Saturday, November 21, 2009

Penye raha pana karaha.....Kuwa makini

Sina hakika ni wangapi wanajua kuwa waajiri hutumia mitandao ya jamii (km facebook, myspace, hi5 na mingine) kuangalia SIFA za yule anayetafuta ajira kabla hawajafikiria kumuajiri?? Ukweli ni kuwa huwa wanafanya hivyo ili kusaka SIFA ZA ZIADA ambazo wengi wetu hatuzioneshi katika Resume na CV zetu za kuombea kazi. Hata namna tunavyojieleza kuwaomba watu watuachie VOICE MAIL huangaliwa na kuhusishwa na aina ya ajira unayoomba.
Ni kwa kutotambua hilo ama kwa kufikiri tumeweka "settings" zetu katika usiri wa kutosha, tunajikuta tukiendeleza maongezi na taswira ambazo kwa hakika ZINAONESHA UPANDE WA PILI wa sisi ambao si wakati wote upande huo unakuwa na manufaa kwetu.
Basi na iwe kumbukumbu kuwa TUNASTAHILI KUWA TULIVYO na kujitahidi kutokuwa na "taswira" zisizo zetu ama kutobeba kile ambacho hatuwezi kumudu gharama zake.
Ni vema kuishi kwenye mitandao hiyo kama ambavyo unaishi maisha ya kawaida ili kukuepusha na "moto-baridi" za maisha.
Nimekumbuka haya baada ya kusoma kisa cha mama mmoja ambaye amepoteza mafao yake baada ya taswira katika ukurasa wake wa facebook kumuonesha mwenye furaha kuliko alivyoandikishwa kazini. Hiki ni kisa cha kweli na mama huyo sasa anajuta kwa kuwa na picha hizo ambazo zimetibua malengo yake a maisha.
Unaweza kufuatilia kisa kamili HAPA
Tuwe makini tusije poteza yaliyo muhimu kwetu kwa raha za muda.
Kumbuka KILA PENYE RAHA KUNA UWEZEKANO WA KUWEPO KARAHA

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka, wengi tunajisahau sana katika mambo kama haya. Wakati mwingine tunabweteka na kudhani mambo mengine tuyafanyayo ni siri yetu.
Thanx kwa kutugutusha.

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante kwa taarifa hii nzuri. ni kweli wengi tunajisahau kabisa.

nanukuu "penye raha pana karaha....kuwa makini" mwisho wa kunukuu.

msemo mzuri ningefurahi kama wengi wangesoma hapa.

Faith S Hilary said...

Kaka hilo nimelitambua siku hizi hizi tu. Na wanaangalia hizi blogu pia! That's what's up if you didn't know (lol). Ndio maana I try to be as "neat" as I can...ila kweli, you can tell so many things about a person and not only about who they say they are. Thanks kwa "kukumbusha" pia :-)

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mnategemea sana kuajiriwa na nyie sasa mnaogopa kuwa wenyewe na mnataka ku-pritend. harafu hivi ni vya wadhungu. wabongo wangapi tuko face (fake) book? waajiri na ofisi zao hawapo

Mzee wa Changamoto said...

Hahahahahaaaaaaa Kamala.
Unanikumbusha rafiki yangu ambaye alikuwa anaona kinyaa kuosha kikombe chake bafuni kwa kuwa maji yake yanatoka kwenye bomba linalo-supply maji ya chooni lakini angeweza kupiga mswaki kwa maji hayohayo.

WaTanzania kupenda kuajiriwa ni MFUMO MZIMA WA ELIMU ambao ndio tulioanza kuupigia kelele ubadilike. Hili basi ntajitahidi kuliandikia siku nikijaaliwa kupata nafasi. Na kuhusu wabongo kuwa Facebook, wapo wengi saana. Zaidi ya maradufu ya wale wanaosoma blogu zetu. Sasa kama mimi na wewe tunaamini tunaweza kuwaelimisha kupitia blogu, ni kwanini tusifanye hivyo kwa wale wasiosoma blogu?
Waajiri wanaingia Kaka na ni kwa kuwa wanafanya kinachofanywa na wengine wa magharibi. Lakini hapa sijasema watu wa-pretend kuwa wasivyo, bali wasiwe vile wanavyosema wako. Ina maana usiseme huvuti sigara kama kwenye pages zako una mipicha kibao ukiwa unavuta. Usiseme hushirikiani na wana reggae ilhali kwenye pages zako unaonekana kama FAN mkubwa wa makundi hayo na usiseme huamini katika u-dini ilhali asilimia kubwa ya post zako ni za ki-dini
Ndilo kubwa nililotaka kushirikiana na wapendwa kuwa as long as unatumia mitandao hii, USISOMBWE NA MKUMBO NA KUWA VILE USIVYOTAKA KUWA ILMRADI UNATAKA KUWAFURAHISHA RAFIKI ZAKO MTANDAONI KWANI HILO LAWEZA KUKUGHARIMU MAISHA YAKO.
Blessings

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kama alivyosema Kamala, kama unategemea kuajiriwa na serikali au kuwa mwanasiasa basi pengine ni bora usiwe na blogu au akaunti ya facebook. Ni wazi kwamba mashushushu wa serikali wanapita huku (wengine naamini ni wanablogu wenzetu pia) na kuangalia kinachoendelea. Kama unategemea kuwa mwanasiasa basi siku moja jambo ulilolisema huku (hata kama ni comment tu) litageuka na kuwa "skandali" ambayo inaweza kukukosesha ulaji. Hebu fikiria Obama kama angekuwa na blogu au akaunti ya facebook. Jamaa wangechimba huko hadi kuibua visivyoibukika.

Kuna wengi tu ambao wapo wasivyo katika haya mambo ya blogu - wanaficha makucha yao na kugeuka walamba viatu kwa mategemeo kwamba siku moja wataweza kupewa ulaji serikalini. Kama ni hivi, ni afadhali kufunga blogu na kufuta akaunti za facebook kwani haina maana. Na kwangu mimi hili ni suala zito ambalo linagusa hata kiini cha maisha yenyewe. Maisha ni nini basi kama unaishi katika unafiki, hofu na maluweluwe ya kujifanya usivyo? Mimi nililijua hili kabla ya kufungua hii blogu.