Thursday, October 23, 2008

MTAZAMO: Pale SERIKALI inapochochea ujinga

Choma tu hivyo vya zamani, twawaletea vipya
Ikulu ya kwanza Tanganyika ilivyotelekezwa huko Bagamoyo
Majengo ya kale "yakipigwa nyundo" kupisha ujenzi mpya huko Tanga
Asante ya picha kwa Da Chemi na MichuziJr
Kama wanangu watakua bila kuona historia ya asili yao basi watapungukiwa ufahamu wa asili yao hali itakayowafanya wawe kama WAJINGA. Na ni aibu kwa Taifa kuwa na kizazi ambacho sio tu hakioni historia yao, lakini yawezekana hata wasiweze kuisoma maana inateketezwa. Haya nimeyaandika baada ya kushuhudia taswira za hivi karibuni ambapo (kama uonavyo taswira hapo juu) vitabu ambavyo vilitumika kuwaelimisha viongozi na wakubwa zetu na pengine sisi wa rika la kati vinateketezwa kwa kuwa wameamua kuja na mitaala mipya / vitabu vipya. Pia majengo ya kale na sehemu za kihistoria zinazidi kuteketezwa kila iitwayo leo kupisha ujenzi wa "vikwangua anga".
Marcus Garvey alisema "A people without the knowledge of their past history, origin and culture is like a tree without roots."
Kama nasi tunakuwa na sehemu ya harakati za kutokomeza historia na na kuwafanya watoto wetu wawe wajinga, basi nasi ni wajinga na tunaochochea ujinga kwa vizazi vijavyo na kama serikali yenye jukumu, usimamizi na ama mamlaka ya kutunza kumbukumbu muhimu za kihistoria kwa ajili ya vizazi vijavyo haifanyi juhudi zozote kutunza historia hizo, basi nayo (Serikali) inachochea ujinga huu.
SERIKALI kuchochea ujinga? Ndio. Wala hujasoma kimakosa. Serikali ndicho chombo chenye mamlaka ya juu zaidi kimaamuzi nchini na chenye uwezo wa kuhakikisha, kuhalalisha na hata kusimamisha mambo mengi yanayotendeka nchini kwa manufaa ya wananchi na hasa vizazi vijavyo.
Lakini kupitia Magazeti tando na habari katika tovuti mbalimbali tumekuwa tukishuhudia ama kusoma juu ya kuharibiwa kwa historia na kumbukumbu nyiingi ambazo zina manufaa saana kwa wanetu na wajukuu wetu wa kisingizio cha "kupisha maendeleo" mapya yajayo. Kwa mtazamo wangu (na narejea tena mtazamo wangu) huu ni Ujinga maana kwa hakika kama walivyosema Morgan Heritage kuwa "every man must know their past, so we can stand firm in the future" nasi tulistahili kuyatunza haya ya kale kwa gharama zozote kwa manufaa ya vizazi vijavyo ili nao baadae waweze kutambua na kuoanisha walipo na walipokuwa wazazi wao. Bila kuwa na cha kuoanisha unadhani watatambuaje na kupangaje mustakabali wao? Ninapoona habari zainazoonesha kuharibiwa kwa sehemu za kihistoria kama ilivyo ubomoaji wa Majengo ya kale huko Tanga kwa kisingizio cha kupisha ujenzi mpya, ama utelekezwaji wa sehemu za kihistoria ambazo watalii na wajukuu zetu wangejifunza mengi juu ya tulikotoka mpaka harakati zetu za uhuru (kama ilivyoripotiwa na Michuzi Jr (hapa)] na sasa nisomapo habari juu ya kuchomwa kwa vitabu vya zamani vilivyotumika katika kutufundisha ili kupisha uingizwaji wa vitabu vipya ambako yaonekana kulianza zamani saana kama ilivyoandikwa na Da Chemi kwenye intro ya habari ya Da Subi (hapa) na Da Subi kwenye blog ya jamii ambako wengi wameona hili kama tatizo (hapa) nahisi kukerwa.
Najiuliza:
1: Ni kweli kuwa Serikali imeshindwa kuyaona haya yanayoonekana machoni mwa ulimwengu wote?
2: Na kama hawakuamua / kuruhusu yatendeke na hawazuii, kwanini nisiseme wanachochea ujinga?
3: Mbona nchi nyingi zinatunza saana "ukale" wao na kujivunia? Tunaona miji ikiitwaa Historical towns ama Old Towns ama Historical Streets ili kuonesha walikotoka na kwa hakika ni kati ya sehemu aghali kuishi ama kununua nyumba zake na zina masharti saana katika kuzikarabati maana hawataki kuharibu mtazamo wa kile kilichokuwapo.
4: Kweli nasi hatulioni hili?
Aibu kwetu na inashangaza saana.
Kwa bahati mbaya sana naona KAMA KUPOTEZA HISTORIA NI UJINGA, NA HAYA YANATENDEKA KWA MGONGO WA SERIKALI, NA HAKUNA KIONGOZI WA SERIKALI ANAYESIMAMA KUYAPINGA AMA KUKANUSHA UHUSIKA WAKE KATIKA HILI, BASI KWA HIARI AMA BAHATI MBAYA NAIONA SERIKALI IKICHOCHEA UJINGA.

Ni mtazamo tuuuuuu na ndivyo nionavyo tatizo. Labda hilo ndilo tatizo.

1 comment:

Fadhy Mtanga said...

Kaka Mubelwa ama kwa hakika nakubaliana nawe kwa uchungu mkubwa. Mimi nimetunza baadhi ya madaftari ya primary ili ikibidi hata wajukuu waje wayaone...lakini serikali inashindwa kufanya hivi.
Ni aibu sana