Tuesday, December 15, 2009

Mzee Jerome Danford Kassembe......Chachu nyingine katika fani

Ilikuwa ni katikati ya mwaka 2004 nikiwa pale Americana Grocery iliyoko Bladensburg, Maryland nikifanya manunuzi ya vyakula na mwenzangu ambapo tukiwa katika "section" ya maharagwe tukawa tunajadiliana kati ya aina zilizopo ni ipi yenye "rojo" kama ya nyumbani. Tulikuwa tukizungumza kiswahili na ghafla nikasikia mtu akitusalimu kwa kiswahili na kusema ametusikia tukiongea kiswahili na kutambua kuwa tulikuwa tukitoka nchi moja.
Ilikuwa ni mshtuko wa furaha na tulisalimiana na kujitambulisha na alipojitambulisha yeye ndipo nilipogundua kuwa aliyesimama mbele yangu alikuwa si mwingine bali ni Mzee Jerome Danford Kassembe. Mtangazaji ambaye kwa miaka mingi nimekuwa nikimsikia "akiunguruma" kupitia IDHAA YA KISWAHILI YA SAUTI YA AMERIKA hapa Washington DC. Nilijitahidi kuwa mtulivu (maana nilishazidiwa na furaha) lakini sikutaka kumuacha aondoke bila kujua kuwa utangazaji ni kati ya vitu ninavyopenda saaana na ningependa kujua wao wanafanyaje. Akasema wala hilo halikuwa tatizo na akanipa kadi yake na pia namba ya simu ya ziada na kuniambia siku yoyote nitakayopanga kwenda basi nimjulishe ili awe mwenyeji wangu. HIYO ILIKUWA KAMA TIMIO LA NDOTO KWANGU. Ziara ya kwanza VOA. Toka kushoto ni Mr Kassembe, Mr Mwamoyo Hamza, Mr Emmanuel Muganda, mimi, Mr Vincent Makori na Mr Aboudshakur Aboud

Nikajipangapanga na nilipogundua siku ambayo nilikuwa siendi kazini nikampigia simu na kupanga kwenda. Hii ilikuwa kati ya safari mwanana saana kuzifanya hapa DC.
Alinipokea, akanitambulisha kwa wafanyakazi wa Idhaa yao na kunitembeza kiasi kuangalia jengo lao lenye studio nyingi zitangazazo habari katika lugha 45 ulimwenguni. Nilijifunza mengi na baada ya yeye kufungua mlango, nilianza kuiona tena ndoto ya kurejea nyuma ya microphone ikielekea kutimia.
Ni mwaka huohuo wa 2004 Mzee Kassembe alinifanyia mahojiano punde baada ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Rais hapa Marekani ambayo yalisikika katika idhaa hiyo ya kiswahili. Yalikuwa ni mahojiano mazuri pia.

Ziara ya Pili VOA. Da Mary, mdau, Uncle Abdoushakur Aboud mimi na aliyekuwa mkuu wa Idhaa Mzee Emmanuel Muganda
Ndani ya studio na Abdoushakur Aboud na Vincent Makori
Lakini kubwa ninalopenda kumshukuru Mzee Kassembe ni kuniwezesha kuunganika na wana VOA ambao hata baada ya kustaafu kwake, nimeweza kutembelea kituo hicho na kupokelewa vema, nimeendelea kukaribisha siku yoyote nitakapokuwa na nafasi na sasa hata nikutanapo na wanaVOA najiona kama mmoja wa wanafamilia.
Mzee Kassembe, mimi na mkuu wa Idhaa ya Kiswahili VOA Dr Mwamoyo Hamza
Nikiwa na wanahabari Sunday Shomary, Mzee Kasembe na Mobhare Matinyi
Ni mambo madogo kama ziara na kuongea na watu wakuangaliao kama "mfano wa kuigwa" (role model) kunakoweza kurejesha ARI na MATUMAINI waliyopoteza. Kwangu kukutana na kupata muda na Mzee Kassembe ilikuwa CHACHU NYINGINE KATIKA FANI NIIPENDAYO SAAANA......FANI YA UTANGAZAJI
ASANTE SAANA MZEE KASSEMBE

8 comments:

Anonymous said...

Nimependa kuwaona woooooooooooote hasa hao wakuu wa VOA.
Shukrani kwa picha na maelezo murua!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nikiwa mwanafunzi wa sekondari shule ya tweyambe iliyoko kule vijijini nilipenda sana kusikiliza BBC na VOA. nilipenda kipindi cha maswaaaaliiiiiiiiiiii na majbu ambacho kilirushwa jmosi kwa muda mfupi tu. niliwakariri watangazaji na maripota wote.

lakini hata hivyo ilikuwa kinyume cha sheria kusiliza redio shuleni kwetu kwani nakumbuka nilifukuzwa (suspended) kwa kosa la kusikiliza redio, tena taarifa ya habari

Yasinta Ngonyani said...

taswira nzuri pia ni habari nazuri. nasikiliza kila j´mosi na j´pili BBC. Bila hivi siwezi kujua habari za nyumbani. Asante kwa yote.

Mzee wa Changamoto said...

Nashukuru nyote kwa maoni. Binafsi nilifurahi saana kujinafasi ndani ya VOA na kuonana na wakongwe hao waliostaafu (Mzee Kassembe na Mzee Muganda) na wachapakazi wengine.
Kamala uliposema Maswaliiiii na Majibu umenikumbusha mbali sana. Nimekumbuka namna nilivyokuwa nina-tune na kujaribu kujibu maswali kabla haajatoa jibu. Ilinisaidia sana kwani ilikuwa kama "chemsha bongo" (quiz) kwa kuwa maswali mengi yalitokana na habari ambazo walishatangaza.
Lakini pia mfumo wao (vyombo vya kimataifa kama BBC, VOA, Deutsche Welle, nk) wa utangazaji ulikuwa wa kiwango kikubwa na ilivutia kuusikila na bado unavutia licha ya MLIPUKO wa hizi Fm Radios.
Kuhusu kukatazwa kusikiliza redio hilo nalikumbuka na naomba nisitie neno. Kwani ndio TANZANIA YANGU HIYOO...INAYOZIMA MOTO KWA PETROLI.
Mwisho nikukumbushe Kamala....ulikuwa ukimsikiliza Richard Mambombotela wa KBC?
Hahahahaaaaaaaaaaa
Kwa kanda na nyanda za Tweyambe natumai ulimsikiliza na mafunzo yake ya Kiswahili
Blessings

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Jerome Danford Kassembe, Charles Hillary, Julius Nyaisanga, Leonard Mambo Mbotela, Ummy Oumilkheir Hamidu na Tido Mhando ni baadhi ya watangazaji wachache ambao wana/walikuwa na upekee fulani katika utangazaji wao. Kuna kitu fulani ambacho daima kinakufanya utake kuwasikiliza - haidhuru hata kama wanachokitangaza ni matangazo ya vifo. Ni wabobezi katika fani yao.

Mzee wa Changamoto - una "clips" zo zote ukiwa mbele ya maikrofoni? Kama unazo, tuwekee hapa bloguni tukusikie ulivyokuwa ukiunguruma.

Mzee wa Changamoto said...

Kwanza nirekebishe kwenye jina ni Leonard kama alivyosema Kaka Matondo na si Richard.
Kaka Matondo, clips nilizonazo najaribu kuziweka kwenye CD niweze kuzitunza na kuzi-post (kutokana na ombi lako)
Still nilikuwa rookie lakini nikizisikiliza huwa nacheka saaaana. Inafurahisha mno
Lakini nikifanikiwa kuziweka katika CDs ntaziweka hapa
Blessings

Sisulu said...

asante kwa ripoti yenye mashiko. DAIMA MBELE

ROBIN ULIKAYE said...

NAKUONEA WIVU KWA BAHATI YA KUONANA NA JEROME DANFORD KASEMBE, BASI NIKIWA DARASA LA SITA BABA YANGU ALIKUWA AKIFUNGUA SAUTI YA AMERIKA KILA SAA MOJA NA NUSU MIMI SAMBAMBA NAYE,SAUTI NILIYOTAKA KUISIKILIZA ILIKUWA YA JEROME DANFORD KASEMBE, NILIPENDA ALIVYOKUWA AKIJITAMBULISHA KWA KUWEKA MKAZO KTK JINA LAKE, ACHILIA MBALI SAUTI YAKE TAMU KUISIKILIZA,NILIAPA KUWA MTANGAZAJI KWA SABABU YA MVUTO ALIOKUWA NAO KWANGU, NAMPENDA SANA KASEMBE AMEFANYA NDOTO YANGU ITIMIE, BINAFSI NATAMANI SAAANA KUONANA NAYE AU HATA NIPATE MAWASILIANO YAKE JAPO NIMSHUKURU KWA MUNGU KUMTUMIA AWE ROLE MODEL WANGU. MZEE WA CHANGAMOTO BAADA YA KUSTAAFU MZEE JEROME YUKO WAPI UNAJUA? NISAIDIE MAWASILIANO YAKE NATAMANI SANA KUMSHUKURU.NIMESHAKUWA MTANGAZAJI NINA NDOTO ZAIDI NA YEYE AMEHUSIKA SANA, PLZ NITUMIE KTK 0716 676 947 au ushindifm@yahoo.com au Mwawulikaye@yahoo.com