Monday, June 1, 2009

Bado nalia kuwa nilimlilia.

Tarehe 30 mwezi wa tano miaka 4 iliyopita nilikuwa nimemtembelea ndugu huko Delaware. Nikiwa kwa ndugu huyo huku nikijiandaa kurejea nyumbani Maryland, nilipata kadi na kuamua kupiga simu nyumbani kuwajulia hali na hasa kujua hali ya Mjomba wangu mpendwa ambaye alikuwa akiumwa. Baba alipopokea simu, tulipata jibu kuw Mjomba wangu Sylivester alikuwa ameuvua mwili na kutangulia mbele ya haki. Niliumia saana kwa kuwa nilikuwa nampenda sana. Kisha nilianza kulia kuwa nililia kwa kuwa kwa tafsiri yangu mimi, kulia ni kutokubali kuwa wakati wa mjomba kupumzika ulikuwa umefika na hakika alistahili kupumzika baada ya kutenda mema mengi tena kwa mapambano ya hali ya juu.
Mjomba alikuwa mtu mwema kwangu na kwa wengi na alikuwa akisisitiza kuhusu kusaka maendeleo kwa kiwango chochote cha uwezo ulionao na hilo alilifanya kwa matendo.

Mjomba alikuwa akiniusia kutumia muda vema na kutumia kila nafasi ninayopata kusaka mafanikio mema na ya halali.
Mjomba alikua akiishi maisha ya imani na utendaji.
Alikuwa mtu wa mwisho kwenda kumuaga kijijini na alinisindikiza huku akiniusia mengi ambayo mpaka sasa yanajirejea kama mwangwi akilini mwangu. Ni kama alijua kuwa mwendo aliokuwa akinisindikiza ndio ulikuwa wa mwisho wa mimi naye kutembea pamoja duniani.
Siku aliyofariki ndiyo nilikuwa nimenunua CD ya Luciano iitwayo HAIL THE COMFORTER na nilipoingia kwenye gari na kuwasha, wimbowa WORK THINGS OUT ukaanza kusikika. Niliusikia kwa makini na kuurudia wimbo huo kwa mwendo wa saa moja na nusu. Tangu wakati huo, kila niusikiapo, humkumbuka Uncle wangu mpendwa.

Leo ni miaka minne tangu mjomba Sylivester azikwe, na kwa bahati mbaya napata ugumu kuzuia machungu yangu juu yake. Na kila siku nimkumbukapo nasikiliza wimbo huu kwa ajili yake.
Natambua siku zinasonga lakini nikijitahidi kujizuia kumlilia uncle, bado nalia kwa kuwa nilimlilia.
God Will Work Things Out

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Mzee wa Changamoto pole sana tena sana. Nalia pamoja nawe kwani nakuelewa kabisa. Na nakushauri lia sana kwani kulia ni moja ya kutoa uchungu wako. Natumanini Mjomba wako yupo nawe kila siku amini. Astarehe kwa amani.

Fadhy Mtanga said...

Pole sana kaka. Wanasema kama kulia ni faraja kwako, basi usijizuie kulia ujisikiapo kufanya hivyo.
Pole sana kaka, lakini hakika sote twaelekea huko.
Bwana alitoa, Bwana alitwaa, jina lake libarikiwe.
Twamuombea uncle apewe pumziko la amani milele.
Amen.

Anonymous said...

Apumzike pema.
Pole kwa uchungu na kilio cha kumkosa mjomba'ko.
Inshaalah tuna imani ya kuonana kwa Manani.