Kisha akasema jina langu ni gumu na ningehitaji "nick name". Nikamshangaa kwa kuwa yeye ana jina ambalo KWETU lingeitwa ambavyo asingeelewa. Jina lake ni FREDRICK ambalo utalisoma huko mbele tunavyolitamka "kwetu".
Lakini nikaishia kuwaza kwanini majina yanakuwa "MAGUMU" kwa wengine? Kwanini imuwie vigumu kusema Mubelwa lakini aseme Schwarzenegger
Ni kwanini aliye nyumbani ataweza kusema Nzunzulima ama Lutatinisibwa ama Ng'wanambiti ama Kitururu na hata Ngonyani na ashindwe kusema majina mengine?
Nikawaza majina ya kwetu, kama yangu na mengine kama ya Kakangu Lutatinisibwa, Lutabasibwa, Mkagendage, Kokuijuka, Mutalemwa na mengine mengi yawashindayo watu. Lakini nikageukia upande wa pili kuangalia majina ya "wazungu" yawashindayo wa-Haya wenzangu (hasa wakongwe).
Basi ukienda kwetu ukasikia baadhi ya majina, waweza dhani ni mapya ama ya kilugha kumbe sivyo.
FREDERICK.... Wewe waitamka hivyo wakati kwetu ni FIDILISHI
SYLVANUS uijuayo wewe, kwetu yaitwa SILIBWANDI.
SYLYVESTER unayoifahamu, kwetu ni SILIBWELI.
JUDITH kama ya "Komando" kwetu ni YUDESI.
Yapo mengi ya kuwaza na kuwazua kuhusu uitwaji wa majina
JE! Ni utashi wa waliotangulia ili kukufanya wewe uchukie majina ya wengine? YAWEZEKANA.
Kwani kuna lipi gumu la kumfanya mzungu ahangaike na Mubelwa na aweze Schwarzenegger?
Kuna ugumu gani katika Frederick kwa mhaya kuacha kujaribu kuliita sawa akaliita Fidilishi?
Labda ni yaleyale niliyofunzwa mwanzoni mwa miaka ya '90 nilipokuwa mikoa ya kusini kuhusu ndugu zetu wa ukanda wa Msumbiji ambao walijichora nyuso zao kuharibu thamani yao kwa WAKOLONI (ama madalali wao), NA INASEMEKANA ILIFANYA KAZI.
Labda na ndugu zangu hawakupenda watu wengi wachukue majina ya ki-magharibi wakaamua "kuyaharibu" na kama ndivyo basi walifanikiwa kwani naamini waHaya ni kati ya makabila machache yenye watu walio na majina yao ya asili.

Labda pia ni kampeni ya watu wa Magharibi kuhakikisha majina yetu hayaingii kwao.
Labda majina hayo ya ki-magharibi hayawapendezi wa-Haya..... na labda majina haya ya wa-Haya hayasomeki kizungu, lakini naamini NI ZAIDI YA MAJINA HAYA NA WA-HAYA.
Kwani kwenu kunalipi la hivi?
NAWAZA KWA SAUTI TUUU

Thursday, August 12, 2010

Ni mimi, sisi, wao ama mazingira?

Haya sasa. Nyakati zaenda na pengine wapo ambao kama mimi wanaendelea kukubaliana na ile dhana ya ZA KALE NI DHAHABU.
Lakini bado nawaza kama ni kweli kuwa vingi ya vya kale ni bora kuliko vya sasa.
Na hili laweza kupingwa kwa kuangalia tafsiri ya UBORA wa kitu ama vitu.
Binafsi nimekuwa nikiamini kuwa utendaji wa kazi wa kizamani ulikuwa ukihusisha akili za kibinadamu zaidi ya ilivyo sasa ambapo karibu kila kitu ni automated.
Nirejee kwenye MUZIKI. Nimekuwa mpenzi mkubwa wa Marehemu "TX" MOSHI WILLIAM na kitu kikubwa kilichokuwa kikinifanya kupenda tungo zake ni namna alivyoleta uhalisia wa maisha katika tungo hata zilizokuwa zilizokuwa zina mafumbo.
Ninapozungumzia muziki wa zamani kugusa maisha simaanishi kuwa muziki wa sasa hauna ujumbe na kugusa maisha ya sasa.
Lakini naendelea kujiuliza kama Ni mimi, sisi kama mashabiki ama mazingira ya maisha ya sasa? Nakumbuka kati ya nyimbo zilizokuwa zikinipa taswira ya kinachoimbwa ni huu wa Tuma (japo hii ni remix)

