Wednesday, December 8, 2010

Tanzania yangu....Ikimbiayo kivuli chake mchana, jangwani..

Wakati wa kuanza kwa harakati na kampeni za ubinafsishaji na uwekezaji kulikuwa na meengi mema "yaliyootwa" na wengi vikionekana kama suluhisho katika kuupa nguvu mfumo mzima wa uchumi nchini. Lakini kumetokea mfululizo wa mambo ambayo "yanalazimika" kuibuliwa ambayo hayaoneshi kuwa waliolezea manufaa ya uwekezaji, waliopewa dhamana na kusimamia na kuendesha uwekezaji na waliotakiwa kunufaika na uwekezaji huo wako kwenye kurasa napengine "dunia" tofauti za mafanikio na manufaa ya uwekezaji huo. Tumeshuhudia watu "wanaotetea" habari hizi za uwekezaji na wanaowatetea wawekezaji wakiwa na kauli tofauti wanapobanwa juu ya yale ambayo mara nyingi yanakuwa yameonywa na wafanyakazi wa chini wa makampuni na ama mashirika hayo. Kuanzia mikataba ya RICHMOND, ATCL, BOT, NUWA mpaka misukosuko mingine iliyokumbana na uwekezaji kama mahoteli yanayobadili majina kila baada ya miaka kadhaa na sasa shirika la reli tunabaki kujiuliza kama nia ya uwekezaji ni kwa wananchi ama wawezeshaji wa uwekezaji. Hivi majuzi nimesikia kwa juu juu suala la gharama za mafao ya Tanesco na kabla sijabahatika kulisoma kwa umakini, nasikia MGAO UMEANZA. Nimemsikiliza msemaji wa Tanesco "akijijingisha" na aliyokuwa akisema kisha nikaishia kuwaza. NI LINI SERIKALI ILIJENGA KITUO KIPYA CHA UZALISHAJI WA UMEME? NI LINI TULISHUHUDIA UKARABATI WA MITAMBO HII UENDAO SAMBAMBA NA IDADI YA WATUMIAJI? NI IPI FAIDA YA TANESCO NA NI WAPI IENDAPO? NI NANI AWAJIBIKAYE KWA FAIDA YA SHIRIKA HILI? Niliwahi andika kuhusu nchi hii na harakati zake za KUMWAGILIA MAJANI BADALA YA MIZIZI na hili ndilo nionalo. Tanzania ya sasa HAIMUWAJIBISHI anayeshindwa kuleta maendeleo kwa kuwa hajaiingiza nchi kwenye hasara. Kama shirika lilitakiwa kuendeshwa kwa faida, ni kwanini haipatikani na kama inapatikana na si ya kutosha kuleta MITAMBO MIPYA, ni kwanini wasiseme ni sababu gani inayosababisha uzalishaji usitoshe? Ni kama vile kila tulichoachiwa na wakoloni ama viongozi wa awali ndicvho tulichonacho japo twajisifia kuwa na maendeleo. Hebu tazama hizi taswira za mabwawa ya uzalishaji umeme na unijulishe kama unakumbuka kuwa wameshakarabati.
Bwawa la uzalishaji umeme la Kidatu
Photo: http://www.industcards.com/hydro-africa.htm. Bwawa la uzalishaji umeme la Kihansi
Photo: http://www.industcards.com/hydro-africa.htm. Ama tazama picha ya Magomeni iliyoachwa na mkoloni kisha ulinganishe na uijuayo sasa. Magomeni iliyoachwa na mkoloni. Ilikuwa inaeleweka mitaa na mipango miji. Nenda sasa uone. Picha kwa hisani ya Michuzi Blog Najua wananchi wanahadaishwa kuwa maendeleo ni hivyo "vikwangua anga" lakini najiuliza tunakoelekea bila maegesho na barabara za kutosha. Bila mifumo ya majitaka. Hivi hawa wote waki-flush vyoo na mtaro ukaziba Dar si itafurika kwa maji-choo? Picha toka PBase.com 
Nasikia mikataba inasainiwa ya kuendeleza mji (hasa Dr) na "vikwangua ana" vinazidi kuongezeka, lakini kinachosikitisha ni kuwa DAR ES SALAAM YA MKOLONI ILIKUWA IMEPANGWA NA KUJENGWA VEMA KULIKO AMBAVYO INAWEZA KUWA MWAKA 2015 Na majengo "yanayoota" bila kuona ukarabati na upanuzi wa mifumo ya maji, umeme na majitaka na hata maegesho na barabara. 
Kwa nje yaonekana kama maendeleo lakini nahisi tunakaliza "bomu la vinyesi" kwani mitaro ikiziba sijui hao wawekeza tunaowaalika tutawatoaje kwenye mafuriko ya majitaka? 
Labda WATEKELEZE WALICHOSEMA HAPA kwenye video hii hapa chini
 
 Lakini hii ndio TANZANIA YANGU...IKIMBIAYO KIVULI CHAKE MCHAAAA TENA JANGWANI. Kila aionaye anaisikitikia. Na njia pekee ya kuepuka dhahama ni kukabiliana na kivuli hicho Ni wakati wa kuacha kukimbia tatizo na kujikita kwenye kulitatua
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

3 comments:

Mbele said...

Tatizo hapa ni ujinga na ufisadi. Ujinga umezagaa kila mahali, na ndio maana watu hawaelewi ubaya wa ujenzi wa aina hii. Halafu, kwa upande wa wanaojenga, kuna huu ujinga na kuna pia ufisadi.

Matokeo yake ni kama unavyosema, kwamba kama Taifa, tunajitengenezea hilo bomu ambalo litatulipukia, na pia tunajichimbia kaburi.

Bado tunadiriki kusema Mungu ibariki Tanzania. Siamini kama Mungu anaibariki jamii inayoendekeza ujinga na ufisadi.

emu-three said...

Tatizo kubwa ni ubinafsi ambao unawatawala viongozi wetu. Kwa mfano kama ikitokea tenda, uue hapo kuna `dili' na mkubwa au wakubwa kupata chochote au ten parcent! Sasa inapofikia kupanga jambo la kimaendeleo kama halina `dili' litadoda, ndio maana kila kitu atafute mfadhili...! Vinginevyo itafutwe tenda ambayo kutakuwa na dili ndani yake!
Hivi kuna gharama gani ya kupanga `mipango miji' Kwanini isubiriwe mapakaakoma wananchi wajijengee wenyewe kiholela, halafu ndio mipangoo hiyo iwepo, ina maana jiji hili halina ramani? Najiuliza bila majibu.
Kama umepata kiwanja na unataka ujue uhalali na ramani ya kiwanja chako, jaribu kufuatilia kwa wanaohusika, utakoma ubishi...utakata tamaa, kwanini...ubinfasi, ...vinginevyo cheza na `ubongo wako'! Kwani jiji hili, na nchi hii ni ya wabongo!

Fadhy Mtanga said...

Nchi hii kuna mambo yanasikitisha sana.