Monday, March 8, 2010

Li wapi kaburi la CHAMUDATA?

Image from Toon Pool
Siku za Jumatatu mara nyingi huwa twapata burudani ya muziki wa Dansi hapa "barazani". Kwa bahati mbaya ni kuwa yule "host" wangu wa miziki aliondoa huduma hiyo bila taarifa kwa wanachama hivyo nikapoteza miziki yote ambayo nilikuwa nimeihifadhi kwenye mtandao wake kuniwezesha kupata "codes" za kuweka hapa.
Lakini kabla sijazungumzia MUZIKI WA DANSI basi ni vema kumjadili anayestahili kuulea muziki na wanamuziki wa Dansi nchini. Nazungumzia CHAMA CHA MUZIKI WA DANSI TANZANIA (CHAMUDATA).
KUNA ANAYEJUA CHAMUDATA INAENDELEA VIPI?
Kwa hakika chama hiki (kama kipo) kinastahili kujikita zaidi katika kuuendeleza muziki na hata wanamuziki wake. Lakini tofauti na utekelezaji wa jukumu hilo, chama hiki kimekuwa kikiishiwa nguvu na kupoteza mwelekeo na hata kuonekana kukumbwa na kashikashi za hapa na pale na hasa za kiutawala. Ni miezi mitatu iliyopita niliposoma kuhusu kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti wake Juma Ubao amejiuzulu. Katika HABARI HII, Mzee Ubao alinukuliwa akisema "Nimechukuwa uamuzi huu kwa sababu zifuatazo, (kwanza ) viongozi tuliopo madarakani hatuna ushirikiano na mapenzi baina yetu, hivyo kuendesha shughuli za chama kwa usiri, chuki na kubaguana. Hivyo kushindwa kufikia malengo ya chama tangu tulipoanza kukaimu nafasi hizi kama vile kushindwa kufanya uchaguzi mkuu ambao chama kimeshindwa kufanya kwa takriban miaka 12".
Sikushangazwa na kujiuzulu huku kwani "malezi" na "muendelezo" na hata "harakati" za kuzisaidia bendi zetu kukua katika "MUZIKI WA DANSI WA TANZANIA" hatuzioni tena. Nakumbuka niliposikia kuhusu Mashindano ya Bendi Bora Tanzania (MASHIBOTA) ambayo kama yangefanyika kwa ufasaha na kuongezewa chachu mbalimbali za uhakika, yangekuwa CHANGAMOTO NJEEMA kwa bendi zetu na muziki.
Labda pia kuwaangalia walezi wa CHAMUDATA ambao ni BASATA ambao kwa mujibu wa tovuti yao, wanasema
KAZI ZA BASATA
Kwa mujibu wa Sheria no. 23 ya mwaka 1984 iliyounda Baraza la Sanaa la Taifa, kazi za Baraza ni:
◦Kufufua na kuhimiza maendeleo ya kazi za sanaa.
◦Kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya sanaa.
◦Kutoa ushauri, na misaada ya kitaalamu kwa watu au asasi zinazojihusisha na sanaa.
Kuratibu shughuli za sanaa zinazofanywa na watu au asasi mbalimbali.
◦Kutoa na kuimarisha mipango ya mafunzo kwa wadau wa sanaa.
Kuishauri Serikali juu ya mambo yahusuyo maendeleo na uzalishaji wa kazi za sanaa.
◦Kuhamasisha maendeleo ya sanaa kwa njia ya maonyesho, mashindano, matamasha, warsha na semina.
◦Kusajili wasanii na wale wote wanaojihusisha na shughuli za sanaa
.

Kumbuka kuwa waweza kupitia matoleo mengine ya miziki ya "Zilipendwa" yaliyowahi kubandikwa bloguni humu kwa kuBOFYA HAPA, ama kupitia mitandao rafiki HAPA na pia kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania HAPA

1 comment:

Bennet said...

Wamejisahau na watu wakawasahau ndio maana hata kwenye tamasha la malaria hawakualikwa wakati bendi ni nyingi tu na karibia zote ziko juu