Friday, January 30, 2009

Them, I & Them... BURNING SPEAR. Together

Kama kuna jambo ninalojiuliza bila kupata jibu (na pengine sitaweza kupata) ni kile kinachosababisha waAfrika (wenzetu) kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha mateso na vifo vya waAfrika wenzetu kwa uchu wa madaraka. Sijui ni kipi wanachofurahia hapa waonapo watu wanateseka na kufa kwa kuwa tu wamefanya maamuzi mabaya ama wanalazimisha kusikika kwa haja zao?
"Gen" Laurel Nkunda
Wiki hii wametangaza kukamatwa kwa Gen Laurent Nkunda aliyeongoza mapigano ya muda mrefu huko Kongo katika kile anachokiita maamuzi yake ya kutaka "kuikomboa" Kongo. Nkunda ambaye hati ya kukamatwa kwake kimataifa ilitolewa tangu mwaka 2005, alikuwa akihusishwa na ushirika wake na Rwanda juu ya mauaji, mateso na ubakaji unaofanywa na kundi alilokuwa akiliongoza la Rally for Congolese Democracy (RCD) linaloshutumiwa kusababisha zaidi ya watu milioni moja kuyakimbia makazi kutokana na vita vilivyoua maelfu. Lakini kwa ushirikiano wa majeshi ya Rwanda ameweza kukamatwa wiki hii Kilelelezo kuonesha uathirika wa Kipindupindu huko Zimbabwe
Huko Zimbabwe wiki hii tumeona taswira za nini kinaendelea kwenye kambi za kutibu Kipindupindu ambapo yasemekana zaidi ya watu 3,000 wamepoteza maisha huku zaidi ya 57,000 wakiugua na kufanya maradhi haya kuvunja rekodi ya maambukizi ya maradhi barani Afrika kwa miaka 14 iliyopita. Bofya hapa ujisomee. Cha kusikitisha ni kwamba Viongozi wenye dhamana na uwezo wa kuweka na kutekeleza sera za kusaidia waathirika wapo kwenye mikutano ya namna ya kushirikiana kwenye madaraka. Joseph Kony

Nako UGANDA kumeripotiwa Jumatano ya wiki hii kuwa kikundi ama jeshi la Lord's Resistance Army linaloongozwa na Joseph Kony na ambalo kwa zaidi ya miongo miwili limekuwa likipigana na askari limeua zaidi ya watu 100 katika mji wa Tora ulioko kaskazini mashariki ya Kongo. Hiyo yafanya idadi ya waliouawa na kundi ama jeshi hilo kufikia 900 tangu mwezi uliopita. Ni waafrika wenzetu, wanaotaka kutuletea maendeleo na ambao wanatuua ili kuweza kulazimisha kupatikana ama kutekelezeka kwa mahitaji yao.Bofya hapa kusoma

WOW!!!!
Ndipo nimkumbukapo Winston Rodney a.k.a Burning Spear ambaye katika wimbo wake TOGETHER ameanza kuimba kwa kuuliza swali kuwa "Do you enjoy terrorizing your area? Do you enjoy killing your brothers? Do you enjoy killing your fathers? Africa they use to chain us together." Sijui kuna tofauti gani kati ya mauaji ya "wakoloni" na haya ya sasa maana wote wanaua asilimia kubwa ya wasio na hatia. Burning ameendelea kuwakumbusha waAfrika kuwa twaweza kuwa wamoja, kufanya mambo mema na kuonesha uAfrika halisi alitaja mengi ambayo kama waafrika twaweza kuyafanya kuuonesha ulimwengu yale tuwezayo kuyafanya tofauti na vile walivyotufanya wakoloni. Baadhi ya aliyosema ni pale anaposema "we can show the world that we're not worst kind of brothers, we can show the world that we can live together, we can show the world that we can move together."......."it's getting from bad to worse, throw down your arms and guns"

Burning Spear ktk onesho lake hapa MD Dec 08
Msikilize Burning akiimba juu ya umoja kwa waAfrika anapoimba TOGETHER. Ni kutoka katika albamu yake aliyoipa jina la OUR MUSIC

**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndio umesema vyema. ni swali zuri kwamba, kwa nini kuna majamaa yanayofurahia kuuwa wenzao? wewe umeliongelea kibaguzi zaidi kwamba waafrika wenzzao, lakini sote ni binadamu bila kujali makundi.

hawa majamaa wana siri zao na ndio maana hawakamatiki au wankamatika kijinga. ni ile tabia ya binadamu wa leo kupenda mali kuliko utu na ubinadamu wake mbele ya mwingine.

siku zote kuna watu migongoni mwao wanaowapelekea mali wanazoiba na ndio maana huwezi kusikia eneo lisilo na madini, nk linapiganiwa sana.

laikini tatizo ni letu sote. mtu anayetamani anasa, akipewa mkataba mnono kwamba apigane, atakataa? tunahitaji kutanguliza utu na heshima kwa viumbe vya muumbaji vinginevyo tutaishi matajiri harafu tufe masikini

Mzee wa Changamoto said...

Kuna ukweli katika ulilosema kuwa nimeiongelea kibaguzi zaidi. Labda ni kwa kuwa ninasikitishwa na hali iliyopo ambapo nchi zisizotengeneza silaha na ambazo zimefungiwa kufanya biashara na nchi yeyote barani Afrika ndizo zinazouana tena kwa silaha za kisasa, na ndio wanaoshikilia migodi ya madini kama ulivyosema na nchi zenye kuja na silaha mpya na kali kila mwaka wala hawana haja nazo maana hakuna hata dalili ya vita nchini kwao. Nina makala ijayo iulizayo juu ya hili. Juu ya hawa wapiganaji ambao wana vizuizi vya kibiashara kwa miaka kadhaa na hakuna anayefanya kazi na bado wananunua silaha "made in peaceland". Mkataba ni upi na wanalipa vipi? Na kwanini inapotokea kutoelewana baina yao wanakamatika kiraihisi? Si tuliona Savimbi? Tunaona Nkunda? Sasa ni wangapi wauawe kabla Kony na wengine hawajatiwa mbaroni? Yaonekana wanaweza kukamatika, lakini ni mpaka waoneshe nia ya kuacha "bizinesi" waifanyayo na hao wawapao sapoti.
Asante Kamala na heshima kwako mkuu