Thursday, September 17, 2009

Tanzania Yangu.... Ijengayo Ghorofa ikipuuza msingi

Siku chache zilizopita tumemshuhudia Rais Jakaya Kikwete akienda kwenye vyombo vya habari "kuzungumza na wananchi". Binafsi kumshuhudia Rais akienda "kujibu hoja na maswali ya wananchi" ilikuwa kama kichekesho fulani (najitahidi kutohusisha na tukio kubwa la mwakani). Nikaishia kujiuliza maswali kadhaa ikiwemo
Ni kwanini aanze Rais "kuzungumza na wananchi" na sio wajumbe wa nyumba kumikumi, watendaji wa vijiji, makatibu kata, makatibu tarafa, wabunge, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na kisha Rais? Yaani tunaanzia juu kwenda chini???
Kwani Rais ametumia mfumo gani wa kukusanya maswali na maoni ama hoja hizo? Na mfumo huo unamkutanisha ama kuwawezesha na watu wangapi nchini kueleza waliyonayo? Mfumo wa emails na text messages unawapa waTanzania wangapi wenye uhitaji nafasi ya kuwasiliana na Rais? Huu ni kwa WATU WENYE UCHUNGU NA NCHI LAKINI SI WALIO NA MACHUNGU YA NCHI. Wapo ambao hawawezi kumudu hata gharama za hiyo vocha ya kutuma ujumbe mfupi.
Tumeshuhudia Serikali yetu ikileta mambo ya ajabu nchini na kuuremba "ujuujuu" wa maisha ya mtanzania ilhali wenye shida halisi hawaguswi. Tunaona tunavyoishi kwa mipango ya "uchaguzi hadi uchaguzi" inavyoweka kando mahitaji halisi ya waTanzania.
Tunaambia kuwa tunajengewa mji na nchi ilhali tunaona kuwa tunazibiwa mifumo ya maisha. Picha hizi mbili za hapa chini zanikumbusha alilosema Nasio kuwa "you're looking good from afar, but you're far from looking good" Tunaona tunavyoambiwa kuwa tunajengewa majengo ya kisasa ilhali hakuna mifumo ya kutosha ya kusambaza na kutawanya majitaka. Mitaro yote imeziba... Tunajenga miji ya kiangazi pekeeee???
Rais wangu anazunguka Dunia akiwahimiza wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza Tanzania ilhali tunajua kuwa hatuna umeme wa kuwatosha hata wananchi tulionao tena bila viwanda. Hivi wakija tutawafanyaje wao? Ama tutahamisha umeme wa wananchi kwa wawekezaji?
Tunasikia kelele za kuendeleza elimu kuwa ya kisasa wakati hakuna madarasa wala walimu wa kutosha. Na hata walimu waliopo wanasota na maisha ambayo hawastahili kuishi na wale wanaostaafu wanahitaji miaka kadhaa kufuatilia mafao yao ambayo wanaweza kutoyapata. Wanaolitumikia taifa kwa uaminifu wanafikia hatua ya kuambiwa "serikali haina pesa hivyo baadhi ya malipo yako hutoyapata". Sijui serikali inajengaje elimu kwa kupuuza wadau wakuu wa elimu hiyo? Ni ghorofa bila msingi???
N hawa wazee wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (hapa chini) nao hakuna asiyejua wanavyohangaika. Nikiwaza kwa undani naona:
Ongezeko la mishahara laonekana kwa walio juu, Nafuu ya maisha iko kwa wenye nacho. Usikivu wapatikana kwa walio juu na MAISHA BORA NI KWA KILA MTANZANIA ALIYE JUU.
Nina hakika wengi waishiyo maisha ya hali ya chini hawajaona mabadiliko chanya ya utawala uliopo baada ya uhuru kwani kila kionekanacho kuboreshwa ni kwa wale wenye nacho.
Na ndio maana naishia kujiuliza kuwa inakuwaje Tanzania inajenga ghorofa bila kujali msingi wake???
Naacha.
Tuonane NEXT IJAYO
PICHA: Mjengwa, Dr Faustine

4 comments:

Tandasi said...

Ndugu yangu Mubelwa nchi hii imejaa maigizo, keki ya taifa inaliwa na wachache,tabaka la wakwezi linapanuka sana tu usomi unazidi kupungua kwa sababu kidato cha nne kinageuka darasa la saba,viongozi wanatumia mgawanyo wa pato la taifa kama kipimo cha umaskini badala ya kupima ustawi mzima wa maisha ya wananchi,mabepari wa kiafrika ndio viongozi wa nchi,nakumbuka maneno ya mwandishi P. bundala wa kitabu cha Je waafrika ndivyo tulivyo? ambaye anaamini umaskini mkubwa wa Wafrika ni umaskini wa FIKRA na hii ndio inazaa yote haya.-ASANTE KWA WAZO ZURI

Albert Kissima said...

Huduma ya umeme kwa sasa hapa Tanzania hairidhishi hata kidogo,kila kukicha unakatika,siku yapita umeme haupo.BIMA za afya zabagua magonjwa,utaambiwa kwa ugonjwa huu bima haiwezi tumika,dawa hizi kwa bima huwezi kuzipata,da!, ni nyanja nyingi sana ziigusayo jamii zaendeshwa juu juu tu na kiubabaishaji,yani ilimradi vitengo vya kutoa huduma vipo tu na majina makubwa lakini utoaji wa huduma zenyewe ni ziro. Najiuliza kwa kusoneka saaana sijui ni lini tutaondokana na wimbi hili la kukandamizwa(kwa ridhaa yetu).Ukweli ni kwamba hakuna uhusiano wowote wa maendeleo ya nchi na wananchi wenyewe,kila mmoja kwa namna yake atajua ni kwa namna gani atastand yeye kama yeye na aweze kuishi, ndio maana wenyewe kwa wenyewe twaibiana,twauana,yani twafaidiana kiujumla, "struggle for exstance" na "survival for the fittest" vyote kwa pamoja ndani ya wahanga wa umasikini uliokithiri.

Faith S Hilary said...

Nchi kubwa lile unajua? hehehe...bwana kaka yangu unajua mie hata nikiwa serious nacheka tu so anyway...mie naona nchi ile hata bila rais inakwenda tu kwasababu kila mtu anajitafutia mwenyewe...sijui mambo ya misaada ya vyandarua kwa mama wajawazito na mengine etc... sidhani kama kila mtanzania ana hiyo so called "maisha bora"...as usual...ni mawazo yangu tu :)

Yasinta Ngonyani said...

Ninanukuu "Ni kwanini aanze Rais "kuzungumza na wananchi" na sio wajumbe wa nyumba kumikumi, watendaji wa vijiji, makatibu kata, makatibu tarafa, wabunge, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na kisha Rais? Yaani tunaanzia juu kwenda chini???"mwisho wa kunuuu. ni kweli hata mie nimekuwa najiuliza mara zote kwa nini????