Monday, December 21, 2009

Ni wapi tulipopoteza UTU, UPENDO, HESHIMA ......

Mtoto Edwin Donald Myaye (4) aliyeuawa kikatili kwa ushirikiano wa nduguye.
Maelezo ya Da Flora yanasema "walichofanya vijana hawa wasiokuwa na huruma kwanza inasemekana walimlawiti mtoto kisha wakamziba mdomo na pua kwa kitambaa na kumfungia mawe makubwa mabegani, mikononi, na miguuni kisha wakamtumbukiza ziwani akiwa yuu ngali hai."
Mazishi ya Kaka Mdogo Edwin Donald. Picha zote kwa hisani ya Da Flora
Siku ya kwanza kuanzisha kipengele cha Za kale vs maisha ya sasa nilianza na wimbo DUNIA IMANI IMEKWISHA wake Marijani Rajabu. Katika wimbo huo alizungumzia mengi kuhusu mabadiliko ya thamani baina yetu katika miaka hiyo. Lakini hakuna ambalo lingeweza kumuandaa kukutana na hali iliyopo sasa.
Mwaka 2001, mwanamuziki Joseph Haule alitoa albamu yake ya kwanza kama msanii solo akaiita MACHOZI, JASHO NA DAMU ambamo aliimba kuhusu kuuana kunakoendelea, kuondoka kwa utu baina yetu kuanzia kuibiana ajalini, kuuawa kwa vikongwe na mengine mengi.
Sasa Tanzania ya leo inazidi kutumbukia kwenye lindi la kutendeana maovu. Wengine wanauita UNYAMA lakini mimi napinga, kwani wanyama hawafanyiani ukatili ambao binadamu twafanyiana kwa lengo kusaka mafanikio. Nadhani tumevuka ukatili wafanyianao wanyama. Kibaya zaidi imetoka kwenye MTUMWA vs MTWANA ama TAIFA vs TAIFA na sasa imefika kwa waTanzania na inakwenda chini mpaka kwenye kiwango cha wanafamilia / wanandugu kuuana ili kupata ama kwa tamaa ya kupata pesa. Tumesoma yule mzee aliyetuhumiwa kuwaleta walevi wenzake kumuua bintiye albino. Tumesoma ukatili wanaofanyiwa watu na ndugu zao na wengine kupoteza maisha, lakini sikuwahi kusoma jambo lililonisikitisha kama HABARI HII niliyoisoma kwenye blog ya Da Flora Lauwo.

Licha ya tatizo la UTU, UPENDO, HESHIMA na mengine ambayo wananchi na wanadamu tunatakiwa kuwa nayo, naishia kurejea kwenye maswali nijiulizayo kila mara kuwa SERIKALI YENYE DHAMANA YA KUWASHUGHULIKIA WATU HAWA IKO WAPI?

Maasi yanazidi nyumbani na yaonekana hayakabiliwi ipasavyo. Bado hakuna anayehoji. Si wabunge wala wananchi. Inasikitisha kuwa HAKUNA MWENYE KUSIKIA UCHUNGU WA WATU KAMA MAMA WA MTOTO EDWIN DONALD ambaye kwa hakia anahitaji kuona mkondo wa sheria ukichukua nafasi yake haraka kuwashughulikia waliomuua mwanaye, na kisha kuona sheria hiyohiyo ikizuia wengine kuwa wahanga wa hali kama iliyoikumba familia yake.

Twasikia mauaji, mauaji, mauaji lakini baada ya mazishi na machache yasemwa kuhusu wauaji na adhabu zao.
Hatuhitaji kusubiri watuhumiwa wasakwe na kuuawa ndio tujiulize tulikojipoteza.
Tujiulize NI WAPI TULIPOPOTEZA UTU, UPENDO, HESHIMA NA THAMANI KWA WENZETU???
Heaven Help Us All

3 comments:

Anonymous said...

Aina ya kifo imenisababisha nikapatwa na uchungu wa ajabu. Duniani ubinadamu ni bidhaa adimu. Ukatili umekuwa mbaya zaidi na zaidi. Aliye na ulimwengu huu atayaangalia haya hadi lini?

Yasinta Ngonyani said...

Dunia imekwisha kwa kweli!!na kama inakwisha basi ni uMIMI TU.

ShazRon said...

Is there any way to read this in English?