Tuesday, June 16, 2009

Kama hauko juu ya juu, basi shuka chini uwe juu

Mawazoni kama Kaka Mkodo wa K.
Hakuna ubishi kuwa kuna ngazi tatu za maisha ambazo ni Juu, Kati na Chini. Na katika ngazi hizo kila ngazi ina ngazi tatu yaani ngazi ya juu ina juu, kati na chini na ya kati vivyo hivyo na pia ya chini.
Hiyo inaweza kumaanisha kuwa aliye chini katika ngazi ya juu hana thamani (zaidi ya sifa) kuliko aliye juu katika ngazi ya kati
Lakini bado kuna ukweli kuwa aliye chini katika ngazi ya juu ana heshima kuliko aliye juu katika ngazi ya kati japo mwenye heshima ana nafasi ndogo sana ya kutumia heshima hiyo kuinufaisha jamii.

Swali:
Kwani hujaona watangazaji wasio na majina kwenye redio kubwa wanapotoka na kwenda kuwa waelimishaji wakubwa kwenye redio ndogo?

Ama wasanii wasiowika kwenye vikundi vikubwa lakini wanaweza kuwa waelimishaji wakubwa na walio juu wanapokwenda kwenye vikundi vidogo?


Labda!
Walikuwa juu (kwenye sehemu zenye majina) na hawakuwa juu ya juu (maana hawakuwa na nafasi ya kuitumikia jamii huko) na sasa wameamua kushuka chini (kwenye sehemu zisizo na majina makubwa sana) na kuwa juu (kwa kuonesha uwezo na utumishi wao halisi)

Ama:
Umesahau ulivyokuwa m'babe na mtemi wakati unamaliza darasa la saba (L.Y)na kisha ukaingia kidato cha kwanza ukawa "cha mtoto"?

Ndio!
Kama wanasiasa wanaogombea urais kila uchaguzi na kushindwa wangeamua kugombea ubunge nina hakika kuwa wangepata, na hapo wangekuwa na nafasi na uwezo wa kuikosoa zaidi serikali kwa mamlaka na nguvu waliyonayo. Wangeweza kuisahihisha serikali ndani ya mfumo halali na pengine kuongeza idadi ya wapinzani na kisha kuinyoosha serikali badala ya kumuacha Dr Slaa akiibana serikali peke yake (maana hata wenzake wengine wamefyata mkia).

Swali:
Kwani Mrema, Lipumba, Mbowe, na wengine wangekuwa wabunge unadhani Bunge lingekuwa na ladha gani? Si hata wale wabunge "wafyata mkia" wangepata ujasiri wa kusema yale watakiwayo kuwasemea wananchi?

Ninaloamaanisha:
Ni kuwa wanasiasa wetu wanapenda juu (urais) ambako hawako juu (hawaaminiki na hakuna dalili za wao kupata karibuni), basi wangeshuka chini (ubunge) wawe juu (wawe wengi, wenye nguvu na uwezo wa kuibadili serikali kama haitendi sahihi) na hapo tungeweza kuibadili nchi.

Kumbuka kuwa huu ni mtazamo tu wa namna nionavyo tatizo. Labda nionavyo tatizo ndilo tatizo
Naacha!
Ila nawakumbusha wale "wapandao" kuwa wakiwa wanafikiria kuelekea juu basi wakumbuke usia wa Lucky Dube kuwa "be good to the people on your way up the ladder cause you'll need them on your way down" aliouimba kwenye chorus ya THE WAY IT IS. Nakuacha naye

Ni lini wenzetu hawa watakapo-rise up, waka-wise up kisha waka-shake up akili zako na ku-wake up kujua lipi ni jema kwa jamii yao? Lazima waamshe vichwa vyao. Wacha Everton Blender awaambie katika LIFT UP YOUR HEAD

BLESSINGS
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

kaziii kwelikweli. nawe umeanza kuwanza kama kaka Simon:-)

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

sime, sasa wewe utaitwa kinguchiro, si unajua kitururu/katururu au obutururu inamaanisha nini kwa kihaya?

sina cha kusema ila sijajua tofauti ya aliye juu na chini. mimi huwa naona watu tu na madaraja siyaoni kamwe!

kuna anayejisaidia kwenye ndoo, choo cha kioo, shimo nk, lakini wooote wanatimiza lengo, harufu, rangi nk ni ileile. kuna anayekula chakula cha ghrama kuubwa na ndogo lakini wote wanaishia kuuwa njaa au kujenga mwili, labda unielezee kwa kina hayo madaraja yanafanyaje kazi na walioko njuu mnafananaje! ni swali tu, AU?

chib said...

Nami nilifikiri nimefungua blog ya Kitururu wakati nilikuwa nimeclick ya mzee wa changamoto. Nikasema hii keyboard namna gani!!
Mchanganuo wako ni wa aina yake, unaweza kukaa siku nzima unautafakari ukweli huo..

Anonymous said...

i follow your blog!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Makala fupi nzuri yenye kufikirisha sana...Asante.

Kitururu - uwanja wako "unavamiwa" sasa!

Kwa wengi kushuka chini ni dalili ya kushindwa na hili halikubaliki.

Na wakati mwingine unaweza kushuka chini na ukashindwa kufanya lolote la maana.

Bwana Momose Cheyo - mbunge wa Bariadi Mashariki na mwenyekiti wa UPD taifa aliacha kugombea uraisi uchaguzi uliopita na kugombea ubunge ambao alipata. Sina uhakika kama kushuka kwake kumesaidia lolote!