Wednesday, February 18, 2009

BURIANI JOSEPH MAINA

Picha kwa hisani ya Issa Michuzi
Japo muda umekuwa finyu lakini nimeona ni vema kurejea kibarazani kutoa heshima kwa mwanamuziki huyu. Joseph Maina amekuwa msanii kwa muda mrefu na japo wengine hawajamsikia ama hawakupata kumfahamu, lakini amekuwa nguzo kubwa katika uimbaji katika bendi ya Msondo Ngoma Music Band. Na leo nilipokuwa napitia habari za nyumbani kwenye majamvi yetu nikakutana na habari za kifo chake cha ghafla.
Imenisikitisha kwa kuwa
Kwanza licha ya uwezo mkubwa aliokuwa nao, Maina hakuwa mtu wa kupenda kusikika. Ni wachache wanaoweza kukutajia nyimbo ambazo Joseph Maina ameimba kama lead vocalist na hiyo haikuonekana kumsumbua.
Pili inaniuma kwa kuwa licha ya nyota hawa kuendelea kujisogeza pembeni ya muziki wetu, bado wasanii hawaonekani kutaka kurejea kwenye muziki ulioipa na unaoipa Tanzania heshima ulimwenguni. MUZIKI HALISI AMA WENYE VIONJO VYA KITANZANIA.
Naamini mengi yamesemwa na mengi yatasemwa na wanaomuenzi nyota huyu, lakini napenda kukushirikisha katika wimbo huu ambao alishiriki kuimba. Utamsikia Joseph Maina katika ubeti wa pili akiimba "na mimi nimeyazingatia aliyoniusia Mama eeee". Sasa sikia hii inayosikitishwa. Wimbo ulitungwa na Marehemu Othman Momba na kuimbwa kwa kushirikiana nao Marehemu TX Moshi William na Marehemu Joseph Maina. Pia gitaa zito la besi lilipigwa naye Marehemu Suleiman Mwanyiro "Computer"
Ni wimbo maalum ambao Marehemu Momba alimuimbia mkewe Lucy Bandawe.
BURIANI JOSEPH

1 comment:

Anonymous said...

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wengi wa wasanii hawa, japo wana vipaji vikubwa, hawafaidi matunda ya kazi zao kwani kazi zao zinakwapuliwa na wajanja na kusambazwa hovyo hovyo. ..Tunahitaji mabadiliko katika jambo hili.

Joseph Maina, pumzika salama. Njia ni hiyo hiyo moja kwetu sote.