Monday, August 22, 2011

Neno la Dada Joyce na CHANGAMOTO YA MAISHA yetu


Dada Joyce Mshana-Collins akiwa pembeni ya picha iliyowekwa saini, ya rafikie wa muda mrefu Marehemu Kidee Bendera. Hii ilikuwa baada ya misa ya kumuombea Kidee iliyofanyika Jumamosi Aug 20 katika kanisa la Calvary Lutheran Church, Silver Spring, MD.
MAISHA. Nimejifunza kuwa yana kazi ama nia moja tu. KUFUNZA. Na ni kufunza kwafanyika kwa njia mbili, KUFUNZA NINI LA KUFANYA ama NINI LA KUTOFANYA. Na mafunzo haya ni ya "kutwa-kucha". Lakini sote twajua kuwa huwezi kujifunza kama hujaamua na kuwa tayari kujfunza. Niliwahi kuandika na kuuliza mambo kadhaa ambayo nitakuja kuyarejea kuhusu maisha yetu sisi bin-adamu na wale tuwapendao.
Jumamosi ya juzi nilihudhuria Misa ya kumuaga Dada yetu mpendwa Kidee Bendera-Tazani ambayo kwa hakika ilikusanya watu wengi na niliweza kuonana na wengine ambao kwa miaka kadhaa tumeshindwa "kukutana kwa hiari". Nikawaza mengi juu ya MAISHA yetu na hata 'UHIARI WA LAZIMA' tulionao maishani mwetu. Mengi yalitendeka (kama ilivyo katika taratibu za misiba) na mengi yalisemwa. Ila jambo ambalo ningependa kushirikiana nanyi hapa ni MANENO MACHACHE yaliyokuwemo kwenye barua aliyoandika Dadangu Joyce Mshana Collins kwa rafikiye wa miaka mingi sana, Marehemu Kidee. Dada Joyce ambaye alijuana na marehemu kwa takriban robo karne, alitukumbusha sote kuwa binadamu tunadhani fulani amekufa nasi tunaishi, japo ukweli ni kuwa wenzetu wanaanza kuishi wakati sisi ndio tuko kwenye utaratibu wa kufa. Hii ilikuwa changamoto kubwa kwangu (na naamini kwa wengi pia) maana binadamu tumekuwa na desturi ya "kuwaza kinyumenyume" hata pale tunapojua ukweli wa tuwazacho. Nilishawahi kutoa "mfano wa BIMA YA MAISHA ambayo licha ya ukweli kuwa ni BIMA YA KIFO, bado hakuna anayetaka kukubali ukweli na kuiita hivyo. Kwao ni BIMA YA MAISHA ambayo huitumii maishani bali ukifa."
Nawawaza "waamini" na "waumini" wenzangu ambao tuna imani na MAISHA BAADA YA KIFO lakini tunashindwa kukubali ukweli kuwa ni sisi wenye shaka kwa kuendelea kung'ang'ania maisha yaishiyo na kusahau ama kupuuza maisha tuaminiyo. Aliyoongea Dadangu huyu sio tu yalinifanya niwaze mara mbili kuhusu ukweli wa kila tufanyacho, bali hata tuishivyo.
LABDA ni kwa kupuuza hili, watu wanataka "kutanua" hapa duniani.
LABDA ni kwa kupuuza hili, watu wanalimbikiza mali hapa duniani.
LABDA ni kwa kupuuza hili, watu wanakosa heshima kwa binadamu ambaye mbele ya Mungu watakuwa na kuishi maisha sawa na usawa.
LABDA ni kwa kupuuza hili, watu wanathamini maisha ya sasa zaidi ya yale waaminiyo wajayo.
LAKINIIII.....Swali larejea palepale kwamba ni kwanini binadamu ajuaye haya bado hataki kuishi katika ukweli? Je ni ubinafsi kama nilioulizia HAPA?
NI MAISHA ninayotaka tuyaangalie kwa JICHO LA NDANI ili kuweza kujitambua (kama nilivyoeleza HAPA) na kuishi katika KWELI.
Kauli ya Da Joyce imenirejesha kwenye sehemu ya wimbo wa Winston Hubert McIntosh aliyeuliza kwanini wote twataka kwenda mbinguni lakini hakuna aliye tayari kufa? Bado tutarejea alipoeleza Dadaa kuwa tunajali kipoteacho na kupuuza kidumucho.
Nikirejea nilipoanzia, kuwa MAISHA NI MAFUNZO, na kama umeamua kuwa makini, katika kila kitendekacho utakuwa na moja ya chaguzi mbili za kujifunza, NINI CHA KUFANYA ama NINI CHA KUTOFANYA. Binafsi, neno la Dada Joyce limeboresha mtazamo wangu kuhusu maisha, na naamini kama utachukua muda wako, na kutafari alichosema, utakuwa na jibu la swali la NINI MAISHA HAYA YANAMAANISHA KWAKO. Na kwa kuTAMBUA hilo, itakusaidia kujua ni vipi uishi na kwa kuishi kwako, ndipo utakapotimiza LENGO LA KUISHI WAKATI UKIPUNGUZA UISHI ILI KUWEZA KUELEKEA KWENYE UISHI.
Neno ni kuwa, binadamu tunadhani fulani amekufa nasi tunaishi, japo ukweli ni kuwa wenzetu wanaanza kuishi wakati sisi ndio tuko kwenye utaratibu wa kufa.
Na hili ni wazo la jambo, jambo lililoonwa kwa "jicho la ndani"
Luciano anasema, SERVE JAH

UWE NA WIKI YENYE BARAKA, YENYE KUANZA KUUTAMBUA MWANZO WA MWISHO WA MAISHA YAKO, UTAKAOANZISHA MAISHA YAKO.

Jicho la ndani ni kipengele ambacho huangalia mambo kwa "undani" zaidi na kujaribu kutafuta suluhisho kutokana na tafakari ya tatizo. Kwa maandiko mengine kuhusu kipengele hiki, BOFYA HAPA

7 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hakika hii ni changamoto kweli ya maisha yetu...Ningependa na kufurahi kama ujumbe huu ungesomwa na watu wengi ..maana kuna watu ambao wana imani na sasa imani zao zinapotoshwa sana hasa wakiamini mambo mengine kama ya ushirikina.

Ebou's said...

Hizo ni changamoto zilizopo katika maisha yetu ya kila siku, tunasoma kutokana na matokeo yanayotukumba, bali binaadamu tumejiendekeza sana na tabia za kusahau na kutojali thamani ya matokeo yalitukumba ili kujifunza zaidi cha msingi, ni kuzingatia, kuwa na ushirikiano pamoja na kuzidisha upendo juu ya hilo.. maana hata na mimi ilinikusa sana hutuba ya kwenye barua aliyoandika Dadangu Joyce Mshana Collins nilipoisikiliza na kufikiria sana sisi Watanzania tuliopo njee ya nchi yetu. M/mungu atujaliee turudi makwetu kwa salama na amani.. Good job Mzee wachangamoto!

Anonymous said...

Kwa kifupi tu ,kifo nikitu ambacho binaadam hukiogopa.ila kifo hichohicho kiki tokea huchukua muda tukikitafakari,na baada ya hapo hutoweka katika mawazo yetu natuna endelea na hamsini zetu.kifo hakizoeleki pindipo kinapo tokea.tume umbwa ili tufe,kwamaana hiyo kila mtu ananjia zake katika hili, nijinsi gani atajiandaa na maisha yake akiwa hapa duniani,ndiyo maana kuna walokole,waganga,wachawi,nk wote hawa niwamoja katika jamii zetu,kupanga ni kuchagua,na maisha ni matamu lakini mafupi.mfano, maisha alio ishi Remy Ongala nifundisho,kwani alitabiri safari yake, na hata mwisho alikufa akiwa katika imani ya kilokole,kutoka uanamuziki pamoja na anasa zote za dunia,lakini mwisho amekufa kifo ambacho alikitabiri akiwa duniani.Kaka.S

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ni changamoto kweli. ndo maana huwa nakataa kuwa muumini wa dini yoyote ile hata kama naenda au siendi kwenye nyumba za ibada kwani naamini maisha niliyonayo yana umuhimu kuliko yatarajiwayo na sitokufa kamwe kwa hiyo sitaki kuaminishwa chochote kile eti kinakuja kwani nipo nilikuwepo na nitakuwepo

Anonymous said...

Nduguyangu,Kamara. nyumba za ibada hazina tatizo,ila chamuhimu katika maisha nikuwa na utaratibu wako dhidi ya maisha yako uwapo hapa duniani.kuwa naimani nimuhimu sana,hii nikwa mitazamo yangu,kwani kama binadamu huwezi kuwa nakitu usicho kiamini ambacho kwako wewe ndiyo nguzo amamuhimili kwa kila jambo utakalotakafanya kwa faida yako.kwangu mimi naamini dini na mungu yupo.ila nahakikisha kwa ufahamu wangu imani yangu hainikwazi,na wala simkwazi mtu. Kaka S

Mzee wa Changamoto said...

Asanteni WAPENDWA.
Binafsi siamini kwamba Kaka Kamala haamini, bali naamini kuwa kaamua kuamini kuwa haamini.KILA MTU NI MUAMINI
Alichofanya Kaka Kamala ni kuchukua moja kati ya chaguzi tatu za kuamini.
1: Waweza kuamini kuwa unaamini
2: Waweza kuamini kuwa huamini
3: Waweza kutoamini kuwa unaamini

UKIJARIBU KUFIKIRI UTAUPATA UKWELI

emu-three said...

UJUMBE umefika mkuu-TUPO PAMOJA