Thursday, November 12, 2009

Tanzania Yangu....Yenye vingi vyenye u-wingi wa manufaa usio na manufaa kwa wengi.

Ni wazi kuwa wengi wetu tunajivunia mengi tusikiayo kuhusu Tanzania. Na pengine unaposoma kuihusu ndio unaweza kufarijika zaidi. Kuna mengi mengi mema ambayo ukiyasikia unaweza kuwa na kazi ndogo kumvutia mtalii kuitembelea Tanzania.
Lakini jinsi unavyozidi kuyajua na kujua sifa njema ilizo nazo Tanzania Yangu, ndivyo unavyoweza kuzidi kukereka hasa utakapofikiria anayenufaika na u-wingi wa sifa ama rasilimali ama vitu hivyo. Picha toka http://www.kilimanjaroblog.com
Angalia SEHEMU ZA KITALII kama zile za ki-historia za Engaruka, Michoro ya mapangoni ya Kondoa Irangi, Olduvai Gorge, Mapango ya Amboni, Sehemu kama Bagamoyo, Kilwa Kisiwani, Hifadhi ya Gombe, Ziwa Manyara, Ngorongoro, Mikumi, Kilimanjaro, Ruaha, Rubondo, Saadani, Selous, Tarangire na nyingine nyingi ni vitu ambavyo nina hakika kama vingeweza kusimamiwa vema, vingeweza kuwa sehemu ya kutosha kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi.
Tukirejea kwenye UCHIMBAJI MADINI nako tunaona tulivyo nayo mengi na yanavyochimbwa kwa wingi japo manufaa yake kwa jamii hayajidhihirishi waziwazi. Kuanzia Dhahabu, Almasi, Ulanga, Tanzanite na mengine mengi. Nayo yangesimamiwa yangechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla Ramani toka http://www.cppskamloops.com/
Tuna MITO inayotiririka miezi 12 kwa mwaka tena kwa wingi lakini bado tunashuhudia watu wakifa njaa. Hakuna uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji wala uboreshaji wa uzalishaji wa umeme. Tuko nyuma ukilinganisha na Botswana wasio na mvua wala mito na maziwa kama sisi. Hata kama ukubwa wa nchi unatofautiana, lakini hata uwiano wa maji unatofautiana pia. Picha toka http://www.threebestbeaches.com
Tuna FUKWE nyingi ambazo zingeweza kutengenezwa na kuwapa wazawa nafasi ya kupumzika na pia kuwavutia wageni kuja kuingiza pato la kigeni KWA MANUFAA YA JAMII NZIMA lakini licha ya kuona wageni wakija, bado hatuoni manufaa yao kwa jamii. Picha toka www.guardian.co.uk
Tuna VITU ADIMU kama Vyura wa Kihansi (Soma yao hapa) na Dinosaur (Habari zake hapa) ambavyo vyote "vimewekezwa" nje ya nchi na sijui ni waTanzania wangapi wa kawaida wanaojua na kunufaika na uwepo wao.
Leo hii bado wananchi wa kawaida wanahenya na mgao wa umeme wa zaidi ya nusu siku ilhali wachache (wenye jukumu la kuuboresha) hawaonji adha yake.
Wananchi wanaishi maisha ambayo RUSHWA ni sehemu ya "utaratibu" kwa wao kutimiziwa HAKI zao.
Wananchi wanasafiri kwa hofu kwa kuwa miundombinu iko isivyostahili kuwa na ni hatari kwa maisha ya wengi wetu. Barabara, vyombo vya angani, majini vyote havionekani kuwekewa mkazo wa usalama wa abiria na serikali.
Hospitalini hako huko hakusemeki kwani kunatia kichefuchefu na hakuna harakati za wazi (achilia mbali za kampeni zinazoanza) kusaidia kutatua hili
Maji bado ni bidhaa adimu kwa wananchi wengi wa vijijini na hata hayo wayapatayo si salama kwao.
Najiuliza kama tuna yote haya ya kujivunia, ni kwanini wanaojivunia si wote kama Tanzania ni yetu sote???
Unapoijua Tanzania yangu, utaona vingi vyenye u-wingi wa manufaa lakini usio na manufaa kwa wengi.
Blessings

5 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

tatizo ni kwamba nyie watanzania mnaoweza kuona mambo kwa undani na kwa uzuri baada ya kuonja elimu ya mkoloni na mambo yake, mumekimbia na kuhamia kwa mkoloni na kuendelea kuwa mtumwa wake badala ya kurudi kijijini na kumwelimisha mtanzania aliyemwacha huko maenda kutafuta maarifa.

sasa mko mbali na mnaonekana kuona matatizo ya mtanzania kuliko yeye mwenyewe na kumsemea.

kwa hiyo ni sehemu ya....

viva afrika said...

tanzania tanzaniaa
nakupenda kwa moyo wote
nchi yangu tanzania
jina lako ni tamu sana.

huu ni wimbo uliopoteza mantiki ukiwa na jicho la uchunguzi!

Albert Kissima said...

hii ni changamoto kubwa kweli kweli na wote tuwaze ni kwa namna gani tutatoka kwenye dimbwi hili. Tuna kila sababu ya uchumi wa nchi kupanda kila kukicha na maisha ya mtanzania kuwa bora zaidi kwa kupitia yote uliyoyaahinisha. Tuwaze na tuwazue, mchawi ni nani na tukishamgundua tujue tutafanya nini.

Bennet said...

Hii hali inaumiza sana, maana hamna hata kitu kimoja ambacho serekali yetu imeweza kukifanya barabara kwa usahihi, kila kitu ni usanii mtupu

Yasinta Ngonyani said...

Mmmmmhhh!!!