Showing posts with label Jungu kuu. Show all posts
Showing posts with label Jungu kuu. Show all posts

Saturday, December 25, 2010

PRIDE FM Live....Zawadi yangu ya NOEL

Ndio nimekuwa "nikilia" saana kusikiliza radio za nyumbani. Na nimekuwa shabiki mkubwa wa kusaka na kutangaza radio za Tanzania zitangazazo moja kwa moja
Na leo nilipopata salaam za krismasi toka kwa Kaka Ramadhani Lutambi wa Pride Fm nikakuta maelezo ya kuiskiliza MOJA KWA MOJA. Nami nikayafuata na sasa KRISMASI yangu inanogeshwa nao.
Jiunge nao kwenye mtandao hapa http://www.878pridefm.com/index.html ama kusikiliza live kwa kwenda hapa http://www.streamfinder.com/internet-radio-station/26969/pride-fm-radio/ kisha bofya MP3 LISTEN ama unaweza ku-double click anwani http://208.43.81.168:8874/stream?.wma ambayo itafungua Windows Media Player na kukuunganisha live.
Mara nyingine hufungua ki-windows kuuliza kuhusu "local server" nawe wa-click Yes na you're good to go

Asante kwa wana PRIDE FM kwa kutujali tulio mbali. Baraka kwenu nyote

Monday, December 20, 2010

Tunapofunga mwaka, tujali UHAI kuliko pesa.

Ni MSIMU mwingine ambao tunajua kuwa wengi hurejea nyumbani kwa mapumziko ya Krismas na Mwaka Mpya. Na mara zote huwa ni furaha saana msimu huu ufikapo, lakini kama Lucky Dube alivyoimba kuwa "where there's a pleasure, there's always a danger" nami nakumbusha kuwa ule "uroho" wa pesa wa kupandisha nauli, kuongeza safari za mabasi na vyombo vingine vya usafiri bila kujali matengenezo na ukarabati wa vyombo hivyo, mashindano ya "nani atafika wa kwanza" baina ya vyombo hivyo na pia kutenda kazi kwa muda mrefu bila kupumzika kwa waongoza usafiri huo kumekuwa kukizua vilio kila mwaka na hata wale wasiopoteza maisha wanabaki na maumivu ama vilema vya Maisha.
Kuna raha wakati huu wa sikukuu na kuna pesa pia kwa kuwa watu wana uhitaji wa kwenda kujumuika na familia zao, lakini kama wamiliki hawatakuwa makini, basi kutaendelea kuwa na karaha kwa wale ambao licha ya kulipa pesa nyingi, bado wanaweza kutofika waendako, ama kufika wakiwa na maumivu ama mapungufu na kibaya zaidi wasipate malipo yoyote kukidhi matibabu yao kama ilvyotokea kwa baadhi yetu miaka 11 iliyopita.
Tukumbuke kuwa katika kila raha tuisakayo wakati huu wa sikuku, kuna uwezekano wa karaha kuambatana nayo. Na tuwe waangalifu na wajalifun na waheshimifu kwetu na kwa wenzetu.
Amani, Upendo na Usalama kwenu nyote nyakati hizi.

Friday, October 29, 2010

REMEMBERING GREGORY "The Cool Ruler" ISAACS

Kamera ya Changamotoyetu ilikuwepo kushuhudia Hayati Gregory Isaacs akitumbuiza ukumbi wa Zanzibar on The Waterfront March 16, 2008.
Jumatatu ya wiki hii ulimwengu wa reggae ulimpoteza mmoja wa wakongwe huo duniani GREGORY ISAASCS ambaye alifariki nyumbani kwake London kwa saratani ya mapafu (Lungu Cancer). Maradhi hayo aligundulika kuwa nayo mwaka jana.
Nilibahatika kuwa mmoja wa waliohudhuria onesho lake lililofanyika Machi 16, 2008 katika ukumbu wa Zanzibar hapa Washington DC ambapo licha ya kuonekana mdhoofu, bado aliweza kutuburudisha vema kwa nyimbo zake njema zilizompa umaarufu na jina la jukwani la "COOL RULER" Baadhi ya nyimbo alizotumbuiza ni zile zilizompatia umaarufu mkubwa ambazo zilitufanya tusimame muda wote. Nyimbo kama MY NUMBER ONE
Pia alitutumbuiza na nyimbo kama LOVE IS OVERDUE ambao (kama ilivyo kwa nyingine nyingi)ziliwapagawisha kinamama na kinadada.

Pia hakutuacha bila kibao OH WHAT A FEELING ambacho nachi "kilibamba"

Na kama kawaida alimzungumzia "mtabibu wake wa usiku" katika kibao ambacho pengine ndio maarufu kuliko vyote kiitwacho NIGHT NURSE.

Aliweza kutawala vema jukwaa katika muda wote ambao alitumbuiza na kwa hakika wengi wa wahudhuriaji walionekana kufurahia kazi zake na kama uonavyo hapa chini, tabasamu lilionesha kuridhishwa na uwezo wa mkongwe huyuPUMZIKA KWA AMANI GREGORY ISAACS.
KAZI ZAKO ZITADUMU MILELE

Tuesday, September 7, 2010

Natimiza ombi la Prof Matondo

Hapa ndipo nilipokuwa natumika 2001-2003. Still looove it there. Sijui nikirudi watanipokea??????
Kwenye toleo langu la Desemba 19, 2009 kumueleza Mzee Jerome Danford Kassembe (irejee hapa), kakangu Prof Matondo alisema na (hapa nanukuu)"Mzee wa Changamoto - una "clips" zo zote ukiwa mbele ya maikrofoni? Kama unazo, tuwekee hapa bloguni tukusikie ulivyokuwa ukiunguruma."
Nami nilimuahidi kujitahidi kuweka audios zangu za vipindi (ambazo ziko kwenye tapes na katika ubora wa chini) kwenye mfumo utakaoniwezesha kumuwekea hapa naye asikilize, acheke na labda aone tofauti ya kipindi kile na sasa.
Basi nimefanikisha, na japo si katika ubora ambao ninapenda ku-post hapa, lakini naamini zitaweka taswira ya nini tulikuwa tukifanya nyakati hizo.
Sikia mchemko wa "wingi" wa neno chuma kwenye dk ya 14.
Pia katika ku-katakata matangazo na nyimbo nimekuja gundua kuwa neno "msikilizaji" limesikika saana. Kumbuka kilikuwa kipindi kamili nami nimekata na sikuweza kugundua hilo mapema.

Hahahahaaaaaaaaaaaa
FURAHIA

Tuesday, May 18, 2010

HATIMAYE NIMEREJEA........Nilikokuwa

Hatimaye nimerejea wanandugu. Nilikuwa nimebanwa na mambo kadhaa na pia JUMAMOSI nilikwenda kushuhudia maonesho ya wazi ya ndege za kivita. Ilikuwa saafi sana japo ilikuwa ngumu sana kwa mimi kupiga picha na kurekodi video.
Lakini kwa sasa FURAHIA TASWIRA HIZI HAPA CHINI
Ndimi mimi ndani ya cockpit ya C-17. Yaani ile phobia aliyoizungumkia Kaka Mtondo HAPA na HAPA ndiyo ilikuwa kinikwaza. Ndege imetulia wala haijawashwa lakini bado ni mtetemeko
Mzee huyu alikuwa rubani wa vita ya pili ya dunia. Ana story huyooooooooooo.
Watu woote "macho juu"
Kisha ikaja "main event" ya Blue angel.
Hii "ndude" ni hatari. Inapiga "rivasi" hewani na kusonga kipembeni pembeni. Inatua na kuondoka wimawima. Iangalie hapa chini.

Hii JETCAR hapo juu nayo ilinogesha maonesho. Inakimbizana na ndege.
Ona ilivyokuwa imeachwa hapa
Halafu ilivyo-catch up hapa. Kumbuka gari ilianza 0mph wakati ndege ilishakuwa kwenye mwendokasi
Hii ilikuwa timu ya GEICO. Nayo ilinogesha
Na hii ndio C-17. Ndege yenye uwezo wa ku-taxi kinyume nyume na kuruka kwenye runway fupi saana. Angalia mwanzo mwanzo wa video hapa chini

Wednesday, May 12, 2010

Shule Shule Shule... Twafunzwa tufunzapo

Nimekuwa "nikihubiri" kuhusu SHULE hii tuiitayo blogu. Ambayo katika kila uandikalo, kuna uandikiwalo ambalo litakuwa na uelimishaji kwa kila mwenye mtazamo chanya. Na kuna wanaojitolea kuelimisha wakiwa wanaficha utambulisho wao, na wengine wanakuja wazi kuelimisha kile wanachoamini na kukielimisha kwa nguvu zote.
Na leo napenda kuleta maoni ya Kaka Evarist Chahali aliyotoa kwenye ileeee mada niliyoandika kuwa Blog zetu na "maradhi" ya Bongo flava (irejee hapa).
Kaka Chahali anaelimisha na kuendeleza mjadala akisema
"Naomba kukupongeza kwa uchambuzi huu makini.Pamoja na pongezi hizo,naomba uniruhusu kutofautiana nawe japo kidogo.Kwa mtizamo wangu (unaoweza kuwa si sahihi) lengo la kuanzisha blogu linabaki kuwa miliki ya bloga husika.Kwa mantiki hiyo,bloga anaendelea kuwa na haki na uhuru wa kuendeleza maudhui ya awali ya kuanzisha blogu yake kama ambavyo anavyokuwa na uhuru wa kubadilika kulingana na sababu mbalimbali (kwa mfano kwenda na wakati,kutanua hadhira,nk).Blogu si Biblia au Koran kwamba kubadili cbochote ni kukufuru.
Pia,tunaweza kuwa hatuwatendei haki bloga 'wanaoendeshwa na kusaka umaarufu,au 'wanaoiga'au 'wanaokurupuka',nk kwa vile kile tunachoita kusaka umaarufu,kuiga au kukurupuka kinaweza kabisa kuwa ni sehemu ya ubunifu wao.Na katika 'kuiga' huko inawezekana wanachofanya ni kufuata mkondo wa vinara wa fani.Tunashuhudia kwenye soka,kwa mfano,wanasoka chipukizi wanavyojitahidi 'kuiga' idols wao kama Beckham,Messi,nk.Kama 'kuiga' huko kunaweza kuzaa maendeleo basi nadhani ni jambo jema.Kumuiga mzee wa changamoto ili nami niweze kuitumikia jamii kiufanisi au haya nikidhi tu mapendezeo yangu si jambo baya (kwa mtizamo wangu).
Halafu,ninahofu kuwa bloga 'wageni'au'wachanga' wanaweza kutuona hatuwatendei haki 'kwa kuhukumu kazi zao'.Wanaweza kujiuliza tumepata wapi mamlaka ya kuunda vigezo vya ubora wa blogu (kwa kuzingatia mazingira yetu).
Sambamba na hilo ni swali nililowahi kujiuliza huko nyuma: tunablogu kwa ajili ya jamii au kwa ajili yetu?Jamii ni mkusanyiko wa watu wenye akili,upeo,ladha na matamanio tofauti,na kwa hali hiyo ni vigumu 'kuiridhisha' yote.Nafsi,kwa.upande.mwingine,ni moja.Ni mimi au wewe au yeye.U-moja huu unarahisisha kuridhika.Ni rahisi kuridhisha nafsi yangu kuliko ya mtu mwengine au kundi.Kwa.mtizamo wangu,alimradi bloga 'hachafui hali ya hewa' basi anaweza kufanya 'ile kitu roho yake inapenda' iwe ni kufuata nyayo ( 'kuiga') nguli wa fani au 'kuja kivyake'.
Binafsi sina tatizo na kukopi na kupasti alimradi huyo 'mkopaji' anaweka angalizo kuwa alichoweka hapo ni kwa mujibu wa au hisani ya flani.Hivi magazeti,radio na televisheni si ndio wanaongoza kwa kukopi habari?Na si kwamba kila mara wanafanya hivyo kwa kupenda bali habari zao nyingi hupatikana kutoka chanzo kimoja,hususan 'wire services'.Si ajabu kukutana na Habari kutoka Reuters au AFP ikiwa kama ilivyo kwenye magazeti,tv,redio na tovuti mbalimbali duniani.Sanasana itakuwa imeongezwa maneno mawili matatu au picha.Nafahamu kuwa neno linalotumika ni subscription lakini kimsingi ni copy and paste.
Tukumbuke kuwa si kila anayeanzisha blogu anataka kuelimisha,kuhabarisha,kuburudisha au kukosoa.Kwa vile kimsingi blogu ni mithili ya personal diary japo kwa mazowea tu inatarajiwa kuwa kama chombo cha habari basi kilicjomo humo kinategemea zaidi matakwa ya mmiliki kuliko sisi 'tunaoamua wenyewe kutembelea diary husika' (pengine diary si neno mwafaka lakini nadhani nimeeleweka).Kama kilichomo humo hakiendani na ladha,matarajio au matakwa yetu,tunaachana na diary hiyo.
Nimalizie kwa changamoto ndogo.Ukitafuta blogu zinazojihusisha na teknolojia ya android,kisha ukatembelea japo 20 tu,naamini utaafikiana nami kuwa exclusive content kwenye chapisho ina ugumu."

