Sunday, September 18, 2011

Za Kale vs Maisha ya Sasa...NAJIBU TELEGRAM

Maisha yetu yanabadilika jinsi tukuavyo na tuishivyo. Yanabadilika na kubadilisha mfumo mzima wa maisha ambao unabadilisha fikra zetu kila uchao. Tulishapa kuongelea namna ambavyo DUNIA IMANI IMEKWISHA hapa, na sote tunatambua kuwa kuisha kwa imani ndiko kunakotulazimisha kuishi kwa msaada wa "fulani" ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa. Tunahitaji jicho la ziada ama kuhitaji shuhuda kwa karibu kila kitu tufanyacho. Kusaini chochote, kununua chochote na hata kusuluhisha kitu tunahitaji kuwa na shuhuda kwa kuwa imani si kama zamani na mfumo mzima wa maisha umeondoa kujiamini ama kuaminiana ndani mwetu. Ukweli ni kwamba imani kwa sasa ni tofauti na zamani.
Zamani migongano ya kifamilia ilikuwa ya kifamilia na ilisuluhishwa na wanafamilia zaidi. Heshima baina ya wanafamilia ilionekana kuwa kubwa kuliko sasa, na hata masuluhisho miongoni mwa wanafamilia nayo ilikuwa ya ndani. Sasa hivi mambo yamebadilika na sina hakika kama ni maendeleo ama la, lakini bado naamini MAMBO YA NDANI YANASTAHILI KUBAKI NDANI (japo yategemea ndani kukoje).
Ndoa zilikuwa zikisemekana kujadiliwa na kutatuliwa ndani ya nyumba / familia tofauti na sasa ambapo yaonekana "pesa" na mawakili wamechukua nafasi kubwa ya UAMINIFU WETU. Lakini tunaendelea kukumbushana kuwa japo twaishi tuishivyo, zipo zama ambazo maisha yalikuwa na MIPAKA. Na ndio maana leo tumeamua kujiburudisha, kujielimisha na kujikomboa kwa kibao hiki.
Leo katika kipengele hiki tunao DDC Mlimani Park wana Sikinde Ngoma ya Ukae ambao chini yake Cosmas Thobias Chidumule wanaeleza walivyosuluhisha "mgogoro" uliopo kati ya kaka ya Chudumule na Mke wa Kakaye huyo.Burudika ukijifunza.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

No comments: