Nilipofika kwenye gari nikaelekea kwenye kiti changu ambacho kilikuwa namba 3C na ilikuwa ni dirishani. Nilipofika pale nikamkuta Binti mmoja amekaa kwenye kiti hicho cha dirishani. Nikamuomba anipishe nikae lakini aliamini ile ilikuwa seat yake. Ni kweli kuwa ilikuwa ngumu kuzijua kwani namba hazikuandikwa kwenye viti, bali kwenye sehemu ya kuweka mizigo. Na hazikuonesha ipi ni ya dirishani na ipi ya ndani. Binafsi nilikuwa na hakika kwani nilimuomba Kaka Frank Kanjanja ambaye ni "mwenyeji"wa mabasi hayo anitafutie nafasi ya dirishani (Nadhani ilikuwa ni kwa ajili ya kununua nitakacho katika vile vituo vya dk chache). Tulieleweshana na binti huyo na akaelewa. Kisha akasema huwa ana matatizo ya kifua na huhitaji hewa safi hivyo akaomba kama angeweza kukaa dirishani. Nilimhakikishia kuwa atakaa hapo, lakini baada ya basi kuondoka kwani ningependa kuwapungia ndugu walionisindikiza. Kaka wa binti huyo kabla hajashuka aliniomba nimsaidie mdogo wake njiani kwani ni mara yake ya kwanza kusafiri njia hiyo na alikuwa akielekea Bukoba niendapo mimi. SIKUWA NA TAABU NA HILO.
Safari ilianza na baada ya kuagana na ndugu, nilimwacha binti yule akae dirishani. Hakukuwa na matata mpaka tulipofika Namanga. Kukawa na kucheleweshwa kuhusu masuala ya bima na mambo mengine ya ki-miliki ambayo mwenye gari alionekana kutoyatimiza. Tulicheleweshwa hapo kwa takribani masaa 6. Muda huo, dereva wetu ambaye tuliongea machache katika dk za mwanzoni, aliutumia kupumzika. Baadaye tuliruhusiwa. Nikaongozana na mdogo wangu kukamilisha taratibu za UHAMIAJI kama wengine na tulipomaliza hayo safari ilianza na tukafika Nairobi usiku wa manane tukasimama kwa muda kupata mlo. Kama kawaida nilikuwa na "mdogo wangu" wa hiari na tulikuwa tukifurahia safari.
Tuliondoka Nairobi na kuendelea kuchanja mbuga. Basi lilikuwa likienda mwendo wa kasi kuliko maelezo na hakuna aliyeonekana kujali kwani sote tulikuwa tukiamini kuwa dereva alikuwa akijitahidi kufidia yale masaa 6 tuliyochelewa pale Namanga. Kwa hiyo alikuwa akijitahidi tufike muda wa kawaida. Majira ya saa 10 usiku, yule binti alianza kusinzia na kwa kuwa alikuwa na begi la mgongoni, nikamshauri aliweke mapajani kisha ajiegemeze hapo huku kichwa kikiwa kimegusa kiti cha mbele kumpa "sapoti". Alifanya hivyo. Bahati mbaya ni mimi niliyeshindwa kufanya hivyo kwani nililaza kiti changu mpaka mwisho na kusinzia. Muda mfupi baadae niliamshwa na sauti ya break na kisha kishindo kikubwa saana. Pengine kikubwa kuliko chochote nilichowahi kusikia.
Kukawa kimya kwa sekunde kadhaa kisha vikasikika vilio. Nikarejewa na fahamu. Nikajua kuwa tuko ajalini na kwa kuwa nilikuwa dirishani, akili ya kwanza ikawa "ruka kupitia dirishani". Nikachungulia nje na sikuona gari kisha nikafanya hivyo. Nilipofika nje nikatua sentimita chache toka ulipo mwili wa dereva. Sikuamini nilichokiona. Alikuwa ameharibika kichwa tu na kwingine kote alikuwa sawa. Ni mtu ambaye tuliongea Nairobi (huwa napenda saana kuhojiana na waendesha vyombo kujua hisia zao wanapochukua dhamana ya roho zote hizo) na sasa uso haukuwa ukitambulika. Kichwa kilisagika saana na kingeweza kufunikwa na viganja vyangu viwili. Niliangalia saa yake ikaonesha saa 11 alfajiri. Sikuwahi kuona maiti iliyoharibiwa kichwa namna ile. Niliogopa saaana. Nikajaribu kuzunguka kuona kama kuna mtu mwingine pale nje. HAKUWEPO!! Niliogopa zaidi. Nilitamani kurejea ndani lakini dirisha lilikuwa juu sana. Na nilipoangalia mazingira, tulikuwa kwenye nyika. Nikaogopa kuhusu wanyama. Nikasikia sauti ya mtu akitaka nimsaidia kumpokea mtoto ili naye ashuke dirishani kwani gari tuliloonga liliingia mpaka kwenye mlango na kuuziba. Na injini ilipasuka na kutoa mvuke wa dizeli na mchanganyiko wa dizeli na damu vilivyoimwagikia injini na kuungua viliweka harufu mbaaya sana ambayo mpaka sasa huwa naihisi (wakati mwingine). Nilimpokea yule mama mtoto na kisha kuanza kushusha watu wengine. Hii ilikuwa na unafuu kwangu kwani nilipata watu wa kukaa nao pale chini na uoga ulianza kunitoka.
Baada ya muda yakaanza kupita magari ambayo yalisimama na kuchukua abiria waliokuwa tayari kwenda hospitali. Sikuwa na maumivu hivyo niliamini kuwa niko sahihi. Nilisaidia waliokuwa wanataka kwenda hospitali na kusubiri utaratibu wa kupata mabegi yetu. "Mdogo wangu" hakuwa ameumia sana. Alikuwa na ka-mchubuko kidooogo kwenye uso. Akanisihi niende hospitali lakini nilimpuuzia nikidhani ni "ukosefu wa uzoefu wa kusaifiri, usichana na utoto" vinavyomfanya aogope. Nilimhakikishia kuwa niko Ok japo hakunielewa. Da Mdogo alikuwa akiniona nami sikuwa nikijiona. Baada ya muda mfupi nikashangaa kuona karibu kila mtu ananiangalia mimi na nikigeuka kuwaangalia wanajiangaliza pembeni. Nikaenda kumfuata mdogo wangu kumuuliza kulikoni lakini nilipomuona nilishindwa kuongea. Nikajaribu tena na tena nikashindwa. Nikaanza kuhisi maumivu na kitu cha ziada mdomoni. Aliponiona akanisihi niende hospitali, lakini nikaenda kwenye kioo cha gari la polisi kuachama niangalie kilichopo mdomoni. Nilipofika hapo ndio nikagundua kuwa nilikuwa kwenye hali mbaya. NILIKUWA NIMEKATIKA ULIMI, NIMECHANIKA UFIZI, SEHEMU YA TAYA, NIMEPASUKA JUU YA JICHO LA KULIA, CHINI YA LIPS MARA MBILI NA JICHO LILIKUWA LIMEFUNGA NA USO UMEVIMBA.
Nilikaa chini na hapo nilikuwa tayari kwenda hospitali. Da Mdogo akamueleza askari ambaye ndiye alikuwa amefika kuwa "kakake" amekaa nyuma ya basi na ana majeraha na maumivu. Baada ya kuniona, askari akasema gari lolote litakalofuata ataliamuru linipeleke NAKURU PROVINCIAL HOSPITAL. Bahati mbaya lililotokea lilikuwa ni lori (semi-trailer). Nikapakizwa humo na "mdogo wangu" na safari kuelekea hospitali ikaanza. Kwa bahati mbaya, (kwa mujibu wa dereva wa lori) sheria ya barabarani ya Kenya haiwaruhusu wenye magari ya mizigo kuingia pale, hivyo akatushushia ilipo "short cut" ambayo ilikuwa inakatisha makaburini. Tukatembea mwendo kiasi na kufika Hospitali.
