Monday, May 31, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa......USIA KWA WATOTO & TUPATUPA

Baadhi ya wasanii wa Juwata Jazz Band. Watatu waliosimama toka kushoto (kwao) ni Joseph Maina, Tx Moshi William na Athuman Momba ambao wote sasa ni marehemu. Lakini ujumbe wao utadumu milele
Sina hakina ni wangapi walibahatika kupata nafasi ya kuusiwa na wazazi wao kuhusu mabadiliko ya maisha kulingana na nyakati mbili (ujana wa wazazi na wetu sisi). Ni ukweli kuwa kuna mabadiliko meengi ya kimaisha kuanzia thamani ya pesa mpaka, matumizi yake, umuhimu wa kuweka akiba na mengine mengi.
Pengine huwa tunausiwa lakini si kwa kuongea kama BABA/ MAMA NA MWANA, bali mara nyingi ni wakati wa kugombezwa na kufokewa.
Lakini pia si wengi ambao katika hali ya kirafiki wanaweza kueleza matatizo wanayopitia kwa kuwa walishindwa kuwa na umiliki mzuri wa pesa zao. Ni CHANGAMOTO YETU sote kuweka malengo mema na kuelekeza mabadiliko ya maisha kwa wale watutegemeao.
Leo hii tunao JUWATA JAZZ BAND (ambao sasa wanafahamika kama Msondo Ngoma Music Band) ambao wanakuja na nyimbo zao mbili kuhusu umuhimu wa kupanga vema matumizi. Wa kwanza ni Usia kwa watoto na wa pili ni Tupatupa ambao ni juu ya kijana anayejutia matumizi yake mabaya ya pesa.
Katika USIA KWA WATOTO, twasikia nafasi ya BABA anayewakusanya watoto na kuwaeleza maisha yalivyokuwa huko alikotoka na kuwafananishia na namna yalivyo hivi sasa. Si jambo lionekanalo kufanyika zaidi kwa jamii yetu hivi sasa, lakini ni lazima VIJANA watambue maisha yalivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ili kuweza kutambua fika kama wanaendelea kwa kuwa na mambo mapya ama wanaendeleza yale yaliyowahi tokea.
Lakini pia katika TUPATUPA tunamsikia kijana ambaye maisha yalimnyookea na sasa yamemgeuka na anatumia nafasi hiyo kutoa USHUHUDA wa namna ambavyo maisha yanaweza kubadilika na kukufanya uwe na maisha ambayo hukuwahi kuyawaza ulipokuwa na pesa.
ANAISHI KUWAONYA WALIMWENGU KUWA "mkifuata anasa mtapoea kaka mimi"
Sikiliza, burudika na jifunze.

Kisha TUPATUPA

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli maisha ya zamani yalikuwa safi sana "kuishi kufuatana na wakati" pesa ni maua na tena zinaua.... Yaani umenifikisha mpaka nilipokuwa miaka miwili/mitatu nikimsikia mamangu akiimba miimbo hii kama vile sala ya baba yetu. Upendo Daima.

Nuru Shabani said...

Ni kweli kwa maisha ya sasa ni wazazi wachache sana ambao hukaa wakaongea na watoto wao kuhusiana na maisha na uwekaji wa akiba ya pesa.
Kuna mtangazaji mmoja wa siku nyingi kuna siku nilikuwa naongea naye masuala ya muziki hasa huu wa kizazi kipya aliniambia kuwa siku hizi hakuna wanamuziki kuna wasanii wa muziki na ndiyo maana hata tungo zao hazina uzito kama miziki ya zamani, kama hizo za usia kwa watoto na tupatupa.
Asante kaka

Mzee wa Changamoto said...

Karibu saaana Nuru. Ni muda mrefu sijaweza wasiliana nawe. Shukrani kwa kutembelea na kusomwa kilichoandikwa hapa.
Nimependa ufafanuzi wa huyo mtangazaji wa siku nyingi kuhusu sanaa ya muziki. Ni kweli kuwa sanaa yetu ina "wasanii" wengi. Hata kwenye uigizaji tuna WANAOIGIZA MAIGIZO badala ya kuigisha maisha halisi kupata maigizo.
Ni kama vile wanaigiza kitu kilichoigizwa tayari.
Inasikitisha.
Na ndio maana ukisikiliza nyimbo zilizopigwa kwa ufasaha kama hizi za miaka kadhaa iliyopita unapata HISIA halisi ya kiimbwacho. Na hata usikilizapo michezo ya redioni, unapata hisia ya tukio kuliko kuangalia video za kisasa.
SIJUI TUWASAIDIEJE MAANA NAO NI WAGUMU KUJIFUNZA
Baraka kwako na kwa Da Yasinta pia