Monday, March 23, 2009

Za Kale vs Maisha ya sasa. DUNIA IMANI IMEKWISHA


Marijani Rajabu enzi za ujana wake. Picha kwa hisani ya Kaka Issa Michuzi
Kama nilivyoeleza mwisho wa wiki iliyopita kuwa tutaanza kuleta kipengele kipya cha muziki wa kale lakini tukijitahidi kuhusisha na maisha ya sasa. Ni ombi ambalo lililetwa na baadhi ya watu na kwa kuwa lilikuwa na msingi (kuliko idadi) nikakubaliana nalo hasa kwa kuwa nami pia nilishafikiria kitu kama hiki. Hii ni kwa sababu mimi pia ni mpenzi wa miziki halisi inayogusa maisha ya jamii yetu. Muziki wenye kuikomboa na / kuielimisha jamii. Ambao unasisitiza kwenye kujitambua na kuwawezesha wananchi kunyanyuka na kupiga hatua mbele badala ya kukaa na kubweteka kuisubiri serikali kufanya kila kitu.
Na tunapozungumzia miziki ya zamani badi hatuwezi kumuweka kando Jabali la Muziki Marijani Rajabu. Akiwa mmoja wa watunzi mahiri wa muziki nchini Tanzania, Marehemu Marijani aliweza kuyaeleza kwa ufasaha kabisa yale ambayo yanaikumba jamii nyakati hizo (na kwa bahati mbaya mengi bado yanaendelea tena kwa aina na kiwango kipya na kikubwa).
Tunafungua naye dimba hili kwa kibao chake DUNIA IMANI IMEKWISHA. Humo utamsikia Jabali na wana Dar International walivyoelezea jinsi nyoyo za watu zilivyobadilika, kupungua ama kuisha kwa uaminifu na hata namba ya binadamu ilivyo ndogo ukilinganisha na watu. Pengine wapo ambao hawakutambua namna unavyoweza kuwa mtu usiwe na ubinaadamu. Si tunawaona wanavyoiba pesa ya uma na kuwatesa waliowaweka kwenye nafasi hizo? Si tunaona wanavyowaua ndugu zetu albino ili wawe na mali? Si tunawaona wanavyowaua wenzi wao ili wasigawane mali walizochuma pamoja? Ama huwaoni wanaodhulumu watoto na wajane kwa kuwa hawana mtetezi wa mali zao? Si tunaona wanavyofilisi makampuni ya umma kwa starehe zao binafsi?
Hayakuanza jana wala leo, walishayaona kina Marijani.
Sikiliza Dar International wana Super Bomboka wakisema DUNIA IMANI IMEKWISHA

Kumbuka kuwa waweza kupitia matoleo mengine ya miziki ya "Zilipendwa" yaliyowahi kubandikwa bloguni humu kwa kuBOFYA HAPA, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

4 comments:

Koero Mkundi said...

Wimbo huu wa Dunia imani imekwisha, bado unaendana kabisa na mazingira tuliyonayo sasa.
Hebu angalia jisi wannchi wasivyowaamini viongozi wao, kila kukicha kelele za ufisadi haziishi watu hawawaamini viongozi wao waliowachagua kwa kura nyingi.
Nani alijua kauwa Bwana Mwakinyembe nae ataingia katiaka tuhuma za ufisadi, kila siku watu hawaishi kunyoosheana vidole, kila mtu kwa fisadi.

kaka Mubelwa usishangae na wewe kesho ukaitwa fisadi......

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante sana yaani umeniweka sehemu ambayo hata sijui nisemaje. Huu ulikuwa wimbo ambao marehemu mama yangu alikuwa akiuimba wakati nipo mgongoni kwa hiyo leo nimefurahi sana kuusikia kweli za kale

Anonymous said...

Hakuna anayemuamini mwenzake,dereva teksi hamuamini abiria wake naye abiria hamuamini dereva teksi.

Ndani ya daladala kila unayemuona unahisi ni mwizi unachunga mfuko wako.

Albino hakuna anayemuamini zaidi ya Albimo Mwenzake yaani hata wazazi wao wamewageuza Albino kuwa ni dili linalolipa chapchap.

Bungeni nako hawaaminiani wanaogopa kutupiana uchawi.

Muhimbili mgonjwa hamuamini daktari kwa kuwa kama haujatoa chochote unaweza kufanyiwa operation ya kichwa badala ya mguu.

Raisi hawaamini mawaziri wake kwa kuwa wanaweza kupiga dili la kuuza kijiji kizima kwa kuwa wameahidiwa 10percent.

Kweli dunia imani imekwisha.

Mzee wa Changamoto said...

Kaka Fred kweli umemaliza. Naamini kuisha kwa imani kunamaliza mengi na kupoteza utendaji.
Kuna mengi ambayo walisema, wanasema na bado tunaendelea kuyaona kama vile hakuna aliyekemea.
Kaazi kwelikweli