Na Andrew Chale
JAMII imeaswa kutambua matatizo yanayowakumba watoto mfanano
(mtindio wa ubongo) na kushauriwa kutokuwabagua. Aidha, wametakiwa kuachana na
imani za kishirikina, kwamba watoto hao ni laana kutoka kwa Mungu na kuwaua,
badala ya kutoa elimu kwa wanaowatenga watoto hao.
Mwenyekiti wa Chama cha watu wanaojitolea (Trabajo
Voluntario), Marisa Yussuf Himid aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, alipokuwa kwenye ziara maalum ya kutembelea vyombo vya habari nchini.
Akiwa kwenye ziara hiyo aliweza kutembelea kampuni ya Free
Media Limited ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, na kujionea mambo mbalimbali ya
kiutendaji ndani ya chumba hicho cha habari (Newsroom).
Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Andrew Chale (kushoto) akimtambulisha Mwenyekiti wa Chama cha watu wanaojitolea (Trabajo Voluntario), Marisa Yussuf Himid kwa Mhariri wa Michezo wa gazeti la Tanzania Daima, Tullo Chambo (katikati). |
Hata hivyo, Marisa ambaye alisema matatizo makubwa
yanayowasumbua watoto hao ni kuingiliwa kimwili na wanaume au wanawake
wanaotambua kuwa watoto hao hawana uelewa wa kutosha.
Pia alisema wanawake wengi wanaamua kuwafungia watoto hao
ndani, kwani wengi wamewachukulia kama walemavu wa akili na kudiriki kuwabaka
na kuwaambukiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa imani potofu kuwa jamii yao hiyo
hawapati virisi hivyo.. (Hii si kweli ni upotoshwaji na vitendo hivi vikemewe
na kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika).
“Tumeamua kuita kitengo hiki kwa jina la watoto mfanano kusudi
kuondoa dhana ya watu kufikiri wana mtindio wa ubongo. Hivyo tumekuja kutoa
elimu ya kwamba watoto hawa wana haki kama watoto wengine , tusiwabaguem” alisema
Marisa.
Aliongeza watoto mfanano wanahitaji elimu kama watoto wengine
na wapatiwe huduma za kiafya, ikiwa ni pamoja na tundu kwenye moyo, matatizo ya
macho na upungufu wa vitamini na huduma nyingine.
Pia alisema katika kikundi chao walikuwepo watoto 45, lakini
kutokana na elimu duni ya wazazi, watoto wengine walichukuliwa huku wengine
wakifariki na hadi kufikia watoto 32.
“Mmoja wa wanasiasa na mwanakikundi hiki, Samia Suluhu
anajiandaa kuleta walimu na madaktari watakaojitolea kuwasaidia watoto hao,
kwani hadi sasa tumebaki na walimu watatu tu ambao bado wanaendelea
kuwafundisha,” aliongeza.
Alisema kikundi hicho kinashirikiana na Taasisi ya Zanzibar
Association of Downsyndrome Children (ZADOC) kwa kuwakusanya na kuwapatia
mafunzoa watoto hao kwa kipindi cha miezi sita.
Aliongeza kikundi hicho kilianza mwaka 2005 kwa kuhamasisha
wananchi kujitolea zaidi katika kuwalea watoto mfanano na kuhamasisha jamii
kuwatambua.
No comments:
Post a Comment