Sunday, September 15, 2013

Tanzania yangu. Ivunayo isipopanda (II)


Alhamis wiki hii nilisoma habari kwenye gazeti la Mwananchi kuhusu Bondia Rashid Matumla ambaye amesema kuwa anapigana ili asife njaa
Katika habari hiyo, Matumla amenukuliwa akisema kuwa “Kila kitu changu hivi sasa kinaniendea kombo, nilifanya biashara ya mahindi huko Tanga imekufa vivyohivyo na ile ya mbao, napigana ulingoni nikiwa mgonjwa ili nipate fedha kwani sina fedha kabisa,” Leo nikasoma kuhusu kupokelewa kwa shwangwe kwa bondia Francis Cheka huko Morogoro. Nikawaza mapokezi ambayo Matumla aliwahi kupata na hadhi ya kutumia "VIP" pale kiwanja cha ndege aliyopewa kutokana na mafanikio yake.
Lakini mwisho wake ndio huu aliousema
Najua nilipata kuandika mengi kuhusu haya.
Kuhusu wasanii na watangazaji walioliletea taifa UZALENDO mkubwa. Waigizaji wa michezo ya radioni ambao walitufanya "tugande" kwenye redio zetu kusikiliza michezo ya kuigiza iliyokuwa na mafunzo ilhali wanapata kipato kidogo sana.
Lakini unapofika wakati wa "kula mbivu", inaonekana kuwa MBIVU HIZO ZINAKUWA ZIMEOZA.
Tumeshuhudia wasanii wakichangishwa pesa kwa matibabu.
Wengine ambao wametumikia taifa kwa zaidi ya nusu karne (kama Mzee Muhidin Maalim anaishia kupata msaada binafsi wa wasanii na wadau wengine kabla Serikali HAIJAKUMBUKA KUTOA "CHETI"
Lakini nimeona nirejee BANDIKO hili la Aug 18, 2009 nililobandika chini ya "kichwa" Tanzania yangu. Ivunayo isipopanda
JIKUMBUSHE

Labda TANZANIA YANGU ni jina limaanishalo SERIKALI. Ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa ikijitokeza kupongeza na kuonekana pale penye mafanikio na "kuwa likizo" kwenye matatizo. Ni kweli. Binafsi nilishangaa kuona watu wanashangaa kumuona Naibu Waziri wa michezo kaenda kumpokea Hasheem Thabeet uwanja wa ndege. Wapo waliohoji umuhimu wa Thabeet na wapo waliohoji majukumu ya Naibu Waziri. Kwa ujumla kila mtu alikuwa na lake la kueleza japo kwangu si kila mtu alikuwa na maana katika kutetea hoja yake. Lazima tukubali kuwa Hasheem amekuwa mtanzania wa kwanza kupata nafasi ya kucheza katika ligi ya Taifa ya mpira wa kikapu hapa Marekani NBA na ni lazima apate "attention" toka nyumbani na hasa katika safari yake ya kwanza kurejea tangu ajiunge na Memphis Grizzlies. Na si ajabu kwa SERIKALI kujibaraguza pembeni yake na kuonesha (kama) inajali ilhali tunajua mchango wao katika kufanikisha safari za wengi wenye nia ya kuwa kama Hasheem. Si jambo la kushangaza hata kidogo kwa sisi tunaofuatilia habari za michezo kwa muda mrefu. Hamkumbuki namna ambavyo WAZIRI MKUU alisherehekea ushindi wa Rashid "snake Boy" Matumla wakati ule akiwa kwenye kilele cha uchezaji wake? Matumla akapewa na "pass" ya VIP uwanja wa ndege na sasa sina hakika kama kuna kiongozi anayekumbuka aliko. Sina tatizo na mapokezi na sina tatizo na namna ambavyo viongozi wa serikali wanajitoa kuwapongeza wachezaji na watu mbalimbali wenye kuonesha kufika kilele cha mafanikio yao. KINACHONICHEFUA ni namna ambavyo SERIKALI inakurupuka na kuandaa mapokezi na dhifa na sherehe na hotuba za kuwapongeza wenzetu wanaofanya vema ilhali inapuuza mazingira yanayowawezesha kufika walipo.
Hatukusikia SERIKALI ikijihusisha na maandalizi ya Rashid Matumla ila tukamuona Waziri Mkuu Sumaye akimnyanyua mkono kwa mbwembwe zoote na bendera kuubwa. Hatukusikia serikali ikimsaidia Thabeet (alipokuwa akisaka njia ya kumfikisha alipo) kufikia ndoto zake lakini leo hii, lakini sasa hivi mpaka Rais anamuandalia chakula kumpongeza.
Sijui kwa wasomaji wangu, lakini nimechoshwa na siasa katika maisha ya watu (hasa ambapo hazistahili). SERIKALI ilistahili kushikwa aibu kwa mafanikio BINAFSI yaonekanayo miongoni mwa watu wake na ilistahili kujua ni wapi pa kuanzia kuwekeza. Inaoshindwa kuwahudumia wananchi wake kwenye shida, isijitokeze kwenye raha.
WATU WAMELIA SAANA KUHUSU WIZI UNAOENDELEA AIRPORT LAKINI HAJATUMWA MWAKILISHI NA SASA ANAKUJA NYOTA TUNAMUONA. Kwanini tusikae chini na kupanga program nzuri itakayowawezesha wale wengi wenye ndoto kama za hawa tuwapongezao kuzifikia? Haihitaji akili za ziada kujua hili. Najiuliza meengi kuhusu TANZANIA YANGU. Ni kwanini haiwekezi katika kupata itakayo? Labda niwakumbushe swali alilouliza Freddie McGregor alipowauliza viongozi kuwa "why dont you set the program, so the youth can work and survive. So that they can better themselves and show some progress in their life, teach the youth the positive things and make them realize, no shooting, no looting, bring back the LOVING and where did we go wrong? Msikilize hapa chini
 
Picha: Kutoka kwa Michuzi & Darhotwire

No comments: