Thursday, May 21, 2009

Nimekosa jibu. Nisaidie

Nimeelezwa juu ya Dada mmoja ambaye ana mtoto na hadithi imhusuyo Mama na Mtoto inasikitisha.
Ni kwamba binti huyo alipata mimba ya mmoja kati ya majambazi walilovamia nyumba yao, akam'baka na pia (kwa bahati mbaya) wakamuua Mama yake. Hakuitoa mimba (ambalo ni jambo zuri) lakini swali ni kuwa kutakuwa na mapenzi gani baina ya Mama na Mwana na kuna taswira gani ambayo mama anaiona kila amuangaliapo mwanae? Na pia atakuwa na jibu gani la kumpa mwanae iwapo atamuuliza babake?
Nilipojiweka kwenye nafasi ya kuhusika kujibu hayo, nilikosa jibu. Wewe je?

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka hapo nami najaribu kukosa majibu. Hii ni kadhia yenye kutaabisha kichwa ujaribupo kuijenga taswira halisi. Nadhani, (kwa mtazamo wangu) itamchukua muda mrefu, pengine sana, kwa dada huyo kuwa na mapenzi kwa mzaliwa huyo.
Utata na kigugumizi ni shurti kujidhihiri pindi mtoto ahitajipo ufahamu kuhusu babaye.
Ni hayo tu!

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza kabisa napenda kumpa pole sana huyo binti na pia kumfahamu baba sio lazima anaweza kumwambia amekufa. Samahani nimeumia sana jinsi watu wanavyofanya.:-(

chib said...

Kusema ukweli habari hii imenichoma sana. Nafikiri pia huyo dada atakuwa na uchungu sana, lakini kwa kuwa akina mama wameumbwa na upendo asili, sidhani kama atamchukia huyo mwanawe kwa kukumbuka yaliyompata. Ingawa najua atalaani hadi kufa majambazi yote.DRC na Darfur akina dada wengi wamepata matatizo kama hayo, lakini ni jasiri kwelikweli kwa sasa.

Komredi said...

Nimesoma na kuielewa hadithi husika hapo lakini kwakweli ni kisa cha kusikitisha sana. Kabla ya yote ningependa kumpa pole muhusika wa tukio.
Na kwa upande wake hatakuwa na muda wa kusahau kilichompata na kusababisha maumivu mengi kwa wakati mmoja, kuna kitendo cha majambazi kuingia kwenye nyumba yao, kuna kitendo cha kuuliwa mama yake, halikadhalika kuna kitendo cha kubakwa ambacho kitampelekea kutosahau maishani mwake mpaka siku yake ya mwisho kitendo ambacho kimepelekea kupata ujauzito na ndio itakuwa sababu ya yeye kutosahau tukio hilo kwa kila atakapo mwangalia mwanae. Kwani atakuwa anakumbuka njia zilizosababisha kuja kwa mwanae duniani ni za utata na za kusikitisha. Na huwenda ikapelekea kilio kwa kila atakapoulizwa na mwanae kuhusu babaye na huwenda wakati mwengine akaulizia hata alipo bibiye na hata akimwambia bibiye amekufa inawezekana atataka kujua ugonjwa au historia ya ugonjwa wa bibiye mpaka ukapelekea kifo chake.
Mimi naona kwa kifupi huyu dada hatokuwa na jibu la moja kwa moja kwa mwanae. Ni habari ya kusikitisha sana, hata mimi naona niishie hapa maana naona kamchozi kimeanza kudondokea kwenye keyboard.
Daaaahhhhh kuna binadam wanaroho mbaya na ni makatili sana. wamemuulia mama yake kisha wakambaka pia inawezekana waliondoka na mali.