Thursday, June 4, 2009

Taji "Master T" Liundi.... Mzee wa Vipaji

Master T .........Picha kwa hisani ya Michuzi Blog
Leo katika kujipumzisha nilikuwa nikipitia "taswira" za nyumbani na ghafla nikakumbana na hii ya Master T nami ambayo tulipiga punde baada ya kumaliza kurusha kipindi cha Msanii Tanzania nilichofanya kwa niaba ya Sister V aliyekuwa na udhuru siku hiyo. Hii ilikuwa ni mwaka 2002 pale 100.5 Times Fm ambako Master T alikuwa Meneja wa Vipindi.
Napenda kutoa heshima na shukrani kwa Master kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kaika kuibua vipaji. Hili linaweza kutoonwa na wengi kwa kuwa hawajui harakati za Master T lakini amekuwa katika kuibua vipaji katika nyanja mbalimbali tangu alipopata nafasi ya kumuwezesha kufanya hivyo.
Master T ni mmoja wa watangazaji wa kwanza wa kituo cha kwanza binafsi cha Redio One Stereo ambao pia waliiwezesha kuvuma vema na kuanika uwezekano wa wengine kufuata nyayo. Pale alihangaikia uibuaji na uboreshaji wa Muziki utakaoweza kututambulisha waTanzania. Waliofanya naye kazi Redioni wanaweza kutambua hili, kama ambavyo alinukuliwa Mike Pesambili Mhagama alipohojiwa juu ya chimbuko la neno Bongo Flava ambapo alisema "Taji “Master T” Liundi alikuwa ni kivutio cha aina yake si tu kwa uwezo wake wa kuchambua mambo mbali mbali, bali pia kwa mahojiano yenye ukina na wanamuziki mbali mbali, uwezo wake wa kuongea lugha zaidi ya tatu na kwa ubunifu. Ikumbukwe yeye ndiye mwanzilishi wa neno “Chombeza”, neno alilolibuni kumaanisha kubembelezana kiaina kati ya wapendanao hasa nyakati za usiku alipokuwa akipiga kipindi maalumu cha nyimbo za taratibu. Neno hili sasa ni maarufu sana huko Tanzania." Bofya Hapa kusoma zaidi mahojiano hayo
Binafsi namfahamu Master kama mtu aliyeibua "kipaji" nilichoonesha. Aliweza kutoa nafasi kwa wale alioamini kuwa wanaweza kufanya vema, na ndivyo ilivyokuwa kwangu ambapo alinipa nafasi na maelekezo ya kuonesha uwezo wangu ambao niliutumia vema kwa miaka miwili niliyokuwa Times Fm. Pale tulikuwa na watangazaji wengine ambao walipewa nafasi kama niliyopewa mimi na wengine wanaendelea kuunguruma na kung'ara zaidi hata wakati huu. Na hata nikiwa pale, bado Master T aliendelea kuibua vipaji kupitia Talent Show iliyokuwa ikifanyika ndani ya Ukumbi wa ASET Kinondoni na lengo likiwa ni kuibua vipaji vya muziki (hasa wa Bonbgo Flava). Master ni mfikirifu, mtanabaishaji na mchambuzi wa hali ya juu. Kwa muda mchache niliokaa naye studioni, naweza sema kuwa ni kati ya wachambuzi wachache waliokuwa wakisikika redioni na kati ya viongozi wachache waliochukia kuripoti kile kilichosemwa bila wewe kukijua kwa zaidi. Alitaka undani wa habari kuliko ripoti
Ni Master huyuhuyu ambaye sasa anaendelea na "mission" yake kwa kuibua vipaji vingine katika masuala ya U-Model kupitia blog yake ya U-MODO (Bofya hapa kuitembelea) ambapo nako kunaonekana kuzidi kukubalika.
Nina hakika kuwa huko aliko TBC anaendelea kufanya kile afanyacho wakati wote, na kama wanaJamii, tunastahili sio tu kuiga mifano ya wale wawekezao wasichoweza kukitoa maishani mwetu, bali kujua kuwa kuwekeza katika kuinua, kuendeleza na kuboresha vipaji vya wenzetu ni jambo lenye umuhimu sana kwani linahakikisha ukombozi halisi wa umsaidiaye na kumfanya asiwe tegemezi na kisha kuwa msaada kwa jamii nzima kwa ujumla. Kama wasemavyo Morgan Heritage hapo chini, twahitaji kusaidiana na kuinuana kama kweli twapenda maendeleo
HESHIMA KWAKO MASTER T, kwani hata sehemu kuu ya kazi ifanyikayo hapa, ni matunda ya uibuaji wa vipaji ulioanza kabla sijakutambua na unaoendelea nao.
Baraka Kwako

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli tenda mema usingoje shukrani Duniani hapa.Mungu awalinde wote wenye moyo huu wa kusaidia wanaohitaji misaada.

Faustine said...

Namfahamu Taji Kwa miaka mingi. Nakubaliana na tathmini yako. Ni kijana mbunifu, mwenye kuona mbali na aliye na busara.
Namtakia kila la heri katika kile anachofanya kwa sasa.

Mdau
Faustine

Anonymous said...

Mubelwa, unayo sifa ya pekee katika uwaenzi na kuwatunuku wale wote unaojifunza lolote kutokana na maisha yao au habari zao au shughuli zao. Umetokea kuwa mtu mmoja ninayemsoma kila kona akishukuru au kunukuu au kuhariri faida aliyopata toka kwa wengine.
Ni vyema kushukuru. Nawe ushukuriwe kwa kushirikisha habari na uzoefu wako.
Naam, huyo ndiye Mube! au mzee wa Chchzzz!

Mija Shija Sayi said...

Nukta77, nakuunga mkono kwa asilimia 100 juu ya kaka yetu Mubelwa.

Bless you Mzee wa Changamoto.