Saturday, January 24, 2009

Tumechoshwa na SALAMU ZA RAMBIRAMBI. Na sasa hatuzitaki

Picha kwa hisani ya Bongo Pix
Picha toka Michuzi Blog

Ndani ya siku 11 za mwaka 2009 (Jan 10 - 21) tumeshihudia ajali mbili kubwa zilizoripotiwa (maana nina hakika kuna zitokeazo ambazo hazifiki kwenye vyombo vya habari) na ambazo zimetwaa / kuchukua zaidi ya roho 44 za raia wasio na hatia. Ni ajali ambazo kila "uchunguzi wa awali" huonesha namna fulani ya uzembe kwa upande mmoja wa wahusika. Kinachofuata ni SALAMU ZA RAMBIRAMBI toka kwa viongozi wa serikali zikifuatiwa na "maombi" ya kuwaombea wapone haraka warejee kwenye kulijenga taifa.
Lakini mbona bado tunapata ahadi tuu na hakuna mipango dhabiti ya kupunguza hili? Ni kwanini serikali haithamini na kuonesha kwa vitendo harakati zake kuzuia hivi vifo vya makumi wasio na hatia? Mbona sasa kla mtu akikwambia anasafiri inabidi "UFUNGE NA KUOMBA" mpaka atakapokutaarifu kuwa amefika?
Serikali inastahili kufanya zaidi ya kutuma salamu za rambirambi. Kwenye salamu zake za wiki hii, Rais Kikwete "ameunguruma" akisema "hatuwezi kuvumilia kutokea kwa ajali hizi wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria za usalama barabarani zipo. Tufanye jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wetu kupunguza kwa kiwangi kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo zimeshapoteza maisha ya wenzetu wengi"
MTAZAMO WANGU: Tatizo si kusema bali ni kutekeleza. Hawa wanaotangazwa kuwa wamepona na wameruhusiwa haimaanishi kuwa hawako kwenye maumivu tena makali. Binafsi nimekuwa kwenye maumivu ya ajali kwa miaka 9 sasa, hivyo natambua kuwa mtu kutoka akiwa anatembea ama bila mchubuko haimaanishi kuwa ataweza kuendelea na maisha yake kama zamani. Ni lazima hizi bima zihusishwe, ukaguzi wa magari uwe wa makini, ukaguzi wa waendesha vyombo uwe wa kweli na RUSHWA isiweke pembeni thamani ya roho za watu.
Naamini Rais anajua UOZO uliopo kwenye kitengo anachokizungumzia na ataweza kuwekeza katika kuokoa maisha ya nguvukazi inayopotea.
Naamini sasa ni wakati wa kutenda maana TUMECHOSHWA NA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, NA SASA HATUZITAKI KWA KUWA TWATAKA KUTOKOMEZWA KWA AJALI HIZO

2 comments:

Anonymous said...

Kweli. Kwanini hawajitahidi kuzuia ajali? Viongozi wanafanya nini wakati wananchi wanateketea?

moruo said...

kweli,muda wa mabadiliko ni sasa