Thursday, December 17, 2009

Kuna wewe wangapi ndani ya wewe?

Picha kutoka http://www.designyourway.net
Labda wengine watasema mmoja. Lakini si kweli. Nijuavyo mimi ni kuwa kuna takribani wewe wanne ndani yako ambao kwa nyakati tofauti hukufanya uwe unavyokuwa mbele ya watu fulani kuhusu jambo fulani kwa wakati fulani ili kitokee kitu fulani.
Ni "wewe" hao wanne ambao wanastahili kushirikiana vema na wangu wanne ina wa yule ili kuweza kuifanya dunia hii kuwa mahala pema pa kuishi.

Labda tuanze kwa kuwaangalia hao kina wewe wanne waliomo ndani mwako.
1: Wa kwanza ni yule ambaye kwa wakati ama tukio ama swali ama mahala ama kazi ama kitokeacho mbele yako anakuwa ANAJUA, NA ANAJUA KUWA ANAJUA. Huyu ni yule wewe anayekuanya uonekane "una akili" na mwenye suluhisho kwa lile uulizwalo. Lakini wewe huyu ndiye aliye chanzo cha dharau kwa wengi akiamini kuwa ana uwezo kuliko wengine ambao wako katika aina nyingine ya u-wao.

2: Kuna yule wewe ambaye ANAJUA LAKINI HAJUI KUWA ANAJUA. Mara nyingi huyu ni yule wewe wa kujilaumu ambaye kila linapotokea jambo anaishia kusema "nilijua itakuwa hivi" ama "sijui kwanini sikujibu hivi maana nilijua ndio jibu" na kauli nyingine nyingi kuonesha kuwa alikuwa amekaribia kuwa sahihi japo hajawa sahihi. Huyu ni wewe wa "nge" ambaye sentensi zake mara nyingi ni kama vile ningefanya. ningewahi, ningeamua, ningejaza n.k

3: Wewe wa tatu ni yule ambaye HAJUI NA ANAJUA KUWA HAJUI na huyu ni kati ya walio wakarimu saana. Wewe huyu ni yule ambaye ukiulizwa unakuwa na uwezo ama ujasiri wa kusema "kwa kweli sijui ila muulize..... anajua". Huyu huwa hana majivuno na ni mtu wa majibu mafupi na muhimu. Pengine anakuwa wa "kujivunga" pale anapoamua kutokuwa wazi kuwa hajui japo anajua pa kupata suluhisho.

4: Na wewe wa nne (ambaye si wa kuwa naye sana) ni yule ambaye HAJUI NA HAJUI KUWA HAJUI. Yaani huyu ni wewe wa ajabu sana. Mwenye akili ambazo mara nyingi huja kuthibitika kutokuwa murua kwa wakati wa uwepo wake. Ambaye anaweza kubisha ukweli asijue kuwa ndio ukweli na baadae kuishia kuumbuka.


Lakini kama nilivyosema awali. Kila mtu anao hawa watu wanne ndani ya u-moja anaoamini kuwa nao na ni kwa sababu huwezi kuwa katika u-wewe wa aina zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Na japo waweza kubadilika kutoka mmoja kwenda mwingine kwa wakati mfupi na bila wewe kujijua, lakini sote twapitia u-sisi huu na kwa nyakati tofauti twaweza kukumbuka kufanya kati ya hayo yaliyoandikwa hapo juu. Na wakati mwingine si kusema tu, bali hata kuwaza. Yaani kuwaza kuwa kitu fulani kitakuwa hivi na baadae kikawa hivyo, ama kisiwe hivyo ama kufikia wakati ukarejea mawazo yako na kusema "sikuwa sahihi"
Labda jiulize kuwa sasa hivi uko kwenye u-wewe gani maana hilo pia litaathiri namna utakavyoelewa usomacho hapa
Tuonane "NEXT IJAYO"

5 comments:

Halil Mnzava said...

Sawa mzee,hii ni changamoto ya sisi kujitambua ki ukweli!!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

na labda umeongelea upande wa mwili wa akili (mind). kuna pia sisi Miili, sisi Roho, sisi Hisia na mwili wa akiili (mind)

lakini pia binadamu ni kiumbe wa ajabu sana katika minajili ya sisi kama uwepo/nguvu

Mzee wa Changamoto said...

Ni kwewli Kamala kuwa nimeongelea upande huo mmoja. Najaribu kutochanganya zote kwa pamoja na sijawa na ufahamu wa kutosha katika pande nyingine.
Labda ukimaliza "asali-mwezi" (honeymoon) yako tutajadili hizo pande nyingine kwa upana zaidi

Faith S Hilary said...

1. Huyu wa kwanza huyu anaweza kukufanya uwe na maadui kibao maana kila mtu likifika swali au jambo wataanza kunong'ona. Ndio kina sie tunanyamaza sometimes lol

2. Huyu anatokea mara nyingi tu, halafu sana inaweza kutokea pale mtu mwingine kajibu kitu then some of us go "I wanted to say that!"

3. Huyu ni mpenzi wa walimu kule praimari (primary school), maana mwalimu anajua kama hujui ila basi tu akuaibishe mbele ya watu. This one is not my favourite.

4. Huyu hehe, unaweza kurushiwa keki (pie) usoni maana unaweza kujibu/kusema utumbo kabisa.

Ni hayo tu :-)

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Hii inaonekana kama ni ile falsafa ya mlevi niliyowahi kuigusia hapa.

http://matondo.blogspot.com/2009/01/falsafa-ya-mlevi-1_30.html

Binadamu ni kiumbe tata. Vipi sasa tukianza kuongelea roho, hisia na mengineyo (cf. Kamala?).