Wednesday, July 31, 2013

Tanzania yangu....Isiyoendelea kwa kukosa viongozi "wanaoendekeza ujinga"

ONYO: REJEA KUSOMA KICHWA CHA BANDIKO HILI NA UHAKIKISHE UMEELEWA KABLA HUJAENDELEA NA BANDIKO HILI
Dunia ya sasa inaonekana kwenda kwa kasi
Yaani.....
Kasi (pengine) kuliko uwezo wa baadhi ya watu na mazingira KUAMBATANA na kasi hiyo.
Ni katika hilo, tunakuta baadhi ya mazingira (nchi yangu ikiwemo) ikishindwa kupitia hatua zote zinazostahili kupitiwa kuweza KUSONGA MBELE na mabadiliko hayo.
Matokeo yake ni kuwa watu wanaruka baadhi ya hatua na wanashindwa kuwa na ukamilifu wa pale walipo.
Hivi sasa, kile kinachoonekana kama UJANJA nchini mwangu ndicho kinachonisikitisha
Na ni hicho kinachonifanya niamini kuwa BILA TAFSIRI HALISI YA UZALENDO, basi hiki kionekanacho kama UJANJA kitatupeleka pabaya.
Na ndio maana niliandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook kuwa
"Kwa kuwa nchi yetu imejaa WAJANJA.
Na......
Kwa kuwa kuongoza nchi ya wajanja KIJANJA hakutuletei maendeleo,
Mimi nadhani .....
Tujaribu UJINGA"

Nililomaanisha ni kuwa, kutokana na KUKIMBIZA MAENDELEO KULIKO MWENDO WAKE NA KUPUUZA HATUA ZA KUYAFUATA, nchi yetu imejikuta ikitafsiri MAENDELEO na UJANJA kama vitu ambavyo ni matokeo ya njia za mkato kujibufaisha.
Leo hii, mtu anayekwepa kodi anaonekana MJANJA.
Leo hii, mtu anayepokea rushwa na kunufaika bila kukamatwa anaonekana MJANJA
Leo hii, mtu anayetajirika haraka hata kwa kuvunja miiko ya kazi anaonekana MJANJA
Leo hii, mtu anayepokea mishahara ya wafu wizarani anaonekana MJANJA
Na mengine mabaya ambayo ni NJIA ZA MKATO NA ZISIZO HALALI ambazo zinamnufaisha zinahesabiwa kuwa UJANJA
Na kwa hakika
Anayelipa kodi anavyotakiwa, anaonekana MJINGA
Anayefuata sheria katika atendayo anaonekana MJINGA
Anayehimiza HAKI kwa wote anaonekana MJINGA
Anayekataa rushwa hivi sasa anaonekana MJINGA
Anayeonekana kuwajali wananchi anaonekana MJINGA
Yaani, mfumo mzima unaomfanya mtu kutwaa madaraka, umeandamwa na watu ambao fikra zao ziko kwenye KISASI cha kujilimbikizia kama ambavyo walilimbikiza waliotangulia na kumnyima yeye FURSA SAWA aliyohitaji ama kustahili kuwa nayo.
TUNAKUWA KWENYE MAUMIVU
Maumivu ambayo sasa hayatokani na NJAA, bali ni maumivu yanayosababishwa na KUVIMBIWA kutokana na yule mwenye njaa kula kupitiliza na kusababisha maumivu ya UPANDE WA PILI wa kile kilichoonekana kuwa SULUHISHO.
Tatizo linalotukabili si la WATU, bali ni namna tunavyowapata watu hao na kuwadhaminisha madaraka.
Niliandika
"Sasa hivi hata nchi yangu Tanzania iongozwe na Masia na Mtume, iwapo MFUMO UTAKAOTUMIKA NI HUU ULIOPO, bado upande pekee wa maendeleo tutakaoelekea ni wa MAENDELEO HASI.
Tatizo la Tanzania si watu walio madarakani, bali ni MFUMO unaowaweka pale, unaowaongoza katika kuongoza na unaowawajibisha."

Januari 7, 2009 niliandika POST HII yenye kichwa DIKTETA NI NANI NA KWANINI TWAMHITAJI
Na humo, nikaandika
"Najua akitokea mtu akalazimisha baadhi ya mambo ya maana kutendeka nyumbani basi ataitwa dikteta (na kwa bahati mbaya nasi tutashabikia hata kama si tafsiri yetu).
Najiuliza akitokea "kiongozi" akalazimisha kusimamishwa kwa mikataba yote ya madini ili ipitiwe upya hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha viongozi wakuu waliosababisha mabilioni ya hasara serikalini wachunguzwe licha ya katiba waliyoshindwa kuitii kutosema hivyo hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha wabunge kujenga ofisi na kutumia muda mwingi majimboni mwao kama walivyoahidi wakati wa kampeni hataonekana dikteta?
Atakayelazimisha utendaji wa mikoa kulingana na rasilimali zake kuwanufaisha wananchi wake na kisha nchi nzima huyo hataonekana dikteta?
Najua kuwa atakayewafikisha viongozi wakuu mahabusu ataitwa dikteta kwa kuwa amekwenda kinyume cha katiba, lakini sijui kwa nini katiba imlinde yule ambaye ameivunja kujilimbikizia mali na kuitia serikali hasara kubwa?
Kama huyu atakayetenda haya niliyosema hapo juu, atakayevunja mikataba ya ujenzi wa miundombinu yenye utata, atakayehakikisha ahadi za wananchi zinatekelezwa na waahidi hasa wabunge, atakayeshurutisha matumizi mazuri ya rasilimali za wananchi kwa manufaa ya sehemu husika, atakayeshinikiza malipo kwa wafanyakazi ambayo mpaka sasa haijajulikana kwanini hawajalipwa ilhali waheshimiwa wanapata pesa zao bila malimbikizo, atakayehakikisha kuwa mkulima wa anapata senti zake zote alizoikopesha serikali na ambazo anatumia pesa nyingi kufuatilia kuliko atakazolipwa, atakayesimamisha ziara za nje na ndani za viongozi (zisizo za lazima) na atakayeamua Tanzania iwe ya manufaa kwa wa Tanzania kwa kutumia kila kilichopo Tanzania ataitwa DIKTETA, basi namuombea awepo."


NI KWA KUWA HUYU ATAKUWA DIKTETA KWA KUTEKELEZA MEMA AMBAYO WASIO WEMA WATAUONA KAMA UJINGA 

Narejea...
Kwa kuwa VIONGOZI WETU WANATOKA KWENYE JAMII, NA NI JAMII INAYOTAFSIRI MEMA KUWA "UJINGA", BASI NI MPAKA TUTAKAPOPATA VIONGOZI WANAOENDEKEZA "UJINGA", NCHI YETU HAITAENDELEA.

Mungu Ibariki Tanzania.

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

emuthree said...

Mkuu kuna usemi usemao, `bora kupata, sio kufika...' unaweza ukafika ukawahi na mapema lkn mwenzako akaja kachelewa, kwa `ujanja' akapata wewe uliyewahi, ukisubiri `utaratibu' ukakosa...ndio huku tulipo!