Sunday, May 2, 2010

Kwaheri ya Christiane Amanpour

Christiane Amanpour ni kati ya waandishi makini wa nje ya Afrika ambao wamekuwa CHACHU ya habari maishani mwangu. Nimekuwa nikimfuatilia saaana na kwa muda mrefu na UJASIRI WAKE (hasa wa kuripoti toka maeneo ya vita) ulinifanya nigande kuiangalia CNN kila wakati nikitaraji kumuona akifanya kazi. Na sasa ameondoka CNN baada ya kuwa nao kwa miaka 27.
Kuna waliosema watam-miss lakini nadhani mimi si mmoja wao. Nitaendelea kumuangalia huko ABC alikohamia na kwa hakika ataendelea kutuletea habari kamili na sahihi kama alivyofanya akiwa CNN
Mtazame katika kipindi chake cha mwisho alipoaga

Changamoto's day out

Mbele ya Landing Gear ya Airbus A330 na mbele yake ni moja ya ndege za Concorde ambazo zilistaafishwa na sasa iko makumbushoni.
Amani, Heshima na Upendo kwenu waungwana nyote.
Kwanza niwaombe radhi kwa kushindwa kuonekana hapa tangu Alhamis. Ni pilika za maisha tuuuu ambazi zilinisonga kwa siku za Ijumaa, Jumamosi na sasa Jumapili nimepata ahueni. Kwa maana hiyo vipengele vya Them' I & Them na Waliwaza nini havikuweza kuwepo wiki hii. Lakini kuna sababu.
Nilikuwa nashughulikia pilika kadhaa zilizonipeleka mpaka kwenye MAKUMBUSHO MBALIMBALI hapa DC Metro.
Makumbusho hayo yalinifanya nishangae namna ambavyo wenzetu hawa wamekuwa makini kwenye kutunza vile vya kale ambavyo si tu sehemu kubwa ya utalii, bali pia kuwawezesha wajao (watoto na vizazi vijavyo) kujua na kuheshimu walikotoka na hata kuthamini mchango mzima wa waliowafikisha hapo kwa kuangalia walikopitia na walivyopitia mpaka kusika hapo walipo.
Kwetu (Tanzania) ni tofauti saana. Niliwahi kuandika PALE SERIKALI INAPOCHOCHEA UJINGA (hapa) na nazidi kuamini katika hilo kwa kuangalia juhudi za serikali za wenzetu kutunza asili yao ilhali sisi twaikimbia yetu kuwaiga wao (na hatuna dalili ya kufika kwenye u-wao licha ya kuwa tumeshaupoteza u-sisi)
Na wacha niungane nanyi katika taswira hizi za vituo cha makumbusho ya Taifa ya mambo ya anga vya Steven F. Udvar-Hazy na The National Air and Space Museum on the National Mall
Concorde; Max Speed 2.04 Mach 2179 km/h Boeing B-29; "the primary aircraft in the American firebombing campaign against the Empire of Japan in the final months of World War II, and carried the atomic bombs that destroyed Hiroshima and Nagasaki." Lockheed SR-71 Blackbird; "THE FASTEST AIR BREATHING, MANNED JET PLANES IN THE WORLD"
Boeing 707; "served 18 years as a flying test laboratory before it was turned over to the Smithsonian Air and Space Museum in May 1972."

Soma maelezo yake juu.
The Space Shuttle Enterprise (NASA Orbiter Vehicle Designation: OV-101); The first Space Shuttle orbiter. Soma mwenyewe hilo "dubwana" ni nini. Niliposoma maelezo yake nikashituka..

Tuesday, March 30, 2010

Robo mwaka inakatika....Tumesonga mbele ama nyuma???

Amani, Heshima na Upendo kwa wana-blog wote.
Kwanza namshukuru MUNGU kwa baraka ya uhai ambayo mimi nawe tunayo.
Pili nikupe pole kwa harakati za maisha ambazo sote twazipitia kufanikisha yale mema tupendayo.
Nafurahi kuwasiliana na kila mmoja wetu kuweza kuwaza changamoto zilizo mbele yetu kama JAMII YA WANA-BLOG wenye lengo la kuigusa jamii na kisha tujiulize kama tunasonga mbele ama nyuma katika harakati zetu. Nashukuru kwa blogs na tovuti mpya ambazo zinachipuka na kuendeleza nia njema ya kuigusa jamii. Kaka Luta Kamala aliwahi kuandika akijuliza KWANINI TUNA-BLOG? (Bofya hapa) na hata Kaka Chambi Chachage aliuliza kama uwepo wa blogu zetu unakuza ama kufifisha tasnia nzima ya uandishi (Ipitie hapa). Jibu halisi tunalo mioyoni mwetu kulingana na dhamira tulizonazo.
Lakini kwa ujumla, haijalishi ni sababu gani ilikufanya u-blog, mwisho wa safari sote tunajikuta na zao moja ambalo ni JAMII. Awekaye picha anataka kuionesha jamii alichokiona, ahabarishaye anataka kuihabarisha jamii. Yule aandikaye Utambuzi anataka jamii ijitambue. Anayeweka kumbukumbu ni sababu anataka jamii ije isome baadaye. Atangazaye biashara anataka jamii ijue ilipo huduma. Afunzaye mapishi, mitandao, mavwazi, mitindo nk, woote wanalenga katika kuielimisha jamii.
Kwa maana nyingine sote twaiandikia JAMII.
Lakini je, mwaka huu ambao unamaliza robo yake ya kwanza wiki hii unaonekana kuwa hatua gani kwetu? Tumeshuhudia KUTHAMINIKA KWA KAZI ZA BLOGGERS kwa aina mbalimbali.
Tuliona wenzetu wakitunukiwa vyeti vya kuthamini kazi zao, tumesikia wengine (kupitia utambulisho wa blog zao) wamepata nafasi ya kushiriki vipindi vya idhaa za kimataifa kufanya uchambuzi wa habari. Hivi juzi tumemuona Kaka Michuzi akishiriki Diaspora huko London kwa nafasi yake kama blogger. Hizi ni chachu kwetu kuwa kuna kuonekana mchango wa kile tufanyacho na pia kuna kukua kwa ueleweka wa kazi zetu.
Ninalowaza ni VIPI TUNAWEZA KUWEKA NGUVU NA JITIHADA ZETU PAMOJA KUWEZA KUITUMIKIA VEMA JAMII?
Mafanikio ya blogger mmoja mmoja yanaweza kudhihirisha kuwa TUNAWEZA na tunalostahili kufanya ni kushirikiana na kuwa makini katika kila jema tutendalo.