Tulipokelewa kwa haraka na kupewa matibabu ya awali. Hawakusubiri utaratibu wa kawaida katika kuandikisha, hivyo kila karatasi ilifaa kuwa cheti cha matibabu. Nilishuhudia Daktari aliyekuwa "off" siku hiyo akija na pyjama kusaidia baada ya kusikia habari za ajali. Hilo lilinonesha alivyo na wito na kazi / hudumayake. Wakati nasubiri kupelekwa chumba cha upasuaji, ilipitishwa miili kadhaa kati ya tuliokuwa nao ambao kwa bahati mbaya walifariki. Mpaka wakati huo, namba ya waliofariki tuliyoambiwa ilikuwa 15. Niliingizwa kushonwa ulimi (sikuwahi kusikia kabla na sijawahi kusikia baada ya hapo) na shughuli nzima ilichukua masaa mawili. Mizigo yangu yote alikuwa nayo Da Mdogo na kwa muda huo niliokuwa huko, watu walizidi kupoteza maisha. Hakujua nilipo, hakujua waliokufa baada ya hapo ni kina nani, na hakujua mimi ni nani, na ndugu zangu ni kina nani na mizigo yangu angeifanyia nini. Nilipotoka kwenye upasuaji nikakutana na Mama mmoja ambaye alisema mdogo wangu alikuwa akinitafuta na hakujua nilikuwa wapi. Sikushangaa kwani nilihamishwa vyumba vya upasuaji kama viwili. Alifurahi kuniona na ndipo tuaulizana majina na contact zozote "in case". Ndipo nilipomjua RENATHA BENEDICTO. Binti aliyekuja kuwa sauti yangu kwa muda wote uliosalia wa safari. Tulipelekwa kuoneshwa wodi na zilisikitisha. Nilimwandikia Renatha kuwa mama ni nurse na tungeweza kuendelea na safari. Akafanikiwa kuwashawishi wauguzi kuwa mwendo wa Nakuru-Bukoba ingekuwa Ok kama wangenifunga bandeji ya kutosha. Wakafanya hivyo naye akaenda kunitafutia kimiminika cha kula pamoja na dawa ya maumivu kwani ganzi ilianza kuisha na nilianza kusikia maumivu kila nilipochomwa.
Tukaenda Polisi na kupewa fomu za kujaza (PF3), kuchukua mabegi yetu toka kwenye basi ambalo lilikuwa limewekwa hapo na kisha tukapakiwa kwenye basi jingine la Tawfiq kuelekea nyumbani. Basi LILIKUWA LIMEPWAYA SAANA KWANI ZAIDI YA WATU 20 TULIOKUWA NAO KWENYE BASI LA AWALI HAWAKUWA NASI.
Tulianza safari na tulipata huduma nzuri saana mpakani mwa Kenya na Uganda kisha kuingia Tanzania. Safari yetu ikawa salama na tukafika Bukoba Mjini jioni ya tarehe 24 Dec.
Umati uliokuwa ukisubiri ulikuwa mkubwa na nilikuja kuambiwa kuwa wengi hawakujua nani kapoteza maisha, nani kapona na kama basi lingekuja na miili ya marehemu ama la.
Basi liliposimama Mama mmoja aliomba tufanye sala ya pamoja kumshukuru Mungu kwa kutunusuru na ajali ile mbaya na kuwaombea wenzetu waliotangulia mbela ya haki. TUKAFANYA HIVYO
Kisha mlango ukafunguliwa na tukashuka. Tulipokelewa na ndugu na binafsi kumuona Mamangu ilinipa faraja sana. Ni yeye pekee aliyekuwa amebaki mjini kwani familia nzima ilishaenda kijijini kwa ajili ya XMass na yeye alitakiwa aondoke nami.
Niliagana na Da Mdogo na msaidizi wangu mkuu na wa hiari Renatha na kuahidiana kutafutana baada ya kufika Dar.
Niliwasiliana naye mpaka mwaka 2002 alipoenda Chuo cha Ualimu Songea ambapo hatujaweza kuwasiliana mpaka sasa. Na ndio maana mpaka leo hii NAMSAKA RENATHA BENEDICTO
Namshukuru Mungu kwa miaka kumi niliyoongeza. Nimepitia mikononi mwa watabibu wengi na shukrani zangu kwa Dr Abdnego Kinasha na Dr Ismail wa taasisi ya mifupa MOI kwa matibabu yao, wafanyakazi wa kitengo cha mazoezi Muhimbili na MOI na wote walioweka mikono yao kwenye kunitibu.
Nimekuwa katika maumivu ya mgongo kwa miaka 10 sasa na nimepitia kila aina ya matibabu iliyoonekana kuwa na uwezekano wa kunipa nafuu na licha ya hayo yote, bado namshukuru Mungu kwa uhai.
Nawashukuru WAZAZI NA WALEZI ambao wamekuwa pamoja nami kila siku kuhakikisha niko sawasawa.
Na namshukuru msaidizi wangu, penzi na mzazi mwenzangu Esther ambaye tangu mwaka 2001 amekuwa akikumbusha juu ya umuhimu wa njia sahihi za kupunguza maumivu na kujali mgongo.
Ni miaka 10 sasa ya maumivu yangi, lakini KINACHOSIKITISHA NI KUWA HAKUNA HATUA ZA MAKUSUDI NA MAKINI ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI YETU KUHAKIKISHA KUWA WENGINE WENGI HAWAPOTEZI MAISHA YAO AMA KUWA NA MAUMIVU KAMA NILIYONAYO MIMI.
Takwimu zasikitisha na zaonesha kuwa ajali ni kati ya vinavyotuua zaidi na TANZANIA TUNA BARABARA ZIUAZO ZAIDI ULIMWENGUNI kama ambavyo ilinukuliwa HAPA
Namshukuru Mungu kwa miaka kumi niliyoongeza. Nimepitia mikononi mwa watabibu wengi na shukrani zangu kwa Dr Abdnego Kinasha na Dr Ismail wa taasisi ya mifupa MOI kwa matibabu yao, wafanyakazi wa kitengo cha mazoezi Muhimbili na MOI na wote walioweka mikono yao kwenye kunitibu.
Nimekuwa katika maumivu ya mgongo kwa miaka 10 sasa na nimepitia kila aina ya matibabu iliyoonekana kuwa na uwezekano wa kunipa nafuu na licha ya hayo yote, bado namshukuru Mungu kwa uhai.
Nawashukuru WAZAZI NA WALEZI ambao wamekuwa pamoja nami kila siku kuhakikisha niko sawasawa.
Na namshukuru msaidizi wangu, penzi na mzazi mwenzangu Esther ambaye tangu mwaka 2001 amekuwa akikumbusha juu ya umuhimu wa njia sahihi za kupunguza maumivu na kujali mgongo.
Ni miaka 10 sasa ya maumivu yangi, lakini KINACHOSIKITISHA NI KUWA HAKUNA HATUA ZA MAKUSUDI NA MAKINI ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI YETU KUHAKIKISHA KUWA WENGINE WENGI HAWAPOTEZI MAISHA YAO AMA KUWA NA MAUMIVU KAMA NILIYONAYO MIMI.
Takwimu zasikitisha na zaonesha kuwa ajali ni kati ya vinavyotuua zaidi na TANZANIA TUNA BARABARA ZIUAZO ZAIDI ULIMWENGUNI kama ambavyo ilinukuliwa HAPA
NI MIAKA 10 BAADAE. BADO NATOA SIFA NA SHUKRANI KWA MUNGU KWA UHAI NA WOTE WEMA WALIO HAI
25 comments:
What a memory to live with huh?
Long story but I read every line (the end was about to make cry *sniff* - no skimming here) na siwezi ku"picture" au kuimagine how terrified you were on this occassion. First to realise you just had an accident, then realising that there are dead people around you and then you are injured more than you think you were. Probably you thought the injury was as little as your dada mdogo.
Kweli shukrani zote kwa mwenye enzi na anajua anachokifanya kwa kila binadamu kwa makusudi yake. Brings me back to what I say to many people "everything happens for a reason"
Pole na mgongo though...10 years is a long time...and counting.
Pole sana mkuu . Mimi sina comment zaidi.
Pole sana, ni kumbukumbu nzito kuishi nayo lakini ndiyo maisha tena, nani ajuaye la kesho kwa yeyote aliye hai zaidi ya Mungu nasi waja wake hatuna jinsi zaidi ya kupokea na kuenda?
Pole sana.
mzee wa changamoto pole sana. you cheated death and still remember every detail of what happened 10 years. mbaya sana. kama Candy1 your sad story takes a reader through every word. really scary.as one writer once said 'stories create people create stories' what about developing this story into a 100-page (or more) book?. just to make it the most unforgetable incident in your past life.
utakufa tu na hii uliponakwa bahati mbaya. lazima ufe. ukipata ajali y a pili ndo hivuyo tena nSHOMILE WEYE
Dunia bado ilikuwa inakuhitaji. Tunashukuru bado upo nasi, lakini.... ni kama nightmare vile!!
Kwa NDUGU zangu nyote ambao siku zote tupo pamoja. Nasema bado nashukuru kuwa nanyi. Na naamini ndio sababu nipo mpaka leo.
Labda kwa "kiumbe" ANON ambaye kwa uoga na ukosefu wa ujasiri umeamua kujificha, nataka kukwambia (japo huwa sina desturi ya kujibu ma-anon) sidhani kama kuna asiyejua kuwa atakufa. Kila mtu atakufa na sitoshangaa kama utanitangulia. Kinachozungumziwa hapa ni namna ambavyo tunaweza kuyatumia maisha baada ya kunusurika katika kitu fulani.
Hatua ya kwanza kwa mtu kusonga mbele ni kujitambua na kama hujatambua umuhimu wa kilichopo mbele yako huwezi kukitumia ipasavyo. Naamini wewe bado waamini katika BAHATI jambo ambalo si la kweli. Hakuna bahati isiyofanyiwa kazi na kama unaamini hata kupona kwangu ni bahati mbaya, basi utambue kuwa una "bahati mbaya" ya kushindwa kutambua kuwa hakuna BAHATI MBAYA.
Kila kitokeacho hutokea kwa sababu na kwa tukio hili nimejifunza mengi, nimeonana na wengi na hata maisha niishiyo sasa kwa kiasi fulani yameboreshwa na mawazo ya wengi ambao nilikutana nao katika kusaka tiba ya maumivu niliyonayo.
NILIKUA kwa namna fulani baada ya hapo na hata MTAZAMO na MAONO yangu juu ya maisha ulibadilika.
Labda nikwambie kuwa hii haikuwa ajali ya kwanza wala ya mwisho ila ilikuwa kubwa kuliko zilizowahi kutokea.
Jambo ninalotaka kukwambia ni kuwa UWEPO WAKO HAPA si BAHATI MBAYA kama ambavyo unaweza kujidhania bali ni namna nyingine ya KUTOA CHANGAMOTO KWA CHANGAMOTO ZILIZOPO HAPA.