Lakini kuna TUNDA SPECIAL yao

Na hata MASIMANGO yao TOT-Plus

Nihamie kwenye MICHEZO YA KUIGIZA. Michezo hii ilikuwepo tangu awali na labda tofauti ni kuwa "enzi" hizo tulikubali kuwa hii ilikuwa michezo ya kuigiza, tuliikubali na kuendelea kuiboresha kwa namna hiyo. Ninaloona sasa ni MAIGIZO YA MAIGIZO na "kurushwa daraja" na kuitwa MUVI.
Hayati Mzee Pwagu ambaye maishani mwake alikuwa zaidi ya muigizaji. Waliokuwa waelimishaji wakubwa waliofanya kazi kwa ufanisi na kuleta taswira halisi ya wazungumzacho licha ya kuwa walikuwa wakisikika tu redioni na si kuonekana. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
Photo credit:
Bongocelebrity.com
Ninalowaza ni kama kweli kuwa vya kale vilikuwa na ubora ama ni mtazamo wangu ama ni mtazamo wetu sisi wasikilizaji wa sasa?
Ama ni mazingira ya maisha ya sasa ambayo yanatufanya kuthamini kile kilichopita? Labda sikiliza maigizo ya enzi hizo

Tuesday, April 20, 2010

Chemsha Bongo na RUSHWA ya Tanzania

Kila ninaposikia "mheshimiwa mtarajiwa" anaeleza namna atakavyopambana na RUSHWA nchini Tanzania, nasikia wakipanga kuendesha vita wakiingia madarakani.
Na kwa walio wengi nchini Tanzania, "hawamtupi" mtu awapae rushwa kupata nafasi ya uongozi.
Sasa kama kupinga rushwa ni mpaka wawe kwenye madaraka na kama bila kutoa rushwa hawawezi kuwa kwenye madaraka, ina maana bila rushwa hawataweza kupinga rushwa.
Ina maana watatakiwa watoe rushwa ili waweze kupata nafasi za kupiga vita rushwa (ambayo inawaweka kwenye nafasi nzuri ya kupokea rushwa nono zaidi)
Swali ni kuwa, WATAPINGAJE RUSHWA IKIWA NI LAZIMA WAITUMIE KUFIKA NAFASI ZA KUIPINGA?

Wednesday, April 14, 2010

Vigezo vya Utoto, Ujana na Uzee ni vipi?