Tunapoianza robo ya pili ya mwaka 2010, tuangalie nyuma na kujiuliza, robo ya mwaka inakatika....Tumesonga mbele ama nyuma??


Na hii iwe CHANGAMOTO YETU sote

Baraka kwenu nyote

Tuesday, March 16, 2010

ASANTE Dk. KINASHA... MAISHA MEMA UYAANZAYO SASA

Dr Abednego Kinasha (kati) ambaye alikuwa Rais wa The College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA) akiwa na Makamu Rais wa The Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI) Profesa Frank Keane (shoto) na Rais wa The Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI) Profesa Gerald O'Sullivan katika picha hii ya Mei 8, 2008.
Image from RCSI.IE
Nilipofunzwa somo la UJASIRIAMALI chuoni Dodoma, nilifunzwa sababu kuu tatu za kufanya kazi ambazo ni SABABU ZA KIUCHUMI ambazo ni kwa zile kazi ambazo wafanyao wanafanya ili kupata pesa hata kama hawapendi wafanyalo. Pia kuna SABABU ZA KIJIOGRAFIA ambazo ni kwa wale ambao wanapenda kusafiri na kupanua uwigo wao wa ulimwengu ikiwa ni pamoja na kazi zihusishazo kusafiri. Kisha kuna SABABU ZA KI-UTU ambazo huusisha watu ambao WANAFANYA KAZI ZA WITO na kwa hakika wafanyalo ni huduma zaidi ya kile walipwacho. Ndipo hapa tukutapo waalimu, waokozi / zimamoto na hata madaktari na wauguzi.
Ugumu wa elimu juu ya kazi na nia za watu kufanya kazi ni kuwa mwenye nia yoyote kati hizo tatu anaweza kuwa popote kwa sababu yoyote, na namna pekee ya kujua ama kuona nani anafanya kazi kwa nia gani ni kwa kumuona akitenda kazi hiyo.
Nami maishani mwangu nilibahatika kumuona Dr Kinasha akitenda kazi ya wito.
Kwa wanaofuatilia hapa wanakumbuka post yangu ndeefu ya Desemba 22 2009 iliyokuwa na kichwa cha habari MIAKA 10 BAADAE (Loooong Personal story) Isome hapa ambayo ilizungumzia ajali niliyopata. Katika post hiyo nikazungumzia juu ya msaada nilioupata toka kwa Dada ambaye nikingali natafuta mawasilianao naye, Dada Renatha Benedicto.
Ambalo sikuendeleza kwenye habari hii, ni kuhusu matibabu ambayo nilianza kuyapata kutibu mgongo wangu. Nakumbuka nikiwa chuoni Dodoma mwanzoni mwa mwaka 2000, nilipata maumivu makali saana ya mgongo kiasi cha kushindwa kutembea na nilihofia maisha yajayo kwa kuwa sikuwa na imani kama kuna siku ningeondokana na maumivu yale. Nilipopata nafuu nilirejeshwa nyumbani kwa matibabu. Ni hapo nilipopelekwa Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) na kuonwa na Dk Abednego Kinasha.
Nilitibiwa na Dk Kinasha na Dk Ismail Shariff (kwa sisi wagonjwa tupendao kujimilikisha twasema "ndio wakawa madaktari wangu") kwa muda wote niliohudhuria pale na hata nilipokuwa narejea likizo niliendelea kuangaliwa nao.
Lakini licha ya kunitibu, Dk Kinasha na Dk Shariff waliendelea kufuatiia maendeleo yangu hata nilipokuwa nje ya Dar wakiuliza ndugu waliokuwa na mawasiliano juu ya maendeleo ya mgongo wangu.
HAPO NDIPO UJUAPO KUWA KUTIBU NI ZAIDI YA KAZI KWAO.... NI WITO.
Nimekuwa na maumivu haya kwa muda mrefu lakini sasa niko vema. Na natambua kuwa haijalishi ningepata Daktari bingwa wa vipi huku nilipo, kama Dk Kinasha na Dk Shariff wasingefanya lililo sahihi, basi pengine sasa hivi nisingekuwa na uwezo wa kusogeza mwili wangu bila msaada wa mtu. Ni usahihi wa matibabu ya awali walionipa ambao umenifanya niendelee kuwa nilivyo sasa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, nilizungumza na Dadangu ambaye alinitaarifu kustaafu kwa Dr Kinasha. Ilikuwa ni HISIA MCHANGANYIKO. Zile za kufurahi kuwa anaenda kupumzika baada ya utumishi wa miaka mingi. Lakini pia kukawa na hisia za kuwafikiria mamia ya wagonjwa ambao watakosa huduma sahihi na ya ukarimu ambayo mimi na wengine wengi tumepata katika kipindi kirefu cha utu na utumishi wa Dr Kinasha. Najua kuwa hata "anapostaafu" bado ataendelea kuwatumikia wengi kama ambavyo aliendelea kunijulia hali hata kama sikuwa Dar kwa matibabu. Ni haya mema ambayo watu wanafanya kama sehemu yao ya maisha ya kila siku, yanayotufanya binadamu kuuona UBINADAMU WA KWELI kama alivyoandika Kakangu Matondo akikumbuka SIKU ALIYOKUTANA NA UBINADAMU WA KWELI PALE MUHIMBILI (isome hapa)
Ni wema huu wa kuwa msikivu, mkarimu, mkweli na mwenye busara aliouonesha Dr Kinasha wakati na baada ya matibabu unaonifanya kuendelea kumuona miongoni mwa HEROES waliopata kugusa maisha yangu. Kama alivyosema Lucky Dube kwenye wimbo wake hapa chini kuwa "Do you see the smile on their faces after you've done what you're doing? Do you see satifaction on their faces, after you have blessed them with your gift. You dont think it's much, but for them it means a WORLD. They wake up in the morning and wish you were there. You don't have to lie to gain their trust"

Leo hii natembea, nakimbia, nacheza na hata kufanya kazi na kulea familia yangu changa kwa kuwa Dk Kinasha alishiriki katika matibabu yangu ya awali.
Nakutakia maisha mema katika "ustaafu" uuanzao Dokta na popote uendapo tambua kuwa NATHAMINI SAANA MCHANGO WAKO.

ASANTE SAANA Dk. KINASHA...NAKUTAKIA MAISHA MEMA UYAANZAYO SASA

Thursday, March 11, 2010

Yaliyofichwa kwa viongozi yalifunuliwa kwa wasanii (II)

Image from NINI TALK
Katika wimbo wake wa War and Crime, LUCKY DUBE alisema "Every where in the world People are fighting for freedom. Nobody knows what is right. Nobody knows what is wrong.......... I'm not saying this because I'm a coward. But I'm thinking of the lives that we lose everytime we fight. Killing innocent people, women and children yeah. Who doesn't know about the government, who doesn't know about the wars going on" Hakuna anayefahamu haya akashangazwa na kinachoendelea sasa ambapo kila upande unaotofautiana na mwenzake unasingizia FREEDOM kama sababu ya kufanya wafanyayo. Hakuna ajuaye aliye na asiye sahihi. Kinachofuata hapo ni kile alichosema Bob Marley katika wimbo wake wa Real Situation aliposema "Check out the real situation, Nation war against nation. Where did it all begin? When will it end? Well, it seems like: total destruction the only solution". Haya yanaendelea kuwa kweli leo hii ikiwa ni karibu miongo 3 tangu Bob afariki. Na mpaka leo twaona namna wale wapiganao wanavyoamini kuwa kuteketeza mali na maisha ya wasio na hatia ni namna ya "kutuma ujumbe" kwa wapinzani "wasicheze nao" Lakini ni kwanini ulimwengu uendelee kuangalia haya na kuhalalisha ukiukwaji huu wa haki za binadamu na hasa watoto? Maxi Priest aliimba akiwaasa viongozi kuwa "Slow down everyone, pay attention, let us reason for awhile. I'm worried about this everyday killing that is turning into style. Don't try to convince its normal, playing with human rights. I Don't know about you but I know its brings tears to my eyes. And I cry for the children, and I pray for them. That someday consciousness will once again. Be the answer to our prayers......
How many more lives do you need for your game? Cause we're counting. How many more mothers will you leave in pain? Cause it's mounting. Could you give me a time or a day, how much longer will we have to wait, will there be sunshine and no trace of crime when I wake? Now I'm tired ".

Dunia ya sasa (kama ambavyo tumeona na kusikia huko Nigeria wiki hii) inatawaliwa na watu ambao wanazidi kusaka njia za ajabu katika kudhihirisha maisha na uwezo wao. Wanaoona sawa kutesa na kuua wenzao ili "kutuma ujumbe kwa maadui zao" na hata "kutesa ndugu zao" ili kudhihirisha "uwezo" wao katika matendo ya kikatili. Ni hapo ambapo hata ZIGGY MARLEY alijiuliza "why we lose ourselves just to find who we are?"
Na hili si tatizo kwa viongozi tu, bali hata wananchi wa kawaida ambao kwa "kisingizio" cha hali ya maisha na mfumo wa kisiasa, wanajikuta wakifanya ukatili na mauaji kwa ndugu na binadamu wenzao. Kisingizio ni "system" ambayo BOB MARLEY alihoji kama twaweza kuiacha itusababishe kuua ndugu zetu aliposema "would you let the system makeyou kill your brotherman?"
Na hawa VINGOZI wa dunia ndio wanaotushangaza kwa namna wanavyopuuza suluhisho la matatizo na kuendelea kuuzunguka kusaka kile wakionacho kama suluhisho ilhali wanaongeza tatizo.
Wanapuuza kuwa kinachokosekana ulimwenguni ni UPENDO baina ya wananchi na ambao kwa sehemu nyingine unachochewa na hawa wajiitao viongozi. Na LUCIANO amewashangaa viongozi hawa kwa kukimbia wanachosema wanasaka na hivyo wanakosa suluhisho. Anasema "i see the leaders of these world keep trying to make this world better place for living, still they just can't understand why is it so hard to do it. I guess the system is just not working, there's too much ism skism, why can't they try something new? It is time we understand.... together we can build a better land ........WHAT WE NEED IS LOVE"
Binafsi natambua kuwa kuna wakati tutakuwa sawia kwani licha ya viongozi hawa kutojali kilio na mateso ya wananchi-wataabika, MUNGU tumwaminiye ATATUFUTA MACHOZI kama asemavyo GRAMPS MORGAN katika wimbo wake WASH THE TEARS hapa chini

HEAVEN HELP US ALL

Tuesday, March 9, 2010

MIAKA 102, na bado anafanya kazi. Tena JAJI

Image and video from Wesley E. Brown Inn of Court
Wapo wanaopanga mipango miiingi ya namna watakavyostaafu wakiwa na miaka 65 (ama zaidi au pungufu kulingana na sheria za mahala husika). Na pengine nami ni mmoja wao.
Lakini wiki moja iliyopita nilikuwa nasoma kuhusu Jaji Wesley E. Brown wa Wichita, Kansas ambaye ana umri wa miaka 102 na bado anafanya kazi. Yasemekana alianza pilika za maisha akiwa na miaka 10 na mpaka sasa hajaonesha nia ya kuacha kazi. Katika HABARI HII, Jaji Brown amesemwa kuwa katika kazi hiyo kwa miaka 48 sasa chini ya maraisi 10 tangu ateuliwe na Rais John F. Kennedy mwaka 1962.
Amesema hajui atafanya nini atakapoacha kazi kwani amekuwa akifanya kazi maisha yake yote.
Kaka Matondo alishaeleza kuhusu KURUHUSU KIZAZI KINACHOMALIZA MUDA WAKE KITUFUNDISHE KABLA HAKIJATOWEKA na pengine wengi tuaweza kujifuza mengi toka kwa Jaji huyu ili tujue ni vipi ameendelea kufanya kazi kwa miaka 40 tangu atakiwe kustaafu?
Tazama Video yake hapa chini ambayo ilirekodiwa na kuoneshwa miaka 3 iliyopita (alipokuwa na miaka 99)
NB: Larry Hatteberg did the following story on Judge Brown when he was just 99 years old. The lead in is by Daryn Kagan.