Kuna la kujifunza katika maoni yako na pengine watu wajue kuwa "bado watu wa namna yako wenye kuwatambua watu kwa ukabila mna-exist katika jamii"
Si jambo la kujivunia kuwa na watu kama wewe, lakini ili jamii isonge, wanastahili watu kama wewe.
Karibu tena
Blessings
Pole sana Mkuu!
...Umejieleza vizuri sana.....Sasa hivi na-appreciate context ya maoni yako katika hoja zangu kuhusu wingi wa ajali na upotevu wa maisha unaoambatana na ajali hizi nchini Tanzania.
...Shukuru Mungu kwa kukuachia uhai wako uhai....Pole kwa maumivu unayoendelea kuyapata.
Mdau
Faustine
Hakuna Mungu kama wewe!! Pole kaka yangu kwa yote yaliyokuta. Shukrani wifi yetu Esta kwa yote pia.
Mubelwa kwa nini usipeleke tangazo kwa michuzi la kumtafuta sista mdogo? naamini itarahisisha kazi ya kumpata kwani kama sio yeye lazima ndugu au marafiki zake wanamtembelea Michuzi.
Stay blessed Kaka.
**Huyo anony hapo juu nahisi atakuwa ni mtani wako, watani wana visa si mchezo.
Pole sana kaka Yngu Mubelwa, naamini mungu alikuwa na makusudi yake ili uendelee kuwa hai ili tuje kujuana kupitia mtandao na ili uendelee kutuelimisha kupitia kibaraza chako cha Changamoto.
Kaka Pole sana kwa yaliyokukuta, ni jambo la kumsukuru mungu kuwa bado uko nasi na tunaendelea kujifunza si kupitia kile uandikacho bali pia kupitia simulizi hii ambayo kwa kweli inahuzunisha.
Kwa kweli kuna mengi ya kujifunza kupitia simulizi hii.
Blessings
Mungu ni mkubwa. Pole sana, Tunamshukluru mungu sana kwani yote mema utendayo leo tungekosa.
Na pia asante kwa kutushirikisha katika ujumbe huu. Upendo daima.
Kaka mimi nakuomba uendelee kumsaka yule mdogo wako wa Hiari.
Rasta hapa.
Kaka pole sana, simulizi hii inasikitisha sana, pia napata funzo kuwa maisha yanahitaji uvumilivu, ujasiri na kutokata tamaa.
Pole kwa maumivu yaendeleayo kukusumbua, na naamini kwa uwezo wa Mungu maumivu hayo yatakwisha. Nakuombea maisha mema yenye baraka, amani, upendo na furaha tele.
Kaka pole sana: mungu alipenda uendelee kuwepo ktk dunia hii ili umtumikie mpaka atakapo kuita tena tena!. ashukuliwe mungu - maana kwa idadi hiyo waliokufa sio mchezo, kwanini wao nasio wewe, mungu anampango na makusudi na wewe, endelea kumshikili na kumwomba yeye daima. pole sana kwa maumivu yanayo kupata lakini amini ipo siku yatakwisha.
Kuhusu jambo la kumtafuta dada mdogo, kama upo Dar au kama kuna ndugu yako yupo hapo, ajaribu kwenda pale wizarani na uombe kitabu cha majina ya walimu waliopangiwa kufundisha sehemu mbali wakitokea chuo cha ualimu Matogoro( Songea) kwa mwaka ule ambao unadhani kwamba alimaliza. au kama unamtu kule Songea itakuwa rahisi zaidi kupitia njia hiyo hiyo aende pale chuoni,,
japokuwa ni njia ya mzunguko sana lakini inaweza kukusaidia wewe kujua baada ya kumaliza chuo pale matogoro - Songea alipangiwa wapi ili uweze kumfuatlia zaidi. kila la heri bro!