Siku chache zilizopita nilikuwa nikiwasiliana na rafiki yangu mmoja ambaye tumekuwa tukiwasiliana kwa muda kupitia blog na facebook. Mawasiliano ya sasa yalikuja siku chache baada ya kuwa nimebadili picha yangu ya ukaribisho kwenye blog na ukurasa wa mbele wa Facebook na hilo lilimfanya aingie kwenye ukurasa wangu wa taswira na kuanza kuzipitia.
Rafiki huyu ambaye amekuwa akisoma maandishi yangu ya hapa kwa muda mrefu, aliniomba radhi kisha akaniuliza "hivi kaka una umri gani (kama hutojali mimi kukuuliza) na nilipomtajia akashangaa na kucheka. Kisha akasema kwa muda woote aliokuwa akisoma maandishi yangu, alikuwa akinibashiria miaka 45 na zaidi. Lakini alishangazwa kujua alikuwa kanikuza kwa zaidi ya muongo na nusu.
Sikuwaza saana siku hiyo mpaka juzi nilipokuwa napitia taswira mbalimbali kisha nikakutana na moja niliyopiga na wafanyakazi wenzangu wa 100.5 Times FM.
Nikakumbuka siku hizo ambapo niliwa ndio kwanza nimevuka miongo miwili, Sister V alikuwa na SALIMIA USALIMIWE PARTY iliyowashirikisha wasikilizaji wa kipindi hicho ambao walikutana ofisi za Times kupanga mikakati ya kufanikisha "party" hiyo. Nikiwa natoka studio, mwenzangu niliyekuwa nafanya naye kipindi akaniita jina. Nikaitika anakinieleza aliloniitia na nilipoanza kuondoka Mama mmoja akaniuliza "wewe ndio Mubelwa Bandio?" Niliposema ndio akasonya kisha akasema "kumbe ni mtoto tu. Siku zote nakusikiliza nadhani mtu mzima zaidi yangu." Nikajichekelesha ki-unafiki na kuondoka.
Sasa haya mawili yamenifanya niwaze VIGEZO VYA UTOTO, UJANA NA UZEE NI VIPI?
Picha: Maisha na Mafanikio Blog
Ni kukua kwa uzazi ama? Kwani huyu binti anayesemekana kuwa na umri wa miaka 10 aliyejifungua ataendelea kuitwa mtoto? Je mtoto anaweza kuwa mtoto?
Ni uwezo wa kimaamuzi ama? Vipi kuhusu hapa Marekani ambapo kijana wa miaka 18 haruhusiwi kunywa pombe mpaka atimize miaka 21 (nadhani kwa uwezo wa kuamua akishalewa) lakini anaweza kupelekwa vitani akiwa kama askari ambako atafanya maamuzi ya kuua ama kutoua.
Ni muonekano wa mtu ama? Picha hizi zilipigwa mwaka mmoja. Kwani zote zaonesha "ujana" ulio sawia?
Ni mitindo ya mavazi na nywele ama?
Nasikia watu wakisema "yule naye miaka yaenda lakini mitindo yake ya nywele ama mavazi yake ama maongezi yake ni kama mtoto.
Ni muonekano wa mvi kama aliouliza Dada Yasinta hapa ama?

Ndio maana bado nawaza kuwa VIGEZO VYA UTOTO, UJANA NA UZEE NI VIPI?

Tuesday, April 6, 2010

OYSTERBAY ama OYSTER BAY? Nawaza kwa sauti. Niwazue

Kule Mtwara kuna mto waitwa LUKULEDI. Yaani Mto Lukuledi. Na hadithi niliyowahi kuipata ni kuwa mto ule uliitwa hivyo baada ya mzungu aliyekuwa ukingoni mwa mto huo (ambaye inasemekana hakuwa akijua kiswahili wala "ki-kwao" kumuona binti akizama na kisha kujitahidi kutotoa sentensi ndefu na kuwaonesha waliokuwepo pale kuwa "look..Lady is drowning" [usiniulize kuhusu usahihi wa Sarufi (grammar)] lakini nilichosimuliwa ni kuwa "look...lady" ndio iliyokuja kuwa "LUKULEDI". Sasa leo nimejiuliza kuhusu huu ufukwe maarufu wa "OSTABEI" uliopo Dar. Asili ya jina hili ni wapi?

Hawa hapa chini ndio Oysters Image from American Feast's Sustainable Food Blog
Na huu hapa chini ndio ufukwe huko Dar ambao waitwa Oysterbay. Image from Webshots
Ninalowaza ni uhusiano wa Oysters hawa na Bay hiyo.
Je! Kuna mwenye taarifa kamili ama usahihi wa kwanini ufukwe huu ulipewa jina la Oysterbay? Ninaamini wengi wa wakazi wa mji wa Dar hawaelewi asili ya jina hili na sitashangaa kama wengi hawafahamu uhusiano wa jina la hao Oyster na Bay hiyo (kama upo ulio halisi kuhusisha kupatikana kwa jina lake)
Leo nimewaza kuhusu hili na kwa kuwa taarifa ama habari nyingi kuhusu mahala, vitu na nchi yetu hazipatikani mtandaoni, nimeona niweke swali langu hapa ili nisaidiwe kuwazua.
Hivi ni Oysterbay ama Oyster Bay? Na asili yake ni nini?? Nawaza tu kwa sauti..NIWAZUE.
Kumbuka hiyo Oysterbay / Oyster Bay iko Dar Es Salaam. Mji aliouimba Ras Nas
Burudika naye hapa chini huku "ukinisakia" jibu

