Thursday, March 5, 2009

Nguvu baina yetu isiyo na nguvu ndani mwetu, yenye nguvu kwetu.


Ndio.
Ni nguvu ambayo twaweza kuitumia japo huwezi kuipima kwa namna tupimavyo nguvu nyingine, lakini inaweza kufanya mengi na kutuepusha na yale ambayo hata kwa nguvu tulizonazo hatuwezi kuyatenda kwa urahisi namna hiyo.
Nazungumzia NGUVU YA KUKUBALI KUELEWA TUAMBIWACHO. Wengine wanaita kusikia lakini kuna kusikia na usielewe kama ilivyo kwa aangaliaye na asione.
Pengine tukiangalia mataifa makubwa yanavyohangaika kupambana na wasiowaona, unadhani wangeweza kukaa chini na kuelewa kile wanachoonywa kabla hawajaingiza miguu huko vitani wangeingia gharama za mali na uhai wa watu kama waingiavyo sasa?
Ama kama "watawala" (na hapa sijasema viongozi maana najua viongozi sasa ni wachache na hawatendi haya) wangesikia kilio cha wananchi na kujitahidi kukamilisha kinacholiliwa badala ya kutumia hilo kuwachuma kwa kuomba rushwa tungekuwa katika hali tuliyopo sasa?
Ama watu wangeelewa wanavyoambiwa juu ya usawa uliopo kati ya watu wa rangi tofauti za ngozi wangeendekeza na kuendelea ubaguzi na matabaka? Na unadhani tungelia tuliavyo kwa kuwa tu ndugu zetu ma-albino wanauawa?
Ama kama kilio chetu kingeweza kufika huko "siasani" unadhani ufisadi ungeendelea kuwa namna ulivyo?
Tukitazama nguvu ya kutoelewa waambiwacho inavyoigharimu jamii, utaona kuwa kuna nguvu kubwa sana ya usikivu na uelewa ambayo inastahili kuheshimiwa japo haina kipimo kama upimavyo nguvu ya "kubeba chuma", lakini ambayo ikitumiwa vema inaweza kuepusha matumizi yasiyo ya lazima ya nguvu zetu na kuepusha usumbufu na hata upoteaji wa maisha ya watu.

Tuonane "next Ijayo"

6 comments:

Anonymous said...

Naelewa unamaanisha nini! japo ni ngumu kwa juu juu kuelewa nini unaniishacho. Nguvu hiyo ndani mwetu ni dhaifu, nguvu hiyo ndani mwetu hatujaifanyia mazoezi. Iko ndani mwa kila mmoja wetu, inafanya kazi lakini wengi hatujairuhusu ioneshe kazi zake!

Ndio maana kama wataka kufanya kitu, kutoka ndani unasiki usifanye, ukifanya unapata madhara baadae unasema roho yangu ilisita kufanya hivi! ukiifuatilia kwa makini nguvu hiyo inakufanya uishi maisha ya utaratibu maana utasikia na kufanya kile uambiwacho!

Koero Mkundi said...

Hivi kumbe na wewe umekuwa mtambuzi?
Nimejifunza jambo hapo.

Yasinta Ngonyani said...

Ndio; ngoja niseme kitu hasa hii ya "mtoto kuwa mtundu hasikii" ni kweli wengi wanafikiri ya kwamba watoto watundu na wasiosikia dawa yake ni viboko. Ni kitendo ambacho mimi nakataa kabisa kwani ukishamzoesha mtoto viboko ndo yatakuwa yale ya hasikii kwa sababu ataona ni kawaida tu. Kinachotakiwa ni kumuelewesha kwa upendo na pia ikibidi kaa naye chini na mwelekeze. Naamini hii nguvu tunayo ndani mwetu kama dada Mary alivyosema ni kwasababu hatujaifanyia mazoezi tu. Kazi kwelikweli

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

tatizo kama kweli lipo ni kwamba huwa hatujifunzi ya ndani mwetu bali yanje yetu na hivyo hubakia kuona ubaya wetu kupitia kwa wenzetu tuwaitao wabaya.

mamaa

Albert Kissima said...

Hii nguvu inafanya kazi sana,
mtu anataka kuangalia jua linapochomoza,
lakini anakazana kuangalia magharibi,
mtu anaweza kuangalia na kuona,lakini atakachokitoa yeye kikawa tofauti kabisa na alichotazama na kukiona,vilevile anaweza kusikia na akaelewa vizuri, lakini ktk kukitoa alichokielewa ni juu yake mwenyewe,
hapa inategemea sana na mtu mwenyewe.

Ni dhahiri shahiri,
wanaofanya ufisadi,wala rushwa,wafujaji wa mali ya uma,
wanafahamu hali ya umasikini wa hao wanaokandamizwa,hata kuawa kwa albino na matukio ya ujambazi,mtu kuuawa kwa sababu ya shilingi mia,yote haya tmasikini ,hali ngumu ya maisha inachangia sana,
nguvu hii inafanya kazi sana,lakini inapuuzwa,ndio maana kuna ahadi za uongo,sera zisizotekelezeka,
ameeleza kwa kirefu padre Karugendo kwenye gazeti la raia mwema toleo no 71.
Da! Ndio niliyokuwa nayo,hata kama sijaelewa,lakini nilichokiandika naimani kinaeleweka.


"waongezee wenzako furaha zaidi ya uliyowakuta nayo"

Christian Bwaya said...

Kusikiliza ni gharama yenye faida. Lakini ni wangapi wetu tunaweza kusikiliza "kilivyo" badala ya kujaribu "kusikia" tunachotaka kusikia?