Kaka pole sana: mungu alipenda uendelee kuwepo ktk dunia hii ili umtumikie mpaka atakapo kuita tena tena!. ashukuliwe mungu - maana kwa idadi hiyo waliokufa sio mchezo, kwanini wao nasio wewe, mungu anampango na makusudi na wewe, endelea kumshikili na kumwomba yeye daima. pole sana kwa maumivu yanayo kupata lakini amini ipo siku yatakwisha.
Kuhusu jambo la kumtafuta dada mdogo, kama upo Dar au kama kuna ndugu yako yupo hapo, ajaribu kwenda pale wizarani na uombe kitabu cha majina ya walimu waliopangiwa kufundisha sehemu mbali wakitokea chuo cha ualimu Matogoro( Songea) kwa mwaka ule ambao unadhani kwamba alimaliza. au kama unamtu kule Songea itakuwa rahisi zaidi kupitia njia hiyo hiyo aende pale chuoni,,
japokuwa ni njia ya mzunguko sana lakini inaweza kukusaidia wewe kujua baada ya kumaliza chuo pale matogoro - Songea alipangiwa wapi ili uweze kumfuatlia zaidi. kila la heri bro!
Kaka pole sana: mungu alipenda uendelee kuwepo ktk dunia hii ili umtumikie mpaka atakapo kuita tena tena!. ashukuliwe mungu - maana kwa idadi hiyo waliokufa sio mchezo, kwanini wao nasio wewe, mungu anampango na makusudi na wewe, endelea kumshikili na kumwomba yeye daima. pole sana kwa maumivu yanayo kupata lakini amini ipo siku yatakwisha.
Kuhusu jambo la kumtafuta dada mdogo, kama upo Dar au kama kuna ndugu yako yupo hapo, ajaribu kwenda pale wizarani na uombe kitabu cha majina ya walimu waliopangiwa kufundisha sehemu mbali wakitokea chuo cha ualimu Matogoro( Songea) kwa mwaka ule ambao unadhani kwamba alimaliza. au kama unamtu kule Songea itakuwa rahisi zaidi kupitia njia hiyo hiyo aende pale chuoni,,
japokuwa ni njia ya mzunguko sana lakini inaweza kukusaidia wewe kujua baada ya kumaliza chuo pale matogoro - Songea alipangiwa wapi ili uweze kumfuatlia zaidi. kila la heri bro!
Sijui niseme nini hapa ila nakumbuka miaka ile haya mabasi yalikuwa nduki sana na yaliuwa kwa kiasi na maisha yanaendelea. naamini ulijifunza mengi kama unavyokiri lakini duh ni uzoefu mkubwa juu ya mwanzo na mwisho wa maisha yetu kama miili au wanadamu.
DUh
Pole sana kaka yangu hii habari imeisoma kwa siku 2 nimekuwa nairudia niyakusikitisha sana.
Mungu wetu ni mwema sana na kila jambo limpatalo binadamu,linamakusudi yake kweli unakila sababu ya kumshukuru mungu.
nilipofikia karibu na mwisho wa story yako machozi yamenilengalenga na una HAKI YA KUMTAFUTA RENATHA.
Nakuombea kwamba umpate ili umpe shukrani hasa sasa tunapoingia katika mwaka mpya wa 11 wa kumbukumbu ya tukio hilo.
Kaka pole sana. Umelielezea tukio hili kwa ufasaha mkubwa sana.
Nothing just happen, everything happen for a reason. Kuna kusudi la wewe kubaki hai mpaka leo. Bila shaka kwa miaka kumi hii umeshalifahamu.
Amani kwako Mubelwa
Mengi yameshasemwa.
Bila ajali hii sidhani kama tungekuwa na Mubelwa tuliye naye sasa!
Mipango ya Mungu daima iko sahihi ati!
Sad Story, I was tearily-eyed the whole time. I think living with the pain this long is daunting but more so seeing the bodies of those who departed everytime it plays in your mind. I am very sorry my dear.
Usifiwe Mungu Milele hata Milele..love you Mubelwa..
Post a Comment