"Tuonane "Next Ijayo"

Monday, February 8, 2010

Nawaza kwa sauti..... Nisaidie kuwazua

Iwapo kutafanyika AUDITING kwenye Bunge letu "tukufu" kutuwezesha kujua ni wabunge wangapi wanaofanya kazi sawa na malipo yao, unadhani ni wangapi watakaonekana kulipwa sawa na "huduma" yao kwa taifa?
Nawaza kwa sauti tuuu, nisaidie kuwazua

Tuesday, December 29, 2009

Nawaza kwa sauti......Niwazue

Picha toka www.ica.org.uk
Desemba 20 mwaka jana niliuliza swali kuwa Ni kweli sote tu-wabinafsi? (Jiulize hapa) na ninaendelea kujiuliza swali katika nyanja na maisha ya aina mbalimbali.
Leo nimewaza kuwa ikiwa mtu ataamua kuoa na kuchangisha michango ya harusi, lakini unachangia bila kuandika mahala popote kuwa ulitoa kiasi fulani, unadhani ni wangapi watatoa kiasi kama ambacho wangetoa iwapo wangewekwa kwenye kumbukumbu ya waliochangia harusi hiyo?
Ama je! Ikitokea muoaji akaomba mchango wa harusi lakini akaomba harusi isiwe na sherehe ili pesa mtakayochanga iwasaidie kuanzia maisha, ni wangapi wangekubaliana na wazo hilo?
Ni kweli twafanya tuyafanyayo kwa kuwa tunapenda kuyafanya ama twafanya kwa kuwa yanatunufaisha na kuturidhisha kwa namna fulani?
Ndio maana narejea kulekuleeee nilikowahi kusimulia kuwa Tunajidanganya wenyewe kudhani tunawajali wenzgine.(Bofya hapa kujikumbusha)

Nawatakia mwanzo mwema wa mwisho salama wa mwaka.

Blessings

Wednesday, October 28, 2009

Wapi ulipo "mstari mwembamba" kati ya UBISHI na IMANI?

Pichani ni rafiki yangu DiJaro ambaye kwa sasa ni kati ya wale wafanyao vema pale TBC Fm. Na miaka ya mwanzo ya 2000 nilibahatika kufanya kazi naye pale Times Fm. Kwa bahati mbaya, wapo waliokuwa wakimkatisha tamaa saaana na kujaribu kumzuia kutekeleza "ndoto" zake. Lakini mara zote tulipokuwa tumeketi nje ya studio (ambako kulikuwa na benchi) tuliongea mengi na kupeana moyo na mara zote alionekana KUAMINI KATIKA AAMINICHO na alikuwa akiamini kuwa yeye ni bora kuliko walivyokuwa wakimuona na tatizo kubwa ni kuwa hakuwa amepewa nafasi ya kuonesha uwezo wake halisi.

Katika vipindi vya Matukio ya wiki na Michezo nilivyobahatika kuongoza pale Times Fm, DiJaro aliweza kushiriki mara kadhaa na kwa hakika alionesha alichokuwa akiamini. Lakini si kwa waliokuwa wakiamini vingine kwani kwao, DiJaro hakuwa na uwezo.

Baadae "alipotea" ambako sikujua nami "nikapotelea" huku nilipo ambako sina hakika kama anajua niliko. Lakini nikasikia namna ambavyo aliendelea "kukua" na kuwa alipata nafasi ya kazi PRT na nikaanza kumsaka na naendelea kumsaka. Hiyo ilikuwa zaidi ya faraja kwangu kwani aliweza KUDHIHIRISHA alichokuwa akijariu kuonesha kwa muda mrefu bila mafanikio.

