Thursday, December 10, 2009

Nini Chanzo???

Taswira hizi hapa chini za kusikitisha nimezipata toka kwenye Blog ya Kaka Albert G. Sengo alipoandika kuhusu MACHIMBO MADOGO MAPYA YA ALMASI NYAMONGOLO WILAYANI MISUNGWI MWANZA. Kuziona taswira hizi na kuangalia kinachotokea baada ya "kumalizika" kwa uchimbaji huu kumenifanya nijiulize maswali mengi ambayo nilijadilina na Prof Mbele mwanzoni mwa wiki. Hapa tunarejea kwenye maswali ya NANI MWENYE DHAMANA YA KULINDA NA KUTETEA MAZINGIRA NA RASILIMALI ZETU? Ni kwanini mwananchi anayechimba akijua fika kuwa anaharibu mazingira aendelee kuchimba? NA YUKO WAPI MTAWALA / KIONGOZI / MTENDAJI anayepaswa kusimamia ustawi wa eneo hili na watu wake?

Kama ningetakiwa kujibu swali hili ningesema TATIZO NI U-MIMI unaoendelea kulimung'unya taifa letu.
Hakuna anayejali mazingira kama unavyoona. Achimbaye anajali pato analopata, mwenye shimo anajali madini anayosaka na mwenyekiti ama mtendaji wa eneo hilo naye anajali "cha juu" atakachopewa (kwani siamini kama hajui kinachoendelea hapo)
Mwanzo wa kazi unavyokuwa. Kwa mujibu wa Kaka Sengo. Aliyesimama pembeni ndiye "mmiliki" wa "chimbo" hili
Na haya ni maliwato ya machimboni
Kazi "imechanganya" na hapo ni machimbo manne, wamiliki tofauti na hawana muingiliano wowote

Machimbo hubaki kama yaonekanavyo hapa. Yako wazi na HATARI kwa wakazi na mazingira. Waweza kuona kuwa hapa palikuwa na bado ni makazi ya watu

NINI CHANZO CHA KUJIHARIBIA KILICHO CHETU?
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

6 comments:

Anonymous said...

Mube, hii habari na picha ndivyo vimenitambulisha kwa G. Sengo wala sikuwa naifahamu blogu yake. Nimekutana na picha huko, nimeazimu kuzitumia kwa faida ya kumbukumbu, na sifa zote zimwendee Sengo!

Mbele said...

Mzee wa Changamoto, hii inatisha. Ni vigumu hata kujua mtu uanzie wapi kuitathmini hali hii.

Uroho upo hapo. Yaani kila mtu anachukua chake mapema na kwenda zake. Usalama wa mazingira sio shauri lake. Huyu ni mwananchi.

Baada ya muda utasikia serikali imeuza eneo kama hili kwa kampuni ya nje. Kampuni itakuja na maguvu kuwasambaratisha hao wananchi. Mapigano na hata mauaji yatatokea.

Kampuni nayo itaanza kazi ya kuhamisha madini na kuchafua zaidi mazingira. Ikimaliza kuchimba, inatuachia mashimo na jangwa. Ndio urithi wa vizazi vijavyo.

Kweli Bongo ni kichwa cha mwendawazimu. Kila mlevi ruksa kujifunzia kunyoa.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mimi nilishafika katika machimbo ya Dhahabu kule Geita kabla hayajauzwa. Sikwenda kuchimba bali nilitumwa kumnasua kijana wetu mmoja aliyekuwa "amekwama" huko na hakuwa na msaada wo wote.

Kwa kifupi ni kwamba suala la ulinzi wa mazingira halikuwepo. Eneo zima lilikuwa limejaa mashimo na watu walikuwa wanaishi katika mazingira machafu na ya hatari mno.

Mbaya zaidi - hakukuwa na onyo lolote kuhusu kuhusu matumizi hatari ya madini ya Mercury kwa afya ya binadamu. Ni hatari na hakuna anayejali. Na ukiangalia vizuri anayefaidika hasa na dhahabu ile ndipo utashangaa. Mgodi wa Geita umeshauzwa na sasa sijui hali huko ikoje.

Anonymous said...

ah mi naona sawa tu hao wananchi wajichimbie wale lamsingi ni kuzingatia usalama,maana hata hao watawala unaozungumza wakija watauza lasilimali za mtanzania kwa wazungu na pesaziingie mifukonimwao na wananchi wasifaidike na chochote kile....yaani hii nchi we acha tu...Dula wa Norway

Albert G.Sengo said...

Isitoshe migodi hii iko kama mita 25/30 kutoka barabara kuu iendayo Shinyanga - Dar es salaam. Kama sote ni vipofu na ikabahatika mmoja wetu mwenye nia nzuri akawa na jicho japo moja la kutizama, basi na tumtangulize mbele ili sisi makumi sambamba na yeye tushikane mikono kulifikia tundu la pango ambalo hatukumbuki kwamba tulitumbukizwa au tulitumbukia wenyewe tehe tehe....Inapendeza kuona kwamba jicho la mtanzania mmoja linaweza kutuongoza kuuona mlango wa pango hatimaye kujinasua....CHANGAMOTO oyeeee!!!!!

Bennet said...

Na hizi mvua zilizoanza kunyesha itakuwa balaa sasa hivi mtasikia watu wamefunikwa na vifusi