Sunday, May 30, 2010

Nawaza. Hivi ni mimi, wao ama mfumo wa maisha usiopingika?

Kwa walio wengi, TEKNOLOJIA ama u-SASA vyatakiwa kumaanisha UBORA. Na ni hapo ninapowaza kama UBORA huo tunautafsiri katika usahihi wake. Nimekuwa nikiwaza na bado nawaza kuhusu mifano mambo haya na hii ni mifano michache ambayo ningependa kushirikisha KUWAZA ili kujua kama niwazalo ni wazo langu, ni wale niwawazao ama ni mfumo wa maisha ambao mimi, wao na wewe hatuna uwezo wa kubadili?
Ninapowaza MAENDELEO, TEKNOLOJIA na UWEZESHWAJI WA SASA katika fani na maisha, nashangaa kuona bado ya kale yanaendelea kuwa na UBORA kuliko sasa. Uncle Charles Hilary. Mkongwe ambaye tangu akiwa enzi za RTD amekuwa zaidi ya nyota kwangu. SABABU?? Msikilize anaposoma Habari, anakuwa na sauti iendanayo nayo, anapotangaza matangazo ya vifo ni sawia, akiwa kwenye muziki unapenda, atangazapo mpira utapenda, atoapo uchambuzi wa mambo mbalimbali utashangazwa na upeo. Sasa hivi uliza ni wangapi wenye "viwezeshwa" vya kompyuta wanaweza hayo?
Photo credit:
Da Candy
Nianzie kwenye Habari. Siku hizi natambua kuwa kuna VIFAA VYA KISASA vyenye nuweza kumsaidia mtangazaji kuwa na sauti nzuri na kufanya mengi apendayo tofauti na ilivyokuwa miaka ya themanini. Lakini ni mtangazaji gani hii leo nyumbani Tanzania anaweza simama na kusema ni bora kuliko wale waliozungumzwa HAPA?. Lakini twajua kuwa watangazaji wetu wa sasa wanasifika kwa kazi njema na wanapata tuzo nyiingi kila mwaka kwa "kazi nzuri"
Hili lanifanya niwaze kama TEKNOLOJIA inaonekana kutupa kiburi na kudhani tutaweza kutenda kila tupendalo hata kama hatuna vipaji. Tunasikia "stereo" nzuri lakini ujumbe, maudhui, fikra, uchambuzi, upembuzi na mtiririko wa matangazo ni sikitisho.Kipa Athumani Mambosasa akidaka mpira wakati Simba na Yanga zilipokwaana uwanja wa Nyamagana 1974
Photo Credit:
Michuzi Blog
Labda nirejee kwenye michezo. Ninatambua kuwa timu za sasa zina vifaa viingi vya kuwasaidia wachezaji wawe katika hali nzuri njeeema kimchezo. Wana gyms, wanakula vema wanafuata ushauri nasaa kuwapima na kuwaweka katika "shape' ili wawe vema. Lakini licha ya tuzo na sifa na mapato mazuri wapatayo, ni nani anaweza kusimama ndani ya Tanzania na kusema yeye ni mlinda mlango mzuri zaidi ya wakongwe kama kina Athuman Mambosasa? Na kama hakuna, ina maana hawafanyi kazi kama walivyotakiwa ama ni mazingira hayawaruhusu kuwa vile walivyokuwa wakongwe hao? Photo Credit @Reuters via Dominion Post
Ama tukizungumzia soka ulimwenguni, kuna mchezaji yeyote ambaye leo hii anaweza kusimama na kusema ni bora kuliko PELE?
Nawaza kama ni wachezaji wa siku hizi wanaocheza chini ya kiwango, ama ni sisi tunaowapima isivyo vema ama ni mfumo wa maisha unaowafanya wa kale kuendelea kuwa wakali?
Labda nirejee kwenye sanaa ya maigizo. Nimekuwa mfuatiliaji wa mambo ya maigizo kwa miaka mingi. Shukrani kwa wazazi wangu ambao wamenijengea mwanzo mzuuri wa kupenda sanaa hii. Nimekuwa pia nikishiriki maigizo tangu nikiwa na miaka 5. Lakini ninaposikiliza michezo ya zamani (baadhi ziko HAPA (kwa Da Subi) na kuangalia video za michezo ya kuigiza ya siku hizi, nashangaa kuwa NINAPATA HISIA ZA TUKIO HALISI nisikilizapo hizi za kale kuliko niangaliapo video hizi. Hayati Mzee Pwagu ambaye maishani mwake alikuwa zaidi ya muigizaji. Waliokuwa waelimishaji wakubwa waliofanya kazi kwa ufanisi na kuleta taswira halisi ya wazungumzacho licha ya kuwa walikuwa wakisikika tu redioni na si kuonekana. Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
Photo credit:
BongoCelebrity.com
Nawaza kama licha ya teknolojia iliyopo, kuna muigizaji yeyote anayeweza kusema anawakilisha na kuwasilisha hisia na ujumbe wake vema kuliko waliofanya haya kwa "zana za kizamani" kama kina Mzee Pwagu, Pwaguzi, Jangala na wengine? Ni kweli kuwa wasanii wa sasa hawajui kuwa wana la kujifunza toka kwa WAKONGWE ama hawaamini kuwa kuna lolote wanaloweza kujifunza? Ama wanajifunza na kutendea kazi lakini mfumo wa maisha wawalazimisha kuwa walivyo?
Sikiliza CLIP hii ya PWAGU NA PWAGUZI ambayo "fundi mitambo" SUBI wa WAVUTI ameitengeneza kutoka East African Tube

