Wednesday, November 12, 2008

Hatuwathamini kwa kuwa hatuwajui. Kwanini?

"Everyman must know their past, so we can stand firm in the future" Na haya yalisemwa na Morgan Heritage walipoimba juu ya KNOW YOUR PAST katika albamu yao ya More Teaching. Ni haya tunayokosa katika kujitambua ambayo "yanapelekea" kutotambua mlingano wa tulipo na tutokako. Na huu ni ukweli.
Hivi sasa inapofika Ijumaa, mimi na wenzangu wapenda "za kale" ama wengine wanaziita "zilipendwa" tunajimwaga ukurasa huu wa BONGO CELEBRITY kupata burudani hiyo. Ukiingia kwenye sehemu ya maoni utaona watu wanauliza hivi aliyeimba huo ni nani? Aliwahi kupigia bendi gani na wengine kutoa majina na miaka isiyo na hakika. Inasikitisha kuwa wasanii wetu NGULI ambao wamesaidia kuielimisha jamii, kuiburudisha na hata kutimiza matakwa ya viongozi kwa kuwakusanyia hadhira wanapojiandaa kuhutubia ama kukamilisha azma zao kama za Gezaulole wanasahaulika kwa kuwa tu wahusika hawafanyi wanalotakiwa. MASWALI NILIYONAYO
HIVI CHAMA CHA MUZIKI WA DANSI TANZANIA (CHAMUDATA) wako wapi kushindwa kuandaa, kutunza na kuenzi taarifa za wanamuziki wa Dansi nchini?
Kweli leo hii watu wanakosa habari, historia na hata kazi za wasanii walioiweka Tanzania kwenye ramani ya muziki barani kwetu? Leo hii tunakosa kuwajua kina Marijani Rajabu, Balisidya, Mbaraka Mwinshehe, Moshi William, Eddie Sheggy, Adam Bakari, Hemdi Maneti, Ndala Kasheba, Selemani Mwanyiro, Abeli Baltazar na wengine kwa kuwa tu hakuna pa kupata kumbukumbu zao?
Kweli kazi na maisha ya hawa wasanii mahiri yanapauka na kupotea kwa kuwa tu hakuna pa kupata kumbukumbu zao?
Kwanini Chamudata wasiwe na tovuti ya kueleza maisha ya wasanii WOTE wenye uanachama?
Nitasema ukweli kuwa wasanii waliojenga msingi wa sanaa nchini hawaheshimiki na kujulikana kwa kuwa wahusika hawafanyi wanalotakiwa kufanya.
Ni jambo la kusikitisha kuona wasanii wetu wamefanya kazi kuubwa sana wakati wa maisha na wapo wanoendelea kufanya hivyo, lakini HATUWATHAMINI KWA KUWA HATUWAJUI. Na swali ni Kwenini?
Huu ni MTAZAMO WA CHANGAMOTO YETU KWETU na ndivyo namna nionavyo tatizo. Labda ndilo tatizo.

No comments: