Tuesday, February 3, 2009

Ni jina, ni kabila, ni dini, ni lugha, ni midundo? Dah!! Vipo? Ama twapotosha?

Mara nyingi nimekuwa nikikutana na hili swali la "jina lako ni nani?" nami bila hiyana nawapa yote mawili. Mubelwa Twin'Omukama (litamke vizuri) kisha wengine wajuao natokea Tanzania watauliza kabila na wasiojua kuwa kuna makabila watauliza dini. Nawaambia kisha wanauliza "hauna jina la kikristo?" Amaaaaaa!!!

Sikuwahi kujiuliza maana halisi ya swali hilo. Lakini swali hili likaja kuibuka zaidi ilipokuja wakati wa uchaguzi na hata kuapishwa kwa rais wa Marekani ambaye kwa mujibu wa wenye akili zenye mrengo fulani, eti jina lake la kati si la kikristo na wakataka hata kuhoji atatumia kitabu gani kuapa.

Swali likaja kichwani mwangu kuwa "kuna jina la kikristo ama kiislamu kweli? Ama kwa ujumla kuna jina la ki-dini?

Ni kweli kuwa yapo majina ya dini ama waliokuwa na dini walikuwa na majina ya aina fulani? Mbona majina yangu yana maana ya kidini zaidi ya mengine yaitwayo ya kidini?

Nilidhani majina yana asili na asili ni sehmu ambazo zina makabila na yanaitwa kwa maana fulani, lakini si udini. Hivi hatujipotezi hapa?
Nyumbani kumwita mwana Yesu ni Kosa japo Emmanuel si neno. Ila wenzetu wa Marekani ya kusini wana Jesus (wanatamka HESUS) na iko Ok.
Wenzetu waumini wa dini fulani walipotaka kuanzisha ibada kwa lugha ya kiarabu watu wakahoji, wasanii wa Makoma walipoimba nyimbo kwa muziki wa asili yao ambayo kwetu ni midundo ya anasa tukahoji.
Labda tunakompliketi mambo kuliko yalivyo. Labda tumekaririshwa kuhusu upana wa dini na kupewa mipaka ya nini tufikiri kuhusu dini. Labda, labda, labda.....

SIJUI

4 comments:

Koero Mkundi said...

hata mimi huwa najiuliza swali hilo hilo.
Wanafunzi wenzangu wananiulizaga jina langu la ubatizo, nami huwa nawaambia kuwa sina kwani nililikana mara tu nilipokuja kujua maana yake.

Yaani sitaki hata kulisikia

Simon Kitururu said...

Aliniua George foreman kwa kuamua kuwaita watoto wake wote watano wakiume George.- George Jr., George III, George IV, George V, na George VI.:-)

Haya majina kiboko hivi nikibadili jina huku ughaibuni na kujiita Yesu nitafanywa nini bongo?

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Suala la majina...Unajua Kuna watu wanaofikiri kwamba wanammiliki Mungu na kwamba wengine inabidi tuwaombe ruhusa tunapotaka kufanya jambo lolote linalohusiana na Mungu “wao” Tayari nimeshaulizwa ni kwa nini nina blogu ya nyimbo za dini (nyimbozadini.blogspot.com) wakati jina langu wala siyo la kidini? Jina la kidini ni lipi? Mimi nami si ni mtoto wa Mungu kama Maria na Petro? Ati, jina langu linahusianaje na blogu ya mambo ya dini? Je, kuna uhusiano wo wote wa moja kwa moja kati ya jina la mtu na “utakatifu” wake? Kwani leo nikiamua kujiita Yesu ndiyo nitakuwa mtakatifu? Mbona tunawaona akina Paulo, Daniel, Marko na Maria wakifanya madudu? Je, sisi ambao hatuitwi Paulo, Daniel, Marko na Maria hatutaingia mbinguni kwa sababu tu eti tuna majina ya “kipagani”? Ina maana mbinguni hakutakuwa na akina Masangu, Kamala na Koero? Jina ni nini??? Mimi nilibatizwa nikiwa mdogo na kupewa jina la Deus na kama alivyosema dada Koero nilipokua niligundua kwamba jina hilo halinifai. Niligundua kwamba Deus katika Kilatini ni Mungu na ninajua wazi kwamba mimi siyo Mungu ndiyo maana nikaamua kuachana na jina hilo na kurudia majina yangu ya Kisukuma (ingawa pia kuna akina Masangu na akina Matondo wengi tu kule Afrika Kusini na Congo). Na ninayo furaha kwamba nilifanya hivyo kuliko kuendelea kujiita "Mungu".

Bwana Kitururu ukiamua kujiita Yesu, usishangae siku ukirudi nyumbani watu wakaandamana tena na mabango kabisa!

Subi Nukta said...

Hapa jawabu lake ni moja tu, "The Way You See The Problem Is The Problem".
Misimamo ya jamii tunamokulia ndiyo inayotufunga mawazo na mitizamo yetu.