Thursday, October 1, 2009

Ili "usimchezee" wala "usichezewe".......

Siku kadhaa zimepita tangu Da Yasinta aandike makala yake tulivu na elimishi ya WANAUME NA KAULI HIZI: "HUYO SI WA KUOA, NI WA KUCHEZEA TU" (Bofya hapa kuisoma) ambapo alieleza mengi ya maana kuhusu hali hiyo. Pia wachangiaji walieleza mengi mema kuhusu chanzo na pengine kinachoweza kuwa sababu za hili. Nami sasa "najimwaga" barazani kwa kuja na kinachoweza kuzuia kutokea kwa yote. Yaani "kuchezea" na "kuchezewa"
Na HAKUNA SIRI KUWA SULUHISHO LA HAYA YOTE NI KUJITAMBUA TU....
Ntaanza kwa kurejea makala yangu niliyoiandika May 26 niliposema UTAMBUZI. Elimu ya lazima kwa wote (isome hapa) ambapo nilieleza kile ninachoamini kuwa twahitaji kukifanya ili kuweza kusonga na maisha yetu binafsi ambayo yatawezesha maendeleo kwa maisha ya kila mmoja wetu (ina maana TAIFA nalo litaendelea). Maelezo ya makala hayo ni sawa ama mwanzo wa yale niliyoandika June 12 nilipoandika kuhusu wimbo wa RIVERSIDE (Isome hapa).
Tuanze kwa kujiuliza kuwa
1: Kwanini kuchezeana kunakuwepo (kwa usiwano mkubwa) kwenye jamii ambazo hazijaendelea ama zile zenye uhitaji mkubwa?
2: Kwanini wasio na kazi ndio waathirika wa michezeano hii?
Ni kwa maswali haya haya tunatambua kuwa jamii zilizo na uhitaji ndizo zinazoathirika zaidi na maradhi kama UKIMWI kwa kuwa wanafikia hatua ya kudhani kuwa kuchezewa na kuchezeana ni starehe ama kitega uchumi katika maisha tuishiyo na wengine wanafikia hatua ya kufikiri kuwa ni njia ya kuondoa msongo wa mawazo (stress). SI KWELI.
Tunahitaji KUJITAMBUA. Kila mtu kwa wakati wake anastahili kutambua ni wapi lilipo PUMZIKO la yale yamkumbayo. Na pumziko si lazima liwe la gharama ama aghali, bali laweza kuwa likupalo furaha na faraja (lakini lisilokuathiri kiafya ama kiakili) na yapo mengi ambayo twayapuuza japo yangeweza kuwa MATIBABU HALISI ya halinzeu ngumu za kimawazo.
Pengine niulize kama umeshawahi kumsikia mtu akisema "mie kitakachoniua ni Pombe ama Bangi lakini si wanawake?" Unadhani wanaamisha nini? Asemaye hayo anaamisha kuwa anaamini amepata PUMZIKO na AMETAMBUA kuwa pumziko (kwa mujibu wa yeye) ni hilo aliloliona. Na kila mtu analo PUMZIKO. Ambalo anaweza kulitumia vema kuondoa msongo wa mawazo na kumpa mawazo mapya ya kuendesha maisha yake kihalali na kwa mafanikio zaidi kuliko ilivyo sasa. Tunaona hata WATAWALA wetu wanaoshindwa kujitafutia pumziko na ridhiko la nafsi zao na kuishia KUIIBIA JAMII bila kikomo kwani wanapodhani kuwa utajiri ni nafuu ya matatizo, wanajikuta wakitambua kuwa utajiri hauna kikomo. Matokeo yake ni kuendeleza wizi.
Wale wanaodhani kuwa wameshachoka maisha na sasa wanaona furaha pekee imebaki kwenye kuNGONOka, nao wanaendelea bila kujua kuwa huwezi kuwamaliza kabla hujamalizwa wewe. Wanaodhani kuwa hakuna maisha yaliyo na mwanga mbele yao wanaishia kuamini kuwa kujiua ni suluhisho na pengine wanaona hawawezi "kuondoka peke yao" wanaishia kuua na wengine. Zote hizi ni dalili za kutotambua lilipo PUMZIKO la mtu.


Ukweli ni kuwa kwa kutambua kuwa MUZIKI ama MICHEZO ama MATEMBEZI ama KAZI ZA MIKONO ama MASOMO na hata KAZI vyaweza kuongeza furaha na kukuponguzia msono wa mawazo (stress) unaweza kuepuka mihemko ya mwili na kuacha kuendeshwa na hisia kwani unatambua kuwa pumziko lake liko wapi.


Kuchezea ama kuchezewa ni matokeo ya watu KUSHINDWA KUJITAMBUA na kushindwa kujua lilipo pumziko lao la kimaendeleo badala ya kutafuta "mkato" wa kuridhisha miili huku tukiua akili na afya zetu.

KUJITAMBUA NDIO KITU PEKEE AMBACHO KILA MTU ANAHITAJI ILI "USIMCHEZEE WALA USICHEZEWE

8 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Sawa kabisa na pengine labda kuna wengine hawajui wamefika kufanya nini hapa duniani. Kwa hiyo huwa hawaridhiki na kile walichonacho na pia wakiona yeye anachezewa basi naye anaenda kumchezea mwingine. Kwa sababu hafikirii kama akiendelea kufanya hivi anaumiza jamii. Anataka kubadilika lakini hana subira. Ni kweli kujitambua ni muhimu. Asante kwa kuendeleza mada hii.

chib said...

Mzee wa Changamoto, unaijua stori ya sokwe na masuala ya ngono?, Basi binadamu wameshakuwa kama sokwe kwa masuala hayo tu, ingawa nafikiri kwa sasa wamekufuru!

Simon Kitururu said...

Katika kuchezea au kuchezewa kunahitaji zaidi ya mtu mmoja. Na mara nyingi anayechezewa huwa hajui kwanza kuwa anachezewa mpaka ashtukie au aachwe kabisa. Kwa hiyo siamini kwamba kuna uwezekano wa kujitambua hapo wakati yeye ajualo ni kuwa kapata mpenzi na penzi. Na yoyote aliyewahi kupenda anajua UPOFU wa penzi nafikiri na kama hajui basi ndio rahisi zaidi kuchezewa.

Na siamini michezo ya akili iebobea zaidi nchi zisizoendelea kwa kuwa kwa uzoefu wangu kuchezeana kulikobobea nimekushuhudia zaidi nchi za Scandinavia hata kuzidi Bongo ambako huku ishafikia hata ndoa zenyewe na kuishi bila ndoa Hakuna sana tofauti.

Tukiachana na Kuchezeana na kuangalia hali ya ndoa huku Kaskazini ya Ulaya angalia Mfano; Rais wa Finland Tarja Halonen alipokuwa Rais ndio ikabidi ahamie nyumba moja na bwana yake na kwakuwa Tu kuna Safari za nchi kibao walikuwa wanashindwa kujua jinsi ya kudili naye akija na Bwana ndio ikabidi aolewe na hii ni baada ya jamaa lililomuoa kufikiriwa linachezewa tu . Sasa huyo ni Rais, fikiria wengine sasa.Iceland waziri wake mkuu anajulikana kwa kuwa anakiriwazi kuwa ni Msagaji na kaumiza wadada kadhaa moyo.

Nachojaribu kusema ni kwamba nachoamini kujitambua hakuchagui nchi wala maendeleao. Na ukipenda unaweza ukawa unachezewa bila kujijua na labda unafikiri ni wewe unachezea. Na nahisi kujitambua sana nako kuna madhara ukifikiria binadamu si malaika na uwezo wa kutambua wote kibinadamu kunawatakaodai haiwezekani!

Ni wazo tu!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...
This comment has been removed by the author.
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mzee wa Changamoto - unaongelea kujitambua kupi? Kujitambua kama anavyojitambua Kamala au? Je, haiwezekani kujitambua na bado ukaendelea kuchezea/kuchezewa/kujichezea/kuchezesha/kuchezeshwa/kuchezeka...?

Nilikutana na jamaa mmoja zamani ambaye aliniambia kwamba yeye kufa na UKIMWI si neno kwani anaamini kwamba kama asipokufa na UKIMWI basi kitu kingine kitamuua. Cha kushangaza huyu jamaa ni daktari (MD) na alinifafanulia kwamba ni kazi bure kwa binadamu kujaribu kujikinga na kitu kimoja na kuvipuuza vingine kwani ni vitu vingi mno vinavyoweza kumuua. Kwa mantiki ya falsafa yake ni kwamba kuchezea/kuchezewa/kuchezeana si jambo baya kama hilo ndiyo hasa linalokupa furaha hapa duniani.

Baadaye niligundua kwamba kuna watu wengi sana wanaoishi kwa kufuata falsafa hii ya kutojali ya "eat well, exercise and die anyway" UTAMBUZI

Dada Yasinta - wewe umeshajua ulifika hapa duniani kufanya nini? Ulijuaje? Pengine hii itasaidia na wengine waweze kujua walikuja hapa duniani kufanya nini - kama siyo kuvuta bangi, kuchezea/kuchezewa na....

Simon Kitururu said...

Pointi yako Profesa Matondo imenikuna!

Duh!Ili haki ya anayechezewa bila kujua na anayechezea mwenye tambuzi anachezea ipatiwe haki , nami naomba labda Mzee wa changamoto fafanua kidogo Article hii tusijetoka nje ya ulichokuwa unamaanisha kwa kubwabwaja.

Sisulu said...

Kama mzee wa changamoto unaamini katika uchaguzi basi utakubaliana na mimi kuwa uchaguzi wa mpenzi ndio jawabu la je unayekuwa naye uhusiano wenu ni imara au la,binadamu asili yao ni kubadilika kitabia NA kila kitu hivyo mazuri yaliyomo kwenye uhusiano yalindwe, mabaya yatokomezwe na yana yoibuka kuharibu uhusiano yadhibitiwe,utakapobweteka kushughulika nyufa, utagundua umekuwa ukichezewa kwa muda mrefu sana.. Hata hivyo NGONO ni starehe kwa mwanaume sina uhakika na wanawake kama ni hivyo pia, awe ni tajiri au maskini. Kikubwa tujenge utashi wa kuwa raia wema na kuwajali wengine -hatutachezea wengine!. naomba kuwasilisha hoja.

Mzee wa Changamoto said...

Duh!!!
Nazidi KUTAMBUA UTAMBUZI WA WATAMBYUZI WENZANGU AMBAO UNANITAMBULISHA KILE KILICHOTAMBULIWA AMA KUTOTAMBULIWA NAMI.
Nawashukuru wote mliochangia. Ntarejea kujibu hoja. Wacha nimalizie "shughuli" za kuniweka na shibe kisha nitarejea