Video copyright holders Daryn Kagan (introduction) and Larry Hatteberg (feature).

Tuesday, December 22, 2009

MIAKA 10 BAADAE (Loooong Personal story)

Ilikuwa alfajiri ya tarehe 22 Dec mwaka 1999 ambapo niliwahi na kuingia kwenye basi la Tawfiq tayari kwa safari ya kuelekea Bukoba kuonana na wazazi kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. Safari yenyewe ilikuwa ya ghafla mno kwani mwanzo hakukuwa na mabasi (yalishajaa) lakini Tawfiq walipoangalia "UHITAJI" wa wasafiri kwenda Bukoba kupitia Nairobi na Kampala, wakaamua kuongeza basi jingine siku hiyo ya Tarehe 22. Tuliwathamini kwa hili kwani tulijua kuwa wanatujali sisi wateja wao. Ambalo hatukujua ni kuwa basi hilo lingeendeshwa na dereva (inayesemekana alikuwa peke yake) aliyeendesha toka Bukoba mpaka Dar na siku moja baadae angegeuza nasi kuelekea Bukoba.
Nilipofika kwenye gari nikaelekea kwenye kiti changu ambacho kilikuwa namba 3C na ilikuwa ni dirishani. Nilipofika pale nikamkuta Binti mmoja amekaa kwenye kiti hicho cha dirishani. Nikamuomba anipishe nikae lakini aliamini ile ilikuwa seat yake. Ni kweli kuwa ilikuwa ngumu kuzijua kwani namba hazikuandikwa kwenye viti, bali kwenye sehemu ya kuweka mizigo. Na hazikuonesha ipi ni ya dirishani na ipi ya ndani. Binafsi nilikuwa na hakika kwani nilimuomba Kaka Frank Kanjanja ambaye ni "mwenyeji"wa mabasi hayo anitafutie nafasi ya dirishani (Nadhani ilikuwa ni kwa ajili ya kununua nitakacho katika vile vituo vya dk chache). Tulieleweshana na binti huyo na akaelewa. Kisha akasema huwa ana matatizo ya kifua na huhitaji hewa safi hivyo akaomba kama angeweza kukaa dirishani. Nilimhakikishia kuwa atakaa hapo, lakini baada ya basi kuondoka kwani ningependa kuwapungia ndugu walionisindikiza. Kaka wa binti huyo kabla hajashuka aliniomba nimsaidie mdogo wake njiani kwani ni mara yake ya kwanza kusafiri njia hiyo na alikuwa akielekea Bukoba niendapo mimi. SIKUWA NA TAABU NA HILO.
Safari ilianza na baada ya kuagana na ndugu, nilimwacha binti yule akae dirishani. Hakukuwa na matata mpaka tulipofika Namanga. Kukawa na kucheleweshwa kuhusu masuala ya bima na mambo mengine ya ki-miliki ambayo mwenye gari alionekana kutoyatimiza. Tulicheleweshwa hapo kwa takribani masaa 6. Muda huo, dereva wetu ambaye tuliongea machache katika dk za mwanzoni, aliutumia kupumzika. Baadaye tuliruhusiwa. Nikaongozana na mdogo wangu kukamilisha taratibu za UHAMIAJI kama wengine na tulipomaliza hayo safari ilianza na tukafika Nairobi usiku wa manane tukasimama kwa muda kupata mlo. Kama kawaida nilikuwa na "mdogo wangu" wa hiari na tulikuwa tukifurahia safari.
Tuliondoka Nairobi na kuendelea kuchanja mbuga. Basi lilikuwa likienda mwendo wa kasi kuliko maelezo na hakuna aliyeonekana kujali kwani sote tulikuwa tukiamini kuwa dereva alikuwa akijitahidi kufidia yale masaa 6 tuliyochelewa pale Namanga. Kwa hiyo alikuwa akijitahidi tufike muda wa kawaida. Majira ya saa 10 usiku, yule binti alianza kusinzia na kwa kuwa alikuwa na begi la mgongoni, nikamshauri aliweke mapajani kisha ajiegemeze hapo huku kichwa kikiwa kimegusa kiti cha mbele kumpa "sapoti". Alifanya hivyo. Bahati mbaya ni mimi niliyeshindwa kufanya hivyo kwani nililaza kiti changu mpaka mwisho na kusinzia. Muda mfupi baadae niliamshwa na sauti ya break na kisha kishindo kikubwa saana. Pengine kikubwa kuliko chochote nilichowahi kusikia.
Kukawa kimya kwa sekunde kadhaa kisha vikasikika vilio. Nikarejewa na fahamu. Nikajua kuwa tuko ajalini na kwa kuwa nilikuwa dirishani, akili ya kwanza ikawa "ruka kupitia dirishani". Nikachungulia nje na sikuona gari kisha nikafanya hivyo. Nilipofika nje nikatua sentimita chache toka ulipo mwili wa dereva. Sikuamini nilichokiona. Alikuwa ameharibika kichwa tu na kwingine kote alikuwa sawa. Ni mtu ambaye tuliongea Nairobi (huwa napenda saana kuhojiana na waendesha vyombo kujua hisia zao wanapochukua dhamana ya roho zote hizo) na sasa uso haukuwa ukitambulika. Kichwa kilisagika saana na kingeweza kufunikwa na viganja vyangu viwili. Niliangalia saa yake ikaonesha saa 11 alfajiri. Sikuwahi kuona maiti iliyoharibiwa kichwa namna ile. Niliogopa saaana. Nikajaribu kuzunguka kuona kama kuna mtu mwingine pale nje. HAKUWEPO!! Niliogopa zaidi. Nilitamani kurejea ndani lakini dirisha lilikuwa juu sana. Na nilipoangalia mazingira, tulikuwa kwenye nyika. Nikaogopa kuhusu wanyama. Nikasikia sauti ya mtu akitaka nimsaidia kumpokea mtoto ili naye ashuke dirishani kwani gari tuliloonga liliingia mpaka kwenye mlango na kuuziba. Na injini ilipasuka na kutoa mvuke wa dizeli na mchanganyiko wa dizeli na damu vilivyoimwagikia injini na kuungua viliweka harufu mbaaya sana ambayo mpaka sasa huwa naihisi (wakati mwingine). Nilimpokea yule mama mtoto na kisha kuanza kushusha watu wengine. Hii ilikuwa na unafuu kwangu kwani nilipata watu wa kukaa nao pale chini na uoga ulianza kunitoka.
Baada ya muda yakaanza kupita magari ambayo yalisimama na kuchukua abiria waliokuwa tayari kwenda hospitali. Sikuwa na maumivu hivyo niliamini kuwa niko sahihi. Nilisaidia waliokuwa wanataka kwenda hospitali na kusubiri utaratibu wa kupata mabegi yetu. "Mdogo wangu" hakuwa ameumia sana. Alikuwa na ka-mchubuko kidooogo kwenye uso. Akanisihi niende hospitali lakini nilimpuuzia nikidhani ni "ukosefu wa uzoefu wa kusaifiri, usichana na utoto" vinavyomfanya aogope. Nilimhakikishia kuwa niko Ok japo hakunielewa. Da Mdogo alikuwa akiniona nami sikuwa nikijiona. Baada ya muda mfupi nikashangaa kuona karibu kila mtu ananiangalia mimi na nikigeuka kuwaangalia wanajiangaliza pembeni. Nikaenda kumfuata mdogo wangu kumuuliza kulikoni lakini nilipomuona nilishindwa kuongea. Nikajaribu tena na tena nikashindwa. Nikaanza kuhisi maumivu na kitu cha ziada mdomoni. Aliponiona akanisihi niende hospitali, lakini nikaenda kwenye kioo cha gari la polisi kuachama niangalie kilichopo mdomoni. Nilipofika hapo ndio nikagundua kuwa nilikuwa kwenye hali mbaya. NILIKUWA NIMEKATIKA ULIMI, NIMECHANIKA UFIZI, SEHEMU YA TAYA, NIMEPASUKA JUU YA JICHO LA KULIA, CHINI YA LIPS MARA MBILI NA JICHO LILIKUWA LIMEFUNGA NA USO UMEVIMBA.
Nilikaa chini na hapo nilikuwa tayari kwenda hospitali. Da Mdogo akamueleza askari ambaye ndiye alikuwa amefika kuwa "kakake" amekaa nyuma ya basi na ana majeraha na maumivu. Baada ya kuniona, askari akasema gari lolote litakalofuata ataliamuru linipeleke NAKURU PROVINCIAL HOSPITAL. Bahati mbaya lililotokea lilikuwa ni lori (semi-trailer). Nikapakizwa humo na "mdogo wangu" na safari kuelekea hospitali ikaanza. Kwa bahati mbaya, (kwa mujibu wa dereva wa lori) sheria ya barabarani ya Kenya haiwaruhusu wenye magari ya mizigo kuingia pale, hivyo akatushushia ilipo "short cut" ambayo ilikuwa inakatisha makaburini. Tukatembea mwendo kiasi na kufika Hospitali.
Tulipokelewa kwa haraka na kupewa matibabu ya awali. Hawakusubiri utaratibu wa kawaida katika kuandikisha, hivyo kila karatasi ilifaa kuwa cheti cha matibabu. Nilishuhudia Daktari aliyekuwa "off" siku hiyo akija na pyjama kusaidia baada ya kusikia habari za ajali. Hilo lilinonesha alivyo na wito na kazi / hudumayake. Wakati nasubiri kupelekwa chumba cha upasuaji, ilipitishwa miili kadhaa kati ya tuliokuwa nao ambao kwa bahati mbaya walifariki. Mpaka wakati huo, namba ya waliofariki tuliyoambiwa ilikuwa 15. Niliingizwa kushonwa ulimi (sikuwahi kusikia kabla na sijawahi kusikia baada ya hapo) na shughuli nzima ilichukua masaa mawili. Mizigo yangu yote alikuwa nayo Da Mdogo na kwa muda huo niliokuwa huko, watu walizidi kupoteza maisha. Hakujua nilipo, hakujua waliokufa baada ya hapo ni kina nani, na hakujua mimi ni nani, na ndugu zangu ni kina nani na mizigo yangu angeifanyia nini. Nilipotoka kwenye upasuaji nikakutana na Mama mmoja ambaye alisema mdogo wangu alikuwa akinitafuta na hakujua nilikuwa wapi. Sikushangaa kwani nilihamishwa vyumba vya upasuaji kama viwili. Alifurahi kuniona na ndipo tuaulizana majina na contact zozote "in case". Ndipo nilipomjua RENATHA BENEDICTO. Binti aliyekuja kuwa sauti yangu kwa muda wote uliosalia wa safari. Tulipelekwa kuoneshwa wodi na zilisikitisha. Nilimwandikia Renatha kuwa mama ni nurse na tungeweza kuendelea na safari. Akafanikiwa kuwashawishi wauguzi kuwa mwendo wa Nakuru-Bukoba ingekuwa Ok kama wangenifunga bandeji ya kutosha. Wakafanya hivyo naye akaenda kunitafutia kimiminika cha kula pamoja na dawa ya maumivu kwani ganzi ilianza kuisha na nilianza kusikia maumivu kila nilipochomwa.

Tukaenda Polisi na kupewa fomu za kujaza (PF3), kuchukua mabegi yetu toka kwenye basi ambalo lilikuwa limewekwa hapo na kisha tukapakiwa kwenye basi jingine la Tawfiq kuelekea nyumbani. Basi LILIKUWA LIMEPWAYA SAANA KWANI ZAIDI YA WATU 20 TULIOKUWA NAO KWENYE BASI LA AWALI HAWAKUWA NASI.

Tulianza safari na tulipata huduma nzuri saana mpakani mwa Kenya na Uganda kisha kuingia Tanzania. Safari yetu ikawa salama na tukafika Bukoba Mjini jioni ya tarehe 24 Dec.
Umati uliokuwa ukisubiri ulikuwa mkubwa na nilikuja kuambiwa kuwa wengi hawakujua nani kapoteza maisha, nani kapona na kama basi lingekuja na miili ya marehemu ama la.

Basi liliposimama Mama mmoja aliomba tufanye sala ya pamoja kumshukuru Mungu kwa kutunusuru na ajali ile mbaya na kuwaombea wenzetu waliotangulia mbela ya haki. TUKAFANYA HIVYO

Kisha mlango ukafunguliwa na tukashuka. Tulipokelewa na ndugu na binafsi kumuona Mamangu ilinipa faraja sana. Ni yeye pekee aliyekuwa amebaki mjini kwani familia nzima ilishaenda kijijini kwa ajili ya XMass na yeye alitakiwa aondoke nami.

Niliagana na Da Mdogo na msaidizi wangu mkuu na wa hiari Renatha na kuahidiana kutafutana baada ya kufika Dar.

Niliwasiliana naye mpaka mwaka 2002 alipoenda Chuo cha Ualimu Songea ambapo hatujaweza kuwasiliana mpaka sasa. Na ndio maana mpaka leo hii NAMSAKA RENATHA BENEDICTO
Namshukuru Mungu kwa miaka kumi niliyoongeza. Nimepitia mikononi mwa watabibu wengi na shukrani zangu kwa Dr Abdnego Kinasha na Dr Ismail wa taasisi ya mifupa MOI kwa matibabu yao, wafanyakazi wa kitengo cha mazoezi Muhimbili na MOI na wote walioweka mikono yao kwenye kunitibu.
Nimekuwa katika maumivu ya mgongo kwa miaka 10 sasa na nimepitia kila aina ya matibabu iliyoonekana kuwa na uwezekano wa kunipa nafuu na licha ya hayo yote, bado namshukuru Mungu kwa uhai.
Nawashukuru WAZAZI NA WALEZI ambao wamekuwa pamoja nami kila siku kuhakikisha niko sawasawa.
Na namshukuru msaidizi wangu, penzi na mzazi mwenzangu Esther ambaye tangu mwaka 2001 amekuwa akikumbusha juu ya umuhimu wa njia sahihi za kupunguza maumivu na kujali mgongo.
Ni miaka 10 sasa ya maumivu yangi, lakini KINACHOSIKITISHA NI KUWA HAKUNA HATUA ZA MAKUSUDI NA MAKINI ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI YETU KUHAKIKISHA KUWA WENGINE WENGI HAWAPOTEZI MAISHA YAO AMA KUWA NA MAUMIVU KAMA NILIYONAYO MIMI.
Takwimu zasikitisha na zaonesha kuwa ajali ni kati ya vinavyotuua zaidi na TANZANIA TUNA BARABARA ZIUAZO ZAIDI ULIMWENGUNI kama ambavyo ilinukuliwa HAPA

NI MIAKA 10 BAADAE. BADO NATOA SIFA NA SHUKRANI KWA MUNGU KWA UHAI NA WOTE WEMA WALIO HAI

Friday, December 18, 2009

Kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa

Toka malezi mpaka makuzi. Na sasa mapenzi na kuelekea malezi tena. Kama Kakangu Kamala ni mtu wa kwenda na wakati, basi masaa 61 toka sasa atakuwa anaanza hatua mpya ya maisha. Hatua ya kuondoka katika hadhi ya u-mimi na kuingia kwenye hadhi ya u-sisi. Atakuwa anaungana na wake wa moyo katika ndoa itakayofungwa ndani ya moja kati ya sharika za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri hapo jijini Dar. HONGERA (in advance) KWA WOTE.
Lakini kabla hajawa nusu ya alivyo sasa ili kuungana na nusu nyingine kuwa kitu kimoja, napenda kumzungumzia Kamala huyu wa sasa anapoelekea "countdown" ya ndoa yake
Labda ukitaka kumjua zaidi waweza kuSOMA HISTORIA YAKE na naamini hilo laweza kukusaidia kujua ni kwanini yuko alivyo ama kwanini anena anenavyo. Lakini hakuna ubishi kuwa kuna mengi mema ya kuangalia, kusoma na kujifunza kuhusu Kamala.
Kaka huyu amekuwa mstari wa mbele katika kutetea watoto na mara kadhaa amekuwa wazi kusema anavyowapenda watoto .
Na amekuwa wazi kuwa ana mapenzi na watoto kutokana na historia ya maisha yake. Kwa waliyoisoma wanaweza KUSIKITIKA kwa maisha ya utoto aliyopitia lakini bado naendelea kuamini kuwa alipewa hayo kwa kuwa Mungu alijua kuwa ataweza kuhimili na kuinuka na kisha kuwa USHUHUDA KWA WENGI. Twaambiwa "JAH WILL NEVER GIVE US MORE THAN WE CAN BEAR". Namna ambavyo Kaka Kamala ameweza kubadili huzuni kuwa ushuhuda ndicho kitu kikubwa ninachojivunia kwake. Kamala ameweza kugeuza kilio cha wengi kuwa faraja kwa wengi. Ameonesha njia kwa maisha aliyopitia na sasa amekuwa kama mtetezi na mwelimishaji kwa jamii. Nilipokutana na Kamala Dec '07.
"Kapera" huyu anayeelekea kumaliza kipindi chake cha u-moja, anapenda saana kuzungumza kile aaminicho. Na aaminicho husemwa kwa kujali zaidi mantiki kuliko "urembo" wa kisemwacho. Wanaopata tabu na maoni yake ni wale wasiomfahamu. Binafsi nilibahatika kumuona, kumsikia na kuongea naye japo kwa ufupi. Kama ilivyo kwa wengi, Kamala huandika kama anavyoongea na kama hujui ama huwezi ku-imagine uoneaji wake, lazima utapata taabu kutafsiri. Lakini dawa ni kufanya nilivyowahi kusema kuwa jikite kwenye "point of view" ya maoni yake kuliko "tone" ya maandishi yake.
Na sasa Kakangu huyu anaelekea kuwa Mume na twataraji awe Baba. Well!! Kuwa Mume na U-baba vyaja na vyeo vingine lukuki kama ushemeji, ujomba na menginenyo mengi. Na najua kuwa kwa kutumia uzoefu wa maisha alioshirikiana nasi hapa na kwenye vibaraza vyetu mbalimbali, kuna mengi ambayo JAMII inaelekea kupata toka katika FAMILIA hii mpya.
Na ndio maana nimeona leo ni vema nikaandika namna nijivuniavyo kuhusu Kamala. Kutoka mabadiliko ya malezi yake mpaka alivyoyabadili na kukua kwa mtazamo chanya na sasa anapoelekea kwenye mapenzi yanayotegemewa kuleta malezi kwa jamii nyingine.
Kila la kheri kwa Kaka Kamala na familia-tarajiwa nziiima na nawatakia kila lililo jema katika yale mema mtendayo.
Blessings