Thursday, February 5, 2009

Kweli ni uwekezaji, lakini ni kwa manufaa ya nani?

Wakati wa kuanza kwa harakati na kampeni za ubinafsishaji na uwekezaji kulikuwa na meengi mema "yaliyootwa" na wengi vikionekana kama suluhisho katika kuupa nguvu mfumo mzima wa uchumi nchini. Lakini kumetokea mfululizo wa mambo ambayo "yanalazimika" kuibuliwa ambayo hayaoneshi kuwa waliolezea manufaa ya uwekezaji, waliopewa dhamana na kusimamia na kuendesha uwekezaji na waliotakiwa kunufaika na uwekezaji huo wako kwenye kurasa napengine "dunia" tofauti za mafanikio na manufaa ya uwekezaji huo. Tumeshuhudia watu "wanaotetea" habari hizi za uwekezaji na wanaowatetea wawekezaji wakiwa na kauli tofauti wanapobanwa juu ya yale ambayo mara nyingi yanakuwa yameonywa na wafanyakazi wa chini wa makampuni na ama mashirika hayo.
Kuanzia mikataba ya RICHMOND, ATCL, BOT, NUWA mpaka misukosuko mingine iliyokumbana na uwekezaji kama mahoteli yanayobadili majina kila baada ya miaka kadhaa na sasa shirika la reli tunabaki kujiuliza kama nia ya uwekezaji ni kwa wananchi ama wawezeshaji wa uwekezaji. Angalia shirika la TRL ambalo licha ya kutembelewa na viongozi wa juu wa serikali kufuatia matatizo yanayoelezwa na wafanyakazi, hatuoni HATUA MADHUBUTI za kusimamisha yatendekayo. Na leo nilipoisikia na kuisoma habari ya "jaribio la kusafirisha injini mbili za treni kwenda India nikajikuta nauliza tena swali la uwekezaji na manufaa yake.
Mimi si mchumi na wala si mtawala wa mashirika lakini nikajiuliza kama ni nafuu kwa shirika lenye mkataba wa kuendesha miundombinu hiyo muhimu kwa miaka 25 kupeleka hizo blocks zilizotengenezwa Canada nchini India kwa matengenezo kuliko kuwekeza kwenye karakana na mtaalamu nchini? Najiuliza (kama ni kweli) kuwa kwanini hizo injini mbili zilizotangulia matengenezoni hazijarejea na wanataka kupeleka hizo nyingine? Kwanini mali ya wananchi inakosa mtu wa kuilinda na kuihakiki ufanisi wake? Ni hawahawa wawekezaji ambao wametangaza nyongeza ya nauli kwa asilimia 11.6 kuanzia katikati ya mwezi huu, ni hawa hawa waliolaza watu kwa siku kadhaa, ni hawahawa wawekezaji ambao wasafiri wanalalamikia hali za mabehewa ilivyo mbaya, ni hawahawa wawekezaji ambao tunasikia wanabadilisha vichwa vya treni na kuweka hivyo vivutavyo mabehewa saba. Ni hawahawa, ni hawahawa ni hawahawa ......
Kweli twataka uwekezaji, lakini ukija Tanzania uje kwa manufaa ya nani?

1 comment:

Subi Nukta said...

Injinia Mubelwa,
Ukianza kuhesabu vifaa vilivyoibwa kisha ujumlishe na vile vilivyotelekezwa kwa ubovu mdogo tu unaweza kushangaa kama neno 'ukarabati' huwa linapewa umakini wake katika mipango ya kawaida na kama ndivyo, je, ni nani huwa anafuatilia kuhakikisha kuwa mipango inafanyika na kutekelezwa. Kaazi kweli kweli.