Nimalizie na wanamuziki. Hapo wala sina ninaloweza zaidi ya kuuliza kuna anayeweza kusimama kidete leo hii kusema kuwa ana "masauti" ya kuwazidi waliotangulia kama Marijani Rajabu, Hemedi Maneti, Moshi William na wengine?
Ndivyo walivyokuwa wakirekodi miaka hiyo. Tofauti na sasa ambapo wasanii wanaweza kurekodi "track" moja moja na kwa msaada mkubwa wa "copy, cut and paste" na bado kuna "effects" za kompyuta.
Photo credits:Picture Depot
Ama licha ya teknolojia iliyopo sasa, kuna anayeweza kusimama na kusema anapiga reggae bora kuliko Bob Marley ambao walikuwa wakirekodi kwa zana "duni" ukilinganisha na za sasa?

Ni hapa ninapowaza tena kama twategemea kuliko tunaloweza kupata toka kwa washiriki wetu wa sasa ama ni kweli kuwa washiriki wa kale walikuwa na mengi ambayo wa sasa hawayapati kutokana na sababu fulani za kimfumo wa maisha?
Kwani ni mimi tu niwazaye haya ama?
Naishia kujiuliza hivi NINAWAZA NINI?
***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

5 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka kuhusu Chalz Hilary we acha kabisa.

Hiyo daka ya Mambosasa imenisuuza mno.

Kuhusu Pele usipime ingawa Maradona alikuwa mkali zaidi yake.

Nimesikitika kuondokewa na Mzee Pwagu. (Mungu amlaze pahala pema peponi. Amina)

Hiyo ya The Wailers mkuu najua unajua ni kiasi gani nimesuuzika moyo.

Wenzetu walikuwa orijino kabisa. Na walifanya yale ambayo hata hawa wanaotumia kompyuta hawawezi. John F Kennedy alipata kusema, 'a man is still an extraordinary computer of all.'

Sikiliza mikito ya Bob uone kama hii inayofanyiwa manjonjo na kompyuta kama inaona ndani.

Hawa waliwaza vitu vya aina yake.

Hapa naandika huku nasikiliza 'Trenchtown'

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mh, kuna mafunzo mengi hapa kwamba inabidi tuache chata, muda unakwenda namaisha katikamwili twaja kuyaacha

Maisara Wastara said...

Mh! nimesoma kisha na mie nikabaki nikijiuliza hivi Kaka Mubelwa aliwaza nini kuanzisha hii Segment ya waliwaza nini?

Lakini kuna jamo lingine ambalo kaka Mubelwa Naomba nalo ulijadili katika kipengele hiki cha waliwaza nini.
jambo lenyewe ni hili la Blog...
Hivi hawa walioanzisha hiyo sijui niite Web inayotuwezesha kuanzisha hizi blog zetu za kupigia Talalila kama anavyosemaga kaka Kitururu, nao waliwaza nini?

Na huwa najiuliza kama Teknolojia hii ingekuwepo enzi za mwalimu Nyerere angeweza kweli kustahimili hizi Talalila zetu katika blog?

Je na sisi tunaoanzishja blog tuliwaza nini......Nimejiuliza mpaka nikabaki kushangaa tu mwayego

Kaka Mubelwa samahani kwa kupiga talalila hapa kwenye blog yako, naomba univumilie mie Tegelezeni...

Anonymous said...

mambo kaka mzima jamani?

Mzee wa Changamoto said...

Ndugu yangu Anon.
Kwanza asante kwa kuendelea kunitembelea na pia karibu zaidi kwenye mawasiliano ya email. Natumai wewe ndiwe uliyekuwa ukinisaidia na kuulizia kuhusu Renata. Kama ndiwe, basi niandikie changamoto@gmail.com
Kuna mema ya kuwasiliana nawe.
Blessings