Tuesday, April 17, 2012

Tanzania Yangu.....Isiyojua kuziba ufa wala kujenga ukuta (III)

Ni juma moja kamili tangu Tanzania na ulimwengu ushuhudia mzishi ya mmoja wa nyota wakubwa katika tasnia ya filamu nchini Tanzania, Bwn. Steven Kanumba. Na pia ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa mpenziwe na mtu wa mwisho kuwa naye akiwa hai, Bi Elizabeth Michael "Lulu".
Na ni ukweli usiopingika kuwa ndani ya wiki moja (ama niseme siku tatu za Jumamozi hadi Jumanne), tumeshuhudia jina KANUMBA likitajwa, kuandikwa na kuelezwa kwa wingi (pengine) kuliko jina jingine lolote miongoni mwa waTanzania.
Mengi yaliandikwa kuhusu kifo chake, mengi yamehusishwa na kifo chake na wengine hata wakajaribu "kuchunguza" kifo chake kwa namna kilivyomkuta na ambavyo angeweza kukiepuka.
Na wengi wanaamini kuwa (pengine) asingekufa iwapo asingekuwa na MPENZIWE Elizabeth Michael almaaruf Lulu.Na sasa mtoto Lulu (namuita mtoto kwa kuwa kwa mujibu wa wazazi wake, na kwa vyeti walivyosema watawakilisha, Lulu bado hajatimiza miaka 18) anabebeshwa lawama kubwa na HUKUMU kuhusu kifo cha aliyekuwa msanii na mpenzi wake, Steven.
Wengi wamefikia hatua ya kumuita Lulu MUUAJI kutokana na mashitaka yanayomkabili japo hajakutwa na hatia.
Ni kweli kuwa Lulu alikuwa mtu wa mwisho kuwa na Kanumba wakati akiwa hai, na ni kweli kuwa kifo chake kimeelezwa hapa kuwa kilitokana na tatizo la mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain Concussion, bado haijawa wazi kuwa ni kipi kilichosababisha Kanumba kuanguka hasa kwa kuwa uchunguzi wa awali wa Polisi uliotangazwa hapa na Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela ulionyesha kuwa POMBE kali (Whisky) aina ya Jacky Daniel ilikuwa moja ya sababu za kifo chake.
Lakini TUHUMA ZOTE ZA LULU ZINATOKANA NA UKWELI KUWA WATU WANAANGALIA TATIZO HILI KUANZIA April 6, 2012 badala ya kuangalia zaidi ya hapo.
Nimekwishasema mara kadhaa kuwa "japo dalili za mti kukauka zinaonekana kwenye majani, lakini ukitaka kurejesha uhai wa mti haumwagilii majani, bali unamwagilia mizizi". NI WAKATI WA KUANZA KUANGALIA MZIZI WA TATIZO HILI.
Na hii ndio njia pekee itakayoleta suluhisho pekee.

KWANZA.....WAZAZI WA LULU.
Tumesikia mara kadhaa kuhusu kauli tata juu ya umri wa Lulu. Polisi wanasema ana miaka 18 huku wazazi wake wakihimiza kuwa atatimiza miaka 17 tarehe 17 mwezi huu.
Lakini mtu yeyote anayemfuatilia Lulu ama habari zake anajua kuwa amekuwa akisema kuwa ana miaka 18, na kwa wakati wote huo, wazazi wake wamekuwa kimya juu ya hilo.
Ni wakati ambao WAZAZI WANATAKIWA KUWA WAFUATILIAJI WA MAISHA YA WATOTO WAO.
Na kwa hakika naamini kuwa kama Lulu alikuwa mdogo kiasi hicho, hata MIKATABA YAKE YA KAZI ILIPASWA KUSIMAMIWA NA WAZAZI.

PILI......WASIMAMIZI WA FILAMU NCHINI
Huu Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) unajua fika kuwa watoto wanatumika kwenye kazi za filamu, lakini haionekani kuwa kulikuwa ama kuna mkakati maalum wa KUWAWAJIBISHA WALE WANAOWATUMIA WATOTO HAWA KIMAPENZI. Ukiweka pembeni utata wa kauli kuhusu umri wa sasa wa Lulu, bado yasemekana alianza mahusiano na wasanii wenzake muda uliopita kidogo. Kwa maana nyingine, hata kama alianza miaka miwli iliyopita, kuna "MTU MZIMA" ALIYEKUWA AKIFANYA MAPENZI NA MTOTO MDOGO. Ni sheria zipi zinazowalinda watoto kwenye tasnia ya filamu nchini? Na ni wapi ilipo nafasi ya wazazi kwenye kufuatilia mienendo ya watoto wao?

TATU..... WANAHABARI.
Hawa wamekuwa wakihukumu mpaka BARAZA LA HABARI NCHINI limeingilia kati na kutoa onyo kuhusiana na kauli mbaya zinazotolewa. Na naamini hii ilikuwa ni kwa WAANDISHI WA HABARI ambao wako chini ya uangalizi wa Baraza hilo.
Lakini pia wapo "WAHANDISI WA HABARI" ambao hawakujali na hawajali MAADILI YA UANDISHI na wameshindwa hata kuheshimu kesi, marehemu, mtuhumiwa na jamii kwa kuandika watakalo na kuweka picha watakazo. Ni wakati ambao Baraza la Habari Tanzania linatakiwa kuikumbusha jamii kuwa "kuwa na uwezo wa kupata picha inayoweza kuwa habari, haimaanishi kuwa inakupa haki ya kufaya hivyo" Ningependa kujua waliopiga picha za maiti ya Kanumba ikiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti na kama walifuata taratibu za kisheria kwa kufanya vile.

NNE......JAMII.
Ni kweli kuwa mtu anapokufa tunaogopa kusema ukweli wowote kumhusu? Ni kweli kuwa iwapo Kanumba angeumia tu na kubaki hai, lawama zote zingeenda kwa Lulu? Ama kwa kuwa Kanumba amefariki basi kile ambacho tungemlaumu nacho iwapo angekuwa hai sasa kinahalaliswa?
Lulu si mtu kamili, Lulu ana makosa yake, lakini ukweli ni kuwa Kanumba alikuwa muharibifu kwa kuwa na mahusiano na mtoto mdogo wa umri huu. Na zaidi ni kuwa jamii imekuwa ikiwanufaisha wale wanaoandika habari kuhusu Lulu kwa kununua magazeti, kuyasoma na hata kufurahia ama kumkebehi na kupuuza NIA HASA ya kumsaidia mtoto huyu.
Vyombo vya habari vimeandika habari ambazo JAMII ILIPASWA KUSHITUKA NA KUULIZA
Kama ni kweli kuwa binti huyu ndio kwanza ametimiza miaka 18........
1: Ni vipi ameweza kuwa na wanaume 10 ndani ya kipindi kifupi?
2: Kama alianza kabla. Ni hatua zipi zilizochukuliwa kuwanasa waliomtenda MTOTO?
3: Kama ni uongo. Ni hatua gani zilizochukuliwa kwa mwandishi huyo?

Kama nilivyosema kwenye tovuti JUKWAA HURU ya Kakangu Rama Msangi, "Tumetengeneza “guruneti” tukasahau tulipoliweka, sasa tumelikanyaga, limetulipukia, tunajifanya hatukimbuki kuwa “NI UBUNIFU WETU”

Tusipojifunza kutokana na kifo cha Kanumba, tutaendelea kuona matukio kama haya yakijirudia, na kwa kuendelea kutumalizia kizazi.
Ningependa kuona wale "waliomkula" mtoto Lulu akiwa na umri mdogo wanafikishwa mahakamani ili wakabiliane na mashtaka. WANAJULIKANA, NI MAARUFU, NA WALISHIRIKI VEMA KWENYE MAZISHI YA MTU AMBAYE "ALIENDELEZA WALICHOANZISHA WAO"
Lakini pia ninawaza kama hili litatokea maana naizungumzia TANZANIA YANGU..... ISIYOJUA KUZIBA UFA, WALA KUJENGA UKUTA

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

By the way ......... HAPPY BIRTHDAY ELIZABETH "LULU"

4 comments:

Emmanuel said...

kaka umesema vema. Nchi yetu inahitaji watu kuijenga hiki kizazi na kuiandaa jingine. Kila mtu ka kachoka vile

Anonymous said...

Well said kaka! - Mary

mwaijande said...

maelezo yako ni ukweli mtupu laiti kama kungekuwa na ufuatiliaji wa sheria basi huenda sheria mpya ingetungwa kutokana na haya maelezo au la some amendments should be made to the existings laws if there is one. kazi nzuri bandio

mwaijande said...

maelezo yako ni ukweli mtupu laiti kama kungekuwa na ufuatiliaji wa sheria basi huenda sheria mpya ingetungwa kutokana na haya maelezo au la some amendments should be made to the existings laws if there is one. kazi nzuri bandio