Tuesday, November 30, 2010

Kosa la kwanza la Rais Kikwete......

ONYO: Usisome kama nia yako ni kusoma sio KUELEWA. Rais Jakaya Kikwete akihutubia taifa punde baada ya kuapishwa kuongoza nchi kwa awamu ya pili. Photo credit: Chingasite
Ni kweli kuwa UCHAGUZI UMEMALIZIKA na sasa ni harakati mpya za kuanza KUIJENGA Tanzania yetu katika muhula wa mwisho wa awamu ya nne ya uongozi wa Taifa.
MOSI nirejee ambayo nilishasema awali, NAWAPONGEZA woote walioshiriki katika mchakato wa kumsaka "kiongozi bora" atakayeleta mabadiliko yenye manufaa kwa wananchi.
Shukrani kwa
1: Walioshinda kushinda,
2: Walioshinda kushindwa (ambao wamefanya "juu chini" kutangazwa washindi)
3: Walioshindwa kushinda
Haijalishi "umeangukia" katika kundi gani hapo juu, lakini utakuwa umepata changamoto nzuri ama katika kutekeleza utakiwayo kutekeleza sasa kwa wananchi waliokuchagua, ama katika kujipanga upya kwa uchaguzi ujao kwa wanaopanga kugombea tena.

PILI, nieleze kuwa kumekuwa na MATUMAINI YA MAFANIKIO katika muhula huu. Na matumaini haya yameonekana kuwa makubwa sana. Watu wengi wametabiri UTENDAJI katika awamu hii kwa kuwa wamewekewa watu ambao hawakuwemo katika mfumo wa uongozi uliopita. Kwa maana nyingine, BUNGE LA SASA LINA MABADILIKO KIDOGO na hasa mabadiliko yaliyohusisha "kuanguka kwa vigogo" kadhaa wa chama tawala ambao hakuna aliyetaraji wangeng'olewa kirahisi na watu wa upinzani. Ilishangaza wengi kuona wagombea wa chama tawala licha ya kuwa na "viwezeshwa" vya hali, mali na "mfumo", bado waliweza kukosa nafasi walizozipigania kwa nguvu. Lakini TAFSIRI YAKE SI NGUMU.... WATU WAMECHOSHWA NA VIONGOZI WASIOWAJALI.
Lakini kwa wale ambao wanadhani "ndugu hawa" walioenguliwa ama kunyimwa ridhaa ya kwenda bungeni ndio wamekwisha kisiasa, wanastahili kufikiria mara ya pili.
Tumeanza kuona harakati za Raisi kutumia HAKI YAKE YA KIKATIBA kuteua wasaidizi wake katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza kazi zake. Tumeshaona uteuzi wa BARAZA LA MAWAZIRI ambalo kwa heshima na taadhima niliwaomba MAWAZIRI WAORODHESHE WATATENDA NINI, VIPI NA KUFIKIA LINI? (Irejee hapa). Sijajua VIGEZO vya uteuzi huo, na wala sina hakika kama katika vyeo vya kuteuliwa kuna ambacho kina "udogo" wa utendaji ukilinganisha na ubunge. Najua wakuu wa mikoa (ambao kama nilivyosema hapa nawaona kama MZIGO KWA SERIKALI NA WANANCHI na CHANZO CHA KUDIDIMIA KWA MAENDELEO NCHINI), na pia kuna wakuu wa wilaya, kuna makatibu wa wizara, wabunge wa kuteuliwa, mabalozi n.k. Na pia tumeona ambavyo Mhe Raisi ameanza kwa kuteua wabunge ambao mmoja wa wateuliwa AMEZUA GUMZO (hapa) kutokana na kuhusishwa na tuhuma ambazo bado hazijathibitishwa kwa wananchi.
Lakini bado nawaza kama Waheshimiwa wastaafu kama Mhe. Lawrence Masha, Mhe Monica Mbega, Mhe Phillip Marmo, Mhe Getrude Mwongela, Mhe Batilda Buriani na wengine wengi hawatanyakua nafasi za kuteuliwa. Ninawaza pia kuwa kama niko sahihi (kwamba hakuna cheo cha kuteuliwa chenye udogo wa shughuli kuliko ubunge), ni kipi kitamfanya Mhe Raisi ateue watu ambao wameshindwa kuwatumikia wananchi wao ilhali wanajua fika kuwa watakuja kuwaomba kura miaka 5 ikiisha? Kama watu hawa walipuuza NGUVU YA KURA YA WANANCHI mpaka yalipowakuta ya kuwakuta, ni vipi watawajibika ilhali wanajua atakayewateua hawatamuomba kura na hataenda tena kwa wananchi kuomba kura kwa kuwa muhula wake umeisha?
SINA HAKIKA KAMA RAISI ATATEUA YEYOTE KATI YA "WALIOSHINDWA KUSHINDA" UCHAGUZI lakini pia sitashangazwa na hili japo nitasikitika sana.

Na katika kumalizia sentenzi iliyo kichwa cha habari hii, nasema.......
KOSA LA KWANZA LA RAISI KIKWETE LITAKUWA NI KUPUUZA NGUVU NA MAONI YA WANANCHI YA KUTAKA MABADILIKO IKIWA ATAWATEUA WATU WALIOSHINDWA KATIKA UCHAGUZI ULIOMALIZIKA.
Hili litakuwa kosa kama atateua yeyote kati ya walioshindwa na halitakuwa kosa mpaka atakapotekeleza kile ninachoona kina uwezekano wa kutendeka.
Mpaka wakati huo, naendelea KUFUNGA NA KUOMBA kwamba Mheshimiwa Raisi aheshimu matakwa, nia na haja ya mabadiliko iliyooneshwa na wananchi.

Na hivi ndivyo nionavyo tatizo lijalo na natunza haki ya kukosea na kukosolewa. Labda namna nionavyo tatizo ndilo tatizo.

Tuonane "NEXT IJAYO"

No comments: