Ni MSIMU mwingine ambao tunajua kuwa wengi hurejea nyumbani kwa mapumziko ya Krismas na Mwaka Mpya. Na mara zote huwa ni furaha saana msimu huu ufikapo, lakini kama Lucky Dube alivyoimba kuwa "where there's a pleasure, there's always a danger" nami nakumbusha kuwa ule "uroho" wa pesa wa kupandisha nauli, kuongeza safari za mabasi na vyombo vingine vya usafiri bila kujali matengenezo na ukarabati wa vyombo hivyo, mashindano ya "nani atafika wa kwanza" baina ya vyombo hivyo na pia kutenda kazi kwa muda mrefu bila kupumzika kwa waongoza usafiri huo kumekuwa kukizua vilio kila mwaka na hata wale wasiopoteza maisha wanabaki na maumivu ama vilema vya Maisha.
Waswahili wanasema "aisifiaye mvua imemnyea" nami ninavyoandika hivi ni kwa kuwa miaka 9 kamili iliyopita (Des 23, 1999) tulipata ajali mbaya ya basi la Tawfiq huko Nakuru Kenya ambako zaidi ya watu 10 walikufa papo hapo na inasemekana namba ya waliofariki ilifika 20 (japo hatukuthibitishiwa na sishangazwi na hili). Mpaka leo nina kumbukumbu "mbichi" ya kilichotokea hasa baada ya mtu tuliyekuwa tukiongea muda mchache kabla ya ajali kupoteza maisha. Iliuma kusikia tetesi kuwa Dereva (ambaye naye kwa bahati mbaya alifariki)hakupumzika aliporejea toka safari yake ya kwanza siku hiyo (ambayo ilikuwa ikichukua zaidi ya masaa 30) na tulipata ajali hiyo mbaya kwa kile kilichoonekana kuwa alisinzia na kuligonga gari la mizigo lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara na ambalo alilipita alipokuwa akirejea Dar (tulisikia akiitwa/ akiamshwa alipoanza kwenda nje ya barabara ambapo ilikuwa too late kukwepa lori hilo). Ilisikitisha pia kuona wengi tulioanza nao safari kuiwahi Krismas tuliwaacha Nakuru. Majeraha yalikuwa ni kwa viwango mbalimbali lakini kusikia ajali zinaendelea tena kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika inaniuma sana kwa kuwa mpaka leo hii naendelea na matibabu yaliyotokana na ajali hiyo.
Kuna raha wakati huu wa sikukuu na kuna pesa pia kwa kuwa watu wana uhitaji wa kwenda kujumuika na familia zao, lakini kama wamiliki hawatakuwa makini, basi kutaendelea kuwa na karaha kwa wale ambao licha ya kulipa pesa nyingi, bado wanaweza kutofika waendako, ama kufika wakiwa na maumivu ama mapungufu na kibaya zaidi wasipate malipo yoyote kukidhi matibabu yao kama ilvyotokea kwa baadhi yetu.
Tukumbuke kuwa katika kila raha tuisakayo wakati huu wa sikuku, kuna uwezekano wa karaha kuambatana nayo. Na tuwe waangalifu na wajalifun na waheshimifu kwetu na kwa wenzetu.
Amani, Upendo na Usalama kwenu nyote nyakati hizi.
Tuesday, December 23, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
2 comments:
MTWIBA NIKIKUPA POLE NITAKUWA KAMA VILE NAKUKUMBUSHA MACHUNGU YALIYOPITA.
YALIYOPITA SI NDWELE, TUGANGE YAJAYO, NIVYEMA UKIWAKUMBUSHA MADEREVA NA WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI KUCHUNGA USALAMA WA ABIRIA HASA KATIKA KIPINDI HIKI CHA MWISHO WA MWAKA.
KIPINDI HIKI NI KIGUMU SANA KWANI AJALI NYINGI ZA KIZEMBE ZINATOKEA SANA KIPINDI HIKI CHA MWISHO WA MWAKA.
Cha ajabu ni kwamba sina uhakika ni kwanini binadamu mpenda siku kuu anachagua lini sikukuu hataikiwa kama ya kukimbizwa na ng'ombe kama wafanyavyo Spain!:-(
Post a Comment