Wednesday, May 27, 2009

RECYCLING: Moja ya hatua kuu za maendeleo Tanzania

Niliandika kuhusu UTAMBUZI na kugusia (japo kwa juu juu) kuhusu kujitambua na faida zake. Hii ni hatua ya kwanza ya kusonga kimaisha maana utaweza kujua utakacho kabla hujapanga namna ya kukipata. Na ili ujue utakacho, lazima ujijue wewe kujua udhaifu na uimara wako katika harakati za kukisaka. Kwa ufupi naona UTAMBUZI kama HATUA SAHIHI YA KUHAKIKISHA HUJIPOTEZI KATIKA HARAKATI ZA KILE UDHANIACHO NI KUTAFUTA MAENDELEO.
Na katika kusaka maendeleo huku kuna suala moja kuu ambalo si tu linaonekana kuonesha mafanikio kwa wenzetu, lakini likitumiwa vema laweza kuwa na manufaa kwetu. Nalo ni namna ya kutumia takataka katika kuboresha maisha. Wenyewe wanaita ku-RECYCLE. Kuna faida nyingi za kufanya hivi na zinatofautiana kulingana na ukubwa ama manufaa yake. Lakini pia lazima tukiri kuwa si kila kitu kinachopitishwa katika mfumo huu ni kizee / kikuukuu, bali hata kile kipya kisichofaa lakini kinachoweza kurejeshwa mfumoni chaweza kufanyiwa hivyo.
Mifano midogo ni maji ya viwandani. Tunajua kuwa miji yetu haina maji ya kutosha kwa wakazi wake, na taasisi zinazoshughulika na masuala ya mazingira haziwalazimishi wawekezaji kuwa na mfumo huu ambao ungeweza kuyafanya maji kutumika mara tatu ama nne ndani ya kiwanda (hasa katika shughuli za kupoza mashine) kabla hajaenda kuhifadhiwa mahala ambapo yangechukuliwa na kwenda "kutibiwa" kabla ya yale yasiyofaa kabisa kumwagwa mahala salama. Badala yake wenye viwanda wanachukua asilimia kubwa ya maji na kuyatumia vibaya kisha kumwaga sumu yake kwenye mikondo inayotumiwa na wananchi. Ni kutojali afya za wanaowafanya wawe hapo.
Maji yenye kemikali toka kiwandani huko Mbagala, ambayo huingia mto mzinga ambao watu hupata kitoweo toka humo.
Ukizungukia vituo vikuu vya Polisi nchini nako ni balaa. Magari "yanapandana" na kuozeana na kuwa mazalia ya maradhi na wadudu hatari na hakuna anayesema wala kuonekana kuona hili.
Karakana za Reli nazo ni balaa, maana kuna mataruma ya miaka nenda rudi na zile kubwa (kama ya Morogoro) ndio kinyaa kabisa kwa namna ilivyorundika vichwa vya treni visivyo na maana.
Upande wa Taka ngunu nako ni balaa. Ukitaka kujua haya nenda Mwanza msimu wa mvua ujionee zinavyoshuka kwenye mikondo ya maji yatiririshwayo na mvua.
LAKINI YOTE JUU YA YOTE na ambayo ni chanzo cha yote ni AKILI ZA WANANCHI ambazo zinawaweka hawa wasioona na wanahitaji kuwa RECYCLED kwenye madaraka. Hawa watu wana NYASIFU nzuri zenye kuonesha kuwa wamekaa nje ya nchi na kusoma na kushuhudia maendeleao na kushughulikia maendeleo na kuwa sehemu kubwa ya maendeleo lakini wanapotwaa madaraka nao ni kama wanafuta kila "jema" wanalosema wakati wa kampeni.
Ni wakati wa kuamka kwa wananchi, ku-recycle akili mbovu na maamuzi mabovu na kupata mapya yenye mtazamo mpya na nia mpya ili kuwezesha kupatikana kwa maendelo kamili.
Ni wakati wa ku-RECYCLE akili potofu, viongozi wabovu na sera mbovu ili kusaidia kupata chache zenye ubora utakaotufaa waTanzania.
Sitakuwa wa kwanza kujaribu kuelimisha. Culture naye alishafanya hivi na mpaka anakufa wapo ambao hawakumuelewa.
Msikilize anapoeleza alichojaribu katika I TRIED.




1 comment:

chib said...

Nimefurahia na hitimisho lako, recycle mpaka uongozi...