Mimi na yeye TULIAMINI KUWA ANA UWEZO MKUBWA KULIKO ALIVYOKUWA AKIONEKANA AMA KUDHANIWA na kwa wale waliompinga na kumkatisha tamaa walidhani hakuwa na uwezo bali ALIBISHA UKWELI KUWA HANA UWEZO.
Ni wapi ulipo mstari mwembamba utenganishao UBISHI kama alioonekana nao DiJaro (ambao kwa hakika hana) na IMANI aliyokuwa nayo kuwa yeye ni bora kuliko wanavyomdhania?

Na habari ya rafiki yangu huyu yaniacha nikijiuliza kuwa ni wangapi wanaoishia njiani wakikatishwa tamaa na wasiojua uwezo wao halisi? Ni wapi ambapo tunaweza kuona ulipo mstari mwembamba wa wale wasiokutakia mema na wale wakuoneshao njia sahihi?
Nawaza tu
Hongera Kaka DiJaro na huko uliko, KAZA BUTI
Blessings

Saturday, September 19, 2009

Swali la kutafakarisha toka kwa Kaka Kamala.

Nimepita kwa Kaka Kamala na kukuta bandiko lake hili ambalo linafikirisha saaana na hakika ni TIBA kwa nafsi ya kila mmoja. Naomba nikushirikishe katika swali litafakarisho. Bandiko hili "nimelinyofoa" kama ilivyo na naliwakilisha vivyo hivyo

Ni wangapi wanaoweza kuridhika?

Maisha yetu ni yale yale ya kukimbizana na kukimbilia kilicho mbali siku zote. Tunatamani mishahara mikubwa, vyeo vikubwa, wenza wa aina fulani fulani. Tunatamani na kuishi kwa utashi zaidi wala sio kwa mapenzi ya kweli na uhalisia kiasi kwamba dunia inatisha si siku zote tunaogopa tu.

Ukiwa na waliokuzunguka, hamkosi kutofautiana, ukiwa peke yako, ndani mwako kuna kelele na vurugu kibao. Unatamani kuwasha redio, kusoma kitabu, gazeti au hata msaafu. Au unatoka ili utembeetembee, mambo yanaboa, duh.

Sasa maisha yanaaza kukutishia. Ni magumu, huwezi kukaa peke yako, unatamani uwe na wengine, ukiwa nao, hamkawaii kukosana na kugombana. Na hii ndio sababu familia nyingi zina migogoro. Tunaona makosa kiurahisi kuliko mazuri au hata kusahihishana. Maisha ni ya masharti kweli kweli.

Tunatafuta mali na kujitahidi kumiliki mali nyiiingi zaidi ili tuumiliki ulimwengu na kuna wanaojiaminisha kuwa wanamiliki ulimnwengu kumbe ni mateso matupu. Unafikiri marais na wabunge wana amani yoyote na kuona maana halisi ya maisha? Hawana. Wanatawaliwa na hofu, huzuni ni kuhangaika ili waendelee kuwa madarakani.

Tunakufa kwa presha kwa sababu ya kutaka kumiliki kitu fulani na tunasahanu kwamba kuna kitu muhimu tunachokimiliki ambacho ndicho cha kujivuna nacho kuliko vinginevyovyote viwavyo. Kitu hicho ni sisi wenyewe. Hakuna awezaye kutumiliki sisi isipokuwa sisi wenyewe tunajimiliki. Badala yake tunakimbizana na vile vya nje yetu tukidhani vitatupa furaha kumbe furaha ya kweli imo ndani mwetu.

Ninapopanga kuanza maisha mapya kwa kurudi kijijini, nafikiri itanisaidia sana kuliko kuendelea kutafuta nisichokihitaji hapa mjini. Utafutaji huo kamwe hauwezi kufanikiwa kwani nikipata hiki, natamani kikubwa zaidi kama wewe vile. Kumbe vitu vichache tu vinanitosha na hivyo naweza kuishi bila stress kule vijijini kuliko kuhangaika na kufukuzana mijini.

