Jinsi miaka inavyozidi kusonga ndivyo mabadiliko katika ubora wa muziki yanavyozidi kuwepo. Kwa nchini kwetu ni kugugumizi kuzungumzia muziki kwa ujumla kama una maendeleo ama kuna maendeleo katika muziki japo wenyewe umegota.
Miongo kadhaa iliyopita Tanzania ilikuwa ikiheshimika sana katika sanaa ya muziki na wasanii wengi wakubwa Afrika waliutambua muziki wetu. Hii ilifanya kuwe na utata kiasi juu ya nani alikuwa anaiga muziki wa nani hasa katika mapigo.
Lakini leo hii tunaambiwa kuwa muziki Tanzania umekuwa. Tunaoneshwa studio utitiri na vyombo vya kisasa, lakini wasanii wachache kuliko waimbaji ambao hawawezi kufululiza masaa mawili ya tamasha kabla sauti hazijawatoka. Sijui tunaendelea kimuziki ama muziki unaendelea kivyetu?
Basi leo tuwasikilize wana Kilwa Jazz. Moja kati ya bendi zilizofanya vema saana. Mtandao shirika wa BONGO CELEBRITY katika bandiko hili la wimbo wa ROSE WAUA, umeeleza historia fupi ya bendi hii nami nainukuu. Ilisema bendi ya Kilwa Jazz ilianzishwa "tarehe 15 Julai mwaka 1953 na kundi la wanamuziki waliokuwa wanatokea Kilwa na waliojimega kutoka Tanganyika Jazz Band.Hao waliongozwa na Ahmed Kipande na kaka yake Hassan Kipande (walihamia jijini Dar-es-salaam wakitokea Kilwa katika miaka ya 1940s,Hassani alitangulia mjini). Huyu Ahmed nasikia alijifunza mwenyewe kupiga Saxaphone. Aliinunua moja kuukuu kutoka kwa mlami mmoja aliyekuwa anafanya kazi Barclays Bank,akajifunza mwenyewe.Dah! Baadaye yeye na kaka yake wakajiunga na Tanganyika Jazz Band iliyokuwa na makao yake makuu pale New Street(siku hizi Lumumba Street).Kaka yake,Hassan,alikuwa anapiga gitaa.Hao walibakia na Kilwa Jazz mpaka ilipovunjika mwaka 1967.
Ingawa mwanzoni Kilwa Jazz ilianzishwa na watu waliokuwa na asili ya Kilwa na marafiki zao zaidi,baadaye wanamuziki kutoka pande mbalimbali walijiunga na Kilwa Jazz.Kufikia mwaka 1966 ilikuwa na wanamuziki takribani 26(15 wa bendi “A” na 11 Bendi “B”) na wanachama zaidi ya 50 wakiwemo baadhi ya viongozi enzi hizo.Usishangae,enzi hizo bendi zilikuwa na wanachama. Katikati ya miaka ya 60s Kilwa walihamia katika jengo lililokuwa linaitwa Madobi pale Kariakoo kuelekea Jangwani. Wakati huo bendi kubwa zilikuwa Western Jazz Band,Dar-es-salaam Jazz Band na wenyewe Kilwa Jazz Band."
Tukumbuke kilio cha Wana Kilwa Jazz waliokuwa wakiumia rohoni kwa kuhitaji nafasi ya kusema na fulani kidogo.
Burudika na elimika kwa kibao hiki Lau Nafasi
** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Napenda nipate lau nafasi, niweze kusema nawe kidogo oh..
Jamani mashairi yake ukiyasikia yanaleta ladha fulani ...
Tunashkuru sana mkuu
Post a Comment