Monday, February 1, 2010

Ni kweli heri ya leo kuliko jana..........

Lakini sote twajua kuwa jana ilitakiwa kuwa heri kuliko mwakani Shule ya Msingi Mlamleni iliyopo Wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani ilivyo Jan/30/10
Picha na Mroki Mroki wa Daily News
Wodi ya Wazazi nchini Tanzania. Ni mwaka 2010. Taswira kwa hisani ya Dr Faustine's Baraza
Tunaelekea uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu. Na tunapoelekea "kuchaguana", tunaanza kusikia hili na lile kuhusu kilichofanyika katika miaka hii minne kuelekea mitano. Lakini ambalo halihitaji kuwa mwanasiasa kulitambua ni UONGO utakaokuja kwa wananchi kutoka kwa wanasiasa kuhusu "HALI ILIVYOKUWA NA ILIVYO SASA"

Nauita uongo kwa kuwa asilimia kubwa ya wanasiasa (na narejea tena kwa kusema ASILIMIA KUBWA) hawajishughulishi na uendelezaji wa maisha ya mTanzania wa kawaida. Wengi wao wapo mijini wakitelekeza majimbo na makazi yao waliyochaguliwa na kuja kuonekana wakati wa mbio za mwenge, ziara za Raisi na nyakati muhimu kama majanga na uchaguzi. Na kwa wakati huo mdogo wanajikita kwenye kubadili kimoja ama viwili vyenye kuonekana kirahisi na kisha wanakuja kusema "kuna maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa wakati naanza kipindi cha ubunge cha 2005 - 2010"

Sasa subiri uje kusikia TAKWIMU zao za nini kimefanyika ambacho wao wanaita "maendeleo". Watakutajia namba za majengo matupu (watakayoita shule) na majengo mengine yanayobatizwa jina la Zahanati / Hospitali. Watakuja na takwimu nzuri kuonesha kuwa Uchumi umepanda / kukua na kisha wataeleza kuwa hata ambapo pamegoma ni kutokana na kuanguka kwa uchumi kulikotokea duniani.

Lakini wananchi tunajiuliza kitu kimoja. NI KWELI KUWA WAMETUMIA KILA MALIGHAFI NA RASILIMALI ZILIZOPO KUENDELEZA MAJIMBO NA MAISHA YA WANANCHI WAO? Jibu ni HAPANA.

Ndio maana utawasikia wanasiasa wetu (bila aibu) wakitaja namna ambavyo maisha yetu sasa ni bora kuliko yalivyokuwa mwaka 2005 japo tunajua kuwa wangetumia Rasilimali zilizopo kwa usahihi, basi mwaka 2005 tungekuwa mbali kuliko ambapo tutakuwa mwakani.
Kuna mambo meeengi sana ambayo YANAHITAJI UELIMISHAJI NA RASILIMALI kuweza kufanikisha. Lakini kwa kuwa na uelimishaji pekee (kama rasilimali na uwezeshwaji wa kifedha haupo) kunaweza kupunguza mengi sana kwani kuna wakati ambao kufanya kitu kimoja ni zaidi ya kutofanya chochote. Sekta kama AFYA inaweza kuhitaji ushirikiano wa uelimishaji hata kama vifaa, pesa na madaktari wa kutosha havijawekwa ama kupatikana.
Mfano wa jambo ambalo uelimishaji unaweza kuwa sehemu ya suluhisho ni hili tatizo la vifo vya kinamama, kama ambavyo Bi Grace Maghembe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala akizungumzia kuhusu tatizo hilo alipohojiwa na kipindi cha IN FOCUS cha Televisheni ya Sauti Ya America (waweza anza sekunde ya 43)
Ninalowaomba wanasiasa wetu ni kuwa watakapokuja kwenye kampeni kutueleza maendeleo waliyoleta:
1: WATUELEZE WAMETUMIA ASILIMIA NGAPI YA RASILIMALI TULIZONAZO NA AMBAZO ZINGEWEZA KUTUMIKA KATIKA KUTEKELEZA WALIYOTEKELEZA?
2: NI ASILIMIA NGAPI YA AHADI ZAO (ZINAZOTEKELEZEKA) ZIMETEKELEZWA?
3: NI WAPI NA VIPI WAMEKOSEA KATIKA KIPINDI CHA 2005-2010 NA WAMEJIANDAA VIPI KUHAKIKISHA HILO HALITOKEI WAKICHAGULIWA TENA?


Labda NI KWELI KUWA KUANGALIA MAISHA YALIPO LEO TWAWEZA SEMA HERI YA LEO KULIKO JANA, LAKINI SOTE TWAJUA KUWA JANA ILISTAHILI KUWA NJEMA KULIKO ITAKAVYOKUWA KESHOKUTWA.
Heaven Help Us All
Blessings



Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

2 comments:

EDNA said...

Yaleyale waliyotuahidi miaka iliyopita ndiyo watakayotuahidi mwaka huu tena....Na kwa kuwa sisi ni wavivu wa kutafakari uozo watutendeao,basi tutawachagua tena tukiamini watatimiza yale waliyoahidi,Kwa kuwa tu wamesema muda haukuwatosha hivyo wanaomba wapewe nafasi nyingine....Ama kweli siasa ni mchezo mchafu.

Faustine said...

Aheri ya JANA kuliko LEO na KESHO haina matumaini makubwa.