Au unasemaje wewe. Unadhani ipo siku utaridhika? Hapana na kwa hiyo ni lazima utafanya kazi mpaka uvunjike, utaamua kuiba na kuwa fisadi kwa kuamini utapata furaha na utaishia kufa kwa hofu na ugiligili kwani kamwe hatokipata kile unachokitafuta nje yako, labda urudi ndani mwako ndimo kilimo humo.

AMINA

Tuesday, September 8, 2009

Nawaza...Niwazue.

LABDA MIMI NI MIMI KWA KUWA HAKUNA MIMI ZAIDI YA MIMI
Sijamuuliza mke wangu na sitathubutu kumuliza kwa kuwa "NINAWAZA KWA SAUTI TU". Mawazo yangu yanauliza kuwa, kwa wale wapendano, HIVI NAMPENDA UMPENDAYE KWA KUWA NDIYE BORA KATI YA WABOVU ULIOWAONA AMA KWA KUWA NDIYE BORA KWA AMBAO UMESHAWAONA? (Best among the worst ama Best so far?)
Nauliza kwa sababu najua kile kiitwacho ubora chaweza kubadilika kulingana na mazingira, watu anaokutana nao na hata upeo wa mtu. Na UBORA huu (uwe ni tabia ama muonekano) ni kati ya vitu ambavyo tunajifunza na kuvibadili na kuvithamini kwa namna tofauti kila siku / kila nyakati. Kwani unadhani tunatumia asilimia ngapi ya uwezo wa ubongo wetu? Wataalamu wanasema tunatumia kati ya 0.1%-10% ya uwezo wa ubongo wetu katika maisha yetu (soma HAPA) na ndio maana najiuliza kama ungeweza kuongeza uwezo wa ubongo wako mara kadhaa (tuseme 2) unadhani ungekuwa unamuona mwenzi wako umuonavyo sasa? Labda angekuwa bora zaidi (maana ungeongeza aina nyingine za ubora) na labda ungemuona hakufai (kwani ungeweza kupunguza maana za ubora). Lakini kwani uzuri ni nini na unaonekanaje miongoni mwa macho yetu?
Unadhani kuna mzuri zaidi ya wewe ujinavyo? Pengine hakuna ajuaye uwezo wako katka kutenda na kuwaza yale yasiyoelezeka na ndio maana unashindwa kumfafanulia mwenzako namna alivyo wa muhimu kwako. Na labda ndio sababu mwenzako hajui madhaifu yako na ndio maana mko pamoja.
Lakini unadhani ungekulia katika mazingira mengine na bado ukakutana na huyo uliyenaye ungeendelea kuwa naye?
Je kama ngekuwa unaishi maisha ya kifahari ama kifukara zaidi ya uliyoishi mlipokutana unadhani ungekuwa naye? Na labda mmoja wenu asingempa mwenzake nafasi ya kudhihirisha kile kilichowaunganisha.
Lakini haya hayatibiki jamani Si ndio???????
Ungekuwa tofauti na ulivyo (kama ninavyouliza hapo) yawezekana usingesona hata haya niliyoandika. Lakini nimeandika kwa kuwa "NAWAZA KWA SAUTI"
Siwezi kujielezea nilivyo na kwanini nampenda nimpendaye na kwanini anipendaye ananipenda. Ila najua kuwa MIMI NI MIMI KWA KUWA HAKUNA MIMI ZAIDI YA MIMI
Wewe je?
Tuonane Next Ijayo

Tuesday, September 1, 2009

Kwani wewe unaona nini?

Image from This14U Blog
Kama wewe ni binadamu basi una sura ifananayo na hii. Na kama unaona nionacho mimi, basi huwezi jiuliza mara mbili KWANINI WAKATI MWINGINE SIKUAMINI? Ni kwa kuwa "ninasoma sura yako"
Ukiangalia taswira hii unasoma nini / neno gani usoni mwake?