Wednesday, December 17, 2008

Tuko tulivyo kutokana na maisha yetu yaliyopita, na kwa ajili ya maisha yetu yajayo

Tunaelekea kuumaliza mwaka 2008. Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 nilisoma "Napasua Jipu" yake Kaka Eric Shigongo wa Global Publishers na akasema "Kuingia mwaka mpya si bahati, ni nafasi ya ziada". Nakubaliana naye na kila mwaka ufikapo natazama nyuma kujiuliza maswali na kufanya tathmini ya maisha yangu kwa mwaka niumalizao. Kuna wakati tafsiri huwa si nzuri na hapo hujiuliza kama nilistahili kuwa na matokeo ya hivyo. Kisha waja ule msemowa UTAVUNA ULICHOPANDA ambao huwa siuamini wakati wote maana sitaki amini kuwa watu wangu nyumbani (kijijini) walipanda UMASKINI, UKOSEFU WA HUDUMA MUHIMU NA MATESO wanayovuna sasa ikiwa ni takribani nusu karne tangu tuwe huru. Naamini kuwa wanaotusaidia kupanda baadhi ya haya tuvunayo. Lakini naamini ya kuwa kama tukiendelea kuishi, basi juhudi za sasa katika maisha tuishiyo na mahusiano tujengayo na wale watuzungukao yataathiri maisha yetu yajayo kwa namna moja ama nyingine. TAZAMA maisha yako uliyonayo sasa na watu wakuzungukao na hata namna ulivyokutana na kuhusiana nao. Pia tazama mazingira yako ya sasa na angalia namna ulivyofika hapo ulipo. Kisha tazama historia ya maisha yako tangu malezi mpaka "links" zilizokufikisha hapo ulipo halafu utathmini yafuatayo. Kama umekulia mjini, unadhani ungekuwa hapo ulipo endapo malezi yako yangekuwa kijijini? Na hao ambao kwa namna moja ama nyingine wamefanikisha uwepo wako katika hali uliyonayo ungeonana nao? Ina maana wasingekuwepo basi wasingekuwezesha na kama wasingekuwezesha basi usingekuwa hapo ulipo. Swali ni kwamba ungekuwa wapi? Na kama kijijini ndiko kulikokufanya uwe na akili, fikra na mtazamo wa maisha ulionao sasa, unadhani ungekuwa mjini ungeharibikiwa ama kutoyathamini maisha kwa namna ufanyavyo sasa? Ama ungeyatambua kwa ubora zaidi? KWANI umeshasoma habari za watu ambao wamefanikiwa saana baada ya kutoka jela na wanakiri kuwa mafanikio yao yametokana na shughuli ambazo hawakuwahi kuzifikiria kabla ya kwenda jela na hawadhani kama kuna mtu angeweza kuwashawishi kuzifanya? Wengine walienda jela kwa kuwa walifanya makosa na kama wasingeenda huko labda wangeuawa na wenye hasira kama Dr Faustine alivyoripoti aliyeuawa siku moja baada ya msamaha wa Rais. Lakini pia walipokuwa wakienda walilaumu hayo wakidhani dunia imewageuka, kumbe ndio ulikuwa wakati wa kuigeuza dunia yao.
NISEME kuwa "mateso" yote yana namna ya tunayoweza kuyatumia kujifunza na kufanikisha maisha yetu kuanzia wakati huo wa mateso kwetu na jamii yetu kwa ujumla. Lucky Dub alisema "It is a give or take world, we gotta take what we can, when we can make the best of it" akimaanisha kuwa katika hali yoyote, kuna upande wenye unafuu na ambao tunaweza kuutumia kutafuta mafanikio halali. Nasio naye akasema "I'm living in the positive, cause i know good will conquer evil, Jah is there to admist the battle, and i know Love will overcome hatred"
KWA HIYO hakuna haja ya kukaa na kulia juu ya maisha tuliyojiingiza ama kuingizwa, bali kuchukua hatua na mtazamo chanya wa kuyabadili kwa njia njema kuelekea mafanikioni. Na hili lawezekana saana kama kwa pamoja tutaamua kuchukua hatua muafaka katika hili tukitambua kuwa maisha yetu yameathiriwa na historia yetu na haya tuishiyo yataathiri mustakabali wetu. Yaani "we're who we are because of our pasts and for our futures"
Na huu ni mtazamo wangu kulingana na namna nionavyo tujionavyo. Naweza kuwa sivyo kwa kuona visivyo.
Blessings

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Mzee changamoto leo darasa nzuri sana! Maisha NI kweli watu lazima tutazame wapi tumetoka na wapi tunakwenda. Ila kuna wengi wanafikiri maisha (mazuri) yanapatikana kirahisi sana. Hapana bila kupata MATESO haiwezekana. kwasababu huwezi kukaa tu na kufikiri yatakuja yanyewe. Hii imenigusa sana nenda kwenye blog yangu na soma kuhusu maisha yangu utaona. asante! ila nashindwa kuendelea

Simon Kitururu said...

Nakubaliana kabisa na mtazamo wako katika swal Mzee wa changamoto!

Unknown said...

Naomba kutofautiana na mtoa mada.
Kwanza siamini kwamba kuna kitu kinaitwa mwaka mpya!!!
Mwaka mpya ni nini?
kama utaishi kwa kuendeshwa na mwaka mpya na ule wa zamani, basi naamini utaishi, katika mashaka makubwa.
Hivi kwa nini tusione kwamba kila siku ni mpya kwetu?
Mimi siishi kwa kuangalia mwaka mpya na sijui ule wa zamani,
Hayo hayanihusu, ninachojali ni kuona kuwa malengo yangu yanatimaia.
Yametimia lini? wakati gani? Hiyo sio kazi yangu.
hakuna mwaka mpya kaka.

Naomba kuwasilisha.

Mzee wa Changamoto said...

Well Kaluse! Nakubaliana nawe kuwa kama kuna mwaka mpya kwangu, basi ni siku yangu ya kuzaliwa. Nadhani ndipo ninapoadhimisha mwaka kamili wa maisha yangu. Lakini sipendi kupingana na ukweli kuwa wapo waadhimishao mwaka mpya kwa mujibu wa kalenda mbalimbali. Zipo hizi tutumiazo sisi, zipo za wahindi, wayahudi na wengine. Wote wana namna yao ya kuhesabu miaka na kisha wana mwanzowa mwaka wauitao mwaka mpya. Na hapa ndipo nilipokuwa nimegota kueleza juu ya mwanzo wa mwaka kwa mujibu wa kalenda itumikayo. Na ni mwanzo huo niliouita mpya.
Blessings