Sunday, June 5, 2011

WALIWAZA NINI?????? Kweli kila mtu na "ngekewa" yake

Picha ya maktaba ikionyesha ndege ikisindikizwa na ndege ya jeshi kuelekea uwanjani kutua
Kama ilikupita, basi habari ni kwamba siku ya jumapili Mei 29, ndege ya United Airlines iliyokuwa na abiria 144 katika safari nambari 990 kutoka uwanja wa ndege wa kimtaifa wa Washington Dulles kuelekea Ghana ililazimika kurejea Dulles, ikiwa imesindikizwa na ndege mbili za kijeshi za F-16. Kisa?....Abiria walikuwa wakipigana ndani ya ndege baada ya mmoja kutaka "kulaza kiti" huku akipuuza ombi la aliye nyuma yake la kutofanya hivyo. Kilichofuata ni ugomvi wa masumbwi ambao ulisababisha usumbufu kwenye ndege hiyo. Ndipo rubani alipokiarifu chumba cha kuongoza ndege kuwa licha ya kwamba abiria walikuwa wameketi, lakini hawakuwa chini ya ulinzi na hakudhani kuwa ilikuwa jambo la busara kuendelea na safari. Labda kuna ukweli kwamba alihofia kinachoweza kutokea wakishaanza masaa kadhaa ya kukatisha bahari ambako asingekuwa na mahala pa kufanya "emergency landing" hivyo akaona ni bora arejee Dulles "kuwashusha". Lakini pia kumekuwa na hisia kwamba magaidi wanaweza kuanzisha kile kinachoweza kuonekana kama UGOMVI baina yao katika harakati za kufanya uhalifu wao.
Sikiliza mawasiliano baina ya rubani na mnara wa kuongoza ndege hapa chini

Ni katika hilo, rubani aliongea na mnara wa kuongoza ndege na kisha ikaamuliwa kwamba ndege hiyo izunguke Washington kwa dk 25 kupunguza mafuta. Ikumbukwe kwamba ndege ya Boeing 767 ina uwezo wa kubeba galoni 16,700 za mafuta, na kwa mwendo wa maili 5000 kwenda Accra, inahitaji karibu kiasi hicho. Lakini pia licha ya uwezo wa kubeba kiasi hicho ambacho ni sawa na tani 57, inaweza kutua nayo. Moja ya ndege za United Airlines Boeing 767. Ni kama ile iliyorejeshwa uwanjani kutokana na ugomvi wa abiria.
Anyway...Mara baada ya uamuzi wa kuirejesha Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dulles uliopo nje kidogo ya Virginia, ndege hiyo iligeuza na kurejea, na punde ilipoingia kwenye anga la Washington DC, ndege mbili za kivita za F-16 zikaizingira ndege hiyi (zikiwa futi 1000 juu yake) mpaka ilipotua. Safari ikaahirishwa mpaka kesho yake.
La kushangaza (kwa upeo wangu) ni kuwa askari waliitwa, wakawaona wahusika na kisha wakawaachia bila kuwafungulia mashitaka yoyote.
1: Yaani watu wamecheleweshwa kwa usiku mzima.
2: Ndege imelazimika kutua na mafuta kuliko inayostahili kutua nayo (kwa wenzangu mnaojishughulisha na vifaa vya usafiri huu mnajua uchunguzi utakaotakiwa kufanyika kuhakikisha iko salama)
3: Ndege za kivita zimerushwa kusindikiza ndege hiyo.
4: Ndege imezunguka kwa dk 25 kuchoma mafuta ili kutua na kisha kujaza kwingine ili wasafiri waondoke na kisha wanasema watu hao hawana makosa?
NI WANGAPI WAMECHELEWA SHUGHULI ZAO kwa kuwa walilazimika kulala Virginia badala ya kuamkia Ghana? Mafuta ya ndege za kivita yanalipwa na nani? Mzunguko mzima wa marubani na ratiba ya ndege je?
NA KAMA HAWAKUFUNGULIWA MASHITAKA.......BASI KWELI WANA "NGEKEWA YAO"
Nadhani wangewekwa mlangoni ili kila anayetoka kwenye ndege "awagonge makwenzi mawili".

Lakini la kuwaza hapa ni kuwa WALIWAZA NINI kupigana kiasi hicho ndani ya ndege? Na je kampuni ya United Airline ambayo haikuwa na mtu wa kuzuia wasafiri hawa, wataeleza vipi kuhusu usalama wa abiria wao? WANAWAZA NINI KUSAFIRISHA WATU WOTE BILA MTU WA KUTULIZA GHASIA?
NAWAZA KWA SAUTI TUUUUUUU!!!!!!!!!!!!!!!

***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya. Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki BOFYA HAPA"***

7 comments:

Fadhy Mtanga said...

duuh....nimeishia kustaajabia kabisa...nini makwenzi? Ningalikuwapo pahala hapo walahi ningaliwakata ngwara za nguvu

Goodman Manyanya Phiri said...

Mashtaka yangekuwa ya nini? Kama mimi nimelaza kiti changu si haki yangu?


Au kama mimi namkemea aliekaaa mbele yangu kwa kulaza kiti chake na kunimwagia chai yangu, mashtaka hata hapo yawe ya nini?


Wendeshamashtaka nao ni waangalifu kutoanzisha kesi ambao hakimu ataitupilia mbali tena kwa kejeli, ndio maana yote hapo, Mkuu!

Mzee wa Changamoto said...

Kaka Fadhy.. We staajabu tu kama mimi. Labda kuna atakayekuja na jibu kwetu.
Kaka Phiri. Mashitaka yangeweza kuwepo (kwa mtazamo wangu).
Siamini kama kilichowafanya warudishe dege ni kulaza kiti, ama kuzuia, bali VURUGU zilizotokea baada ya jaribio la kulaza na kuzuia. Kuwasababisha watu kulala mpaka kesho yake kwa sababu ya vurugu walizofanya ni usumbufu tosha. Kulazimisha ndege za kivita "kuizingira" mpaka itue, ni usumbufu tosha. Kuisababisha ndege kutua na mafuta kiasi hicho ambacho hakipendezwi na watengenezaji, ni usumbufu tosha.
Kuwa na haki haimaanishi kuwa hautashitakiwa usipoitumia vema. Nina haki ya kuongea, lakini naweza kushitakiwa ikiwa nitaongea uongo, matusi ama kashfa.
Kwa hiyo bado naamini WALISTAHILI MASHITAKA

emu-three said...

Unajua mkuu,`kila jambo halitokei hivihivi tu, hutokea ili iwe sababu, huenda hatuijui,...AU WENYEWE WANAJUA, Au hakuna anayejua ila mwenye mamlaka na roho zetu na sisi wenyewe anajua....!

Raymond Mkandawile said...

Nina mashaka huenda hao watu walikuwa ni waafrica wezentu japo sina hakika na hilo,ila ninachotaka kusema ni kwamba huenda huyo mlaza kiti akawa na haki japokuwa alitakiwa pia kutumia busara (please) kwani unaweza ukawa na haki lakini usijue jinsi ya kuidai na kuonekana huna maana..na hicho ndicho kilichotokea hapo wote wakawa mafahari na kuamua kuzipanga ngumi.....
Kwakweli naungana na mzee wa changamoto hawa jamaa waistahili kufunguliwa mashitaka ya kufanya vurugu kwenye halaiki na pia usumbufu waliosababisha ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo...

SN said...

Nadhani wangewekwa mlangoni ili kila anayetoka kwenye ndege "awagonge makwenzi mawili".

Hiyo hapo imenivunja mbavu. Ila mi sikuifikiria saaana; nilijua ni taratibu tu za kiusalama ili kuepuka risks zozote. Ila ndio hivyo, wale jamaa hawajafanywa chochote.

Hii stand up comedy inafanana sana na huu mkasa (no pun intended re: proanity):

http://youtu.be/ksbBMMd3oqA

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Niliisoma habari hii na kufuatilia maoni ya wadau kule Huffington post. Inasemekana ulabu pia ulichangia. Ukikamata mavodka kule juu halafu mtu akakuudhi mambo yaweza charuka...Huyu ndiye binadamu a.k.a Homo Sapiens!