Monday, August 25, 2008

Karibu

Ni mengi ambayo hutokea ulimwenguni ambayo kwa bahati nzuri ama mbaya hatuwezi kujua upande wa pili wayo kwa kuwa hatuwezi kuwa na pande zote kwa wakati mmoja na wala hatuwezi kujua (zaidi ya kuhisi) nini kitatokea ama kingetokea kama tungefanya tofauti na tulivyofanya sasa. Ina maana kuwa maisha ni mapana na yenye mafanikio na maanguko zaidi ya tunavyoweza kufikiria maana hujui kama lile ulilokwepa kulifanya lingekuweka kwenye mafanikio ama maanguko hasa kwa wakati ujao. Nina maana ya kwamba kuna mafanikio yanayopatikana baada ya kupitia majaribio meengi bila kukata tamaa na majaribio wapitiayo wengi waliofanikiwa huwa wanayachukulia kama CHANGAMOTO (challenge) kwao. Nimejifunza kuwa kama kitu hukipendi, basi magumu yake yatakuwa kisingizio cha kuacha ama kutoanza kufanya jambo, na kama wakipenda, basi magumu kwako yatakuwa changamoto kuelekea mafanikio. Tutambue kuwa hatukukimbia kabla ya kutembea na wala hatukutembea kabla ya kutambaa. Hivyo kukaa chini ukaona mafanikio ya walio mbali katika yale upendayo ni CHANGAMOTO kuelekea mafanikio.
Nilipoanza kujishughulisha na mambo ya habari nilipenda kuwa kama nyota nilowaheshimu na kupenda kazi zao, lakini pia niliogopa na kuamua kuweka kando mambo hayo, lakini baadae nilipokubali kukabiliana na CHANGAMOTO hiyo, niliona urahisi wake (japo kidogo) kuelekea zaidi ya nilipodhani ningefika japo sikuwa karibu na wale nilopenda kuwa kama wao. Lakini nikawa mimi kama mimi ndani ya nifanyalo. Nilipoanza mambo ya picha, nikashauriwa na Kaka Michuzi kufanya hiki nifanyacho leo lakini nikawa na visingizio viiingi vya kutofanya hivi kwa kuwa nilishaona mengi mema yafanywayo na walionitangulia nami nikahisi siko karibu nao kwa namna yoyote. Lakini nimegundua kuwa sikuwa sahihi katika hilo. Nimerejea kule nilikoanzia kuwa ni kitu nipendacho kufanya, ni CHANGAMOTO kwangu na nitafanya kwa kuwa najua nitafanikisha.
Na hii iwe CHANGAMOTO YETU ambayo ni KUFANYA KILA JEMA TUTAKALO NA KUPENDA KUFANYA HUKU TUKICHUKULIA MAGUMU YATUKUMBAYO KAMA CHANGAMOTO.
Karibu kwenye "ukanda wa changamoto" (challenge zone) kutoa ama kupokea changamoto mbalimbali.

No comments: