Tuesday, November 11, 2008

Iwe "bifu" la kweli ama "gemu". Ubunifu bado ni ziro

Katika toleo langu la tarehe 30 mwezi Septemba niliandika yale ambayo kwa mtazamo wangu yanaathiri sanaa ya muziki wa sasa nchini Tanzania. Niliandika yale ambayo tumepoteza katika sanaa na ambayo tunaendelea kupoteza kila siku just kwa kuwa tunataka ama kuiga yatokayo nje ya nchi, ama kutengeneza pesa za haraka.

Lakini kuna kitu ambacho sio tu sikukifafanua vema, bali sikukikemea pia na kwa kuwa kinaendelea kujitokeza naona ni vema kuiweka bayana CHANGAMOTO YETU hiyo ili kuweza kukabiliana nayo.

Nimekuwa mfuatiliaji wa muziki kwa muda sasa na jinsi siku zinavyozidi kwenda ndivyo wasanii wanavyokuj na tungo mbalimbali kutafuta heshima. Na kuna watungao yaliyomo kwenye jamii, kuna watungao kuburudisha na kuelimisha na kuna wale ambao wenzao wakishatunga, wao wanaibuka na tungo za kuwajibu. SI mnakumbuka Ngoni Tribe walivyojibu wimbo wa Jay Dee wa WANAUME KAMA MABINTI? Ama mwakumbuka "series" hii ya Sister P alivyopanda chati na ANAKUJA iliyoonekana kumjibu Zay-B. Naye Zay-B akafifia mpaka alipomjibu Inspekta Haruni kwenye wimbo wake NIPO GADO. Sasa majuzi Inspekta naye baada ya kuwa chini kafufuka na tungo ya kumjibu MwanaFA na wimbo wake NDOA HAINA DOA ambao waonekana kufanya vema kama ambavyo nyingine zote zilizofanya.

Hapa nieleweke kuwa sipingi kujibizana na huku kujibizana hakujaanza leo. Kujibizana imekuwa sehemu ya BIASHARA YA MUZIKI kwa miaka mingi na sehemu nyingi na wakati mwingine hupangwa ili kuboresha mauzo japo inapokuwa kweli huishia kusiko kwema kama ilivyokuwa kwa makundi ya Pwani ya Mashariki na Magharibi ya Marekani. Ila suala ni kuwa yaonekana utunzi wa wote hawa na wengine ambao sijawataja ni wa kusuasua na haiwezi kuwa rahisi kwa yeyote ambaye hajawahi kusikiwa wimbo unaojibiwa atakuwa hapati picha kamili na halisi ya kiimbwacho. Yaani ni "kukariri" sehemu ya maneno ya wimbo wa kwanza na kuyajibu moja kwa moja na ndio maana wanaojua wimbo uliojibiwa wala hawahitaji maelezo ya msanii kujua alikuwa akiimba nini ama akimuimba nani!

Labda niwakumbushe kuwa hata Tanzania majibizano hayakuanza jana na wala hayakuanzia kwenye Bongo Fleva ama Taarabu. Ila zamani nyimbo zilikuwa zina picha ambayo kama ulikuwa ukijua kinachoendelea basi ungejua kinachozungumzwa na kama hujui kinachojibiwa hapo unakuwa na taswira nyingiiine kabisa tena yenye mafunzo tofauti na mema kwa jamii. Kwa wale ambao hamkuwahi "kuchimba" maudhui halisi ya nyimbo, mnakumbuka MV. Mapenzi II ya Sikinde? Mnajua ilikuwa dongo kwa walioikimbia Sikinde kwenda kuanzisha Safari Sound? Je Chatu Mkali iliyowajibu Sikinde? Unakumbuka nyimbo Msafiri Kakiri ya Juwata? Unajua ilikuwa ni ujumbe kwa nani? Na Talaka Rejea ya Sikinde? Unajua lilikuwa jibu kwa nani? Lakini kama hujui kuwa kuna majibizano katika nyimbo hizo, huoni pia kuwa kuna mafunzo ya tofauti kwenye Mv Mapenzi inayoelezwa kama meli kwenye bahari yenye dhoruba, ama Chatu na sifa zake za uwindaji msituni, ama mtalakiwa anavyoeleza juu ya talaka rejea aliyopewa? Kwa taarifa yenu, hayo yote yalikuwa madongo lakini bado yalifikisha ujumbe kwa wahusika, yakaelimisha wasiohusika na ndio maana nasema watunzi wetu wa zamani walikuwa makini katika kazi zao na licha ya kuwa na zana duni za kutendea kazi, bado waliweza kuwa na ubunifu wa hali ya juu. Hata kwenye Taarabu kina Sanamu la Michelin, Mambo Iko Huku na nyingine zilikuwa zikiburudisha wasiojua majibizano na kufikisha ujumbe kwa walengwa.

Wasanii wa sasa lazima wakubali kuwa Pesa na kusaka matamasha ya haraka vinawapeleka pabaya. Ndio maana wote kati ya niliowataja hapo juu "hufa" baada ya "single" zao kuchokwa maana majibizano ya kitoto hayadumu.

Sitaki kujua kama kinachoendelea huwa ni "bifu" la kweli ama ni "gemu" la kusaka shows na attention ya media, lakini kwa lolote liwalo, UBUNIFU WENU BADO NI ZIRO.


Ni mtazamo wangu na ndivyo nionavyo tatizo, na yawezekana namna nionavyo ndilo tatizo.

Blessings

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli zamani ilikuwa safi kwani ukirudi nyuma na kusikiliza inaleta raha sana. Nakumbuka wakati nilikuwa mdogo mama yangu alikuwa anaimba wimbo mmoja huu SINA MAKOSA yaani aliupenda sana kwa hiyo hata mimi upo kichwani sasa.

Wasanii wa leo ni kweli wanaingana sana na kweli hii inawapunguzia soko. kwani wao wanataka soko la haraka.

Mzee wa Changamoto said...

Dada Yasinta. Asante kwa mchango wako na naamini wahusika wataweza kuangalia haya na kurekebisha. Wameendekeza "quick cash" na kuacha kazi halisi ya kuelimisha na kuikomboa jamii. Ndio maana hawaimbi lolote wanalohisi litawakwaza wanaowapa show mbalimbali. Nasikitika kusema kuwa wengi wa wasanii wetu wamekuwa WATUMWA wa pesa na matamasha.

Simon Kitururu said...

Muziki umegeuka kuwa kama fast food. Unaupata haraka na kuusahau haraka.Kuna kipindi nilianza kuogopa kuwa hata wanamuziki wa kikweli wa ala Tanzania wangepotea baada ya kuona vikundi kibao vikianza kutegemea playback na MaDJ pekee.Lakini sasa hivi naona bendi za ala zinaanza kurudi, na hata baadhi ya wana bongo fleva wanatumia bendi na sio dj pekee. Natumaini ujumbe mzito utarudi kama tu wasikilizaji wakistukia utamu wa kupewa ujumbe mzito kiufundi na sio kirahisi tu .

Umegusia maswala ya kujibishana ya bendi za enzi, na mengi hata sikustukia kuwa kuna mtu anajibiwa au kusemwa enzi hizo.
Asante kwa topiki.

Mzee wa Changamoto said...

Asante Sana Kaka Simon. Ni kweli kuwa "playback" ilikuwa imeanza kutupeleka kaburini. Lakini nami nashukuru kuwa instruments zimeanza kurejea. Kinachosikitisha ni kuwa pamoja na kuwa na wasanii wengi wenye uwezo mkubwa wa kunogesha miziki yetu, bado wasanii wanakwepa gharama kwa kutowatumia. Mfano wanatumia kinanda badala ya real trumpets ama Guitars. It's never the same.
Lakini bado nakumbuka aliyosema Burning Spear kuwa maendeleao yanaweza kuboresha muziki lakini haimaanishi yabadili. Akimaanisha analofanya ambalo ni kupiga muziki kwa kutumia "vifaa vya asili vya kisasa" Si kinanda ku-replace trumpet, bali trumpet ambayo may be ina ubora zaidi.
Thanx for visiting and see you "next ijayo"